Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kusafiri kwa Meli Majini na Kwenye Nchi Kavu!

Kusafiri kwa Meli Majini na Kwenye Nchi Kavu!

Kusafiri kwa Meli Majini na Kwenye Nchi Kavu!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI POLAND

Ungehisije nahodha wa meli akikualika ujiunge naye kusafiriki kwa meli majini na vilevile juu ya nchi kavu?

KWA muda mrefu bidhaa zimesafirishwa kwa meli kupita maeneo ya maziwa ya Iława, kaskazini mwa Poland. Miaka elfu moja iliyopita, mazao, mbao, na vyombo vya mbao vilisafirishwa kupitia njia ya zamani iliyokuwa maarufu, yaani kuanzia Mto Drwęca kuelekea kusini kwenye Mto Vistula kisha kaskazini kuelekea Bahari ya Baltiki. (Ona ramani.) Kisha mizigo hiyo ilisafirishwa hadi Ulaya Magharibi.

Njia hiyo ya zamani ilipata umaarufu zaidi katika karne ya 13, wakati kundi la Teutonic Knights lilipotwaa sehemu kubwa ya eneo hilo. * Baadaye, kuanzia karne ya 16, mbao za eneo hilo zilihitajiwa sana, na wafanyabiashara wa Gdańsk na wajenzi wa meli kutoka Ufaransa na Denmark walizinunua kwa wingi.

Kwa nini mbao hizo zilipendwa sana? Sababu moja ni kwamba misindano isiyo na vifundo, ambayo hukua katika misitu ya eneo hilo na kufikia urefu wa meta 50 hivi, hutokeza mbao nzuri sana zinazofaa kutengeneza milingoti ya meli. Lakini kusafirisha mbao kupitia njia ndefu ya Mto Drwęca na Mto Vistula kulichukua karibu miezi sita hadi nane.

Kutafuta Njia Fupi

Walipokuwa wakitafuta suluhisho la tatizo hilo, wasafirishaji wa bidhaa walifikiria kutumia maziwa sita marefu yaliyo kati ya Ostróda na Elbląg, karibu na Wangwa wa Vistula. Ikiwa maziwa hayo yangeunganishwa kwa njia fulani, safari ya kutoka Mto Drwęca hadi Bahari ya Baltiki ingefupishwa mara tano! Basi iliamuliwa kwamba mfereji ujengwe ili kuunganisha maziwa hayo. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kujenga mfereji huo kwa kutumia teknolojia duni ya wakati huo. Kwa mfano, wajenzi wangeshughulikiaje kiwango cha maji kilichotofautiana kwa meta 104 katika sehemu yenye umbali wa kilometa kumi?

Licha ya magumu hayo, wafanyabiashara, wenye mashamba, na watengenezaji wa bidhaa wa eneo hilo walitaka kuuza bidhaa zao haraka na kupata faida kubwa. Hivyo, waliendelea kuwachochea viongozi wa Prussia waunganishe maziwa hayo. Hatimaye, mwaka wa 1825, viongozi hao waliamua kujenga mfereji wa kuunganisha mji wa Ostróda, mji wa Elbląg, na bahari. Uamuzi ulifanywa kuhusu njia ambayo ingetumiwa, kisha mtaalamu mmoja akapewa kazi ya kuchora ramani ya ujenzi. Lakini mtaalamu huyo alipogundua kwamba hangeweza kufanya kazi hiyo, alisalimu amri na kuhifadhi ramani aliyochora.

Mhandisi Stadi Aendeleza Mradi

Wapata wakati huo, Georg Jakob Steenke, alihitimu akiwa mtaalamu wa ujenzi katika chuo kimoja huko Berlin, na alikuwa stadi wa uhandisi wa majini. Muda si muda, kijana huyo mwenye ustadi alithibitisha uwezo wake, na katika mwaka wa 1836 akapewa cheo cha kuwa mkaguzi wa kuta za kuzuia maji huko Elbląg. Steenke alichunguza uwezekano wa kutengeneza mfereji huo ambao wakati huo uliitwa Mfereji wa Oberland. *

Kufikia mwaka wa 1837, Steenke alikuwa amefikiria njia mpya na kuchora ramani ya mfereji huo ambao pia ungetumiwa na meli za mizigo. Wakati huohuo alifuatia sana mavumbuzi ya teknolojia iliyohusu uhandisi wa majini. Hatimaye, katika mwaka wa 1844, ujenzi wa mfereji huo ukaanza. Mitaro ilichimbwa katikati ya maziwa yaliyokuwa mahali ambapo mfereji huo ulianzia, na hilo lilisababisha kiwango cha maji katika maziwa fulani kishuke kwa meta tano hivi. Kwa kuwa bado kiwango cha maji kilitofautiana kwa meta 100 hivi, Steenke aliamua kushughulikia tatizo hilo kwa kujenga sehemu 25 za kuinulia meli.

Hata hivyo, baada ya ujenzi wa sehemu tano za kwanza za kuinulia meli, Steenke aliona kwamba njia ya meli ingekuwa nyembamba sana na hivyo kusababisha msongamano wa meli. Bila kuvunjika moyo, alienda Marekani ili kuchunguza jinsi matatizo kama hayo yalivyoshughulikiwa katika ujenzi wa Mfereji wa Morris ambao ulipita katika jimbo la New Jersey. Steenke aliona kwamba sehemu za kuinulia meli za mfereji huo ziligharimu pesa nyingi sana, lakini alipendezwa hasa na jambo moja aliloona huko. Steenke aliona kwamba sehemu fulani za mfereji huo zina majukwaa ya meli ambayo huinuliwa juu ya nchi kavu kwa nyaya za chuma. Steenke aliporudi nyumbani, yeye na wahandisi wengine wawili waliboresha mbinu hiyo na kuitumia. Steenke aliacha mpango wake wa awali wa kutengeneza sehemu za kuinulia meli na badala yake akatengeneza majukwaa manane yaliyowezesha meli kusafiri juu ya nchi kavu. Hebu wazia msisimko wa Steenke katika mwaka wa 1860 wakati ambapo, baada ya majaribio mengi yaliyofanikiwa, sehemu ya kwanza ya Mfereji wa Oberland ilifunguliwa.

Mfereji wa Pekee

Bila shaka, mfereji unaofanya kazi vizuri huwa na sehemu mbalimbali kama vile mitaro, sehemu zilizoinuka, vizuizi vya maji, malango, mifumo ya kuvuta meli, vyumba vya injini, na vifaa vingine. Vitu hivyo vyote huharibika mara kwa mara. Hivyo, miaka 20 baada ya mfereji huo kuanza kutumiwa, jukwaa moja lilijengwa mahali pa zile sehemu tano za awali za kuinulia meli zilizokuwa zimejengwa kwa mbao, kwani zilikuwa zimezeeka. Sehemu kuu ya njia hiyo ambayo iko kati ya Elbląg na Ostróda ina urefu wa kilometa 82 hivi. Njia yote ina urefu wa kilometa 212.

Mfereji wa Oberland, ambao sasa unaitwa Mfereji wa Elbląg-Ostróda, unaonwa kuwa ufundi wa pekee ulimwenguni ulio muhimu sana katika historia. Leo mfereji huo hautumiwi sana na meli za mizigo bali hutumiwa hasa na mashua ndogondogo na meli za watalii. Hata hivyo, katika kitabu chake Kanał Elbląsko-Ostródzki (Mfereji wa Elbląg-Ostróda), Dariusz Barton anaeleza kwamba “ijapokuwa mfereji huo umetumiwa kwa muda mrefu, sehemu zake mbalimbali zingali zinafanya kazi vizuri. Bado zinafanya kazi vizuri kwa sababu zilitengenezwa kwa ustadi sana, na kwa usahihi unaowastaajabisha wataalamu.”

Safiri Pamoja Nasi

Je, ungependa kusafiri pamoja nasi kupitia njia hiyo ya pekee? Tunaanza safari asubuhi huko Ostróda. Tunapitia sehemu mbili za kuinulia meli na kuinuka meta 100 juu ya usawa wa bahari. Tunasafiri polepole tukitazama misitu yenye mibetula, misonobari, na misindano, na vilevile tunaona vinamasi vyenye mayungiyungi yaliyochanua. Sehemu fulani za eneo hilo zimetengwa kuwa hifadhi. Ukiwa huko, unaweza kuona korongo-kisiwa na kibisi katika vichaka au ndege wengine wakitembea polepole kwenye nyasi na kwenye maji yaliyo na kina kifupi.

Baada ya kusafiri kwa kilometa 51, inaonekana kwamba tumefika mwisho wa mfereji! Hata hivyo tunaona nguzo mbili za mawe zinazotegemeza magurudumu makubwa yaliyozungushiwa nyaya nzito. Nahodha anatangaza kwamba tumefika kwenye jukwaa la kwanza, na meli yetu inatua juu ya jukwaa hilo lililo majini.—Ona meli na jukwaa kwenye ukurasa wa 12.

Kisha maji kutoka kwenye tangi la pekee yanatumiwa kuzungusha gurudumu la maji lenye upana wa meta nane. Gurudumu hilo lianzapo kuzunguka linavuta nyaya, jukwaa, na meli tunayosafiria. Tunapovutwa, reli za chuma ambapo jukwaa linapitia, zinatokea juu ya maji, zinatoka nje ya mfereji na kupita upande wa juu wa sehemu iliyoinuka, kisha zinainama kidogo na kushuka kwa meta 550. Lo! Tunasafiri juu ya nchi kavu! Kisha reli hizo huingia tena majini na jukwaa huzama na kuacha kusonga. Meli yetu inaanza tena kuelea juu ya maji huku kiwango cha maji kikiwa kimeshuka kwa meta 21, nasi tunaendelea na safari yetu. Tunapitia kwenye majukwaa matano kama hayo ili tufike Ziwa Druzno ambalo liko sentimeta 30 tu juu ya usawa wa bahari.

Ziwa Druzno ni hifadhi iliyo na wanyama wengi wa pori, na ina zaidi ya nusu ya jamii 400 za ndege wanaopatikana nchini Poland. Ndege hao wanatia ndani korongo, mnandi, furukombe, na tai. Unaposafiri unaweza kuona mbawala, buku, nguruwe-mwitu, sungura-mwitu, simba-mangu, melesi, kongoni, na wanyama wengine. Hatimaye, wakati wa jioni tunafika kwenye bandari huko Elbląg, kaskazini mwa ziwa hilo. Ufuoni kuna magofu ya kasri yanayotukumbusha kuhusu kundi la Teutonic Knights ambalo wakati mmoja lilitawala maeneo hayo na kujenga bandari. Tumesafiri siku nzima kwa meli na bila shaka tutaendelea kukumbuka mambo yenye kupendeza kuhusu safari hii ya pekee!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Teutonic Knights lilikuwa kundi la kijeshi na la kidini la Ujerumani. Mwaka wa 1234, Papa Gregory wa Tisa, alikubali maeneo yaliyotwaliwa na kundi hilo yawe mali ya Papa, huku yakiendelea kutawaliwa na kundi hilo.

^ fu. 11 Mfereji huo uliitwa Oberland, ambalo ni jina la zamani la eneo hilo katika Kijerumani.

[Mchoro katika ukurasa wa 12, 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mchoro wa Mfereji wa Elbląg-Ostróda (Kimo kimeonyeshwa katika meta juu ya usawa wa bahari)

OSTRÓDA

↓ Ziwa Drwęckie

meta 95

Sehemu ya kuinulia meli ya Zielona

meta 96 m

kilometa 4.6 km

Sehemu ya kuinulia meli ya Miłomłyn

meta 99 m

kilometa 82 ↓

kilometa 36.6 km

Sehemu zilizoinuka

kilometa 9.6 km

↓ Ziwa Druzno

sentimeta 30

ELBLĄG

[Mchoro katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Chumba cha injini

Gurudumu la maji

Nyaya za chuma Mtambo wa chini

wa kuvuta nyaya

Jukwaa Reli

 

 

Mfereji wa juu Mtambo wa juu Mfereji wa chini

wa kuvuta nyaya

[Ramani katika ukurasa wa 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Bahari ya Baltiki

Gdańsk

Wangwa wa Vistula

Nogat

Vistula

Drwęca

Iława

Njia fupi kupitia mfereji huo

Elbląg

Sehemu zilizoinuka

Ostróda

[Picha katika ukurasa wa 13]

Meli zilizo juu ya jukwaa huinuliwa na kushushwa kwenye sehemu iliyoinuka

[Hisani]

Zdjęcia: A. Stachurski

[Picha katika ukurasa wa 15]

Picha ya sehemu fulani ya mfereji huo

[Picha katika ukurasa wa 15]

Tuliona kongoni, mbawala, buku, na kibisi tulipokuwa tukisafiri

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Boat: Zdjęcia: M. Wieliczko; all other photos: Zdjęcia: A. Stachurski