Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Maridadi na Matamu!

Ni Maridadi na Matamu!

Ni Maridadi na Matamu!

UKITEMBELEA bustani ya maua utafurahi sana. Utafurahia kuona rangi, maumbo, na miundo tata ya maua. Utanusia manukato yake. Unaweza kugusa petali zake. Lakini vipi kuyaonja? Je, unaweza pia kufurahia ladha ya maua? Kwa karne kadhaa, watu katika nchi fulani wamefurahia ladha ya maua yanayoliwa. Ikiwa umepanda mojawapo ya maua yafuatayo katika bustani yako huenda ukafurahia kuyaonja. *

Waridi

Huenda ua la waridi (jamii ya Rosa) ndilo linalojulikana na kupendwa sana ulimwenguni pote. Mbali na aina za msingi, kuna maelfu ya aina za waridi ambazo zimezalishwa na wanadamu. Kwa kuwa ladha ya maua hutegemea mambo kama vile udongo na joto, inafaa kuonja petali ya waridi au ya ua lingine lolote kabla ya kulitumia kama chakula. Huenda ukatambua kwamba sehemu ya chini ya petali ina ladha chungu. Ikiwa sehemu hiyo ina ladha chungu, ikate, au ikiwa unataka kuandaa ua lote, kula tu sehemu yake ya nje.

Unaweza kutumia waridi kukoleza vyakula vingi. Kwa mfano unaweza kutumia ua hilo kutayarisha saladi na kuongeza jibini na njugu. Unaweza kutumia petali zilizopondwa-pondwa za ua jekundu la waridi kukoleza na kutia rangi rojo unayopenda sana. Pia unaweza kupamba spageti kwa petali za waridi zilizokatwa-katwa. Vilevile unaweza kutumia waridi kukoleza aiskrimu na kinywaji unachopenda sana.

Mung’unye

Kuna maandishi ya karne ya 16 yanayoonyesha kwamba ua la mung’unye (Cucurbita pepo) lililiwa katika mabara ya Amerika, na inaonekana kwamba wenyeji wa asili wa Amerika walikula tu maua ya kiume (yale yaliyokuwa na mashina marefu na membamba) ili kuyaacha maua ya kike (yale yenye tunda dogo sana) yazalishe. Kabla ya kuyapika maua hayo, ondoa majani ya nje yenye miiba. Unaweza kutoa au kuacha sehemu ya kike inayotoa mbegu. Unaweza kufurahia utamu wa maua ya mung’unye ukitayarisha milo na mchuzi kwa mafuta ya mzeituni, mahindi mabichi, na tunda la mung’unye. Ili ladha hiyo ikolee zaidi, kaanga maua ya mung’unye kwa kitunguu, kitunguu-saumu, na viungo vingine unavyopenda. Au unaweza pia kutia mchanganyiko wa jibini, vitunguu, na viungo ndani ya maua hayo. Ukiisha kufanya hivyo, funga miisho yake na uyachovye ndani ya sehemu nyeupe za mayai yaliyopigwa-pigwa na kuchanganywa na viini vya mayai. Mwishowe, nyunyiza chengachenga za mkate juu ya maua hayo halafu uyakaange, nawe utafurahia utamu wake wa pekee!

Ua Maridadi la Garden Pansy

Maua ya garden pansy (Viola wittrockiana) yenye rangi mbili au tatu huwa na madoa meusi kwenye petali ambayo huyafanya yawe na sura ya pekee. Kulingana na kitabu Encyclopædia Britannica, inadhaniwa kuwa hilo ni aina ya ua la mwituni ambalo hukuzwa linaloitwa Johnny-jump-up (Viola tricolor) lililo na rangi ya zambarau, nyeupe, na manjano. Ijapokuwa ua hilo la mwituni linaweza kuliwa, kitabu Edible Flowers—From Garden to Palate kinasema kwamba “huenda likamdhuru mtu likiliwa sana.” Ua hilo hupamba na kuboresha ladha ya saladi za mboga na za matunda. Tumia ua lote kupamba saladi kabla tu ya kuiandaa, baada ya kutia kiungo chenye siki. Pia unaweza kula ua hilo pamoja na mchuzi unaoupenda sana.

Aina ya tatu ya ua la jamii ya Viola huitwa garden violet au English violet (Viola odorata), nalo ni tamu sana linapoliwa na vitinda-mlo na vinywaji. (Ona sanduku “Maua Matamu ya Kukoleza Vinywaji.”) Maua mengine ya jamii ya Viola hayaliwi.

Ua la Daylily Lenye Kupendeza

Mmea wa daylily (wa jamii ya Hemerocallis) huwa na majani mengi yaliyo marefu na membamba, kwenye sehemu yake ya chini. Maua yake yanayonyauka upesi ni tofauti na maua mengine ya kikundi chake cha Liliaceae. Maua hayo yenye rangi ya manjano na nyekundu, yametumiwa kwa muda mrefu kutayarisha chakula. Maua hayo yanaweza kuliwa baada ya kupikwa kwa muda mfupi. Pia unaweza kuchanganya petali zake na viungo vingine unavyovipenda ili kutayarisha rojo halafu uikaange. Kisha ipambe kwa ua lote.

Maua Mengine Yanayoliwa

Ua la yucca (jamii ya Yucca) ambalo hukua hasa katika maeneo makavu sana, lina vitamini na kalisi nyingi. Kula petali tu. Huenda ukahitaji kuzichemsha kwa muda mfupi ili uondoe ladha yake chungu. Maua ya mlimau (Citrus limon), ya mchungwa (Citrus sinensis), na maua ya mnanaa (jamii ya Mentha) ni vikolezo vizuri vya vinywaji, saladi, na vitinda-mlo. *

Bila shaka maua ni zawadi inayopendeza hisi zetu na hufanya maisha yafurahishe. Kwa kweli hizo pia ni sababu nzuri za kumshukuru Muumba wetu mwenye upendo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Majina ya kisayansi yameonyeshwa ili kuyatambulisha maua kihususa.

^ fu. 14 Kuna maua mengine pia yanayoweza kuliwa, lakini yachunguze kwa makini kabla ya kuyala.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

MAUA MATAMU YA KUKOLEZA VINYWAJI

Tia petali au ua dogo katika kila sehemu ya kifaa cha kutengeneza vidonge vya barafu kabla ya kukijaza maji safi. Kisha kitie ndani ya friji. Baada ya kutengeneza vidonge vya barafu, vitie katika kinywaji ukipendacho.

[Hisani]

Kwa mujibu wa kitabu El Cultivo de Hierbas.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

KUTIA MAUA SUKARI

Pigapiga sehemu nyeupe ya yai, kisha uipake kwenye ua kavu kwa kutumia brashi laini. Hakikisha kwamba umepaka sehemu zote za petali. Tumia kichungi kunyunyiza sukari laini juu ya petali. Tikisa ua ili kuondoa sukari ya ziada kisha ulianike kwa saa kadhaa.

[Hisani]

Kwa mujibu wa kitabu Cook’s Thesaurus.

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

TAHADHARI MUHIMU

Maua fulani yana sumu. Hakikisha unachagua yale tu yanayoweza kuliwa. Usile ua lolote ukiwa na shaka.

Usile ua lolote ambalo limenyunyiziwa dawa za kuua wadudu au kemikali nyingine. (Kwa kawaida hilo latia ndani maua yanayonunuliwa madukani na kwenye bustani fulani za miche.) Kula tu maua yasiyokuzwa kwa kutumia kemikali na yaliyo mbali na barabara.

Watu walio na ugonjwa wa pumu au wanaoathiriwa na mimea hawapaswi kula maua.

Sawa na matunda na mboga, maua yanapaswa kusafishwa vizuri hasa ikiwa yataliwa bila kupikwa.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Waridi

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ua la mung’unye

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ua la “pansy”

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ua la “daylily”

[Picha katika ukurasa wa 24]

Maua ya mlimau