Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kazi ya Madaktari Inabadilika

Kazi ya Madaktari Inabadilika

Kazi ya Madaktari Inabadilika

Mwaka wa 1174, Maimonides aliteuliwa kuwa daktari wa familia ya watawala wa Misri, naye alifanya kazi kwa siku nyingi katika makao ya mfalme. Aliandika hivi kuhusu maisha yake ya kila siku: “Mimi hula chakula kidogo mara moja tu kwa siku. Kisha mimi huanza kuwashughulikia wagonjwa, kuwaandikia dawa, na kuwapa maagizo. Wagonjwa huja kutibiwa hata usiku, na nyakati nyingine . . . mimi huchoka sana na kushindwa kuongea.”

SIKUZOTE madaktari wamelazimika kujitoa mhanga. Lakini hali ambazo madaktari wanakabili sasa katika jamii zinabadilika haraka sana. Kazi yao huchosha kama vile ilivyomchosha Maimonides. Lakini je, wao huheshimiwa kama zamani? Hali za leo zimeathirije maisha ya madaktari na uhusiano wao na wagonjwa?

Uhusiano Umebadilika

Katika sehemu fulani, huenda wengine wakakumbuka jinsi daktari alivyobeba dawa zake zote ndani ya mkoba mweusi. Sawa na leo, watu walikuwa na maoni mbalimbali kuhusu madaktari. Madaktari wengi waliheshimiwa kwa sababu ya uwezo wao na cheo chao, na walipendwa kwa sababu ya maadili yao. Kwa upande mwingine, walishutumiwa kwa ada walizotoza, kulaumiwa kwa makosa yao, na watu waliwachambua kwa sababu walidhania hawana huruma.

Licha ya hayo, madaktari wengi walifurahia sana kutibu familia ileile kwa vizazi kadhaa. Waliwatembelea wagonjwa mara nyingi nyumbani kwao, na nyakati nyingine katika maeneo ya mashambani, walikula chakula pamoja na familia waliyoitembelea au hata kukaa usiku wote wakimsaidia mama kujifungua. Mara nyingi, madaktari ndio waliowapendekezea wagonjwa dawa za kutumia. Madaktari waliojitoa mhanga waliwatibu maskini bila malipo, na waliwahudumia watu wakati wowote ule.

Bila shaka, madaktari fulani bado wanafanya hivyo, lakini katika maeneo mengi uhusiano kati ya madaktari na wagonjwa umebadilika sana katika miaka ya karibuni kuliko ilivyokuwa zamani. Mabadiliko hayo yamesababishwa na nini? Hebu kwanza tuzungumzie lile zoea la madaktari kuwatembelea wagonjwa nyumbani.

Kuwatembelea Wagonjwa Nyumbani

Zamani ilikuwa kawaida kwa madaktari kuwatembelea wagonjwa nyumbani, na zoea hilo bado linaendelea katika maeneo fulani. Lakini madaktari wanaacha kufanya hivyo ulimwenguni pote. Gazeti The Times of India linasema: “Madaktari waliowatia moyo wagonjwa vitandani, waliofahamiana sana na familia na kuwa tayari kuwatembelea wagonjwa nyumbani wakati wowote walipohitajiwa, wanazidi kupungua kwa sababu siku hizi madaktari wengi wamekuwa wataalamu wa ugonjwa hususa.”

Kwa sababu ujuzi wa tiba umeongezeka sana, madaktari wengi wanasomea tiba ya ugonjwa hususa na wanafanya kazi wakiwa kikundi. Hivyo, wagonjwa wanaweza kutibiwa na daktari tofauti kila mara wanapoenda kutibiwa. Basi, madaktari wengi hawawezi kuwa na uhusiano wa muda mrefu pamoja na familia moja kama ilivyokuwa zamani.

Madaktari waliacha kuwatembelea wagonjwa nyumbani miaka mia moja hivi iliyopita wakati ambapo walianza kuchunguza magonjwa katika maabara na kutumia vifaa vya kuwapima wagonjwa. Katika maeneo mengi, mashirika ya afya yaliona kwamba madaktari wanapoteza wakati kwa kuwatembelea wagonjwa nyumbani. Sasa wagonjwa wengi wanaweza kusafiri kwa urahisi ili kumwona daktari. Isitoshe, sasa wafanyakazi wa afya na wale wanaotoa huduma za dharura wanafanya kazi zilizofanywa tu na madaktari.

Hali Zimebadilika

Leo ni madaktari wachache wanaofanya kazi kwa kujitegemea. Mara nyingi, huduma za tiba hutolewa na mashirika ya serikali au mashirika mengine ya afya yanayowaajiri madaktari. Hata hivyo, madaktari wengi hawapendi kuajiriwa. Mara nyingi, mashirika hayo huwataka madaktari wawahudumie wagonjwa wengi kwa muda mfupi. Dakt. Sheila Perkins wa Uingereza anasema hivi: “Ninatazamiwa kutumia dakika saba hadi kumi kumhudumia mgonjwa mmoja. Na ninahitaji kutumia sehemu kubwa ya wakati huo kurekodi habari kwenye kompyuta. Hakuna wakati wa kutosha kufahamiana na mgonjwa. Inafadhaisha sana.”

Hali zinazobadilika zimewafanya wagonjwa wawe na mamlaka zaidi. Kuna wakati ambapo maagizo ya madaktari hayangepingwa. Lakini, leo katika nchi nyingi ni lazima daktari amfahamishe mgonjwa kuhusu matibabu mbalimbali na matokeo yake ili mgonjwa akubali kutibiwa akiwa anafahamu vizuri matibabu hayo. Uhusiano kati ya daktari na mgonjwa umebadilika. Watu fulani huona daktari kuwa mtaalamu tu.

Katika ulimwengu huu unaozidi kubadilika, kuna madaktari wengi wanawake. Watu wengi huwapenda madaktari wanawake kwani wao huonekana kuwa wasikivu. Hivyo, inaonekana wanawafanya watu wawaone madaktari kuwa wenye huruma.

Watu wengi wanawapenda madaktari wanaoelewa hisia na mfadhaiko wa wagonjwa. Hata hivyo, ni wagonjwa wangapi wanaoelewa hisia za madaktari na mfadhaiko wanaokabili? Hapana shaka kwamba kufanya hivyo kutaboresha uhusiano kati ya daktari na mgonjwa. Makala inayofuata itazungumzia jambo hilo.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Maimonides

[Hisani]

Brown Brothers

[Picha katika ukurasa wa 4]

Zamani, madaktari walikuwa wakiwatembelea wagonjwa nyumbani