Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Tekinolojia Huzuia Mazungumzo
Gazeti The Times la London liliripoti hivi: “Waingereza wengi huogopa kuzungumza ana kwa ana na watu wengine kwa sababu ya kutumia sana vifaa vipya vya tekinolojia.” Uchunguzi uliohusisha watu wazima 1,000, ambao ulifanywa na shirika la British Gas, ulionyesha kwamba mtu mmoja “hutumia vifaa vya tekinolojia vilivyokusudiwa kuwawezesha watu kuwa na wakati mwingi zaidi,” kwa muda wa saa nne hivi kila siku. Kulingana na ripoti hiyo, “kila siku Mwingereza mmoja hutumia dakika 88 akipiga simu ya waya, dakika 62 akipiga simu ya mkononi, dakika 53 akiandika barua-pepe na dakika 22 akituma ujumbe mfupi wa simu.” Uchunguzi huo ulikata kauli kwamba uwezo wa watu wa kuwasiliana ana kwa ana unaathiriwa. Watu wengi waliohusishwa katika uchunguzi huo walikubali kwamba wao hutuma ujumbe mfupi “ili kuokoa wakati au kuepuka mazungumzo.”
Zoea Linalosababisha Hasara
Profesa Kari Reijula wa Taasisi ya Afya ya Wafanyakazi ya Ufini alisema kwamba uvutaji wa sigara huwasababishia hasara wavutaji, waajiri, na watu wasiovuta sigara. Kituo cha Intaneti cha Shirika la Utangazaji la Ufini kinaripoti kwamba wakati wa kazi unaopotezwa watu wanapovuta sigara “husababisha hasara ya dola milioni 21 kila mwaka kwa uchumi wa taifa.” Inakadiriwa kwamba “wafanyakazi wanaovuta pakiti nzima ya sigara kwa siku hukosa kufika kazini siku 17 kila mwaka.” Kukosa kufika kazini kwa sababu ya ugonjwa huongeza hasara hiyo. Reijula anasema hivi pia: “Uchunguzi unaonyesha kwamba wafanyakazi wanaovuta sigara husababisha misiba mara nyingi.” Pia ripoti hiyo inasema kwamba uvutaji wa sigara huongeza gharama za kufanya usafi na za umeme, “kwani nishati nyingi inahitajiwa ili kuendesha mfumo wa kusafisha hewa.” Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba “watu 250 hivi nchini Ufini ambao hawavuti sigara hufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na kuvuta hewa iliyo na moshi wa sigara wanapokuwa kazini au kwingineko.”
Dawa za Kulevya Zinapatikana kwa Urahisi
Gazeti Wprost linaripoti kwamba huko Poland ni rahisi kupata dawa za kulevya kuliko pombe. “Zinapatikana katika disko zote; vilabu, baa, na vyumba vya kulala; na kwenye vyuo na shule za sekondari.” Isitoshe, katika miji mikubwa, mtu anaweza “kuagiza [dawa za kulevya] kwa kupiga simu na kuzipata haraka sana.” Kulingana na gazeti Wprost, zaidi ya nusu ya vijana wa Poland wametumia dawa hizo “angalau mara moja” kwa sababu zinauzwa kwa bei ya chini, zinapatikana kwa wingi, na watu hufikiri kwamba “dawa zisizotokezwa kiasili hazidhuru.” Kulingana na Katarzyna Puławska-Popielarz, msimamizi wa kituo kimoja cha kuwarekebisha vijana, kutumia kwa muda mrefu dawa ya kulevya inayoitwa speed kumesababisha “visa vya kujiua, ugonjwa wa moyo, kuchanganyikiwa, na kukonda sana.”
Misa ya Kilatini Yaanza Tena
Gazeti Focus linasema kwamba huko Ujerumani “watu wengi wanazidi kupenda misa inayoendeshwa katika Kilatini.” Gazeti hilo linasema kwamba makasisi katika “majiji kama vile Frankfurt, Düsseldorf, na Münster wametambua kwamba ingawa hudhurio linazidi kupungua, watu wengi huhudhuria wakati misa inapoendeshwa katika Kilatini.” Kwa kuwa watu wengi wanapenda Misa ya Kilatini, kanisa moja huko Munich liliongeza idadi ya Misa zinazoendeshwa katika Kilatini kutoka mara mbili kwa mwezi hadi mara mbili kwa juma, kutia ndani wakati wa sikukuu.
Karne ya Vita
Gazeti Buenos Aires Herald linaripoti kwamba “mauaji ya jamii nzima-nzima yamefanya karne ya 20 iwe karne ya umwagaji damu mkubwa zaidi katika historia.” Mauaji hayo huhusisha uangamizaji uliopangwa wa taifa zima, kikundi cha kisiasa, kikundi cha kijamii, au cha watu wa rangi fulani. Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni 41 waliuawa katika karne ya 20. Mfano mmoja wa hivi majuzi ni Rwanda, ambako katika mwaka wa 1994 watu wapatao 800,000 waliuawa, hasa na “raia waliochochewa na propaganda za chuki.” Wasomi wanasema kwamba katika kipindi cha siku 100, watu 8,000 hivi waliuawa kila siku. Kulingana na gazeti Herald, kiwango hicho “kinazidi mara tano kile cha mauaji yaliyofanywa na Wanazi katika vyumba vya gesi zenye sumu wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu.”
Jinsi Mamba Wanavyowinda
Mwanafunzi wa shahada ya tatu katika Chuo Kikuu cha Maryland amegundua jambo ambalo limekuwa likiwatatanisha wataalamu. Aligundua viungo vinavyohisi shinikizo kwenye pua la mamba, ambavyo huwawezesha mamba kugundua viumbe wanaosonga majini. Mamba na viumbe wengine wa jamii hiyo wana uvimbe mdogo kwenye mataya ambao unafanana na madoa madogo. Mwanabiolojia Daphne Soares aligundua kwamba uvimbe huo ni viungo vidogo vinavyohisi shinikizo ambavyo huwawezesha mamba kutambua maji yanapotibuliwa kidogo. Soares anasema hivi: “Viumbe wa jamii ya mamba huwinda usiku wakiwa wameingia ndani ya maji huku wakisubiri viumbe wengine watibue maji. Wao huweka mataya yao juu ya uso wa maji. Wanapokuwa na njaa, wao hushambulia haraka kitu chochote kinachotibua maji.” Viungo hivyo hata vinaweza kuhisi tone la maji linapoanguka juu ya uso wa maji.
Viumbe Wanakula Takataka
Uchunguzi wa kimataifa kuhusu jinsi takataka zinavyoathiri viumbe wa majini ulionyesha kwamba kwa wastani ndege mmoja anayeitwa fulmar, anayepatikana katika Bahari ya Kaskazini, ana vipande 30 vya plastiki tumboni. Gazeti The Guardian la London linaripoti kwamba idadi hiyo “inazidi kwa mara mbili idadi ya plastiki zilizopatikana katika ndege wa fulmar mapema katika miaka ya 1980.” Ndege hao walichunguzwa kwa sababu “wao hula chochote wanachopata nao hawatapiki.” Vitu vya plastiki vilivyopatikana katika matumbo ya ndege wa fulmar waliokufa vilitia ndani vitu vya kuchezea, vifaa vya kazi, kamba, vikombe, mito, chupa, na vifaa vya kuwashia sigara. Dakt. Dan Barlow, msimamizi wa utafiti kwenye Shirika la Friends of the Earth Scotland, anasema: “Kutokana na utafiti huo, tunatambua kwamba viumbe wa majini katika pwani ya Scotland hula takataka.” Gazeti hilo linaongeza hivi: “Zaidi ya jamii 100 kati ya jamii 300 za ndege wa baharini wanaopatikana ulimwenguni hula takataka bila kujua.”
Kutumia Lugha ya Ishara Kwenye Intaneti
Kwa miaka mingi, viziwi wametumia vifaa vya kupiga chapa ili kuwasiliana na marafiki wao na hivi majuzi wameanza kutumia barua-pepe. Sasa, kamera za kompyuta za Intaneti zinawawezesha viziwi kutumia lugha ya ishara kwenye Intaneti. Hata hivyo, kulingana na gazeti National Post la Kanada, “kamera za kompyuta za Intaneti huonyesha pande mbili tu za picha na hivyo mtu hawezi kuona mambo yote, sawa na asivyoweza kumwona mwenzake akiinua nyusi za jicho au akitabasamu wakati anapozungumza kwa simu.” Ni vigumu kuwasiliana kwa njia hiyo kwani habari hupitishwa polepole kwenye Intaneti na pia kuna matatizo mengine ya mitambo. Viziwi hukabilianaje na matatizo hayo? Gazeti Post linasema kwamba watu wanaotumia lugha ya ishara hutoa ishara polepole na kuzirudia nao wamejifunza “kubadili ishara zao ili washinde tatizo la ishara kutoonekana vizuri.” Wanaotumia lugha ya ishara wamegundua kwamba wanapoleta mikono yao karibu na kamera, hiyo huonekana kuwa mikubwa na hivyo wanaweza kukazia mambo wanayosema.