Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nairobi—“Mahali Penye Maji Baridi”

Nairobi—“Mahali Penye Maji Baridi”

Nairobi—“Mahali Penye Maji Baridi”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

“Ni eneo kubwa lisilopendeza lenye umajimaji, eneo lenye upepo lisilokaliwa na watu, na eneo lenye maelfu ya wanyama wa pori wa kila aina. Kwa kuwa kuna kijia cha mikokoteni, yaelekea watu hupita kwenye eneo hilo mara kwa mara.”—THE GENESIS OF KENYA COLONY.

MANENO hayo yanaeleza jinsi eneo la Nairobi lilivyokuwa zaidi ya karne moja iliyopita, yaani, makao ya simba, vifaru, chui, twiga, nyoka wenye sumu, na maelfu ya wanyama wengine wa pori. Wamasai wajasiri walipeleka ng’ombe wao kwenye mto mmoja wenye maji safi unaopatikana huku, kwani jamii zinazohamahama hupenda maeneo ya aina hiyo. Wamasai waliuita mto huo Uaso Nairobi, yaani “Maji Baridi,” nao wakapaita mahali hapo Enkarre Nairobi, yaani “Mahali Penye Maji Baridi.” Baadaye, historia ya Kenya ilibadilishwa kabisa na eneo hilo lililopewa jina la Kimasai.

Jambo moja muhimu lililochangia ukuzi wa Nairobi ni ujenzi wa reli ya Kenya, ambayo wakati mmoja iliitwa Reli ya Kichaa. * Kufikia katikati ya mwaka wa 1899, kilometa 530 za reli hiyo zilikuwa zimekamilika, kuanzia jiji la pwani la Mombasa hadi Nairobi. Wakati huo, wajenzi wa reli hiyo walikuwa wametoka tu kushambuliwa na simba wawili ambao waliwaua wengi wa wafanyakazi wenzao, nao walikabili kazi ngumu ya kujenga reli katika eneo la Bonde Kuu la Ufa. Kwa kuwa reli hiyo ingefika ndani sana nchini, ilionekana kwamba mji wa Mombasa haukufaa tena kuwa sehemu kuu ya kuhifadhi bidhaa. Hata hivyo, ijapokuwa mandhari ya Nairobi haikupendeza, eneo hilo lilionwa kuwa linafaa kutumiwa kama kituo cha kupumzikia cha wafanyakazi na kituo cha kuhifadhia vifaa vya ujenzi. Mambo hayo yalichangia kufanya eneo hilo liwe jiji kuu la Kenya baadaye.

Mapema katika karne ya 20, eneo la Nairobi liliteuliwa kuwa kituo cha usimamizi cha East Africa Protectorate, kama Kenya ilivyoitwa zamani. Ikiwa mipango mizuri ingefanywa mapema, ingesaidia jiji hilo lililokuwa likisitawi. Badala yake, vibanda vilianza kujengwa ovyoovyo karibu na kituo cha gari-moshi. Vibanda hivyo vilijengwa kwa mbao, mabati, na vifaa vingine, na jiji la Nairobi likawa kama mtaa wa mabanda badala ya kuonekana kama kituo cha kimataifa cha wakati ujao. Majengo kadhaa yaliyokuwepo Nairobi mwanzoni mwa karne ya 20 yalijengwa kiholela. Pia, wakaaji walikabili hatari ya kushambuliwa na wanyama wa pori waliokuwa wakitangatanga karibu.

Punde si punde, magonjwa yalitokea katika eneo hilo. Wasimamizi wa kituo hicho kipya walikumbwa na tatizo kubwa kwa mara ya kwanza wakati tauni ilipolipuka. Wangetatuaje tatizo hilo haraka? Maeneo ya mji yaliyoathiriwa yaliteketezwa ili kuzuia tauni isienee! Miaka 50 baadaye, eneo la Nairobi lilibadilika kabisa na kuwa kituo kikuu cha kibiashara na cha kijamii katika Afrika Mashariki.

Jinsi Jiji Hilo la Kisasa Lilivyositawi

Jiji la Nairobi liko meta 1,680 hivi juu ya usawa wa bahari, hivyo linawawezesha watu kuona vizuri maeneo yanayozunguka. Wakati ambapo hakuna mawingu, ni rahisi kuona milima miwili mirefu ya Afrika. Ukitazama kaskazini, utaona Mlima Kenya ambao ndio mlima mrefu zaidi nchini Kenya na wa pili kwa urefu barani Afrika, kwani una urefu wa meta 5,199. Mlima Kilimanjaro uko upande wa kusini, kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania, nao ndio mrefu zaidi barani Afrika ukiwa na urefu wa meta 5,895. Miaka 150 iliyopita, wataalamu na wavumbuzi wa Ulaya walishangaa walipofahamu kwamba theluji na barafu huwepo nyakati zote juu ya mlima huo ulio karibu na ikweta.

Nairobi limekuwa jiji kwa zaidi ya miaka 50, nalo limebadilika kabisa. Majengo marefu yanayozidi kuibuka huonyesha kwamba jiji hilo linazidi kusitawi. Leo unaweza kuona majengo marefu ya glasi na chuma yakimetameta katika mwangaza wa jua. Mgeni anayetembelea eneo kuu la biashara la Nairobi anaweza kushangaa anapoambiwa kwamba miaka mia moja iliyopita mahali hapo palikuwa hatari kwa wanadamu, kwani wanyama wa pori walikuwepo.

Baada ya muda, mambo yakabadilika. Mimea kama vile mijakaranda, mikalitusi, na miwati ililetwa kutoka nchi za nje. Hivyo, miti ikapandwa kwenye vijia vya vumbi, na hadi leo watu wanaotembea kwa miguu hufurahia kivuli cha miti hiyo katika majira ya joto kali. Eneo fulani lililo karibu na jiji hilo, ambalo limetengwa ili kuhifadhi miti, lina angalau jamii 270 za miti. Huenda hiyo ndiyo sababu mwandishi mmoja alisema hivi: “Ni kana kwamba [jiji la Nairobi] limejengwa katikati ya msitu wa asili.” Miti mingi inayopatikana katika jiji hilo huchangia halijoto zenye kupendeza—joto wakati wa mchana na baridi wakati wa usiku.

Jiji Lenye Utamaduni Mbalimbali

Jiji la Nairobi ni kama sumaku kubwa, kwani limewavutia watu wa jamii mbalimbali. Sasa jiji hilo lina zaidi ya wakaaji milioni mbili. Ujenzi wa reli ulipomalizika, watu waliamua kukaa katika eneo hilo. Wahindi waliosaidia katika ujenzi huo, walibaki ili kuanzisha biashara ambazo zilisitawi na kusambaa kotekote nchini. Wafanyabiashara wengine walikuja kutoka Australia, Kanada, na nchi nyingine za Afrika.

Jiji la Nairobi lina watu wa jamii mbalimbali. Unaweza kumwona mwanamke Mhindi akielekea dukani akiwa amevalia vazi refu la Kihindi, unaweza kumwona mhandisi Mpakistan akiharakisha kufika kwenye eneo la ujenzi, pia unaweza kumwona mhudumu wa ndege kutoka Uholanzi akiingia katika mojawapo ya hoteli za jiji huku akiwa amevalia nadhifu, au mfanyabiashara Mjapani akiharakisha kuhudhuria mkutano muhimu wa kibiashara, labda kwenye soko kubwa la hisa la Nairobi. Isitoshe, unaweza kuwaona wenyeji wa jiji hilo wakisubiri magari kwenye vituo vya basi; wakifanya biashara vibandani; kwenye masoko, au madukani; huku wengine wakifanya kazi ofisini au katika viwanda vingi vya Nairobi.

Hata hivyo, inashangaza kwamba ni Wakenya wachache tu wanaoishi katika jiji hilo wanaoweza kuitwa “Wanairobi” halisi. Wakaaji wengi wametoka katika sehemu nyingine za nchi ya Kenya ili kujiruzuku. Kwa ujumla, wakaaji wa Nairobi ni wenye urafiki na wakarimu. Huenda ukarimu huo ndio umeliwezesha jiji hilo kuwa kituo cha mashirika ya kimataifa na ya kitaifa. Makao makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa yanapatikana Nairobi.

Mambo Yanayowavutia Wageni

Kuna wanyama wengi wa pori nchini Kenya. Mbuga nyingi za kitaifa na hifadhi za wanyama wa pori huwavutia maelfu ya watalii kila mwaka. Safari nyingi za utalii hupangwa na kuanza jijini Nairobi. Hata hivyo, watalii huja kutembelea Nairobi pia. Ni majiji machache sana ulimwenguni yaliyo na wanyama wa pori. Wageni huvutiwa na Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi, inayopatikana kilometa 10 hivi kutoka katikati ya jiji hilo. * Mgeni anayetembelea mbuga hiyo anaweza kuona wanyama walioishi jijini zamani. Mbuga hiyo imezingirwa tu na vipande kadhaa vya nyaya. Mnamo Septemba 2002, chui-dume alipatikana katika sebule ya nyumba moja jijini Nairobi. Alikuwa ametoka kwenye msitu ulio karibu!

Jumba la Makumbusho la Nairobi liko karibu na jiji hilo. Mamia ya wageni huenda huko kila siku kujifunza kuhusu historia ya Kenya yenye kupendeza. Jamii nyingi za wanyama wanaotambaa wanahifadhiwa katika hifadhi ya nyoka inayopatikana huko. Mamba anayehifadhiwa huko hababaiki watu wanapomtazama. Kobe aliye katika hifadhi hiyo huendelea na maisha yake ya kawaida licha ya shughuli nyingi zinazoendelea jijini. Nyoka ndio wenye nyumba, nao wanatia ndani swila, chatu, na vipiri. Kwa kuwa kuna viumbe hao hatari, unapaswa kutahadhari unapoona onyo hili: “Jihadhari na Nyoka Hatari”!

Maji Mengine

Ijapokuwa ule mto uliofanya jiji hilo liitwe Nairobi ungalipo, maji yake yamechafuliwa na takataka za viwandani na za nyumbani, sawa na inavyokuwa katika majiji mengi yanayoendelea kukua. Hata hivyo, kwa muda mrefu wakaaji wa Nairobi wamekuwa wakipata “maji” yanayotoka kwenye chanzo cha hali ya juu zaidi. Maji hayo ni ujumbe wa Biblia wa uhai unaofundishwa na Mashahidi wa Yehova.—Yohana 4:14.

Katika mwaka wa 1931, muda mrefu kabla ya jiji la Nairobi kuwa maarufu, Gray Smith na ndugu yake Frank, walitoka Afrika Kusini na kufika Kenya ili kueneza kweli za Biblia. Walitoka Mombasa na kufuata reli, huku wakipitia hali nyingi hatari—hata nyakati nyingine walilala karibu na wanyama wa pori. Waligawa vijitabu 600 na vitabu vingine vya Biblia katika eneo la Nairobi. Leo kuna Mashahidi 5,000 hivi katika makutaniko 61 ya jiji la Nairobi. Kupitia mikutano ya kutaniko na makusanyiko, sasa wakaaji wa Nairobi wanafahamu kazi ya Mashahidi wa Yehova. Wengi wamekubali ujumbe wa Biblia wenye tumaini.

Maisha Bora Wakati Ujao

Kitabu Encyclopædia Britannica kinasema hivi: “Mara nyingi kuna ukosefu mkubwa wa makao katika majiji yenye viwanda . . . Viwanda huchafua hewa na maji.” Hali ziko hivyo jijini Nairobi. Na kwa kuwa kila siku watu wanahamia Nairobi kutoka mashambani, huenda matatizo hayo yataongezeka. Hivyo, huenda jiji la Nairobi likapoteza fahari yake.

Hata hivyo, inafurahisha kujua kwamba hivi karibuni watu wote watafurahia maisha kikamili chini ya Ufalme wa Mungu, na wataishi bila matatizo yanayofanya maisha ya jijini yawe magumu.—2 Petro 3:13.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Kwa habari kamili kuhusu ujenzi wa reli hiyo, ona makala “‘Reli ya Kichaa’ ya Afrika Mashariki,” katika gazeti la Amkeni! la Septemba 22, 1998, ukurasa wa 21-24.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Nairobi

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mlima Kilimanjaro

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mlima Kenya

[Maelezo ya Chini]

Duncan Willetts, Camerapix

[Picha katika ukurasa wa 18]

Soko

[Picha katika ukurasa wa 19]

Frank na Gray Smith, mwaka wa 1931

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

© Crispin Hughes/Panos Pictures