Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maktaba ya Aleksandria Yajengwa Upya

Maktaba ya Aleksandria Yajengwa Upya

Maktaba ya Aleksandria Yajengwa Upya

ILIKUWA mojawapo ya maktaba maarufu zaidi wakati huo. Ilifanya jiji la Aleksandria huko Misri liwe kituo muhimu cha wasomi maarufu. Kutoweka kwa njia isiyojulikana kwa maktaba hiyo pamoja na maandishi yake muhimu kuliathiri sana elimu na maendeleo. Sasa, maktaba hiyo kubwa imejengwa upya.

Jengo jipya la maktaba maarufu ya Aleksandria halina kifani. Jumba kuu la Bibliotheca Alexandrina, kama vile maktaba hiyo mpya inavyoitwa, linafanana na ngoma kubwa iliyoegemea upande. Paa yake iliyotengenezwa kwa glasi na alumini (1)—ambayo ina ukubwa unaokaribia kulingana na ule wa viwanja viwili vya mpira—ina madirisha yaliyoelekea kaskazini ambayo hupenyeza nuru kwenye jumba kuu la kusomea (2). Jengo hilo lina sehemu kuu zilizotengwa kwa ajili ya umma na sehemu fulani yake iko chini ya usawa wa bahari. Paa yake inayometameta yenye umbo la duara, imeegemea upande na inatoka ardhini hadi kwenye orofa ya saba. Kutoka mbali, paa hiyo inapopigwa na mwangaza wa jua hufanana na jua linalochomoza.

Ukuta wa nje wa jengo hilo umejengwa kwa mawe ya matale na una michongo ya herufi za lugha za kale na za kisasa (3). Herufi hizo zilizopangwa kama ngazi huwakilisha mambo muhimu yaliyochangia ukuzi wa ujuzi.

Jumba la kusomea lenye sehemu kadhaa zilizojengwa kama ngazi linafanyiza sehemu kubwa ya jengo hilo (4). Chini ya jengo hilo kuna sehemu inayoweza kutoshea vitabu 8,000,000. Pia jengo hilo lina sehemu za maonyesho, majumba ya hadhara, vifaa maalumu kwa ajili ya wale wasioweza kuona (5), na kitufe kinachofanana na setilaiti iliyo angani (6). Vilevile kuna mifumo tata ya kompyuta na mifumo ya kuzima moto katika jengo hilo la kisasa la hali ya juu.

Jinsi Maktaba Hiyo Maarufu Ilivyositawi

Hapo kale jiji la Aleksandria lilijulikana sana kwa sababu ya vitu mbalimbali vilivyokuwa maarufu lakini ambavyo kwa sasa vimetoweka kama vile mnara wa taa wa Pharos—ambao inasemekana ulikuwa na urefu wa meta 110 na ulikuwa mojawapo ya maajabu saba ya ulimwengu wa kale—na kaburi la Aleksanda Mkuu. Ukoo wa wafalme wa Ugiriki walioitwa Ptolemy ulirithi Misri kutoka kwa Aleksanda na kutawala nchi hiyo hadi wakati Octavian alipowashinda Antony na Cleopatra mwaka wa 30 K.W.K. Jiji la Aleksandria lilibadilika sana wakati wa utawala wa ukoo wa Ptolemy. Kulingana na kitabu Atlas of the Greek World, kwa wakati fulani jiji hilo “likawa kituo muhimu cha kibiashara na utamaduni ulimwenguni.” Jiji la Aleksandria lilipokuwa limesitawi sana lilikuwa na wakaaji wapatao 600,000.

Jambo lenye kuvutia zaidi katika jiji hilo lilikuwa maktaba ya kifalme. Maktaba hiyo, iliyoanzishwa mapema katika karne ya tatu K.W.K. na kuendelezwa na ukoo wa Ptolemy, pamoja na Mouseion (Hekalu la Muses) vilikuwa vituo vya mafunzo na uvumbuzi katika enzi ya Wagiriki.

Inasemekana kwamba maktaba hiyo ilikuwa na hati za kukunja 700,000 zilizotengenezwa kwa mafunjo. Katika karne ya 14, maktaba ya Sorbonne, ambayo ilijulikana kwa kuwa na vitabu vingi zaidi katika kipindi hicho, ilikuwa na vitabu 1,700 tu. Kwa kuwa watawala wa Misri walikuwa wameazimia kuongeza vitabu katika maktaba hiyo, waliwaagiza askari-jeshi watafute vitabu katika meli zote zilizowasili. Ikiwa wangepata vitabu vyovyote, walivihifadhi na kurudisha nakala zake. Inasemekana kwamba wakati Ptolemy wa Tatu alipoazima hati za michezo ya kuigiza ya Wagiriki kutoka katika jiji la Athene, aliweka amana ili aruhusiwe kuzichukua na kuzinakili. Lakini mfalme huyo hakurudisha hati hizo wala kudai amana, badala yake alituma nakala za pili za hati hizo.

Watu wengi wa kale wenye akili walitumia maktaba na jumba la makumbusho la Aleksandria. Wasomi wa huko Aleksandria walileta maendeleo makubwa katika jiometria, trigonometria, na elimu ya nyota, na vilevile katika lugha, fasihi, na tiba. Inasemekana kwamba wasomi 72 Wayahudi walitafsiri Maandiko ya Kiebrania katika lugha ya Kigiriki wakiwa huko, na hivyo kutokeza tafsiri maarufu ya Septuajinti.

Maktaba Yatoweka

Inashangaza kwamba waandishi wa matukio hawakuona uhitaji wa kueleza mengi kuhusu taasisi za Aleksandria. Watu wengi walikuwa na maoni kama haya ya mwanahistoria wa karne ya tatu Athenaeus: “Kwa nini nieleze kuhusu idadi ya vitabu, ujenzi wa maktaba, na vitu vilivyokusanywa katika Jumba la Muses ikiwa watu wote wanajua mambo hayo?” Maelezo kama hayo huwatatanisha wasomi ambao hutaka sana kujifunza kuhusu maktaba hiyo ya kale.

Huenda maktaba ya Aleksandria ilikuwa imetoweka kufikia wakati Waarabu waliposhinda Misri katika mwaka wa 640 W.K. Wasomi hawakubaliani kuhusu wakati na jinsi maktaba hiyo ilivyotoweka. Baadhi yao wanasema kwamba huenda vitu vingi vilivyokuwa katika maktaba hiyo viliharibiwa wakati Julius Caesar alipoteketeza sehemu ya jiji la Aleksandria katika mwaka wa 47 K.W.K. Ijapokuwa sababu ya kutoweka kwa maktaba hiyo haijulikani wazi, habari nyingi sana zilipotea. Mamia ya hati za michezo ya kuigiza ya Wagiriki ziliharibiwa kabisa pamoja na rekodi za miaka 500 ya kwanza ya historia ya Ugiriki, bila kutia ndani maandishi fulani ya Herodotus, Thucydides, na Xenophon.

Kati ya karne ya tatu na ya sita W.K., jiji la Aleksandria lilikumbwa na mchafuko mara nyingi. Wapagani, Wayahudi, na watu waliodai kuwa Wakristo walizozana mara nyingi kuhusu mafundisho ya kifumbo. Mara nyingi, viongozi wa kanisa waliwachochea watu waliofanya ghasia kupora mahekalu ya wapagani. Hati nyingi za zamani ziliharibiwa wakati wa michafuko hiyo.

Kurudisha Fahari ya Maktaba Hiyo ya Kale

Maktaba iliyojengwa upya ilifunguliwa mnamo Oktoba 2002, nayo ina vitabu 400,000. Mifumo tata ya kompyuta huwawezesha watu kuchunguza maktaba nyinginezo. Vitabu vingi ni vya utamaduni wa watu wanaoishi mashariki ya Mediterania. Maktaba ya Aleksandria, inayoweza kutoshea vitabu 8,000,000, itaongeza fahari ya jiji la Aleksandria.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

WATU MAARUFU WA ALEKSANDRIA YA KALE

ARCHIMEDES: Mwanahisabati na mvumbuzi wa karne ya tatu K.W.K. Alivumbua mambo mengi na kutumia sayansi kubainisha uwiano kati ya kipenyo na mzingo wa duara (π).

ARISTARCHUS WA SAMOS: Mtaalamu wa nyota wa karne ya tatu K.W.K. Alikuwa mtu wa kwanza kudai kwamba sayari huzunguka jua. Alitumia trigonometria kujaribu kukadiria umbali wa kufika kwenye jua na mwezi na vilevile ukubwa wa jua na mwezi.

CALLIMACHUS: Mshairi na mtunzaji mkuu wa maktaba wa karne ya tatu K.W.K. Alitayarisha fahirisi ya kwanza ya maktaba ya Aleksandria ambayo iliorodhesha vitabu muhimu vya Wagiriki.

CLAUDIUS PTOLEMY: Mtaalamu wa nyota wa karne ya pili W.K. Maandishi yake ya kijiografia na elimu ya nyota yalikubaliwa na watu wengi.

ERATOSTHENES: Msomi na mmoja wa watunzaji wa kwanza wa maktaba huko Aleksandria, wa karne ya tatu K.W.K. Alikadiria mzingo wa dunia kwa usahihi wenye kustaajabisha.

EUCLID: Mwanahisabati wa karne ya nne K.W.K. Ndiye aliyeanzisha jiometria na uchunguzi wa mwangaza. Kitabu chake Elements ndicho hasa kilichotumiwa katika jiometria hadi karne ya 19.

GALEN: Daktari wa karne ya pili W.K. Vitabu vyake 15 kuhusu tiba ndivyo hasa vilivyotumiwa kwa zaidi ya karne 12.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

All photos, both pages: Courtesy of the Bibliotheca Alexandrina: Mohamed Nafea, Photographer