Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matatizo ya Madaktari

Matatizo ya Madaktari

Matatizo ya Madaktari

“Mtu mmoja na mke wake walikuja kuniona wakitumaini kwamba ningemtibu mtoto wao aliyezaliwa majuzi. Nilipomchunguza nilifadhaika. Ugonjwa wake haungeweza kuponywa. Je, unaweza kuwazia jinsi nilivyohisi nilipowajulisha wazazi hao kwamba mwana wao atakuwa kipofu? Nilihuzunika sana walipokuwa wakiondoka ofisini mwangu. Lakini, punde baadaye mgonjwa mwingine akaingia huku akitazamia nimkaribishe kwa uchangamfu! Hilo ndilo hunifadhaisha.”—Mtaalamu wa macho huko Amerika Kusini.

KWA kawaida wagonjwa hawaendi kumwona daktari ili kuyashughulikia matatizo ya daktari. Wagonjwa huhangaikia tu matatizo yao. Kwa hiyo, ni watu wachache sana wanaoelewa matatizo ambayo madaktari wanakabili kila siku.

Ni wazi kwamba kila mtu hukabili mfadhaiko, na si wanatiba tu wanaokabili mfadhaiko. Hata hivyo, kwa sababu watu wengi hushughulika na madaktari kwa njia mbalimbali, ni muhimu kuelewa matatizo ya madaktari na jinsi yanavyowaathiri.

Madaktari huanza kukabili mfadhaiko mapema maishani wanapotafuta nafasi ya kuingia chuo kikuu. Kisha, wanapoanza mafunzo ya tiba, hisia zao huathiriwa sana. Hapo ndipo hisia na utu wa mwanafunzi wa tiba huanza kubadilika.

Mafunzo ya Tiba Huathiri Hisia

Wanafunzi wa tiba wanaweza kwenda kwenye chumba cha upasuaji hata katika juma la kwanza la masomo. Huenda wanafunzi wengi wasiwe wameona maiti. Wanafunzi wengi huchukizwa wanapoona maiti zilizo uchi na zilizokauka zinapopasuliwa ili kuchunguza viungo vya mwili. Inawabidi wanafunzi watafute njia za kukabiliana na hisia zao. Mara nyingi wao hutumia ucheshi kwa kuzipatia maiti majina ya utani. Ijapokuwa watu wengine wanaweza kuudhiwa na jambo hilo, ni lazima wanafunzi wa tiba wafanye hivyo ili wasiifikirie maiti kuwa mtu.

Kisha, wao hupata mafunzo ya tiba katika hospitali. Kabla ya kufikia umri wa makamo, watu wengi huwa hawafikirii kuhusu ufupi wa maisha. Lakini wanafunzi wa tiba hukabili uhakika huo mapema maishani wakati wanapowaona watu walio na magonjwa yasiyoweza kupona na wanapowaona watu wakifa. Mwanafunzi mmoja alisema kwamba alichukizwa sana alipoona mambo hayo kwa mara ya kwanza. Wanafunzi wa nchi tajiri na hata wa nchi maskini wanaweza kushangaa sana kuona wagonjwa wakinyimwa matibabu kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kuyagharimia.

Madaktari wapya hushughulikiaje mfadhaiko? Mara nyingi inawabidi wafanyakazi wa afya waepuke kujihusisha kihisia na wagonjwa kwa kutowaona kuwa watu. Badala ya kumrejelea mgonjwa kuwa mtu, huenda wakasema, “Daktari, kuna mguu uliovunjika katika chumba cha pili.” Hilo linaweza kuchekesha ikiwa huelewi sababu yao ya kusema hivyo.

Kuwahurumia Watu Kunaweza Kuchosha

Ijapokuwa madaktari wamezoezwa kuwa wanasayansi, wengi wao hutumia muda mwingi sana kuzungumza na wagonjwa. Madaktari fulani huona ni vigumu kuwa na uhusiano wa karibu na wagonjwa. Kama ilivyotajwa mwanzoni, mojawapo ya mambo magumu zaidi anayokabili daktari ni kumpasha mtu habari mbaya. Wengine hufanya hivyo kila siku. Watu wenye matatizo huhitaji kueleza jinsi wanavyohisi, na madaktari hawana budi kuwasikiliza. Kuwashughulikia watu walio na wasiwasi kunaweza kuwachosha sana madaktari.

Daktari mmoja huko Kanada aliandika hivi kuhusu miaka yake ya kwanza-kwanza ya udaktari: “Nilikuwa na kazi nyingi sana: nilitumia wakati mwingi kuwasaidia watu wenye uhitaji; watu waliofadhaika walitaka niwasikilize; watu walitaka niwatibu; watu walitumia hila ili wajifaidi; watu walikuja kuniona; watu walinisihi niwatembelee; watu walinipigia simu nyumbani hata nikiwa kitandani. Kila mahali ni watu, watu, watu. Nilitaka kuwasaidia, lakini nililemewa.”—A Doctor’s Dilemma, cha John W. Holland.

Je, madaktari huacha kufadhaika kadiri wakati unavyopita? Madaktari ambao wamefanya kazi kwa miaka mingi huwa na madaraka zaidi. Mara nyingi, maamuzi mazito yanayohusu uhai wa mgonjwa huhitaji kufanywa papo hapo, na nyakati nyingine yanafanywa bila kuwa na habari kamili. Daktari mmoja wa Uingereza anasema hivi: “Nilipokuwa kijana, sikujali maamuzi niliyofanya, kama vile vijana wasivyojali wanapoendesha gari ovyoovyo. Lakini mtu huthamini uhai zaidi kadiri anavyozidi kuzeeka. Siku hizi, mimi huwa mwangalifu sana ninapofanya maamuzi ya kitiba.”

Mfadhaiko huwaathirije madaktari? Tabia ya madaktari ya kutojihusisha kihisia na wagonjwa inaweza kuathiri uhusiano wao na familia zao. Ni vigumu kuepuka tabia hiyo. Madaktari fulani huonyesha huruma nyingi wanapowasaidia wagonjwa kukabiliana na hisia zao. Lakini wanaweza kufanya hivyo kwa kadiri gani bila kuchoka? Hilo ni tatizo kubwa linalowakabili madaktari.

Wagonjwa Wenye Vichwa Vigumu

Mara nyingi madaktari wanapoulizwa jambo linalowafadhaisha zaidi wanaposhughulika na wagonjwa, wao husema kwamba wanahangaishwa hasa na wagonjwa wenye vichwa vigumu. Labda unafahamu wagonjwa wenye sifa zifuatazo.

Kwanza, kuna wagonjwa ambao humpotezea daktari wakati kwa kusema mambo mengi yasiyo na maana bila kueleza matatizo yao. Kisha, kuna wagonjwa ambao humpigia daktari simu usiku au mwishoni mwa juma ijapokuwa hakuna jambo la dharura, au husisitiza wapewe matibabu ambayo daktari hataki kuyapendekeza. Pia, kuna wagonjwa ambao hawamwamini daktari. Wagonjwa fulani hutafuta habari muhimu kuhusu ugonjwa wao katika Intaneti na vyombo vingine, na hilo linaweza kuwasaidia. Hata hivyo, utafiti wao unaweza kuwafanya wamtilie shaka daktari. Huenda daktari asiwe na wakati wa kutosha kueleza faida zote na madhara yote ya matibabu yanayopendekezwa katika utafiti huo. Madaktari hufadhaika sana wagonjwa wanapokataa kufuata maagizo yao kwa sababu ya kutowaamini. Hatimaye, kuna wagonjwa wasio na subira. Wagonjwa hao huacha kutumia dawa kabla hawajapona, kisha wanatafuta matibabu kwingineko.

Katika maeneo mengine, tatizo kubwa ambalo madaktari wanakabili ni kushughulika na mawakili.

Madaktari Wenye Tahadhari

Katika nchi nyingi, kesi zinazowasilishwa mahakamani dhidi ya madaktari zinaongezeka. Mawakili fulani huwasilisha mashtaka madogo-madogo ili wajitajirishe. Msimamizi wa Chama cha Kitiba cha Marekani alisema kwamba kesi hizo “zinafanya bima za madaktari zigharimu pesa nyingi sana.” Anaongeza hivi: “Kesi hizo husababisha mahangaiko mengine. Shtaka la uwongo linaweza kumwathiri sana daktari kwa kumwaibisha, kumpotezea wakati, . . . kumfadhaisha, na kumtia wasiwasi.” Madaktari fulani wamejiua kwa sababu hiyo.

Hivyo, madaktari fulani hufanya maamuzi kwa kufikiria jinsi watakavyojitetea mahakamani badala ya kujali masilahi ya mgonjwa. Gazeti Physician’s News Digest linasema: “Leo madaktari wengi huwatibu wagonjwa kwa uangalifu sana ili wasishtakiwe.”

Madaktari wanapozidi kukabili hali ngumu, wengi wao hujiuliza jinsi siku za usoni zitakavyokuwa. Wagonjwa wengi pia hujiuliza swali hilo wanapoona magonjwa fulani yakizidi licha ya maendeleo ya kitiba. Makala inayofuata inawapa madaktari na wagonjwa tumaini zuri la wakati ujao.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

KUSHIRIKIANA NA DAKTARI

1. Ili usipoteze wakati, panga mapema jinsi utakavyomweleza daktari tatizo lako kwa ukamili na uanze na mambo muhimu

2. Ikiwa hakuna jambo la dharura, usimpigie simu daktari wakati ambapo hayuko kazini

3. Uwe na subira. Uchunguzi kamili na matibabu yanayofaa huchukua muda mrefu

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

‘KUTIBU MAGONJWA YA KAWAIDA HURIDHISHA’

“Kazi ya udaktari huku hutofautiana sana na ile ya madaktari katika maeneo yaliyoendelea. Huku, watu huona kwamba wakijifunza kazi fulani wataepuka umaskini, hivyo wengi husomea udaktari. Lakini, madaktari ni wengi na nafasi za kazi ni chache. Hivyo, madaktari hupata mshahara mdogo sana. Ni wagonjwa wachache tu wanaoweza kugharimia matibabu katika hospitali za kibinafsi. Ninafanya kazi katika hospitali iliyojengwa zamani. Paa yake inavuja na ina vifaa duni. Kuna madaktari wawili na wauguzi watano. Tunawahudumia watu 14,000.

“Nyakati nyingine wagonjwa hufikiri kwamba siwachunguzi vya kutosha, lakini huwezi kumchunguza mgonjwa mmoja kwa muda mrefu ikiwa wagonjwa wengine 25 wanataka kuhudumiwa. Hata hivyo, mimi huridhika ninapowatibu wagonjwa, hata wale wenye magonjwa ya kawaida tu. Kwa mfano, akina mama huwaleta watoto wao ambao wamekuwa wagonjwa kwa sababu ya kukosa chakula cha kutosha, kukosa maji mwilini, na kuendesha. Watoto hao huwa na macho makavu na sura isiyopendeza. Mimi huwaeleza akina mama jinsi ya kutumia maji yenye chumvi, dawa za minyoo, na dawa za kuua viini. Matibabu hayo yakifanikiwa, mtoto huanza kula tena. Juma moja baadaye, mtoto huonekana tofauti—akiwa na macho maangavu, akitabasamu, na kuchezacheza. Nilitaka kuwa daktari ili nifurahie kuwasaidia watu kwa njia kama hizo.

“Nilitamani kuwatibu wagonjwa tangu nilipokuwa mdogo. Hata hivyo, masomo ya tiba yalibadili kabisa maoni yangu. Niliwaona watu wakifa kwa kukosa kiasi kidogo sana cha pesa walizohitaji ili watibiwe na kuendelea kuishi. Ilinibidi kuwa sugu ili nisihuzunishwe na hali hiyo. Nilianza kuwa na huruma tena nilipoonyeshwa katika Biblia sababu inayofanya watu wateseke na kufahamu kwamba Mungu ana huruma. Siku hizi, ninaweza kulia.”

[Picha]

Dakt. Marco Villegas anafanya kazi katika mji fulani wa Amazonia huko Bolivia