Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukumbwa na Mfadhaiko!

Kukumbwa na Mfadhaiko!

Kukumbwa na Mfadhaiko!

“TATIZO Kubwa Zaidi la Afya Nchini Marekani.” Hicho ndicho kichwa cha makala moja iliyochapishwa na Taasisi ya Mfadhaiko ya Marekani, ambayo ilisema kwamba sasa tatizo kubwa zaidi la afya si kansa wala UKIMWI. Makala hiyo ilisema hivi: “Imekadiriwa kwamba asilimia 75-90 ya mara ambazo watu huenda hospitali huwa ni kwa sababu ya mfadhaiko.”

Hatutii chumvi tunaposema kwamba watu wanakumbwa na mfadhaiko. Kulingana na shirika moja la Marekani, “kisababishi kikuu cha mfadhaiko miongoni mwa watu wazima ni kazi (asilimia 39), na kisababishi cha pili ni familia (asilimia 30). Visababishi vingine vya mfadhaiko vinatia ndani afya (asilimia 10), mahangaiko kuhusu uchumi (asilimia 9), na mahangaiko kuhusu mizozo ya kimataifa na ugaidi (asilimia 4).”

Mfadhaiko haulemei Marekani tu. Katika uchunguzi uliofanywa huko Uingereza mwaka wa 2002, ilikadiriwa kwamba “katika mwaka wa 2001 na 2002, zaidi ya watu nusu milioni nchini Uingereza walifadhaishwa sana na kazi kiasi cha kuwa wagonjwa.” Inakadiriwa kwamba “siku za kazi milioni kumi na tatu na nusu hupotea kila mwaka nchini Uingereza” kwa sababu ya “mfadhaiko unaosababishwa na kazi, kushuka moyo, au mahangaiko.”

Nchi nyingine za Ulaya zinakumbwa pia na hali hiyo. Kulingana na Shirika la Ulaya la Usalama na Afya Kazini, “mamilioni ya watu wanaofanya kazi tofauti-tofauti huko Ulaya wamefadhaishwa na kazi.” Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba “kila mwaka wafanyakazi milioni 41 hivi [katika Muungano wa Ulaya] hufadhaishwa na kazi.”

Vipi juu ya Asia? Ripoti moja iliyotolewa na kongamano lililofanywa huko Tokyo inasema: “Mfadhaiko unaosababishwa na kazi huathiri sana nchi nyingi ulimwenguni, ziwe ni nchi zinazoendelea au zilizoendelea.” Ripoti hiyo ilisema kwamba “nchi kadhaa katika Asia Mashariki, kama vile China, Korea na Taiwan, zimesitawi haraka kiviwanda na kiuchumi. Sasa nchi hizo zinahangaikia sana mfadhaiko unaosababishwa na kazi na jinsi unavyoathiri sana afya ya wafanyakazi.”

Ama kweli, huhitaji kusoma ripoti hizo za utafiti ili utambue kwamba watu wanakumbwa na mfadhaiko. Yaelekea kwamba wewe pia unakumbwa na mfadhaiko! Mfadhaiko unaweza kukuathirije wewe na wapendwa wako? Familia zinawezaje kujua jinsi ya kukabiliana na mfadhaiko? Makala zinazofuata zitazungumzia mambo hayo.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Watu wengi hufadhaishwa hasa na kazi