Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupamba Chuma kwa Dhahabu

Kupamba Chuma kwa Dhahabu

Kupamba Chuma kwa Dhahabu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

VÍCTOR ni mzee mwenye umri wa miaka 74, na uwezo wake wa kuona umefifia kwa sababu ya kutazama vitu vidogo kwa muda mrefu sana. Hata hivyo, macho yake hung’aa kila mara anapoombwa aeleze kuhusu kazi yake ya kupamba chuma kwa dhahabu ambayo ameifanya kwa miaka 50. Víctor, alianza kazi hiyo alipokuwa na umri wa miaka 14, naye ni msanii stadi wa kupamba chuma kwa dhahabu.

Víctor anasema hivi: “Sioni kupamba chuma kwa dhahabu kuwa kazi ya kujiruzuku tu. Pindi fulani nimefanya kazi kwa saa 24.” Yeye hutumia vifaa vyake vya kazi ambavyo ni vikuukuu, huku akichangamka anapokumbuka kazi yake ya kutokeza vyombo vya pekee vya sanaa ambayo ameifanya katika maisha yake yote.

Sanaa ya Damasko Yasitawi Hispania

Wataalamu wa vitu vya kale wamepata baadhi ya vyombo vilivyopambwa kwa dhahabu katika makaburi ya Wamisri, ambavyo vilitengenezwa katika karne ya 16 K.W.K.

Huenda vyombo vya kwanza vya aina hiyo vilitengenezwa nchini China au Misri. Hata hivyo, sanaa hiyo huhusianishwa na jiji la kale la Damasko. Wasanii stadi katika jiji hilo kuu la Siria walipata umaarufu kwa kutengeneza vitu maridadi sana. Jiji la Damasko lilikuwa kituo cha kibiashara kwa kuwa lilikuwa kwenye makutano ya barabara muhimu zilizotoka katika maeneo yaliyo mashariki mwa Mediterania, nchi za Mesopotamia, na za Mashariki. Hilo liliwezesha vyombo vya sanaa vya jiji hilo visafirishwe kutoka Siria hadi maeneo ya mbali.

Katika kipindi cha karne kadhaa, sanaa hiyo ilisitawi huko Ulaya, na kufikia karne ya 16, jiji la Toledo nchini Hispania likawa kituo muhimu cha sanaa hiyo. Panga, mavazi ya vita, ngao, na vifaa vingine vilivyotengenezwa huko Toledo vilipambwa kwa sanaa hiyo ambayo ilivifanya viwe maridadi na vya pekee.

Mapambo Tofauti-Tofauti

Sanaa hiyo iliyofanywa huko Toledo ilihusisha kupamba vyuma vyeusi sana kwa dhahabu na fedha nyangavu. Vyombo vilipambwa kwa herufi za kale za Kiarabu zinazoitwa Kufic na vilevile maumbo ya maua na ya jiometria yaliyotumiwa katika jamii za Waarabu na Mudejar. Acha twende pamoja huko Toledo ujionee jinsi wasanii wanavyoendeleza sanaa hiyo.

Unapotembea katika barabara zilizojipinda za Toledo ya kale, ni rahisi kuwazia jinsi hali ilivyokuwa katika Zama za Kati. Utatambua upesi kwamba bado wasanii hupamba vitu kwa dhahabu. Pia utaona kwamba vitu vingi vilivyopambwa kwa dhahabu kama vile mapambo ya nguo, bangili, vifungo vya shati, pini za kushikilia tai, masanduku ya kuwekea dawa, kastabini, vipuli, na sahani, vinauzwa katika maduka mengi. Isitoshe, katika maduka mengine utaona wasanii wakiwa wameshika uzi wa dhahabu kwa mkono mmoja, huku wakishika kifaa cha chuma kwa mkono mwingine ili kugongelea uzi huo kwenye chombo cha chuma. Hivyo ndivyo wasanii wanavyopamba vifaa vya chuma kwa dhahabu.

Kazi Ngumu ya Kutengeneza Vyombo vya Sanaa

Unapokaribia, utaona kwamba msanii ana vipande vya chuma vya maumbo na ukubwa tofauti-tofauti. Anachagua kipande cha chuma chenye umbo la duara na kuanza kukipamba. Hatua ya kwanza inahusisha kukwaruza kipande hicho cha chuma kwa kifaa cha kukwaruzia, ambacho kimeundwa kwa chuma kigumu zaidi, ili kutokeza mistari inayokingamana. Kisha, yeye hutumia kifaa hicho kuchora umbo analotaka kutokeza.

Baada ya hatua hiyo, msanii huwekelea kipande hicho cha chuma juu ya ubao unaoweza kusogezwa ambao umefunikwa kwa utomvu fulani. Ubao huo hutegemeza kipande hicho cha chuma na kukizuia kisibonyee kinapoendelea kupambwa.

Hatua inayofuata ni kutia uzi wa dhahabu. Msanii hushikilia uzi wa dhahabu kwa mkono mmoja na kuutia polepole kwenye ile mistari iliyokwaruzwa juu ya kipande cha chuma. Sasa kipande hicho huwa na maumbo mbalimbali kama vile ya jiometria, ndege, maua, au hata umbo la jiji la kale la Toledo. Wasanii fulani hupamba chuma kimoja kwa kutumia maumbo hayo mbalimbali.

Kisha msanii hugongelea uzi wa dhahabu ndani zaidi. Katika hatua hii, msanii hutumia kifaa cha kugongea ambacho ni kipana zaidi. Kwa kugongagonga kwa ustadi, msanii huingiza uzi wa dhahabu ndani kabisa ya sehemu zenye mikwaruzo.

Hatua inayofuata ni kuongeza weusi wa chuma. Kipande hicho cha chuma hutumbukizwa katika mchanganyiko wa magadi na nitrati ya potasiamu, ulio na joto la nyuzi 800 Selsiasi. Hilo hufanya chuma kiwe cheusi zaidi. Rangi hiyo ya chuma iliyo nyeusi sana hufanya mapambo ya dhahabu yaonekane wazi zaidi.

Hatimaye, msanii huchonga na kung’arisha mapambo hayo. Kipande hicho kinapochongwa, mapambo ya dhahabu huonekana wazi zaidi. Sehemu zote ndogondogo, kama vile manyoya ya ndege au petali za maua, huchongwa. Kisha kipande hicho hung’arishwa kwa ageti na kufanya uzi wa dhahabu ung’ae huku ukizungukwa na ile sehemu nyeusi. Baada ya hatua hizo zote, umbo linalong’aa hutokea!

Sanaa ya pekee ya kupamba chuma kwa dhahabu imedumu hadi leo kwa sababu wasanii wengi wameiendeleza kwa karne nyingi. Kwa sababu ya jitihada zao, leo tunaweza kufurahia kuwa na vyombo maridadi vya chuma vilivyopambwa kwa dhahabu na fedha.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kifaa kilichopambwa cha kufungua barua kilicho kama upanga

[Picha katika ukurasa wa 17]

Toledo, Hispania

[Picha katika ukurasa wa 17]

Vipuli

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kidani

[Picha katika ukurasa wa 17]

Sanduku la kale la kuhifadhia vito

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kukwaruza

Kutia uzi

Kugongelea uzi

Kuongeza weusi wa chuma

Kuchonga

Kung’arisha

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

All photos: Agustín Sancho

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Corners of page, pendant, and jewelry box: Agustín Sancho