Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuvua Samaki Kwenye Barafu

Kuvua Samaki Kwenye Barafu

Kuvua Samaki Kwenye Barafu

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Finland

KUNAPOKUWA na theluji katika majira ya baridi kali huko Kaskazini, watu hufurahia kufanya shughuli mbalimbali nje. Ili kufurahia mandhari hiyo inayovutia ya theluji na hewa baridi iliyo safi, watu huenda kutembea, kuteleza kwenye barafu kwa kutumia magongo, kutembea kwa viatu vyenye magurudumu, au kuendesha vigari vya kuteleza kwenye barafu. Pia kuna wale ambao hupendelea kuvua samaki kwenye barafu. Nimejiuliza hivi mara nyingi: ‘Kwa nini watu huvutiwa sana kuvua samaki kwenye barafu?’ Hivyo, nilimwomba rafiki yangu Martti, ambaye ni mvuvi stadi, aandamane nami alipokuwa akienda kuvua samaki kwenye barafu.

Nilifika kwa Martti asubuhi na mapema. Tayari alikuwa amekusanya vifaa vilivyohitajiwa, yaani fito, vyambo, viti, na kifaa cha kutoboa barafu ambacho ndicho kifaa muhimu zaidi. Nilihitaji tu kubeba mavazi yanayofaa. Mtu anahitaji kuwa na nguo nyingi zinazoweza kuhifadhi joto. Mvuvi anahitaji nguo hizo kwa kuwa yeye huketi kwa muda mrefu, na kunaweza kuwa na baridi kali katika sehemu zilizo wazi kama vile baharini au kwenye maziwa. Martti huvua samaki baharini kwa sababu yeye huishi karibu na bahari. Ikiwa angekuwa anaishi mbali na bahari yaelekea angevua samaki katika maziwa au mito.

Tunapofika ufuoni na kuanza kutembea juu ya barafu ninajiuliza swali hili: ‘Je ni salama kutembea juu ya barafu?’ Bila shaka ni salama hasa wakati huu wa mwaka, kwani barafu huwa ngumu sana kwa sababu ya baridi. Hata hivyo, unahitaji kuwa mwangalifu unapotembea juu ya barafu. Hata wakati wa baridi kali huenda barafu isiwe ngumu katika sehemu fulani. Ni muhimu kujua jinsi barafu ilivyo, kujua hatari ambazo huenda ukakabili, na kuwa na vifaa vinavyohitajiwa. Baada ya kutembea juu ya barafu kwa muda fulani, Martti anaanza kutoboa shimo kwenye barafu. Anaitoboa haraka sana kwa kutumia kifaa cha kutoboa barafu, na kwa muda mfupi tu anatoboa shimo lenye kina cha sentimeta 70. Kisha Martti anaondoa barafu kwa kutumia kifaa chenye mashimo mengi madogo-madogo. Halafu anaketi kwenye kiti na kutayarisha ndoano yake, kisha anaitumbukiza majini kupitia lile shimo ambalo ametoboa.

Ijapokuwa njia hiyo ya kuvua samaki, yaani, kutoboa shimo kwenye barafu kisha kuvua samaki kupitia shimo hilo, huonekana kuwa rahisi, ni wazi kwamba mtu atafanikiwa zaidi iwapo ana ustadi. Kwa mfano, ni muhimu kuchagua mahali panapofaa ili kuvua samaki. Kwa sababu mara nyingi samaki hukaa mahali pamoja tu wakati wa baridi kali, ni muhimu kujua mahali walipokusanyika. Martti alipokuwa akivua samaki wakati uliopita, aliamua mahali ambapo tutaenda kuvua pindi hii. Ikiwa tungeenda kuvua samaki mahali asipopafahamu, yaelekea angechunguza ramani mapema kwa uangalifu zaidi na kuamua ni wapi panapofaa kuvua samaki mara hii. Isitoshe, mvuvi stadi hufikiria hali ya hewa na jinsi inavyohusiana na kuhama kwa samaki kutoka eneo moja hadi jingine. Anaweza kuwatafuta samaki kwa kutoboa mashimo sehemu tofauti-tofauti. Huenda mvuvi akatoboa mashimo mengi sana kwa siku moja.

Leo, ni kana kwamba samaki wamejificha au hawana njaa, kwani hatukufanikiwa kuvua samaki wowote. Hata hivyo, jambo hilo halituhangaishi. Bila shaka nimefahamu kwa nini watu hufurahia kuvua samaki kwenye barafu. Zaidi ya kuvua samaki, unaweza kufurahia mandhari na maumbile. Martti anakata kauli hii: “Ni kama likizo, hasa kwa wakaaji wa mjini. Inakuwezesha kusahau mahangaiko yako yote.”

[Picha katika ukurasa wa 27]

Kutoboa mashimo kwenye barafu

[Picha katika ukurasa wa 27]

Kifaa cha kutoboa mashimo kwenye barafu