Nchi Yenye Sarafu Kubwa
Nchi Yenye Sarafu Kubwa
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Guam
VISIWA vya Yap viko katika Bahari ya Pasifiki. Visiwa hivyo huwavutia watalii wanaotaka kustarehe kwa kuwa vina hali ya hewa na mandhari ya kupendeza. Lakini mara nyingi wageni hushangaa kuona wenyeji wakiacha pesa zao barabarani.
Katika maeneo yote ya visiwa hivyo, unaweza kuona mawe ya mviringo nje ya majengo na kwenye vijia. Mawe hayo ya mviringo yanayoitwa rai katika lugha ya kienyeji, ndiyo pesa za Visiwa vya Yap. Ijapokuwa watu fulani huweka pesa hizo za mawe nyumbani kwao, watu wengi huweka pesa zao katika “benki” za vijijini. “Benki” hizo hazina walinzi wala wafanyakazi wa kuwahudumia wateja. Pia hakuna majengo ya “benki.” Pesa huwekwa nje badala ya kuwekwa katika vyumba vya kuhifadhi vitu vyenye thamani. Unaweza kuona mawe mengi ya mviringo yaliyo na mashimo katikati yakiwa yameegemezwa kwenye minazi na kuta. Baadhi ya mawe hayo yana kipenyo cha meta nne na uzito wa zaidi ya tani tano.
Huenda umezoea kubeba sarafu mfukoni mwako, lakini sarafu zinazotumiwa katika Visiwa vya Yap ni kubwa sana hivi kwamba haziwezi kutoshea ndani ya gari. Pesa za mwisho za mawe zilitengenezwa katika mwaka wa 1931. Hata hivyo, bado zinatumiwa katika visiwa hivyo. Pesa hizo zilitoka wapi?
Zilipatikana kwa Shida
Kulingana na hekaya, zamani za kale mabaharia fulani kutoka Yap walifika kwenye kisiwa cha Palau na kupata mawe maridadi. Walirudi Yap wakiwa na mawe hayo, nao wenyeji wakaanza kuyatumia kama pesa. Walianza kuchonga mawe hayo katika umbo la mwezi mpevu na kutoboa shimo katikati yake.
Wenyeji wa Yap walichagua kwa makini mawe waliyotumia. Walipendelea kutumia madini ya aragonite na calcite. Madini ya aragonite hupatikana ardhini na katika lulu, nayo madini ya calcite hupatikana kwa kiwango kikubwa katika marumaru. Madini hayo huwa maridadi sana yanapochongwa kwa ustadi. Lakini hayapatikani huko Yap. Hivyo, wenyeji wa Yap waliendelea kwenda Palau ili wapate mawe hayo. Kisiwa cha Palau kiko umbali wa kilometa 400 hivi kusini-magharibi mwa Yap. Hiyo ni safari ya siku tano ukitumia mtumbwi kusafiri kwenye bahari iliyo na mawimbi mengi.
Huko Palau, wenyeji wa Yap walipata kibali kutoka kwa chifu wa eneo hilo kisha wakaanza kuchimba mawe. Kwa kutumia vyombo duni, walikata vipande vya mawe katika mapango yaliyo chini ya ardhi na kuvichonga katika umbo la mviringo. Kazi ya kuchonga sarafu moja ilichukua miezi, na nyakati nyingine hata miaka!
Mashimo yalitobolewa katika mawe hayo ili kuingiza vigingi vilivyotumiwa kuyabeba hadi ufuoni. Kisha mawe hayo yaliyochongwa yaliingizwa katika mitumbwi au mashua zilizotengenezwa kwa mianzi. Ili kusafirisha jiwe kubwa, watu hao walilisimamisha ndani ya maji halafu wakajenga mashua kubwa kulizunguka. Walisafirisha mawe hayo hadi Yap kwa kutumia mitumbwi iliyoendeshwa kwa upepo huku wakipiga makasia kwa nguvu.
Kazi yote hiyo ilifanywa kwa mkono, na ilikuwa hatari. Watu wengi walijeruhiwa au kufa walipokuwa wakikata na kusogeza mawe makubwa kwenye nchi kavu. Pia, safari ya kurudi Yap ilikuwa hatari. Unaweza kuona pesa hizo za mawe katika sakafu ya bahari karibu na Yap na Palau, na hilo huonyesha kwamba baadhi ya pesa hizo za mawe na vilevile baadhi ya watu waliokuwa wakizisafirisha hawakufanikiwa kufika Yap. Hata hivyo, pesa hizo zilizozama majini zinamilikiwa na watu fulani huko Yap. Mawe hayo yana thamani kama vile mawe yaliyo kwenye nchi kavu.
Yana Thamani Gani?
Watu wanapofanya biashara kwa kutumia mawe ya rai, mmiliki mpya wa mawe hayo huyaacha mahali yalipo. Mawe mengi hayajahamishwa kwa miaka mingi, nayo huwa mbali sana na nyumba za watu wanaoyamiliki. Hakuna wizi.
Ili mwizi aibe sarafu za mawe, anahitaji nguvu na ujasiri wa kutosha. Ingekuwa vigumu kwa mwizi kuwa na ujasiri wa kutosha kwani majirani wanafahamu vizuri yule anayemiliki kila jiwe, nao huheshimu sana mali za wengine.
Thamani ya jiwe inaweza kukadiriwaje? Kwanza, unahitaji kufikiria ukubwa wake, umaridadi wake, na jinsi lilivyochongwa. Kisha unafikiria historia yake. Lilichongwa lini? Je, ilikuwa vigumu sana kulikata na kulichonga? Je, watu walikabili hatari au hata kufa walipokuwa wakilisafirisha hadi Yap? Hatimaye, watu wanaofanya biashara kwa mawe hayo wana cheo gani? Pesa za mawe za chifu zina thamani kuliko zile za mtu wa kawaida.
Mwaka wa 1960, wakati benki moja ya nchi ya kigeni iliponunua sarafu ya jiwe yenye kipenyo cha meta 1.5 hivi, watu wa maeneo mengine walipata habari kuhusu historia ya sarafu hiyo. Inasemekana kwamba ilitumiwa tangu miaka ya 1880. Ilikuwa imetumiwa kuwalipa wajenzi wa nyumba fulani. Wakati mmoja, watu wa kijiji fulani waliitumia kuwalipa watu wa kijiji kingine kwa sababu ya kucheza dansi ya pekee. Na baadaye, mwenye nyumba mmoja aliitumia kununua mabati ya kujengea paa. Biashara hizo zote zilifanywa bila kuhamisha sarafu hiyo kutoka mahali ilipokuwa, na hakukuwa rekodi zozote zilizoandikwa za biashara hizo. Habari kuhusu umiliki na historia ya sarafu hiyo zilijulikana sana huko Yap.
Thamani Haitegemei Ukubwa
Mawe ya rai yalipoanza kutumiwa miaka mingi iliyopita, hayakupatikana kwa urahisi na yalikuwa yenye thamani kubwa kwani ni machifu tu walioyamiliki. Mwishoni mwa karne ya 19, watu walitumia vifaa vya chuma kuchonga sarafu nyingi za mawe, kutia ndani sarafu kubwa, kisha wakazisafirisha kwa kutumia meli za mizigo. Ijapokuwa mawe mapya ya rai ni makubwa kuliko yale ya zamani, yana thamani ndogo kwa sababu hayakutengenezwa kwa kutumia njia za kale zilizokuwa hatari.
Hesabu rasmi iliyofanywa mwaka wa 1929 ilionyesha kwamba kuna sarafu 13,281 za mawe, na idadi hiyo inazidi idadi ya wakaaji wa visiwa hivyo! Mambo yalibadilika wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Wanajeshi walichukua na kuvunja baadhi ya mawe hayo ili kujenga barabara za uwanja wa ndege na ngome. Nusu tu ya mawe hayo ndiyo yaliyosalia. Pia watu wanaopenda kukusanya vitu walipora sarafu nyingi za mawe. Sasa, serikali imetunga sheria za kulinda pesa hizo za mawe kwa kuwa zinawakilisha utamaduni wa pekee.
Huko Yap, bado watu huacha mali zao barabarani ili zitazamwe na wapita-njia!
[Ramani katika ukurasa wa 20]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Japani
BAHARI YA PASIFIKI
Ufilipino
Saipan
Guam
Yap
Palau
[Hisani]
Globe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 21]
“Benki” ya pesa za mawe
[Picha katika ukurasa wa 22]
Sarafu fulani za huko Yap zina uzito wa zaidi ya tani tano