Kuhangaikia Urembo Kupita Kiasi
Kuhangaikia Urembo Kupita Kiasi
MARIA * ni msichana ambaye amefanikiwa maishani na ametoka katika familia nzuri. Lakini hana furaha. Kwa nini? Hapendi sura yake. Ingawa washiriki wa familia yao humtia moyo, Maria hufikiri kwamba yeye si mrembo, na hilo humvunja moyo sana.
José ametoka katika familia yenye kuheshimika, hivyo anapaswa kuwa mwenye furaha. Hata hivyo, anafikiri hatapata mwenzi. Kwa nini? José anafikiri ana sura mbaya. Anaamini hawezi kumvutia mwanamke mzuri.
Luis ni mtoto mwenye urafiki aliye na umri wa miaka minane, naye hupenda kwenda shule. Ijapokuwa Luis hufurahia kucheza na wanafunzi wenzake, yeye hulia mara nyingi kwa sababu wao hufanya mzaha kuhusu sura yake. Wao husema yeye ni mnene.
Kuna visa vingi kama hivyo. Tatizo la Maria, José, na Luis halisababishwi na kutojiheshimu. Kusema kweli, hakuna anayefurahia kukataliwa na wengine kwa sababu ya sura yake.
Hata hivyo, katika jamii sura huonwa kuwa muhimu kupita kiasi. Mara nyingi, ni kana kwamba mafanikio hutegemea sura ya mtu. Kwa mfano, watu wenye sura nzuri zaidi hufanikiwa kupata kazi haraka zaidi. Pilar Muriedas, ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa Mashirika ya Afya ya Wanawake ya Amerika ya Latini na Karibea, anasema kwamba kwa wanawake “urembo ni mojawapo ya matakwa muhimu ya mafanikio.” Kulingana na Dakt. Laura Martínez, wanawake wanafahamu kwamba “kupata au kukosa kazi hutegemea sana sura yao.”
Hata wanaume wengi hujishughulisha kupita kiasi kupata umbo zuri. Ama kweli, wanaume na wanawake wengi hujitahidi juu chini kuwa na sura ya kuvutia. Hata wengine hukubali kupata matibabu yanayoumiza na kukataa kula ili wawe na sura nzuri au umbo zuri. Je, kuna faida zozote za kufanya hivyo? Je, kuna hatari zozote?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Majina yamebadilishwa.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Sura ya mtu inaweza kuathiri uwezekano wake wa kupata kazi