Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembelea Bonde la Ngorongoro

Kutembelea Bonde la Ngorongoro

Kutembelea Bonde la Ngorongoro

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Tanzania

“IKIWA malaika wangepiga picha za wanyama katika Bustani ya Edeni, picha hizo hazingetofautiana sana na zile ambazo mtu anaweza kupiga leo akitembelea Bonde la Ngorongoro.” Hivyo ndivyo alivyoandika Reinhard Künkel katika kitabu chake kinachozungumzia eneo hilo lenye kuvutia la Tanzania. Bonde la Ngorongoro ni maridadi sana, na lina maelfu ya wanyama wa pori. Jiunge nasi na ufurahie mandhari!

Mandhari Inayopendeza

Baada ya kusafiri kwa gari kwa saa nne katika barabara yenye vumbi, hatimaye tunafika karibu na Bonde la Ngorongoro. Tunatazama eneo hilo lenye kupendeza tukiwa hotelini. Mandhari hiyo inavutia wee! Wataalamu wa mambo ya asili wamepaita mahali hapo “ajabu ya nane ya ulimwengu,” nasi tunaelewa kilichowafanya waseme hivyo.

Jina Ngorongoro lilitoka wapi? Hakuna ajuaye. Kulingana na Shirika la Uhifadhi la Afrika Mashariki, watu fulani husema kwamba hilo ni jina la Mmaasai mmoja aliyeishi katika bonde hilo, ambaye alikuwa akitengeneza kengele za ng’ombe. Wengine husema kwamba jina hilo ni la kikundi cha mashujaa wa Datogo ambao walishindwa na Wamaasai katika vita vilivyopiganwa katika bonde hilo miaka 150 iliyopita. Lakini tunapowaona pundamilia wakilisha karibu na eneo la kuegesha magari, hatuhangaishwi tena na jina hilo. Tunapopanda gari letu, tunapita karibu sana nao lakini ni kana kwamba hawatuoni. Tunateremka bonde hilo kutazama wanyama wengine.

Bonde la Ngorongoro liko meta 2,236 juu ya usawa wa bahari, nalo ndilo bonde kubwa la volkeno ulimwenguni ambalo sehemu zake za kandokando hazijaporomoka. Lina urefu wa kilometa 19.2 kutoka upande mmoja hadi mwingine, na ukubwa wa kilometa 304 za mraba. Tunashuka kwenye bonde hilo lenye kina cha meta 610 huku tukitazama nje ya madirisha ya gari letu ili kupiga picha. Tulipokuwa juu ya bonde hilo asubuhi kulikuwa na baridi. Hata hivyo kuna joto jingi ndani ya bonde hilo.

Dereva wetu anapotutembeza polepole ndani ya bonde hilo, tunapita karibu na ziwa dogo lenye maji ya chumvi lililo na flamingo wengi wa waridi. Huku kukiwa na anga la bluu, sehemu ya juu ya bonde hilo inaonekana wazi, nasi tunasisimuka sana kusikia sauti za pundamilia na nyumbu na sauti nyingine tusizoweza kutambua. Bila shaka, hii ni paradiso!

Wanyama wa Pori Wanaoishi Humo

Kama tulivyotarajia, tunawaona nyati, tembo, pundamilia, nyumbu, swara, vifaru, na tumbili katika Bonde la Ngorongoro. Tunawaona pia wanyama-wawindaji kama vile duma, fisi, mbweha, na simba wenye manyoya meusi wakitembea-tembea. Tunawaona viboko wakijiburudisha katika kidimbwi. Ni watulivu hata tunapowapiga picha.

Kwa ghafula, dereva wetu anasimamisha gari! Anatuonyesha kifaru mmoja anayepita hatua chache mbele yetu. Kifaru huyo hana wasiwasi, na ni jambo la pekee kumtazama kwa ukaribu katika mazingira yake ya asili. Vifaru wa aina hiyo wanaelekea kutoweka kwani inakadiriwa kwamba katika bonde hilo kuna vifaru wasiozidi 20. Wawindaji haramu wameshikwa katika eneo hili wakiua vifaru kwa sababu ya pembe zao ambazo huuzwa kimagendo ili kutengeneza dawa na mipini ya visu. Askari wa mbuga hushika doria katika bonde hilo ili kuwazuia wawindaji haramu.

Mtu anayependa ndege anaweza kufurahia kuona ndege wengi maridadi kama vile mbuni, tandawala, korongo wenye kibwenzi, nyangenyange, kulastara, karani, shashi domojekundu, na flamingo. Vilevile zaidi ya jamii mia moja za ndege ambao hawapatikani katika Mbuga ya Wanyama ya Serengeti iliyo karibu, wanapatikana katika bonde hilo. Ndege hao wanatia ndani vigogota, kolokolo na aina fulani ya chechele. Pia ndege wanaoitwa longclaw na vilevile ndege wanaoitwa Cape rook ambao hawapatikani kwa urahisi wameonekana huko.

Ingawa wanyama wengi hawatusumbui, ni lazima tukae ndani ya gari letu. Hata hivyo, Wamaasai, ambao huishi karibu na Bonde la Ngorongoro katika nyumba za udongo zilizo na paa la nyasi, hutembea humo wakiwa na mifugo yao. Ni kana kwamba wanyama wa pori wamewazoea.

Mandhari inayopendeza na utulivu wa Bonde la Ngorongoro hustaajabisha sana. Hatuwezi kamwe kusahau safari hiyo.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kifaru

[Picha katika ukurasa wa 15]

Wachungaji Wamaasai wakiwa kando ya bonde hilo

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mwanamke Mmaasai

[Picha katika ukurasa wa 16]

Duma

[Picha katika ukurasa wa 16]

Korongo mwenye kibwenzi

[Picha katika ukurasa wa 16]

Flamingo

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kiboko

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Bonde la Ngorongoro

[Picha katika ukurasa wa 17]

Pundamilia

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nyati

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tembo

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tumbili