Je, Barabara Zote Zilielekea Roma?
Je, Barabara Zote Zilielekea Roma?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRIA
BARABARA za Milki ya Roma ziliunganisha maeneo mbalimbali ya milki hiyo kubwa na jiji lake kuu. Vilevile, barabara hizo ziliwezesha vikosi vya askari-jeshi wa Milki ya Roma kufikia karibu maeneo yote na kuwatiisha watu chini ya milki hiyo. Barabara nyingine ndogo kutoka kwenye mikoa ya Milki hiyo ya Roma ziliungana na barabara hizo kuu. Hivyo ndivyo msemo huu ulivyoanza, “Barabara zote zinaelekea Roma.”
Urefu wa barabara zote za Milki ya Roma ukijumlishwa ulikuwa zaidi ya kilometa 80,000. Leo, tunawezaje kujifunza kuzihusu na kuelewa jinsi zilivyokuwa muhimu katika ulimwengu wa wakati huo? Njia moja ya kufanya hivyo ni kuchunguza ramani ya karne ya 13 inayoitwa Mchoro wa Peutinger.
Wanahistoria wanaamini kwamba Mchoro wa Peutinger ni nakala ya ramani iliyochorwa wakati askari-jeshi Waroma walipokuwa wakitumia barabara hizo maarufu. Katika mwaka wa 1508, Konrad Peutinger, katibu wa jiji la Augsburg, lililoko kusini mwa Ujerumani, alipata nakala hiyo iliyochorwa kwa mkono nayo ikaitwa kwa jina lake. Leo mchoro huo unapatikana katika Maktaba ya Kitaifa ya Austria huko Vienna, nao huitwa Tabula Peutingeriana katika Kilatini.
Hati ya Kukunja ya Barabara za Milki ya Roma
Katika shule fulani, wanafunzi hutumia ramani zenye umbo la mraba. Hata hivyo, Mchoro wa Peutinger ni hati ya kukunja ambayo inapokunjuliwa ina upana wa sentimeta 34 na urefu wa zaidi ya meta 6.75. Mwanzoni mchoro huo ulifanyizwa kwa vipande 12 vya ngozi vilivyounganishwa kwa gundi. Vipande 11 kati ya hivyo vingalipo. Mchoro huo unaonyesha jinsi Milki ya Roma ilivyokuwa wakati wa usitawi wake, kuanzia Uingereza hadi India. Hata ikiwa unafahamu eneo hilo katika ramani za kisasa, huenda ukachanganyikiwa
unapotazama Mchoro wa Peutinger kwa mara ya kwanza. Kwa nini?Mchoro wa Peutinger ulikusudiwa utumiwe na wasafiri wa kale wala si wanajiografia wa leo. Mtu aliposafiri ilikuwa rahisi kutumia ramani iliyokunjwa. Lakini ili sehemu zote ziweze kutoshea kwenye hati ya kukunja, mchoraji wa ramani hiyo alihitaji kufupisha urefu wa kaskazini hadi kusini wa milki hiyo na kuongeza sana urefu wa kutoka mashariki hadi magharibi. Hivyo ramani hiyo haikuwa na vipimo sahihi, lakini ilikuwa rahisi kuifungua, kuitazama, kuikunja, na kuibeba. Msafiri angejua haraka njia bora ya kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine. Hilo lilikuwa muhimu zaidi kwa wasafiri kuliko kujua umbo la Italia, ukubwa wa Bahari Nyeusi, au kujua upande hususa waliokuwa wakielekea.
Mambo mbalimbali katika Mchoro wa Peutinger hutofautishwa kwa rangi mbalimbali. Barabara zimechorwa kwa mistari myekundu, milima kwa rangi ya kahawia, na mito kwa rangi ya kijani. Mchoro huo unaonyesha majina ya mamia ya miji na huonyesha mahali yalipo kwa ishara kama vile nyumba, nyua, na minara. Ishara hizo zinaonyesha majengo yanayopatikana katika kila sehemu. Pia mchoro huo unaonyesha umbali uliopo kati ya miji, vituo vya usafiri, na sehemu za kupumzikia.
Baadhi ya maeneo na matukio yanayotajwa katika Biblia yameonyeshwa kwenye Mchoro wa Peutinger. Kuna maelezo mawili yaliyoandikwa katika Kilatini mahali ambapo Mlima Sinai umeonyeshwa. Maelezo ya kwanza yanasema: “Jangwa ambamo wana wa Israeli walitangatanga kwa miaka 40 wakiongozwa na Musa.” (Yoshua 5:6) Maelezo yale mengine yanasema: “Hapa ndipo walipopewa Sheria kwenye Mlima Sinai.”—Mambo ya Walawi 27:34.
Eneo la Yerusalemu limeonyeshwa kwa maelezo mafupi ambayo yanatia ndani jina tofauti la jiji hilo, yaani, Aelia Capitolina, ambalo limetokana na jina la Publius Aelius Hadrianus, anayejulikana zaidi kama Hadrian. Katika karne ya pili W.K., maliki huyo Mroma aliliita jiji hilo kwa jina lake. Jina la Kilatini la Mlima wa Mizeituni limeonyeshwa pia katika mchoro huo.—Luka 21:37.
Je, Barabara Zote Zilielekea Roma?
Barabara fulani zilielekea Aquileia, jiji lililokuwa kaskazini-mashariki mwa Italia. Katika mchoro huo, jiji la Aquileia linaonekana likiwa na kuta imara na minara ya ulinzi. Aquileia lilikuwa mojawapo ya majiji muhimu zaidi katika Milki ya Roma kwani lilikuwa na makutano ya barabara muhimu na bandari nzuri.
Barabara ya Via Egnatia ilipita Rasi ya Balkan kuanzia Pwani ya Adriatiki hadi Constantinople, na sasa linaitwa Istanbul. Katika Mchoro wa Peutinger, jiji hilo limeonyeshwa kwa picha ya mungu wa kike aliyeketi katika kiti cha enzi akiwa tayari kwa vita. Barabara kadhaa zinaelekea Antiokia ya Siria, ambayo sasa ni jiji la Uturuki la Antakya. Antiokia lilikuwa jiji la tatu kwa ukubwa katika Milki ya Roma, baada ya Roma na Aleksandria. Jiji hilo limeonyeshwa kwa mchoro wa mungu wa kike aliyeketi akiwa na nuru ya mviringo juu ya kichwa chake.
Mchoro wa Peutinger unaonyesha barabara 12 zikielekea Roma. Mojawapo ya barabara hizo ni ile iitwayo Via Appia, au Barabara ya Appia. Kitabu cha Matendo kinaonyesha kwamba mtume Paulo alipitia barabara hiyo katika safari yake ya kwanza kwenda Roma. Paulo alipokuwa safarini, Wakristo fulani walikuja kutoka Roma kwa kutumia Barabara ya Appia na kukutana naye katika Mikahawa Mitatu, ambayo pia imeonyeshwa kwenye mchoro huo.—Matendo 28:15.
Ni ishara gani ambayo imetumiwa kuonyesha Roma katika Mchoro wa Peutinger? Imewakilishwa na malkia mtukufu mwenye vazi la zambarau aliyeketi kwenye kiti cha enzi. Malkia huyo amebeba tufe na fimbo ya enzi zinazowakilisha mamlaka ya milki hiyo juu ya ulimwengu wote iliyotawala kutoka Roma.
Je, ni sawa kusema kwamba barabara hizo zote zilielekea Roma? Ndiyo, hasa unapofikiria zile barabara nyingi ndogo zilizoungana na barabara kuu. Mchoro wa Peutinger unaonyesha jinsi barabara kuu za milki hiyo zilivyowezesha Milki ya Roma kupanuka, na kutiisha mikoa yake kwa miaka 500 hivi. Leo, bado unaweza kutembea kwenye barabara hizo za kale na kuiona Milki ya Roma akilini mwako kwa kutumia Mchoro wa Peutinger.
[Ramani katika ukurasa wa 13-15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mchoro wa Peutinger ni ramani ya pekee ya barabara
HISPANIA
MOROCCO
UINGEREZA
UFARANSA
UJERUMANI
AUSTRIA
Aquileia
Roma
Sehemu iliyoongezwa ukubwa katika ukurasa wa 15
ITALIA
AFRIKA
UGIRIKI
Istanbul
MISRI
UTURUKI
Mlima Sinai
Yerusalemu
SIRIA
Antakya
Bahari ya Caspian
IRAN
INDIA
[Ramani katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mchoro wa Peutinger unaonyesha Roma na maeneo ya karibu
Roma
Aquileia
Istanbul
Yerusalemu
Antakya