Kiwanda cha Kifo
Kiwanda cha Kifo
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UJERUMANI
INASEMEKANA kwamba kiwanda cha Mittelwerk ndicho kilichokuwa kiwanda kikubwa zaidi kuwahi kujengwa chini ya ardhi. Kiwanda hicho kilikuwa katika eneo la njia za chini ya ardhi zenye urefu wa kilometa 20 zilizochimbwa chini ya kilima kimoja katika Milima ya Harz, kilometa 260 kusini-magharibi mwa Berlin, nchini Ujerumani. Kuanzia mwaka wa 1943 hadi 1945, wafungwa wengi katika kambi za mateso walifanya kazi katika kiwanda hicho wakiwa watumwa. Walilazimishwa kutengeneza silaha zilizotumiwa na Serikali ya Nazi, huku wakifanya kazi chini ya hali mbaya sana.
Wafungwa hao hawakutengeneza silaha za kawaida tu. Kiwanda hicho kilitengeneza roketi za V-1 na V-2. Roketi hizo zilisafirishwa kutoka Mittelwerk hadi kwenye maeneo ya kurushia roketi ambayo hasa yalikuwa katika Ufaransa na Uholanzi. Roketi hizo ziliporushwa, zilijiongoza zenyewe na hatimaye kuanguka huko Ubelgiji, Uingereza, au Ufaransa. Wanazi walikusudia kutengeneza roketi yenye nguvu sana kiasi cha kuruka juu ya Bahari ya Atlantiki na kuangusha bomu huko New York. Kufikia mwishoni mwa Vita vya Pili vya Ulimwengu, mamia ya roketi za V-1 na V-2 zilikuwa zimeangushwa katika majiji mengi ya Ulaya. Hata hivyo, hiyo ni idadi ndogo sana inapolinganishwa na idadi ya roketi ambazo Wanazi walitengeneza ili kuzitumia kushambulia maadui zao. Hawakuangusha hata roketi moja ya aina hiyo huko New York.
Jambo Lenye Kuhuzunisha
Baada ya vita kumalizika, wanasayansi na wataalamu wengi wa Ujerumani, ambao walikuwa wamebuni roketi hizo za V-1 na V-2, waliondoka Ujerumani. Baadaye walianza kutumia ujuzi wao katika nchi walikohamia. Mmoja wa wataalamu hao ni Wernher von Braun. Alihamia Marekani na kushiriki kutengeneza roketi ya Saturn iliyotumiwa kusafiri kwenda mwezini.
Leo, kando tu ya kiwanda cha Mittelwerk, kuna mnara wa ukumbusho kwa ajili ya watu 60,000 waliofungwa katika kambi hiyo ya mateso. Mbali na kufanya kazi katika kiwanda hicho chenye baridi na unyevunyevu, wafungwa wengi waliishi humo. Basi haishangazi kwamba kulingana na makadirio fulani, karibu wafungwa 20,000 walifia humo. Watalii wanaweza kutembezwa katika njia hizo na kuona vipande vya roketi vilivyoachwa sakafuni yapata miaka 60 iliyopita. Gazeti After the Battle linasema jambo hili la kuhuzunisha kuhusu roketi za Mittelwerk: “Watu waliokufa wakitengeneza roketi za V1 na V2 ni wengi sana kuliko wale waliouawa zilipotumiwa vitani.”
[Picha katika ukurasa wa 21]
Picha ya 1945 inayoonyesha roketi za V-1 zikiwa kwenye magari ya kukokotwa
[Hisani]
Quelle: Dokumentationsstelle Mittelbau-Dora
[Picha katika ukurasa wa 21]
Watalii wakitembea kwenye njia hizo, huku vipande vya roketi vikiwa vimetapakaa sakafuni