Maaskari Wadogo wa Baharini
Maaskari Wadogo wa Baharini
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA
HUENDA wewe huvutiwa na viumbe wakubwa wa baharini kama vile nyangumi, pomboo, na papa. Hata hivyo, baharini kuna “viumbe hai, vidogo kwa vikubwa.” (Zaburi 104:25) Watu wanaochunguza vitu kwa makini huvutiwa pia na viumbe wadogo.
Kwa mfano, kwenye sakafu ya bahari kuna viumbe ambao wamefafanuliwa kuwa “maaskari wa baharini wenye mavazi ya vita.” Tofauti na maaskari wa kale, wengi wa “maaskari” hao wadogo wana mavazi ya vita yaliyo na rangi na maumbo yanayovutia. Viumbe hao wadogo wa baharini ni wa jamii ya krasteshia, nao huitwa uduvi.
Maisha ya Uduvi
Huenda ukaona uduvi kuwa chakula kitamu tu. * Hata hivyo, uduvi hupitia hatua mbalimbali za ukuzi kabla ya kukamatwa na kupikwa. Uduvi fulani wa kike hushikamanisha mayai yao yaliyotungishwa kwenye matumbo yao hadi yanapoanguliwa, huku wengine wakiyaachilia yabebwe na maji na kukomaa yenyewe.
Mayai hayo yanapoanguliwa, viwavi hutokea. Viwavi hivyo hupitia hatua mbalimbali za ukuzi, na hutofautiana sana na uduvi waliokomaa. Viwavi hivyo hukaa kwa muda fulani katikati ya mimea ya baharini na hatimaye hushuka kwenye sakafu ya bahari. Wao huendelea kukua huku umbo lao likibadilika pole kwa pole hadi wanapokomaa.
Kubadilisha Mavazi ya Vita
Kwa kuwa wana gamba gumu, uduvi waliokomaa huwezaje kukua? Kitabu A Field Guide to Crustaceans of Australian Waters kinasema hivi: “Katika hatua hii, . . . utando laini hufanyizwa chini ya gamba la nje. Kisha gamba la nje huondolewa, na kiumbe huyo hufyonza maji na kuvimbisha utando huo ili kufanyiza nafasi kwa ajili ya ukuzi.” Kitabu Australian Seashores kinasema: “Ni lazima kiumbe huyo aondoe mwili wake wote, kutia ndani viungo vyote (ambavyo ni vingi sana), vikubwa na vyenye nguvu, au vidogo na laini, kutoka katika gamba lake la nje lililo kama koa. Kiumbe huyo hutoa viungo vyake nje ya gamba kama vile mtu anavyotoa vidole vyake kwenye glavu.”
Viumbe hao wa baharini hupitishaje viungo vyao vikubwa, kama vile misuli ya kucha, kwenye nafasi ndogo zilizo katikati ya viungo? Mwandishi W. J. Dakin anasema: “Wanaweza kufanya hivyo kwa kuwa viungo vyao vilivyo na uhai ni laini na vinaweza kupitishwa kwenye nafasi ndogo. Katika hatua ya kufanyizwa kwa utando, damu huondolewa kwenye miguu na kupelekwa kwenye viungo vingine mwilini ili viweze kupenyezwa kwa urahisi gamba linapoondolewa.” Gamba jipya huwa na mistari na rangi ya gamba la zamani na kuna sababu nzuri ya kudumisha vitu hivyo.
Rangi Zinazowaficha na Zile Zinazowatambulisha
Uduvi fulani wanaoishi katikati ya minyiri ya viumbe wa baharini wanaoitwa anemone wana magamba yanayopenyeza nuru kwa kiasi fulani au yaliyo na rangi inayofanana na ya anemone. Uduvi hao wenye rangi kama ya anemone hupata ulinzi kwa kujificha kwenye minyiri ya anemone, nao huwasaidia anemone kwa kuondoa takataka zinazorundamana katika miili ya anemone.
Uduvi wengine wana rangi nyangavu. Mfano mmoja ni uduvi ambao hufanya usafi. Kwa kawaida wao huishi chini ya miamba, na ni kana kwamba rangi yao nyangavu huonyesha huduma za usafi wanazotoa. Samaki walio na vimelea huogelea karibu na makao ya uduvi hao na kuwaruhusu watambae juu ya miili yao. Uduvi hao hawaogopi kuingia ndani ya mdomo na mashavu ya samaki. Kisha uduvi hao huondoa na kula vimelea na ute ulio kwenye gamba la samaki.
Hata iwe wana rangi gani au wanafanya kazi gani, jambo moja ni hakika kuhusu viumbe hao wadogo: mavazi yao yanapendeza sana kuliko mavazi ya askari yeyote wa zamani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Wanasayansi fulani hutofautisha uduvi na kamba kwa kutegemea njia zao za kuzalisha na umbo la mifupa yao.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Uduvi aina ya “hingebeak”
[Picha katika ukurasa wa 23]
Uduvi mwenye gamba linalopenyeza nuru
[Picha katika ukurasa wa 23]
Uduvi aina ya “emperor”
[Picha katika ukurasa wa 23]
Uduvi wa “anemone”
[Picha katika ukurasa wa 23]
Uduvi anayefanya kazi ya usafi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
All photos except cleaner shrimp: © J and V Stenhouse