Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Maisha Yalivyokuwa Katika Vinu vya Czechia

Jinsi Maisha Yalivyokuwa Katika Vinu vya Czechia

Jinsi Maisha Yalivyokuwa Katika Vinu vya Czechia

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI

SAUTI ya magurudumu ya vinu yaliyo na meno ilisikika katika eneo lote la Czechia miaka mia moja iliyopita. Sauti hiyo haikuvuruga utulivu, bali ilifanya eneo la mashambani la Cheki livutie. Vinu hivyo vilikuwa muhimu sana katika jamii.

Nyakati hizo, ilikuwa kawaida kwa mke wa mwendeshaji wa kinu kuoka mkate wenye harufu nzuri baada tu ya unga kusagwa. Hebu wazia jinsi mambo yalivyokuwa wakati mke wa mwendeshaji wa kinu alipoandaa mkate uliotoka kuokwa juu ya meza kubwa. Mkate huo ulinukia vizuri sana! Kisha mwendeshaji wa kinu aliingia. Alipendeza, kwani mwili wake mzima ulikuwa umefunikwa kwa unga mweupe! Kisha aliwaita watu wote wa nyumba yake ili wajiburudishe.

Historia ya Vinu

Kazi ya kusaga nafaka ilianza tangu mwanadamu alipoanza kukuza mimea. Katika taifa la kale la Israeli watu walisaga nafaka nyumbani. Mara nyingi wanawake walisaga nafaka wakitumia vinu vya mkono, nao walifanya hivyo wakiwa wawili-wawili. Pia Biblia hueleza kuhusu mawe makubwa ya kusagia yaliyozungushwa na wanyama.—Marko 9:42.

Unaposikia kuhusu vinu huenda ukawazia vinu vya upepo. Hata hivyo, vinu vilivyotumiwa katika maeneo ya mashambani ya Cheki viliendeshwa hasa kwa maji. Kwa nini? Inaonekana kwamba Wacheki waliona maji yanayotiririka kuwa chanzo kinachotegemeka zaidi na kisichogharimu sana cha nishati ya kuendesha kinu.

Sawa tu na ilivyokuwa katika maeneo mengine ya Ulaya ya Kati, vidimbwi vikubwa, mifereji, na milango ya kudhibiti maji yanayoingia kwenye vinu, ilijengwa huko Czechia. Vidimbwi hivyo vilitumiwa kuhifadhi maji, mifereji ikatumiwa kupeleka maji kwenye vinu, nayo milango ilidhibiti kiasi cha maji yanayoingia. Mifereji fulani ilikuwa na urefu usiozidi meta 20, hali mingine ilikuwa na urefu wa zaidi ya kilometa moja nayo ilipeleka maji yaliyotumiwa kuendesha vinu kadhaa.

Mwendeshaji wa Kinu na Wasaidizi Wake

Miaka mia moja iliyopita huko Czechia, mwendeshaji wa kinu pamoja na watu wote wa nyumba yake waliishi ndani ya kinu. Makao ya mwendeshaji wa kinu na sehemu ya kusagia nafaka zilifunikwa kwa paa ileile moja na kuzingirwa kwa kuta zilezile za mawe. Wakaaji wa eneo hilo walimwita mwendeshaji wa kinu, “Baba Mkubwa.” Ilikuwa rahisi kumtambua kwani kwa kawaida alivalia suruali ndefu nyeupe iliyokunjwa miguuni, kofia iliyopambwa kwa ngozi ya kondoo, na sapatu.

Ilikuwa lazima mwendeshaji wa kinu awe mwenye nguvu kwa kuwa maishani mwake angebeba magunia mengi ya unga. Kazi ya uendeshaji wa kinu iliheshimiwa sana na kwa kawaida mtu alijifunza kazi hiyo kutoka kwa baba yake. Mwana alifundishwa kazi hiyo na baba yake akiwa nyumbani, hata hivyo angeweza pia kufanya kazi na waendeshaji wengine stadi ili aongeze ujuzi wake.

Familia nzima ilikuwa na shughuli nyingi kwa sababu kulikuwa na kazi nyingi katika kinu. Kwa kawaida ilikuwa vigumu kwa washiriki wa familia kufanya kazi zote, hivyo mwendeshaji wa kinu aliwaajiri wafanyakazi wa kudumu au vibarua. Vibarua hao walikuwa waendeshaji wa vinu wenye uzoefu, na kulipokuwa na kazi nyingi waliajiriwa katika vinu mbalimbali. Walilipwa kwa kupewa chakula na makao.

Kwa kawaida, kinu kilisimamiwa na mfanyakazi stadi aliyeheshimiwa sana ambaye aliitwa mwendeshaji mkuu. Alisaidiwa kuendesha kinu na kijana fulani aliyejua vizuri kazi hiyo. Ujuzi na uwezo wa kijana huyo ulipimwa kwa kutegemea ubora wa unga uliotokezwa. Pia kulikuwa na mvulana mwenye akili aliyewatazama kwa makini waendeshaji wa kinu wenye uzoefu ili ajifunze kazi. Mwanafunzi huyo hakupaswa kukengeushwa na kitu chochote.

Mawe ya Kusagia Nafaka

Kitabu cha Biblia cha Ayubu kinataja “jiwe la chini la kusagia.” (Ayubu 41:24) Maneno hayo yaliyoandikwa zamani yanaonyesha jinsi mawe ya kusagia nafaka yalivyotumiwa. Mawe mawili yalihitajiwa, yaani, jiwe la juu na la chini. Jiwe la chini halikusonga, lakini lile la juu lilizungushwa ili kusaga nafaka zilizowekwa katikati ya mawe hayo.

Hapo awali mawe ya kusagia nafaka yalitengenezwa kwa mawe magumu. Baadaye, yalianza kutengenezwa kwa mawe yaliyopondwa-pondwa na kuunganishwa kwa kloridi ya magnesi. Mtaalamu alitengeneza magurudumu yenye meno kwa kutumia mbao ngumu sana. Kazi hiyo ilikuwa ngumu sana kwa kuwa, mbali na kutengeneza maumbo tata, mtaalamu huyo alihitaji kuhakikisha kwamba gia zinaingiana vizuri. Mpangilio wa magurudumu yenye meno uliwezesha sehemu nyingine za kinu zizunguke kasi zaidi. Watu walitambua vinu kwa mlio wa magurudumu hayo yenye meno.

Hadithi za Kicheki Kuhusu Waendeshaji wa Vinu

Ingawa waendeshaji fulani wa vinu walikuwa watu wanyoofu na waaminifu, waendeshaji wengine walikuwa wenye pupa, wadhalimu, na waliwapunja wateja wao. Hivyo, katika nyimbo fulani za kitamaduni, waendeshaji wa vinu na familia zao walidhihakiwa, huku katika nyimbo nyingine wakisifiwa. Nyimbo nyingine ziliwasifu wasaidizi wao kwa kusema kwamba wangekuwa waume wazuri! Nyingine zilihusu mafuriko ambayo yalikuwa tisho kwa mwendeshaji wa kinu na kinu chake. Moto pia ulikuwa tisho kubwa.

Hadithi hizo zilitofautiana kidogo kwa kuwa zilitungwa katika maeneo mbalimbali na wakati tofauti-tofauti. Hata hivyo, hadithi hizo zilizosimuliwa katika eneo lote la Czechia zilihusu habari ileile. Vibarua waliohama-hama ndio waliosimulia hadithi hizo na kuzitilia chumvi. Kwa hiyo, leo kuna msemo wa Kicheki unaosema: “Hadithi husimuliwa huku maji yakitiririka,” ili kuonyesha kwamba huenda hadithi au ripoti fulani imetiliwa chumvi.

Vinu vya Kisasa

Baada ya muda, uendeshaji wa vinu ulionwa kuwa jambo lililopitwa na wakati. Vinu viliboreshwa, na badala ya maji, mota za umeme zilitumiwa kuendesha vinu. Waendeshaji fulani wa vinu walijitahidi juu chini kuendelea na kazi yao, na hivyo vinu fulani vinavyoendeshwa kwa maji viliendelea kutumiwa huko Czechia hadi baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu. Lakini mwaka wa 1948 ulipofika, vinu hivyo viliacha kutumiwa kabisa. Kuanzia mwaka huo, serikali ilimiliki vinu hivyo, na kwa kuwa vinu vingi viliacha kutumiwa, vilianza kuharibika.

Vinu vinavyotumiwa leo havipendezi kama vile vya zamani. Mashine za kisasa hutumiwa kusaga nafaka, na kwa kawaida huendeshwa kwa kompyuta. Silinda za chuma hutumiwa badala ya mawe ya kusagia. Hata hivyo, vinu vya kale vilivyochakaa huendelea kuwavutia wale wanaopenda mazingira matulivu na yenye kusisimua, na vilevile huwavutia watalii wanaotaka kujifunza kuhusu utamaduni na historia.

Leo, maeneo fulani yenye vinu vinavyovutia yametengwa kwa ajili ya tafrija. Wageni wengi huko Prague hutembelea gurudumu la kinu lililoko kwenye kijito cha Mto Vltava kinachoitwa C̆ertovka. Kinu kilichokuwa huko kiliacha kutumiwa mwaka wa 1938 baada ya kuteketea. Hata hivyo, gurudumu lake la maji lenye urefu wa meta 7 hivi, lililojengwa zaidi ya miaka 600 mapema, lilijengwa upya katika mwaka wa 1995 ili kuwakumbusha watu kuhusu utamaduni wa kale. Gurudumu hilo lingali linafanya kazi.

Leo tukiwa tumesimama ndani ya kinu kilichorekebishwa, tunawazia jinsi mwendeshaji wa kinu alivyofanya kazi yake karne moja iliyopita. Tunasikia maji yakipigapiga, huku gurudumu likizunguka. Tunapoondoka, tunasikia sauti ya kinu kwa mbali. Lakini tutaikumbuka daima sauti inayopendeza ya magurudumu yenye meno.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Jiwe la kusagia nafaka

[Picha katika ukurasa wa 22, 23]

1. Kifaa cha kale cha kusafisha nafaka kwa kutumia mkono

2. Kinu

3. Mtaimbo mkuu hupeleka nishati kwenye vinu kutoka kwenye gurudumu linalozungushwa kwa maji

4. Gurudumu hili linalozungushwa kwa maji lina urefu wa meta saba hivi, nalo liliendesha kinu huko C̆ertovka

[Picha katika ukurasa wa 24]

Gurudumu la kinu huko C̆ertovka