Jangwa Lafanywa Kuwa Paradiso
Jangwa Lafanywa Kuwa Paradiso
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Lithuania
MWISHONI mwa karne ya 18, wakaaji wa kijiji kimoja kidogo cha wavuvi walihisi kwamba makao yao yalikuwa hatarini. Kwa miaka kadhaa, rundo kubwa la mchanga lilikuwa likisonga pole kwa pole kuelekea kijiji chao. Walijaribu kuzuia mchanga huo kwa kujenga kizuizi cha mbao chenye umbo la pembe-tatu, lakini hawakufanikiwa. Kufikia mwaka wa 1797, rundo hilo la mchanga lilikuwa limefunika kabisa kijiji chao.
Hilo lilikuwa tukio moja kati ya matukio yaliyotukia katika kipindi cha miaka 80. Katika kipindi hicho, marundo
ya mchanga yalifunika vijiji vingi na kufanyiza jangwa kwenye Rasi ya Curonia yenye urefu wa kilometa 100 iliyo karibu na Pwani ya Baltiki nchini Urusi na Lithuania. Inapendeza kujua kilichosababisha hali hiyo na jinsi eneo hilo lilivyoboreshwa na kuwa sehemu inayowavutia watalii wengi.Matokeo ya Matumizi Mabaya na Vita
Kwa karne nyingi, kulikuwa na mimea mingi na misitu katika Rasi ya Curonia. Wakaaji wa eneo hilo waliwinda wanyama wengi msituni. Kufikia mwanzoni mwa karne ya 18, eneo hilo lilikuwa limepata umaarufu kwa sababu lilikuwa njia ya kutuma barua kati ya Ulaya Magharibi na Milki ya Urusi. Katika kipindi cha amani, idadi ya watu iliongezeka na wanyama wa kufugwa walikula na kumaliza majani. Vilevile watu walikata miti sana msituni. Wakaaji hao hawakufahamu umuhimu wa mimea hiyo waliyoitegemea.
Misitu hiyo iliharibiwa kabisa wakati wanajeshi wa Urusi walipovamia eneo hilo mwaka wa 1757 na kukata miti ili kutengeneza mashua ambazo walitumia kuteka Königsberg (Kaliningrad), jiji muhimu la Prussia. Katika miaka ya baadaye, pepo zilisukuma marundo ya mchanga na kusababisha msiba uliotajwa mwanzoni.
Je, eneo hilo lililoharibiwa lingeweza kurudishwa katika hali yake ya awali? Mfanyakazi mmoja wa posta anayeitwa Georg David Kuwert na baba yake aliyeitwa Gottlieb ni kati ya watu waliosadiki hilo lingewezekana. Katika mwaka wa 1825, walianza kupanda miti katika eneo hilo. Ilikuwa kazi ngumu, yenye kuchosha, na iliyochukua muda mrefu. Kwa zaidi ya karne moja, mamia ya watu waliendeleza mradi huo. Kwanza, walihitaji kuzuia mchanga usitifuliwe na upepo kwa kupanda nyasi zenye mizizi mirefu ambazo zilisitawi vizuri katika mchanga wa eneo hilo. Kisha wakapanda aina tofauti-tofauti za misonobari na mibetula kwenye eneo lenye ukubwa wa maelfu ya ekari. Hatimaye, eneo
hilo lilirudia hali yake ya awali. Sasa asilimia 70 hivi ya eneo hilo lina miti. Watu huhisije wanapotembelea eneo hilo siku hizi?Paradiso Inayowavutia Watalii
Leo, watalii 8,000 hivi hutembelea Rasi ya Curonia kwa siku moja, na hilo halishangazi kwani kuna vivutio vingi. Unaweza kuona vitu mbalimbali, iwe unatembea, unaendesha baiskeli, au kutalii kwa gari. Kongoni, mbawala, mbweha, na nguruwe-mwitu hupatikana katika misitu ya eneo hilo. Aina mia moja hivi za ndege hupatikana huko, na ndege milioni moja hivi hupitia huko kila mwaka. Kuna aina 900 za mimea, na bado kuna marundo mengi ya mchanga ingawa sasa yanapatikana tu katika asilimia 12 ya eneo hilo.
Baadhi ya marundo ya mchanga yana kimo cha meta 50. Inafurahisha sana kutembea juu ya marundo hayo, huku ukiona tu mchanga na anga. Unapotembea, unaona kwamba marundo fulani yana umbo la bakuli lililofanyizwa na upepo. Unapofika kwenye kilele cha marundo hayo, ambapo mchanga husonga unaposukumwa na upepo, unaona mandhari yenye kuvutia. Unaona mazingira ya eneo hilo lote jembamba ambayo yanatia ndani vijiji, misitu, viwanja, na minara ya taa. Upande mmoja kuna mawimbi ya Bahari ya Baltiki; na upande mwingine kuna maji matulivu ya Wangwa wa Curonia.
Wageni huburudishwa na hewa baridi inayotoka baharini. Wengi hufurahia kuruka juu ya mawimbi kwa chombo cha pekee na kutumia mitumbwi. Wengine hutembea polepole katikati ya vijiji vya kale. Nyumba zilizopakwa rangi nyangavu zenye paa za makuti au za vigae huwakumbusha utulivu uliokuwapo zama za kale. Wageni wanapohisi harufu kali ya samaki walioanikwa ili kuhifadhiwa na kuona nyavu zilizoanikwa ili zikauke, wanakumbuka kwamba sikuzote uvuvi ulikuwa kazi kuu katika eneo hilo. Kuna vifaa vingi vinavyoonyesha mwelekeo wa upepo kwani wavuvi hutaka sana kujua upande ambao upepo unaelekea. Vifaa hivyo vimeundwa kwa njia yenye kupendeza sana, na watu hupenda kuvichunguza. Vifaa hivyo viliwekwa kwenye mlingoti wa kila mashua ili kuonyesha kwamba mashua ilikuwa imetoka katika kijiji fulani. Jambo jingine lenye kupendeza ni vipande vya kaharabu ambavyo nyakati nyingine hupatikana ufuoni baada ya kusukumwa na maji. Hasa katika siku zenye mawingu meusi, watalii hutembelea majumba ambayo huhifadhi vito vya kaharabu. Unaweza kuona mabaki ya mimea na wadudu ndani ya baadhi ya vito hivyo.
Basi, haishangazi kwamba mwakilishi wa Lithuania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, aliifafanua Rasi ya Curonia kuwa paradiso. Ni paradiso ambayo imerudishwa katika eneo lililokuwa limeharibiwa kabisa kwa sababu ya matumizi mabaya na vita. Bila shaka, ulimwenguni pote maeneo mengi bado yanaendelea kuharibiwa. Lakini Biblia inatuhakikishia kwamba chini ya Ufalme wa Mungu dunia nzima itageuzwa kuwa paradiso maridadi itakayokaliwa milele na watu wanyoofu.—Isaya 65:17, 21-25; 2 Petro 3:13, 14.
[Ramani katika ukurasa wa 16]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
BAHARI YA BALTIKI
LITHUANIA
RASI YA CURONIA
Wangwa wa Curonia
URUSI
Kaliningrad
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Kuna ndege wengi, mimea mingi, na marundo mengi ya mchanga kwenye Rasi ya Curonia
[Hisani]
Bottom three inset photos: Gedimino Graz̆ulevic̆iaus nuotrauka
Bird and grass: Gedimino Graz̆ulevic̆iaus nuotrauka; background: UAB „Laiko spalvos“
FOTO: A. VARANKA ▼
[Picha katika ukurasa wa 18]
Nguruwe-mwitu
Bata-maji
Kaharabu
[Hisani]
Top three photos: Gedimino Graz̆ulevic̆iaus nuotrauka
[Picha katika ukurasa wa 18]
Maelfu ya watalii hutembelea Rasi ya Curonia kila siku