Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Dawa ya UKIMWI Yahitajiwa Upesi!

Dawa ya UKIMWI Yahitajiwa Upesi!

Dawa ya UKIMWI Yahitajiwa Upesi!

Grace huuza viatu vya bei ghali katika Soko Kuu la Lilongwe, huko Malawi. Anaonekana kuwa mwenye furaha na mwenye afya. Hata hivyo, ijapokuwa anatabasamu, ana matatizo makubwa.

Katika mwaka wa 1993, Grace na mume wake walifurahi sana binti yao Tiyajane alipozaliwa. Mwanzoni, Tiyajane alionekana kuwa mwenye afya. Hata hivyo, muda si muda akaacha kuongeza uzito na kuambukizwa ugonjwa mmoja baada ya mwingine. Tiyajane alikufa kutokana na UKIMWI (ukosefu wa kinga mwilini) akiwa na umri wa miaka mitatu.

Miaka michache baadaye, mume wa Grace akaanza kuwa mgonjwa pia. Siku moja alizimia na kupelekwa hospitalini. Madaktari walishindwa kumwokoa. Mume wa Grace akafa kutokana na athari za UKIMWI baada ya ndoa yao ya miaka minane.

Sasa Grace anaishi peke yake katika chumba kimoja kwenye vitongoji vya Lilongwe. Kwa kuwa ana miaka 30, huenda ukamtazamia aanze upya maisha yake. Hata hivyo, Grace anaeleza hivi: “Kwa kuwa nina virusi vya UKIMWI, siwezi kuolewa wala kuzaa.” *

KWA kusikitisha, kuna visa vingi vya aina hiyo nchini Malawi, ambako inakadiriwa kwamba asilimia 15 ya watu wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Gazeti Globe and Mail linasema kwamba katika hospitali moja ya mashambani “idadi ya wagonjwa wanaolazwa imezidi kiwango cha kawaida kwa asilimia 50, na hospitali hiyo imepoteza zaidi ya nusu ya wafanyakazi” kwa sababu ya UKIMWI. Watu wengi hata zaidi wameambukizwa virusi vya UKIMWI katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Katika mwaka wa 2002, ripoti moja ya Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS) ilisema hivi: “Kwa sasa, watu katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara wanatarajiwa kuishi miaka 47. Ikiwa UKIMWI haungekuwepo, wangetarajiwa kuishi miaka 62.”

Hata hivyo, si bara la Afrika tu linalokumbwa na janga la UKIMWI. Mradi wa UNAIDS unakadiria kwamba watu wazima wapatao milioni nne nchini India wana virusi vya UKIMWI. Isitoshe, UNAIDS inasema hivi: “Kwa kuzingatia idadi ya watu walio na virusi vya UKIMWI, inaonekana watu wazima wengi watakufa hasa kutokana na ugonjwa huo katika kipindi hiki cha miaka kumi.” Ugonjwa huo unaenea upesi sana katika mataifa mengi yaliyokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti. Ripoti moja inasema kwamba huko Uzbekistan “idadi ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI mwaka wa 2002 pekee ilizidi ile ya wale walioambukizwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.” Huko Marekani, virusi vya UKIMWI vingali kisababishi kikuu cha vifo vya Wamarekani walio na umri wa kati ya miaka 25 na 44.

Mfululizo wa kwanza wa makala kuhusu UKIMWI katika gazeti la Amkeni! ulichapishwa mwaka wa 1986. Mwaka huohuo, Dakt. H. Mahler, aliyekuwa msimamizi wa Shirika la Afya Ulimwenguni, alionya kwamba huenda watu milioni kumi hivi tayari wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Miaka 20 hivi baadaye, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI ulimwenguni imeongezeka kufikia milioni 42 hivi. Idadi hiyo inaongezeka mara kumi zaidi ya ongezeko la idadi ya watu! Wataalamu wanasema kwamba hali itazidi kuwa mbaya. UNAIDS inaripoti hivi: “Katika nchi 45 zilizoathiriwa zaidi, inakadiriwa kwamba watu milioni 68 watakufa mapema kutokana na UKIMWI kati ya mwaka wa 2000 na 2020.”

Kwa kuwa idadi ya watu wanaoambukizwa inaongezeka haraka sana, ni wazi kwamba dawa ya UKIMWI inahitajiwa upesi kuliko wakati mwingine wowote. Hivyo, watafiti wa tiba wamejitahidi juu chini kupambana na virusi vya UKIMWI. Wamepata mafanikio gani? Je, kweli UKIMWI utakwisha?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Virusi vya UKIMWI huitwa HIV.

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Ulimwenguni pote, inakadiriwa kwamba watu milioni 42 wana virusi vya UKIMWI; milioni 2.5 ni watoto

[Picha katika ukurasa wa 4]

▪ INDIA Wahudumu wa afya wa kujitolea wanaelimishwa kuhusu UKIMWI

[Hisani]

© Peter Barker/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 4]

▪ BRAZILI Mfanyakazi wa huduma za jamii anamfariji mwanamke anayeugua UKIMWI

[Hisani]

© Sean Sprague/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 4]

▪ THAILAND Mfanyakazi wa kujitolea akimtunza mtoto aliyezaliwa akiwa na virusi vya UKIMWI

[Hisani]

© Ian Teh/Panos Pictures