Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI

Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI

Mafanikio Katika Pambano Dhidi ya UKIMWI

Katika kitabu chake AIDS Update 2003, Dakt. Gerald J. Stine anasema kwamba utafiti kuhusu UKIMWI ni hatua kubwa sana ya kisayansi. Kwa kipindi kifupi, watafiti wamejifunza mambo mengi sana kuhusu ugonjwa huo wenye kutatanisha sana. Wamepata mafanikio gani?

UJUZI na utaalamu wa kitiba umewawezesha watafiti kugundua dawa ambazo zikitumiwa pamoja zinaweza kuwasaidia watu walio na virusi vya UKIMWI. Isitoshe, miradi ya kuelimisha watu kuhusu UKIMWI imefanikiwa katika nchi kadhaa. Lakini je, mafanikio hayo yanaonyesha kwamba ugonjwa huo umeanza kukomeshwa? Je, jitihada za kisayansi na za kuwaelimisha watu zinaweza kuzuia kuenea kwa UKIMWI? Fikiria mambo yafuatayo.

Kutumia Dawa

Gazeti Time la Septemba 29, 1986, lilikuwa na kichwa hiki, “Kuna Tumaini Katika Pambano Dhidi ya Ukimwi.” “Tumaini” hilo lilitokea wakati dawa ya azidothymidine (AZT) ilipojaribiwa. Hiyo ni dawa ya kudhibiti virusi na inatumiwa kutibu watu wenye virusi vya UKIMWI. Inapendeza kwamba watu wenye virusi vya UKIMWI waliotumia AZT waliishi kwa muda mrefu zaidi. Tangu wakati huo, dawa za kudhibiti virusi zimerefusha maisha ya mamia ya maelfu ya watu. (Ona sanduku “Dawa za Kudhibiti Virusi,” kwenye ukurasa wa 7.) Je, dawa hizo zimefaulu kuwatibu watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI?

Licha ya msisimko uliotokea baada ya dawa ya AZT kugunduliwa, gazeti Time liliripoti kwamba watafiti wa UKIMWI “walikuwa na uhakika kuwa dawa ya AZT haiwezi kuponya UKIMWI.” Walisema kweli. Wagonjwa fulani waliathiriwa na dawa ya AZT, hivyo dawa nyingine za kudhibiti virusi zikabuniwa. Baadaye, Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani liliidhinisha dawa mbalimbali za kudhibiti virusi zitumiwe pamoja ili kuwatibu wagonjwa walioathiriwa sana na virusi vya UKIMWI. Wafanyakazi wanaowahudumia wagonjwa wa UKIMWI waliyasisimukia matibabu hayo ambayo baadaye yalihusisha kutumia pamoja dawa tatu au zaidi ili kudhibiti virusi. Kwenye mkutano mmoja wa kimataifa kuhusu UKIMWI uliofanywa mwaka wa 1996, daktari mmoja alitangaza kwamba huenda dawa hizo zikaangamiza kabisa virusi vya UKIMWI mwilini!

Kwa kusikitisha, katika kipindi cha mwaka mmoja, ilionekana wazi kwamba virusi vya UKIMWI haviwezi kukomeshwa hata dawa hizo tatu zinapotumiwa pamoja. Hata hivyo, ripoti moja ya UNAIDS inasema kwamba “kutumia pamoja dawa mbalimbali za kudhibiti virusi kumewawezesha watu walio na virusi vya UKIMWI kuishi maisha marefu zaidi, wajihisi nafuu, na kuendelea na shughuli zao maishani.” Kwa mfano, huko Marekani na Ulaya, matibabu hayo yamepunguza vifo vinavyosababishwa na UKIMWI kwa zaidi ya asilimia 70. Isitoshe, uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba matibabu ya pekee yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi yanaweza kupunguza sana uwezekano wa mama mjamzito kumwambukiza mtoto wake virusi vya UKIMWI.

Hata hivyo, mamilioni ya watu walio na virusi vya UKIMWI hawapati dawa hizo. Kwa nini?

“Ugonjwa Unaowakumba Hasa Maskini”

Dawa za kudhibiti virusi hutumiwa sana katika nchi tajiri. Hata hivyo, Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba katika nchi fulani zinazoendelea, ni asilimia 5 tu ya wagonjwa wanaopata dawa hizo. Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wamefafanua hali hiyo kuwa “ukosefu mkubwa wa haki” na “ukosefu mkubwa wa maadili katika ulimwengu wa leo.”

Katika nchi fulani, wagonjwa wengine hupata dawa hizo na wengine hawazipati. Gazeti The Globe and Mail linaripoti kwamba Mkanada 1 kati ya Wakanada 3 anayekufa kutokana na UKIMWI, hajawahi kutibiwa kwa dawa za kudhibiti virusi. Hata ingawa dawa hizo hutolewa bila malipo nchini Kanada, watu fulani wamepuuzwa. Gazeti Globe linasema kwamba “wale wasiopata matibabu yanayofaa ndio hasa wanaoyahitaji zaidi, yaani, wenyeji wa asili, wanawake na maskini.” Gazeti The Guardian lilimnukuu mama mmoja Mwafrika ambaye ana virusi vya UKIMWI akisema hivi: “Sielewi kwa nini wanaume wazungu ambao hufanya ngono na wanaume wenzao wanaendelea kuishi nami naelekea kufa!” Tatizo ambalo mama huyo alitaja linahusiana na biashara ya kutengeneza na kugawanya dawa.

Huko Marekani na Ulaya, matibabu yanayohusisha dawa tatu za kudhibiti virusi hugharimu kwa wastani kati ya dola 10,000 na dola 15,000 kwa mwaka. Ingawa katika nchi fulani zinazoendelea dawa zilizoigwa za matibabu hayo hugharimu dola 300 au chini kwa mwaka, bado watu wengi walio na virusi vya UKIMWI na wanaoishi katika maeneo ambako dawa hizo zinahitajiwa sana hawawezi kuzipata. Dakt. Stine anasema hivi kuhusu hali hiyo: “UKIMWI ni ugonjwa unaowakumba hasa maskini.”

Biashara ya Kutengeneza Dawa

Haijawa rahisi kutengeneza dawa zilizoigwa na kuziuza kwa bei ya chini. Katika nchi nyingi kuna sheria kali zinazowakataza watu kutengeneza dawa hizo bila idhini. Msimamizi wa kampuni moja kubwa ya kutengeneza dawa anasema kwamba “hilo ni pambano la kibiashara.” Anasema kwamba kutengeneza dawa zilizoigwa na kuziuza katika nchi zinazoendelea ili kupata faida “ni kuwadhulumu watu waliovumbua dawa hizo.” Pia, makampuni yaliyo na haki ya kutengeneza dawa fulani yanasema kwamba kupungua kwa faida kunaweza kusababisha ukosefu wa pesa za kutosha kugharimia miradi ya utafiti na maendeleo ya kitiba. Wengine wanahofia kwamba dawa za bei ya chini za kudhibiti virusi ambazo zimekusudiwa kupelekwa katika nchi zinazoendelea zinaweza kuuzwa kimagendo katika nchi zilizoendelea.

Watetezi wa dawa hizo za bei ya chini wanadai kwamba utengenezaji wa dawa mpya unaweza kugharimu kati ya asilimia 5 na asilimia 10 ya gharama zinazopendekezwa na makampuni ya kutengeneza dawa. Pia wanasema kwamba miradi ya utafiti na ya maendeleo inayosimamiwa na makampuni ya kibinafsi ya kutengeneza dawa hupuuza magonjwa yanayokumba nchi maskini. Hivyo, Daniel Berman, msimamizi wa Mradi wa Kuwawezesha Watu Kupata Dawa za Msingi, anasema: “Kunahitajika kuwa na mfumo wa kimataifa wa kupunguza bei za dawa mpya ili watu katika nchi zinazoendelea wazipate.”

Kutokana na uhitaji huo wa dawa za kudhibiti virusi ulimwenguni pote, Shirika la Afya Ulimwenguni limeanzisha mradi wa kutoa dawa hizo kwa watu milioni tatu walio na virusi vya UKIMWI kufikia mwishoni mwa mwaka wa 2005. Nathan Ford wa Shirika la Médecins Sans Frontières anasema: “Tunatarajia kwamba mradi huo hautakosa kufaulu kama miradi mingine ya Umoja wa Mataifa. Idadi hiyo ya watu milioni tatu ni nusu tu ya watu waliokadiriwa kuwa wanahitaji matibabu ya UKIMWI leo, nayo itaongezeka sana [kufikia mwaka wa 2005].”

Vizuizi Vingine

Hata nchi zinazoendelea zikipata dawa za kutosha za kudhibiti virusi, bado kuna vizuizi vingine. Dawa fulani zinahitaji kumezwa pamoja na maji safi na chakula, lakini mamia ya maelfu ya watu katika nchi kadhaa hula baada ya kila siku mbili. Dawa hizo (mara nyingi tembe 20 au zaidi kwa siku) zinapaswa kumezwa kwa wakati hususa kila siku, lakini wagonjwa wengi hawana saa. Wagonjwa wanapaswa kupewa dawa mbalimbali kulingana na hali zao. Lakini katika nchi nyingi hakuna madaktari wa kutosha. Bila shaka, ni vigumu sana kuwatibu watu kwa dawa za kudhibiti virusi katika nchi zinazoendelea.

Hata wagonjwa katika nchi zinazoendelea wanakabili matatizo ya kutumia dawa mbalimbali pamoja. Utafiti unaonyesha kwamba watu wengi sana hawamezi dawa zote kwa wakati unaofaa. Hilo linaweza kufanya virusi vianze kukinza dawa. Halafu watu wengine wataambukizwa virusi sugu vya UKIMWI.

Dakt. Stine anataja tatizo lingine linalowakumba watu walio na virusi vya UKIMWI. Anasema hivi: “Jambo la kushangaza kuhusu matibabu ya virusi vya UKIMWI ni kwamba nyakati nyingine matibabu hayo husababisha maumivu mengi kuliko ugonjwa wenyewe, hasa ugonjwa huo unapoanza kutibiwa kabla ya dalili kuonekana.” Watu walio na virusi vya UKIMWI ambao wanatumia dawa za kudhibiti virusi huathiriwa na matatizo kama vile ugonjwa wa kisukari, kuenea kwa mafuta katika sehemu mbalimbali za mwili tofauti na ilivyokuwa awali, kuongezeka kwa kolesteroli mwilini, na kupungua kwa uzito wa mifupa. Baadhi ya athari hizo zinaweza kusababisha kifo.

Jitihada za Kuzuia UKIMWI Usienee

Kumekuwa na mafanikio gani katika jitihada za kuzuia UKIMWI usienee na katika jitihada za kubadili mazoea hatari yanayofanya watu waambukizwe? Imekadiriwa kwamba miradi ya kuwaelimisha watu kuhusu UKIMWI nchini Uganda katika miaka ya 1990, ilipunguza kuenea kwa virusi vya UKIMWI nchini humo kutoka asilimia 14 hadi asilimia 8 katika mwaka wa 2000. Vivyo hivyo, jitihada za Senegal za kuwaelimisha raia zake kuhusu hatari za kuambukizwa virusi vya UKIMWI zimewezesha viwango vya kuenea kwa virusi hivyo visizidi asilimia 1 miongoni mwa watu wazima. Mafanikio hayo yanafurahisha sana.

Kwa upande mwingine, jitihada za kuwaelimisha watu kuhusu UKIMWI hazijaleta mafanikio makubwa katika nchi nyingine. Uchunguzi uliofanywa mwaka wa 2002 kuhusu vijana 11,000 nchini Kanada ulionyesha kwamba nusu ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule za sekondari waliamini kuna tiba ya UKIMWI. Kulingana na uchunguzi uliofanywa mwaka huohuo nchini Uingereza, asilimia 42 ya wavulana walio kati ya miaka 10 na 11 hawakuwa wamesikia kuhusu UKIMWI. Kwa upande mwingine, vijana wanaojua kwamba kuna UKIMWI na kwamba hauna tiba, hawajali. Daktari mmoja anasema hivi: “Vijana wengi huona UKIMWI kuwa sawa na matatizo ya kawaida yanayowahangaisha kama vile wataishi na nani, ikiwa watapata chakula kizuri, na ikiwa wataenda shule.”

Basi, si ajabu kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kuwa “huenda kuwalenga vijana kukawa njia bora zaidi ya kupambana na ugonjwa huo, hasa katika nchi zenye watu wengi walioambukizwa.” Vijana wanaweza kusaidiwaje kutii maonyo ambayo wamepewa kuhusu UKIMWI? Je, tunaweza kutarajia kupata dawa ya UKIMWI?

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Mwaka uliopita, asilimia 2 ya watu wanaohitaji dawa za kudhibiti virusi barani Afrika walizipata, ikilinganishwa na asilimia 84 katika mabara ya Amerika

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Dawa za Kudhibiti Virusi *

Katika mwili wa mtu mwenye afya, chembe zinazoitwa helper T huchochea mfumo wa kinga ili upigane na maambukizo. Virusi vya UKIMWI hushambulia chembe hizo hasa. Virusi hivyo hutumia chembe za helper T kutokeza virusi vingine vya UKIMWI, kisha hudhoofisha na kuharibu chembe hizo mpaka mfumo wa kinga unapodhoofika kabisa. Dawa za kudhibiti virusi huzuia virusi hivyo visiongezeke.

Kwa sasa, dawa nne za kudhibiti virusi zinatumiwa katika matibabu. Dawa zinazoitwa nucleoside analogues na non-nucleoside analogues huzuia virusi vya UKIMWI visiathiri DNA ya mtu. Dawa zinazoitwa protease inhibitors huzuia kimeng’enya fulani kilicho ndani ya chembe zilizoambukizwa kisitokeze virusi vipya vya UKIMWI. Dawa zinazoitwa fusion inhibitors huzuia virusi vya UKIMWI visiingie ndani ya chembe. Kwa kuzuia virusi vya UKIMWI visiongezeke, dawa za kudhibiti virusi zinaweza kumzuia mtu aliye na virusi hivyo asipate UKIMWI haraka, kwani ugonjwa huo hutokea mtu anapokuwa amedhoofishwa kabisa na virusi hivyo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 28 Matibabu yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi hayatolewi kwa watu wote walio na virusi vya UKIMWI. Wale walio na virusi vya UKIMWI au wale wanaodhania kwamba wanavyo wanapaswa kupata ushauri wa wataalamu wa tiba kabla ya kupata matibabu yoyote. Amkeni! halipendekezi tiba yoyote hususa.

[Picha]

KENYA Daktari anamshauri mgonjwa wa UKIMWI kuhusu dawa za kudhibiti virusi

[Hisani]

© Sven Torfinn/Panos Pictures

[Picha]

KENYA Mgonjwa wa UKIMWI katika hospitali akipokea dawa za kudhibiti virusi

[Hisani]

© Sven Torfinn/Panos Pictures

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Wanawake na UKIMWI

Nusu ya watu wazima walio na virusi vya UKIMWI ni wanawake

Ilipogunduliwa kwamba wanawake fulani wana ugonjwa wa UKIMWI katika mwaka wa 1982, ilidhaniwa walikuwa wameambukizwa kupitia sindano za dawa za kulevya. Punde baadaye, iligunduliwa kwamba wanawake wanaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI kwa kufanya ngono kama kawaida na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa virusi hivyo. Ulimwenguni pote, nusu ya watu wazima walio na virusi vya UKIMWI ni wanawake. UNAIDS inaripoti hivi: “Ugonjwa huo huwapata hasa wanawake na wasichana waliobalehe ambao huathiriwa kwa urahisi kwa sababu ya hali za kijamii, kitamaduni, kimwili, na kiuchumi, na ambao huwatunza wagonjwa na wale wanaoelekea kufa.”

Kwa nini watu wanaowahudumia wagonjwa wa UKIMWI wanahangaikia sana jinsi ugonjwa huo ulivyoenea miongoni mwa wanawake? Mara nyingi, wanawake walio na virusi vya UKIMWI hubaguliwa zaidi ya wanaume, hasa katika nchi zinazoendelea. Ikiwa mwanamke ni mjamzito, afya ya mtoto wake imo hatarini; ikiwa ana watoto, inakuwa vigumu kuwatunza, hasa ikiwa hana mume. Isitoshe, kwa kulinganisha, ni mambo machache tu yanayojulikana kuhusu hali za kipekee na matibabu ya wanawake walioambukizwa virusi vya UKIMWI.

Hali fulani za kitamaduni huwafanya wanawake wakabili hatari kubwa zaidi. Katika nchi nyingi, wanawake hawaruhusiwi kuzungumza kuhusu ngono, nao hukabili hatari ya kubakwa wanapokataa kufanya ngono. Kwa kawaida, wanaume hufanya ngono na wanawake wengi na kuwaambukiza virusi vya UKIMWI bila kujua. Wanaume fulani Waafrika hufanya ngono na wasichana ili kuepuka kuambukizwa virusi hivyo au kwa kuamini kwamba kufanya ngono na mabikira kunaweza kuponya UKIMWI. Si ajabu kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni linasema hivi: “Jitihada zinapaswa kuelekezwa kwa wanaume (na vilevile kwa wanawake) ili kuwalinda wanawake.”

[Picha]

PERU Mama aliye na virusi vya UKIMWI akiwa na binti yake ambaye hana virusi hivyo

[Hisani]

© Annie Bungeroth/Panos Pictures

[Picha]

THAILAND Wanafunzi wanamtembelea mgonjwa wa UKIMWI ili kujifunza kuhusu ugonjwa huo

[Hisani]

© Ian Teh/Panos Pictures

[Picha]

KENYA Mkutano pamoja na wanachama wa shirika la Wanawake Walio na UKIMWI

[Hisani]

© Sven Torfinn/Panos Pictures

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

Uwongo Kuhusu UKIMWI

Watu walio na virusi vya UKIMWI huonekana wagonjwa. Dakt. Gerald J. Stine anasema hivi: “Kwa wastani, inachukua miaka 10 hadi 12 hivi kabla ya mtu aliye na virusi vya UKIMWI kuanza kuugua UKIMWI. Katika kipindi hicho, mtu aliye na virusi hivyo hataonyesha dalili zozote za ugonjwa huo, ingawa anaweza kuwaambukiza watu wengine.”

UKIMWI ni ugonjwa wa wanaume wanaofanya ngono na wanaume. Mapema katika miaka ya 1980, UKIMWI ulionwa kuwa ugonjwa wa wanaume wanaofanya ngono na wanaume. Hata hivyo, leo katika sehemu nyingi ulimwenguni, watu huambukizwa virusi vya UKIMWI hasa wanapofanya ngono na watu wa jinsia tofauti.

Ngono ya kinywa ni “ngono salama.” Kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, “uchunguzi mwingi umeonyesha kwamba mtu anaweza kuambukizwa virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa kupitia ngono ya kinywa.” Kuna hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo kupitia aina nyingine za ngono kuliko ilivyo kupitia ngono ya kinywa. Hata hivyo, zoea la kufanya ngono ya kinywa limeenea sana hivi kwamba madaktari fulani wanasema kwamba itakuwa njia moja kuu ya kueneza virusi vya UKIMWI.

Kuna dawa ya UKIMWI. Ingawa matibabu yanayohusisha dawa za kudhibiti virusi yanaweza kuzuia virusi vya UKIMWI visienee haraka katika miili ya wagonjwa fulani na kusababisha UKIMWI, bado hakuna chanjo wala dawa ya ugonjwa huo.

[Picha]

CHEKI Kupima damu ili kugundua UKIMWI, unaoweza kutibiwa lakini hauwezi kuponywa

[Hisani]

© Liba Taylor/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 6]

ZAMBIA Wasichana wawili walio na virusi vya UKIMWI wanasubiri kupewa dawa

[Hisani]

© Pep Bonet/Panos Pictures