Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mali za Asili za Dunia Zinapungua

Mali za Asili za Dunia Zinapungua

Mali za Asili za Dunia Zinapungua

“Vitu vyote vya asili vinahusiana, na sasa tunalipia makosa tuliyofanya zamani.”—Gazeti la African Wildlife.

KULINGANA na Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni, tangu miaka ya 1980 mali za asili zinazotumiwa na wanadamu zimezidi mali za asili zinazotokezwa na dunia. * Lakini hilo ni jambo moja tu linaloonyesha kwamba mali za asili zinapungua sana.

Upungufu wa mali za asili za dunia unaweza kukadiriwa pia kwa kuchunguza mifumo ya ikolojia. Usemi “mfumo wa ikolojia” unamaanisha uhusiano uliopo kati ya vitu vyote vyenye uhai na visivyo na uhai katika mazingira ya kiasili. Hali ya mifumo hiyo hukadiriwa kulingana na idadi ya jamii za viumbe wanaoishi katika misitu, maziwa, mito, na bahari. Kati ya mwaka wa 1970 na 2000, jamii za viumbe wanaoishi katika mazingira hayo zilipungua kwa asilimia 37 hivi.

Je, Kuna Mali za Asili za Kutosha?

Ikiwa unaishi katika mojawapo ya nchi za Magharibi, ambako bidhaa hupatikana kwa wingi madukani usiku na mchana, huenda ikawa vigumu kwako kuwazia kwamba kuna upungufu mkubwa wa mali za asili. Hata hivyo, ni watu wachache tu ulimwenguni wanaoishi raha mustarehe. Watu wengi hujitahidi juu chini kupata riziki. Kwa mfano, inakadiriwa kwamba zaidi ya watu bilioni mbili hupata riziki ya dola tatu au chini kwa siku na kwamba watu bilioni mbili hawapati umeme.

Watu fulani husema kwamba umaskini wa nchi zinazoendelea husababishwa na shughuli za kibiashara za mataifa tajiri. Kitabu Vital Signs 2003 kinasema hivi: “Mara nyingi, uchumi wa ulimwengu hauzingatii hali ya maskini.” Watu wengi wanapozidi kung’ang’ania mali za asili ambazo zinaendelea kupungua na kuwa ghali zaidi, maskini hushindwa kupata sehemu yao ya mali hizo. Hivyo, matajiri ndio wanaopata sehemu kubwa ya mali za asili.

Misitu Inaangamizwa

Inakadiriwa kwamba asilimia 80 ya wakaaji wa Afrika hupika kwa kuni. Isitoshe, gazeti Getaway la Afrika Kusini linasema kwamba “Afrika ndilo bara lenye ongezeko kubwa la idadi ya watu [na] la watu wanaohamia mijini.” Hivyo, miti mingi imekatwa katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya kilometa 100 ambalo liko kando ya miji mikubwa katika eneo kame la Sahel, kusini mwa Jangwa la Sahara. Miti hiyo haikukatwa bila sababu. Profesa Samuel Nana-Sinkam anasema kwamba ‘raia wengi sana wa Afrika huharibu mazingira yao ili waendelee kuishi.’

Hali ni tofauti sana katika Amerika Kusini. Kwa mfano, huko Brazili, makampuni 7,600 hivi yana kibali cha kukata miti katika msitu wa mvua. Mengi kati ya makampuni hayo yanamilikiwa na mashirika makubwa ya kimataifa. Makampuni ya kukata miti huuza mti wa mkangazi kwa dola 30 hivi. Hata hivyo, mti huo ukiisha kupitia kwa madalali, wauzaji, na watengenezaji, thamani yake inaweza kufikia dola 130,000 au zaidi, hata kabla ya kifaa kilichotengenezwa kwa mti huo kuuzwa. Si ajabu kwamba mkangazi huonwa kuwa dhahabu ya kijani.

Habari nyingi zimeandikwa kuhusu kuangamizwa kwa msitu wa mvua wa Brazili. Picha za setilaiti zinaonyesha kwamba huko Brazili, eneo la misitu lenye ukubwa wa zaidi ya kilometa 20,000 za mraba liliharibiwa kila mwaka tangu 1995 hadi 2000. Gazeti Veja la Brazili linaripoti hivi: “Kiwango hicho kikubwa cha uharibifu kinaonyesha kwamba eneo la msitu linalolingana na uwanja wa mpira liliharibiwa kila sekunde nane.” Inashangaza kwamba katika mwaka wa 2000, Marekani ilinunua zaidi ya asilimia 70 ya mikangazi kutoka Brazili.

Misitu inaangamizwa pia katika maeneo mengine ya dunia. Kwa mfano, nusu ya misitu ya Mexico iliangamizwa katika miaka 50 iliyopita. Misitu ya Ufilipino imeangamizwa hata zaidi. Kila mwaka, nchi hiyo hupoteza eneo la misitu lenye ukubwa wa ekari 250,000 hivi, na katika mwaka wa 1999 ilikadiriwa kwamba uharibifu huo ukiendelea thuluthi mbili hivi za misitu ya nchi hiyo zingeharibiwa katika kipindi cha miaka kumi.

Ijapokuwa inaweza kuchukua miaka 60 hadi 100 kwa mti mgumu kukomaa, inachukua dakika chache tu kuukata. Basi, si ajabu kwamba misitu yetu inaendelea kuangamia.

Ardhi Inaharibiwa

Mimea inapoharibiwa, udongo wa juu hukauka na kupeperushwa na upepo au kufagiliwa na maji. Huo ndio mmomonyoko wa udongo.

Mmomonyoko wa udongo ni jambo la asili na kwa kawaida si tatizo kubwa ila tu wakati mwanadamu anapouzidisha kwa kutumia ardhi vibaya. Kwa mfano, gazeti China Today linasema kwamba majangwa “yameenea sana kwa sababu ya” dhoruba za mchanga na mambo mengine kama vile ukataji wa miti na kulisha mifugo kwenye eneo moja kupita kiasi. Katika miaka ya karibuni, ukame usio wa kawaida umefanya mikoa ya magharibi na kaskazini-magharibi mwa China iathiriwe na pepo baridi za Siberia zinazovuma nchini humo. Mchanga mwingi sana umepeperushwa, hata kufikia Korea na Japani. Sasa asilimia 25 hivi ya ardhi ya China ni jangwa.

Uharibifu wa ardhi ya Afrika umesababishwa pia na hali kama hizo. Gazeti Africa Geographic linasema kuwa “wakulima wameharibu kabisa udongo wa juu kwa kukata miti ili kupanda mimea.” Inakadiriwa kwamba vichaka vinapofyekwa, udongo hupoteza asilimia 50 ya rutuba katika kipindi cha miaka mitatu. Gazeti hilo linaongeza hivi: “Tayari maeneo yenye ukubwa wa mamilioni ya ekari yamepoteza rutuba kabisa na maeneo mengine mengi yanakabili hatari hiyohiyo kwani mazao katika maeneo fulani yanapungua kila mwaka.”

Inasemekana kwamba tani milioni 500 za udongo humomonyoka kila mwaka nchini Brazili. Huko Mexico, Wizara ya Mazingira na Mali za Asili inasema kwamba asilimia 53 ya vichaka, asilimia 59 ya mapori, na asilimia 72 ya misitu imeathiriwa na mmomonyoko wa udongo. Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo inasema kwamba “mmomonyoko wa udongo huathiri thuluthi mbili hivi za mashamba ulimwenguni. Hivyo, uzalishaji wa mazao unapungua sana huku idadi ya watu ikiongezeka.”

Maji Yana Thamani Kubwa

Mtu anaweza kuishi kwa mwezi mmoja hivi bila kula, lakini asipokunywa maji kwa juma moja hivi atakufa. Hivyo, wataalamu wanasema kwamba upungufu wa maji safi utasababisha mizozo katika miaka ya baadaye. Kulingana na ripoti ya gazeti Time ya mwaka wa 2002, zaidi ya watu bilioni moja ulimwenguni hawawezi kupata maji safi kwa urahisi.

Mambo mbalimbali husababisha uhaba wa maji. Huko Ufaransa, uhaba wa maji husababishwa na uchafuzi, na watu wengi wanahangaikia jambo hilo. Gazeti Le Figaro linasema hivi: “Mito ya Ufaransa imechafuliwa sana.” Wanasayansi wanasema kwamba uchafuzi huo unasababishwa na maji ya mvua yenye nitrati, ambayo hasa hutokana na mbolea inayotumiwa katika kilimo. Gazeti hilo linasema kwamba “katika mwaka wa 1999, tani 375,000 za nitrati ziliingia katika Bahari ya Atlantiki kutoka kwenye mito ya Ufaransa, na kiasi hicho kilikuwa maradufu ya kile cha mwaka wa 1985.”

Tatizo hilo linakumba Japani pia. Yutaka Une, msimamizi wa shirika moja la kuzuia uharibifu wa mashamba, anasema kwamba “wakulima walilazimika kutumia mbolea za kemikali na dawa za kuua wadudu” ili kuzalisha chakula cha kutosha nchini humo. Hilo limechafua maji yaliyo chini ya ardhi, na kulingana na gazeti IHT Asahi Shimbun hilo ni “tatizo kubwa nchini Japani.”

Gazeti Reforma linaripoti kwamba asilimia 35 ya magonjwa nchini Mexico “husababishwa na hali za mazingira.” Isitoshe, uchunguzi mmoja uliofanywa na katibu wa afya ulionyesha kwamba “mtu 1 kati ya kila watu 4 hana mfumo wa kuondoa maji machafu nyumbani; zaidi ya watu milioni 8 huteka maji kwenye visima, mito, maziwa, au vijito; na zaidi ya watu milioni moja hununua maji yanayoletwa kwa lori.” Si ajabu kwamba asilimia 90 ya watu wenye ugonjwa wa kuharisha nchini Mexico huambukizwa kupitia maji machafu!

Gazeti Veja la Brazili linasema kwamba “kwenye fuo za Rio watu hufurahia joto la jua, mchanga mweupe, na bahari. Lakini fuo hizo pia zina bakteria nyingi hatari na mafuta yanayomwagika mara kwa mara kutoka kwenye meli.” Hiyo ni kwa sababu zaidi ya asilimia 50 ya maji machafu nchini Brazili huingia kwenye mito, maziwa, na bahari bila kusafishwa. Hilo husababisha upungufu mkubwa wa maji safi. Mito iliyo karibu na São Paulo, jiji kubwa zaidi la Brazili, imechafuliwa sana hivi kwamba wakaaji huletewa maji safi kutoka kwenye eneo lililo umbali wa kilometa 100.

Katika bara la Australia, uhaba wa maji husababishwa hasa na kurundamana kwa chumvi. Kwa miaka mingi, wenye mashamba walishauriwa wafyeke mashamba yao na kupanda mimea. Kwa hiyo hakukuwa na miti na vichaka vingi ili kufyonza maji yanayotoka juu ya ardhi, na hivyo matabaka ya maji ya chini ya ardhi yalianza kuinuka yakiwa na maelfu ya tani za chumvi. Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Australia linasema hivi: “Tayari eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari milioni 6.2 hivi limeathiriwa na chumvi. Sehemu kubwa ya eneo hilo ndiyo hutokeza mazao mengi nchini Australia.”

Wengine wanasema kwamba ikiwa viongozi nchini Australia wangejali masilahi ya watu kuliko faida wanayopata, huenda tatizo la kurundamana kwa chumvi lingeepukwa. Hugo Bekle wa Chuo Kikuu cha Edith Cowan huko Perth, Australia, anasema hivi: “Kuanzia mwaka wa 1917, serikali zilijulishwa kwamba mashamba ya ngano yanakabili uwezekano mkubwa wa kurundamana kwa chumvi. Katika miaka ya 1920, ilitangazwa kwamba kufyeka mimea husababisha mrundamano wa chumvi kwenye vijito, na katika miaka ya 1930 Wizara ya Kilimo ilikubali kwamba jambo hilo huinua tabaka la maji. Katika mwaka wa 1950, Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Australia lilifanya uchunguzi mkubwa kwa ajili ya Serikali [ya Australia], . . . lakini serikali zilipuuza maonyo hayo na kudai eti wanasayansi wanaegemea upande mmoja.”

Wanadamu Wamo Hatarini

Ni kweli kwamba wanadamu wamefanya mambo mengi wakiwa na nia nzuri. Lakini, wanadamu hawaelewi mengi vya kutosha kuhusu mazingira ili kutabiri kwa usahihi matokeo ya matendo yao. Matokeo yamekuwa mabaya sana. Tim Flannery, msimamizi wa Jumba la Makumbusho la South Australia, anasema hivi: “Kwa kuwa wanadamu wamevuruga sana uhusiano uliopo kati ya mazingira na viumbe na kuharibu ardhi inayowategemeza, wamehatarisha maisha yao wenyewe.”

Basi, suluhisho ni nini? Je, wanadamu watajifunza jinsi ya kutunza mazingira? Je, kweli Dunia inaweza kuokolewa?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Kwa mfano, inakadiriwa kwamba katika mwaka wa 1999, mali za asili zilizotumiwa zilizidi zile zilizotokezwa kwa asilimia 20. Hilo linaonyesha kwamba ilichukua zaidi ya miezi 14 kutokeza tena mali za asili zilizotumiwa na wanadamu katika kipindi hicho cha miezi 12.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Kila Tone Lina Thamani

Unaweza kuhifadhi maji mengi kwa kufanya mambo machache tu.

● Rekebisha mifereji inayovuja.

● Oga kwa muda mfupi unapotumia bomba linalonyunyiza maji.

● Funga mfereji unaponyoa ndevu au kupiga mswaki.

● Tumia taulo mara mbili au tatu kabla ya kuziosha.

● Tumia mashine ya kufua nguo ikiwa tu unaosha nguo nyingi. (Kanuni hii pia inahusu mashine ya kuosha vyombo.)

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Tukitunza Mazingira, Hatutapungukiwa

● Ijapokuwa Australia ndilo bara kame zaidi ulimwenguni, gazeti The Canberra Times linasema kwamba zaidi ya asilimia 90 ya maji yanayonyunyizwa kwenye mashamba nchini humo “hupitishwa kwenye mitaro. Mbinu hiyo ilikuwa ikitumiwa wakati watawala wa Misri walipojenga piramidi.”

● Ulimwenguni pote, inakadiriwa kwamba mtu mmoja hutumia lita 550,000 za maji kwa mwaka. Kiasi hicho kinatia ndani maji yanayotumiwa katika kilimo na viwandani. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba mtu mmoja katika Amerika Kaskazini hutumia lita 1,600,000 kwa mwaka. Nchi moja iliyokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti ndiyo hutumia maji mengi zaidi, kwani kwa wastani mtu mmoja hutumia zaidi ya lita milioni 5.3 kwa mwaka.

● Kulingana na gazeti Africa Geographic, kila mwaka ekari kumi hivi za shamba huhitajiwa ili kutokeza mazao ya kumtosha raia mmoja wa Afrika Kusini. Hata hivyo, nchi hiyo inaweza kutumia tu ekari sita hivi kwa kila raia.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Eneo lililokatwa miti la Sahel, huko Burkina Faso. Eneo hili lilikuwa na miti mingi miaka 15 iliyopita

[Hisani]

© Jeremy Hartley/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 8]

Misitu ya mvua ya Kamerun imeharibiwa kutokana na mbinu ya kilimo inayohusisha kufyeka na kuchoma miti na mimea

[Hisani]

© Fred Hoogervorst/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 8]

Bado uchafuzi unaosababishwa na magari ni tatizo kubwa nchini Marekani

[Picha katika ukurasa wa 8]

Huko Brazili, eneo la misitu lenye ukubwa wa zaidi ya kilometa 20,000 za mraba liliharibiwa kila mwaka tangu mwaka wa 1995 hadi 2000

[Hisani]

© Ricardo Funari/SocialPhotos.com ▸

[Picha katika ukurasa wa 9]

Zaidi ya watu bilioni mbili hupata riziki ya dola tatu au chini kila siku

[Hisani]

© Giacomo Pirozzi/Panos Pictures ▼

[Picha katika ukurasa wa 9]

Maji yaliyo chini ya ardhi katika kisima hiki cha kijiji kimoja huko India yamechafuliwa na vidimbwi vya kuwafuga kamba

[Hisani]

© Caroline Penn/Panos Pictures ▼