Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Corcovado Mbuga Inayovutia ya Kosta Rika

Corcovado Mbuga Inayovutia ya Kosta Rika

Corcovado Mbuga Inayovutia ya Kosta Rika

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Kosta Rika

MBUGA ya Kitaifa ya Corcovado inavutia sana. Iko katika Rasi ya Osa, kwenye pwani ya kusini ya Bahari ya Pasifiki katika nchi ya Kosta Rika iliyoko Amerika ya Kati. Mbuga ya Corcovado inapendeza kwa kuwa ina msitu wa mvua, inapatikana katika mahali patulivu, na ina jamii nyingi za miti, wadudu, wanyama wanaotambaa, na wale wanaonyonyesha.

Ijapokuwa mbuga hiyo ni maridadi, inapatikana mbali na makazi ya watu. Iko katika mojawapo ya misitu mikubwa zaidi ya mvua katika Amerika ya Kati. Huko hakuna mikahawa mingi, hoteli, na maduka mengi ya kuuza zawadi. Mbali na vituo vya wafanyakazi wa mbuga hiyo na vijia vya kutembea, ambavyo vinafafanuliwa na kitabu kimoja kuwa vijia bora zaidi katika mbuga iliyo na msitu wa mvua, hutaona dalili zozote za kuwapo kwa wanadamu.

Msitu Wafanywa Kuwa Mbuga

Mapema katika miaka ya 1970, pendekezo la kufanya msitu huo wa mvua kuwa mbuga ya kitaifa lilifikiriwa kwa uzito. Hata hivyo, jambo hilo halikuwa rahisi. Mradi huo ungehitaji wafanyakazi wengi na pesa nyingi. Katikati ya miaka ya 1970, iliripotiwa kwamba watu walikuwa wakihamia eneo hilo. Isitoshe, kampuni moja ya kukata miti iliyokuwa ikimiliki maeneo makubwa ya ardhi katika msitu huo, ilipanga kuanza kukata miti kwa wingi, na wawindaji wengi sana waliwinda wanyama huko.

Hata hivyo, wanasayansi na wanabiolojia kutoka ulimwenguni pote ambao walitambua umuhimu wa kuhifadhi msitu huo wa mvua waliingilia jambo hilo. Mnamo Oktoba 31, 1975, serikali ya Kosta Rika ilitangaza kuanzishwa kwa Mbuga ya Kitaifa ya Corcovado. Tangu hapo, msitu huo umeacha kuharibiwa na wakataji wa miti na wawindaji.

Vitu Vinavyopatikana Corcovado

Mbuga ya Corcovado yenye ukubwa wa ekari 133,000 ina viumbe na mimea mingi. Kuna mifumo minane hivi ya ikolojia katika mbuga hiyo. Mifumo hiyo ina angalau jamii 500 za miti. Mti mkubwa zaidi katika mbuga hiyo ni msufi. Mti huo una kipenyo cha zaidi ya meta 3 na urefu wa zaidi ya meta 70.

Je, unapenda kutazama ndege? Bila shaka utafurahia kuona jamii 400 hivi za ndege wanaopatikana Corcovado. Mbuga hiyo ina idadi kubwa zaidi ya ndege wa scarlet macaw nchini humo. Ndege hao wanaporuka, rangi zao zinazopendeza huvutia sana wanapopigwa na mwangaza wa jua.

Huenda ungependa kuona viumbe wa ardhini. Basi usitie shaka kwani mbuga hiyo ina viumbe wengi wadogo. Mbuga ya Corcovado ina jamii 116 za amfibia na wanyama wanaotambaa, kutia ndani nyoka aina ya fer-de-lance. Usimtazame sana nyoka huyo mwenye sumu wala usimkaribie kwani ni mkali sana! Kati ya amfibia wanaopatikana huko, kuna chura aliye na ngozi inayopenyeza nuru, ambaye ukimweka juu ya kipande cha glasi, unaweza kuona viungo vyake vya ndani!

Unaweza pia kutazama jamii 140 za wanyama wanaonyonyesha zinazopatikana huko Corcovado. Wanatia ndani jaguar, ocelot, aina nne za tumbili, aina tatu za wanyama wanaokula mchwa, aina mbili za sloth, na aina mbili za armadillo. Pia mbuga hiyo ina jamii 10,000 hivi za wadudu.

Shirley Ramirez Carvajal, ambaye ni mwanabiolojia na msimamizi wa mradi wa kuhifadhi wanyama wa pori katika mbuga ya Corcovado, alimweleza mwandishi wa Amkeni! kuhusu mpango wa kufungilia vifaa vya mawasiliano kwenye shingo za jaguar na wanyama wengine. Vifaa hivyo vitawawezesha wanasayansi kuchunguza mazoea yao ya kula na ukubwa wa makao yao. Habari hizo zitawawezesha wasimamizi wa mbuga kuamua ikiwa mipaka ya mbuga hiyo inahitaji kupanuliwa ili wanyama wapate chakula cha kutosha. Kupanua mipaka ya mbuga hiyo kutawazuia wanyama wasipate kasoro za urithi zinazotokana na kuzalisha viumbe wa jamii ileile ambao huishi karibu-karibu kwa muda mrefu.

Zaidi ya wanyama wengi wa pori, kuna vitu vingine vinavyovutia huko Corcovado. Unaweza kutembelea Pango la Salsipuedes, ambalo linajulikana sana kwa sababu baadhi ya hazina za baharia na mvumbuzi Mwingereza Sir Francis Drake zilihifadhiwa huko. Kilometa chache tu kaskazini mwa Corcovado kuna Ghuba ya Drake, ambako inasemekana mvumbuzi huyo alitua katika mwaka wa 1579 alipokuwa katika safari yake ya kuzunguka dunia.

Wakati mmoja eneo hilo lilikuwa hatarini kwa sababu watu walitamani kupata dhahabu. Harakati za kutafuta dhahabu zilianza katika miaka ya 1930, wakati vipande vya dhahabu vya uzani wa kilo moja hivi vilipopatikana. Baadaye, katika miaka ya 1960, harakati za kutafuta dhahabu zilianza tena, na miaka michache baada ya mbuga hiyo kuanzishwa harakati hizo zikaendelea. Katika kisa hicho cha mwisho, mamia ya wachimbaji walihamia eneo hilo. Katika mwaka wa 1986, serikali ilipiga marufuku wachimbaji wa migodi huko Corcovado.

Sawa na maeneo mengine, eneo la Corcovado linakabili matatizo. Mwandishi wa Amkeni! alizungumza na Gerardo A. Chaves, ambaye ni naibu-msimamizi wa Mbuga ya Kitaifa ya Corcovado. Gerardo alisema kwamba mbali na matatizo ya pesa, ukosefu wa wafanyakazi na vifaa, mbuga hiyo inakabili matatizo mengine kama vile kukatwa kwa miti iliyo nje ya mbuga na uwindaji haramu. Ili eneo la Corcovado liendelee kusitawi, ni lazima matatizo hayo yashughulikiwe haraka.

Bila shaka, Mbuga ya Kitaifa ya Corcovado ni mojawapo ya maeneo ya dunia ambayo hayajaharibiwa sana. Ama kweli, kama tu almasi inavyovutia kwa sababu ya umaridadi na ugumu wake, mbuga hiyo maridadi ya Kosta Rika itaendelea kuwavutia na kuwapendeza maelfu ya watalii ambao huthamini umaridadi wa asili wa dunia. Mbuga hiyo huwakumbusha Wakristo jinsi dunia nzima itakavyokuwa maridadi wakati ambapo Mungu ataifanya kuwa paradiso!—Luka 23:43.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mbuga ya Kitaifa ya Corcovado

[Picha katika ukurasa wa 15]

Msitu wa mvua

[Hisani]

Steve Pace

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kuvu na uyoga

[Hisani]

©kevinschafer.com

[Picha katika ukurasa wa 16]

Msitu wa mvua unafika ufuoni

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Chura

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mtalii akiwa chini ya poromoko la maji

[Picha katika ukurasa wa 17]

Tumbili

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Ocelot”

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Motmot”

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Sloth”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ndege aina ya “scarlet macaw”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Beach: Barbara Magnuson/Larry Kimball; frog: © Michael and Patricia Fogden; waterfall: ©kevinschafer.com; all other photos: Steve Pace