Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Watoto wa Sili wa Visiwa vya Magdalen

Watoto wa Sili wa Visiwa vya Magdalen

Watoto wa Sili wa Visiwa vya Magdalen

NILILENGWA-LENGWA na machozi nilipomtazama kiumbe mwenye manyoya meupe aliyekuwa mbele yangu. Sikuamini kwamba nilikuwa nimejilaza karibu sana na sili mdogo wa harp kwani kwa miaka 20 nilikuwa nimetamani sana kufanya hivyo. Nilisisimuka sana nilipotazama macho yake meusi. Nilitaka kumtazama sili huyo mdogo kila mara alipofumba na kufumbua macho, alipopumua, na kutikisa masharubu yake.

Kikundi chetu cha watalii kilikuwa kimesafiri kwa kilometa 100 juu ya barafu inayoelea katikati ya Ghuba ya St. Lawrence, iliyo kati ya Newfoundland na Kanada. Mimi na mke wangu tulikuwa tumesafiri kwa ndege hadi kwenye Visiwa vya Magdalen, karibu na mahali ambapo kikundi kikubwa zaidi cha sili wa harp huzalia. Watu waliotutembeza walikuwa wametuhakikishia kwamba mavazi yetu ya kuzuia baridi yenye rangi ya machungwa hayangewashtua sili wachanga.

Sili wa Harp

Miguu ya sili wa harp hufanana na mkia wa samaki. Sili wa harp waliokomaa wana alama kama za kinubi mgongoni.

Sili wa harp ni wanyama wanaozaa, nao hupumua na kunyonyesha. Mara nyingi wao huishi katika maji baridi ya Bahari ya Atlantiki Kaskazini. Lakini sili hao wenye nguvu wana uwezo wa kuishi katika eneo hilo lenye barafu. Sili waliokomaa huwa na uzito wa kilo 135 na urefu wa meta 1.6 hivi.

Sili wa harp hutumia makucha yao makali ya miguu ya mbele ili kujivuta juu ya barafu, kutoboa mashimo ili wapate hewa wanapoogelea chini ya barafu, na kujishikilia kwenye mashimo hayo. Miguu yao ya nyuma ni mikubwa kuliko ile ya mbele, nao huitumia kujisogeza. Wanyama hao chapuchapu wa baharini wanaweza kusafiri kilometa 8,000 kwa mwaka.

Sili wa harp huitwa pia sili wasio na masikio, lakini hilo halimaanishi kwamba wao ni viziwi. Sili hao hawana masikio ya nje, bali wana shimo dogo pande zote mbili za kichwa ambalo hujifunga wanapozama. Sili hao wana uwezo mzuri wa kusikia. Wanaweza kutambua mahali ambapo sauti inatoka chini ya maji, jambo ambalo wanadamu hawawezi kufanya!

Sili wa harp wana macho makubwa ambayo huwawezesha kuona vizuri katika mwangaza hafifu chini ya maji. Wanapopigwa na mwangaza wa barafu inayong’aa, mboni za macho yao huwa nyembamba ili kuwawezesha kuona vizuri.

Sili Wachanga

Tulitazama kundi la sili lililokuwa na sili wa kike waliosafiri kutoka Greenland, eneo lililo mbele ya Kanada Kaskazini, ili kuzaana. Wao huzalia juu ya barafu inayoelea ili wasishambuliwe na wanyama-wawindaji. Wao huzaa haraka sana. Kwa kawaida wao huchukua dakika moja hivi kuzaa! Hata kabla hujawa tayari kumpiga picha, huenda mtoto wa sili akawa ameshazaliwa na anakutazama! Punde tu baada ya kuzaa, sili wa kike hugeuka na kutumia pua lake kugusa pua la mtoto wake. Anafanya hivyo ili atambue harufu na sauti ya pekee ya mtoto wake. Kisha atamnyonyesha mtoto huyo peke yake kwa muda wa majuma mawili hivi.

Watoto wa sili huyatafuta matiti ya mama zao haraka. Wanapokuwa na njaa wao husikika kana kwamba wanalia, “Ma, Ma.” Baada ya kula wao hujipenyeza katika ufa ulio kwenye barafu na kulala. Kwa kulala mahali palepale kila mara, wao hupafanya pawe kama kitanda kidogo cha barafu.

Wanapozaliwa, kwa kawaida sili wa harp huwa na uzito wa karibu kilo 10 na urefu wa sentimeta 90 hivi. Mwanzoni, hawawi na mafuta mengi mwilini ya kuwapasha joto, lakini baada ya muda mfupi wao huanza kuyatokeza! Katika siku 12 hivi za kwanza, sili hawa huongeza uzito kwa kilo mbili kila siku. Maziwa wanayonyonya ni yenye lishe kwani asilimia 50 ya maziwa hayo ni mafuta. * Kwa muda usiozidi majuma mawili, sili mchanga atakuwa na uzito wa kilo 35!

Kubadili Rangi

Unaweza kukadiria umri wa sili mchanga kwa kutazama rangi ya manyoya yake. Anapomaliza siku ya kwanza, sili mchanga hukauka na manyoya yake huwa na rangi ya manjano kwa sababu ya umajimaji ambao huzunguka kijusi. Baada ya kupigwa na jua kwa siku tatu au nne rangi hiyo ya manjano hufifia. Kisha manyoya yake hubadilika na kuwa meupe. Baada ya majuma mawili, Mama hutoweka milele.

Sili wachanga hupiga kelele, lakini mama zao hawaitikii. Nyakati nyingine, wao hujikusanya katika vikundi vidogo kwenye barafu ili kujituliza. Muda si muda, mabaka yenye rangi ya kijivu hutokea katika manyoya yao meupe. Kati ya siku ya 12 hadi ya 21, manyoya yao yote hubadilika na kuwa ya rangi ya kijivu, na mwishoni mwa mwezi wa kwanza huwa yamechakaa. Kufikia wakati huu, manyoya yote meupe huwa yametoka naye huwa na manyoya laini ya rangi ya kijivu yasiyopenyeza maji.

Hatua Zinazofuata Katika Maisha ya Sili

Sili hao wachanga hutegemea mafuta yaliyo mwilini mwao hadi njaa inapowalemea na kuwalazimisha kutafuta chakula majini. Hata hivyo, wanapoingia majini hawawezi kuzama kwa sababu wao ni wanono na wana mafuta mengi! Wao hupigapiga maji kwa miguu yao midogo. Kwa njia hiyo miguu yao huzoea kuogelea na wanapofanya hivyo wanapunguza mafuta yaliyo mwilini kiasi cha kuweza kuzama. Sasa wanaweza kula na kushiba, kwani kuna chakula kingi majini kama vile uduvi na samaki wadogo.

Sili wanapokuwa na umri wa mwaka mmoja manyoya yao hutoka tena. Wanapokuwa kati ya umri wa miaka mitatu na saba, wao huweza kujamiiana nao huwa na alama zinazofanana na kinubi mgongoni. Sili wa harp wanaweza kuishi kwa miaka 35.

Twamwona Sili Mchanga

Baada ya kuvaa nguo za kuzuia baridi na kuingiza vifaa vya kutupasha joto ndani ya viatu na mifuko ya nguo zetu, tunapanda helikopta na kusafiri kilometa 80 tukiwa watu 17. Tunapotazama chini tunaona barafu kila mahali. Hatimaye, tunatua juu ya bahari iliyoganda na kuwa barafu. Tunafunga viatu vyetu vilivyo na chuma chini na kuanza kutembea polepole juu ya barafu. Kwa ghafula, tunamwona sili mchanga mwenye manyoya ya manjano nyuma ya mama yake! Anafanana na kiwavi aliye na manyoya anayejitahidi kumfuata mama yake. Ninavutiwa naye mara moja!

Ninajilaza kwenye barafu kwani nikisimama huenda sili akafikiri kwamba mimi ni dubu. Sili wenye watoto wanaweza kuwa wakali sana, kwa hiyo ninasubiri hadi sili ninayemtazama anapoingia ndani ya shimo kwenye barafu. Mtoto wake, ambaye nimemwita Sadie, analala meta sita hivi kutoka mahali nilipo. Ninatambaa polepole na kumkaribia. Sadie anafumbua macho yake taratibu.

Sadie ananikazia macho, nami ninabaki palepale nilipo. Kwa ghafula, Sadie anaanza kunikaribia haraka sana kuliko nilivyotazamia. Anaponikaribia anaonekana kuwa mkubwa, ingawa rangi ya manyoya yake inaonyesha kuwa ana umri wa siku mbili au tatu. Sadie anasimama sentimeta chache kutoka mahali nilipo naye anasogea huku na huku akitikisa pua yake ndogo. Ninamsikia akinusanusa. Ananikaribia na kuanza “kunibusu” usoni na shingoni kwa pua yake yenye majimaji!

Ninastaajabu kumwona mtoto huyo wa sili mwenye kuvutia akijikunja kando yangu na kulala! Hata ninaweka mkono wangu juu ya mwili wake. Manyoya yake madogo laini yanatokea katikati ya vidole vyangu. Ana joto kweli. Ninampapasa na kumkumbatia Sadie hadi wakati tunapoanza kurudi nyumbani. Ninapoinuka polepole Sadie anaendelea kulala.

Ninatokwa na machozi ninapoondoka huku nikimshukuru Mungu wetu, Yehova, kwa kuumba kiumbe huyo mdogo maridadi. Siamini kwamba nimemwona kwa karibu sili mchanga wa harp. Tukio hilo linanikumbusha maneno haya ya mtunga-zaburi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. . . . Na kwa habari ya bahari hii iliyo kubwa na pana, humo mna vitu vyenye kutambaa visivyo na hesabu, viumbe hai, vidogo kwa vikubwa.” (Zaburi 104:24, 25)—Tumetumiwa makala hii.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kwa kulinganisha, asilimia 4 ya maziwa ya ng’ombe ni mafuta.

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

Je, Ulijua?

▪ Kunapokuwa na dhoruba kali au ikiwa hali ya barafu si nzuri, sili wa kike wa harp wanaweza kuahirisha kuzaa kwa siku kadhaa wakitafuta mahali panapofaa pa kuzalia.

▪ Sili wa harp wanaweza kupiga mbizi meta 240 ndani ya maji nao wanaweza kukaa chini ya maji kwa dakika 30 hivi.

▪ Sili wanaweza kulala chini ya maji. Baada ya kila dakika tano au kumi, wao huinua kichwa juu ya maji ili wapumue, kisha wao huzama tena bila kuamka!

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Yai Hukawia Kupandikizwa

Kitabu Seasons of the Seal kinasema kwamba “sili wa kike wa harp aliyekomaa huwa na mimba wakati wote wa mwaka isipokuwa kwa majuma matatu tu. Yeye huchukua mimba kwa miezi saba na nusu.” Hilo linawezekanaje? Kitabu hicho kinaeleza hivi: “Baada ya mimba kutungwa, chembe ya yai lililotungishwa hugawanyika tena na tena, halafu inaacha kugawanyika. Kikundi cha chembe hizo, ambacho ni kidogo kuliko kichwa cha pini, huacha kukua. Kikundi hicho cha chembe huelea ndani ya tumbo la uzazi la sili wa kike. Majuma 11 baadaye, kikundi hicho cha chembe hujipandikiza kwenye tumbo la uzazi na kuendelea kukua.” Kwa nini chembe hizo hukawia kupandikizwa? “Ni lazima sili wa kike azae baada ya kipindi cha mwaka mzima hivi ili kuwe na barafu ya kutosha kuzalia.”

[Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KANADA

[Hisani]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Picha ya setilaiti ya Visiwa vya Magdalen

[Hisani]

NASA JSC

[Picha katika ukurasa wa 24]

Sili mwenye manyoya ya manjano

[Picha katika ukurasa wa 24]

Sili mwenye manyoya meupe

[Picha katika ukurasa wa 25]

Sili mwenye manyoya yaliyochakaa

[Hisani]

© IFAW / David White

[Picha katika ukurasa wa 25]

▼ Wanapoanza kupigapiga maji

[Hisani]

© IFAW

[Picha katika ukurasa wa 26]

Sili mchanga akiwa na mama yake

[Hisani]

© IFAW

[Picha katika ukurasa wa 26]

Sili aliyekomaa akiogelea chini ya barafu

[Hisani]

© IFAW