“Nafikiri Wewe Ndiwe Dakt. Livingstone”
“Nafikiri Wewe Ndiwe Dakt. Livingstone”
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Tanzania
“Katika Novemba 10, 1871, Henry M. Stanley alikutana na David Livingstone, chini ya mwembe uliokuwa hapa.”—Bamba kwenye Nguzo ya Ukumbusho wa Livingstone huko Ujiji katika Ziwa Tanganyika, Tanzania.
NI ZAIDI ya karne moja tangu Stanley aliposema maneno haya maarufu: “Nafikiri wewe ndiwe Dakt. Livingstone.” Hata hivyo, ni watu wachache tu wanaoishi nje ya Tanzania ambao wanajua umuhimu wa tukio hilo.
Hivyo, huenda ukajifunza mengi kwa kutembelea Jumba la Ukumbusho la Livingstone nchini Tanzania. Bw. Mbingo, ambaye anatutembeza, anatukaribisha kwa shauku. Anatueleza hivi: “Mahali ambapo nguzo ile imesimamishwa palikuwa na mwembe mkubwa, na Stanley alikutana na Livingstone chini ya mwembe huo.” Sasa kuna miembe miwili mikubwa mahali hapo. Anaendelea kusema hivi: “Katika miaka ya 1920, mwembe wa awali ulianza kunyauka. Jitihada za kuuokoa hazikufanikiwa. Hivyo, miti mingine miwili ilipandwa kando ya nguzo hiyo.”
Livingstone Alikuwa Nani?
Tukiwa tumeketi chini ya mmoja wa miembe hiyo, Bw. Mbingo anatueleza kwamba David Livingstone alizaliwa mwaka wa 1813, katika mji mdogo unaoitwa Blantyre, huko Scotland. “Ijapokuwa alilelewa katika umaskini, alifanya kazi ili kugharimia masomo yake na alisomea kazi ya udaktari na umishonari.” Tunafahamishwa kwamba Shirika la Wamishonari la London lilimtuma Livingstone Afrika, naye akaishi Afrika kwa miaka 30 na kupata umaarufu kwa kuwa mvumbuzi na mmishonari.
Yule anayetutembeza anatuambia kwamba “Dakt. Livingstone alikuja Afrika mara tatu. Kwanza alienda Afrika Kusini katika mwaka wa 1841. Katika mwaka wa 1845, Livingstone alimwoa mwanamke aliyeitwa Mary Moffat, ambaye alikuwa binti ya mmishonari mwenzake Robert Moffat.” Livingstone na Mary walipata watoto wanne. Ijapokuwa mara nyingi Mary aliandamana na Livingstone katika safari zake, tamaa ya Livingstone ya kuvumbua mambo ilimfanya asitumie wakati mwingi na familia yake. Katika mwaka wa 1862, Mary Livingstone alikufa kutokana na malaria alipokuwa safarini pamoja na mume wake.
Kitabu The New Encyclopædia Britannica kinasema hivi: “Livingstone alikuwa tayari kueneza Ukristo, biashara, na ustaarabu—mambo matatu ambayo alisadiki yangefanya watu kutoka maeneo mengine waje Afrika—kuelekea kaskazini, kuanzia Afrika Kusini hadi katikati mwa bara hilo. Katika mwaka wa 1853, Livingstone alitoa taarifa hii iliyoonyesha waziwazi nia yake: ‘Nitafungua njia ya kuingia maeneo ya ndani ya Afrika, au nitakufa.’” Hivyo, Livingstone hakusafiri ili kueneza injili tu. Alitetea sana jitihada za kumaliza biashara ya watumwa. Isitoshe, uvumbuzi ulimvutia sana hivi kwamba akaweka mradi
wa kuvumbua chanzo cha Mto Nile.Hata hivyo, baadaye Livingstone alitambua kwamba hangeweza kutimiza mradi huo akiwa peke yake. Katika mwaka wa 1857, aliwaambia vijana fulani katika Chuo Kikuu cha Cambridge hivi: “Ninajua kwamba baada ya miaka michache nitakufa katika nchi hiyo, ambayo iko wazi sasa; msiruhusu ifungike tena! Ninarudi Afrika ili nijaribu kufungua njia ya biashara na Ukristo, [je,] mtaendeleza mradi huu ambao nimeanzisha? Nawaachia mradi huo.”
Hata hivyo, Livingstone alisafiri sana katikati mwa Afrika. Alivumbua mambo mbalimbali kutia ndani maporomoko makubwa ya Mto Zambezi, na kuyaita Maporomoko ya Victoria kutokana na jina la Malkia Victoria. Muda fulani baadaye alisema kwamba ‘kitu kilichomvutia zaidi Afrika ni maporomoko hayo.’
Kumtafuta Livingstone
Yule anayetutembeza anatuambia kwamba “Livingstone alianza safari yake ya mwisho katika mwaka wa 1866. Hata hivyo, mgogoro ulitokea kati ya waandamani wake. Baadhi yao walimwacha na kurudi Zanzibar, ambako walieneza uvumi kwamba Livingstone amekufa. Lakini Livingstone aliendelea na jitihada zake. Alianzisha kituo cha safari zake za uvumbuzi huko Ujiji katika ufuo wa mashariki wa Ziwa Tanganyika.
“Hata hivyo, kwa kipindi cha miaka mitatu hivi, watu huko Ulaya hawakusikia habari zozote kumhusu Livingstone. Walifikiri kwamba amekufa. Hivyo, mchapishaji wa gazeti New York Herald alimtuma ripota anayeitwa Henry Morton Stanley ili amtafute Livingstone, awe hai au mfu. Kwa wazi, Livingstone hakuwa mfu wala hakuwa amepotea. Lakini alihitaji sana chakula na vitu vingine na alikuwa mgonjwa. Katika Novemba 1871, mmoja wa watumishi wa Livingstone alikimbia kuelekea kwenye nyumba yake huku akisema hivi kwa sauti: ‘Mzungu anakuja! Mzungu anakuja!’”
Stanley alikuwa amemtafuta Livingstone kwa miezi minane hivi. Alisafiri kuja Afrika kupitia India, na hatimaye akafika katika kisiwa cha Zanzibar mnamo Januari 6, 1871. Katika Machi 21, 1871, Stanley na vibarua 200 walianza safari kutoka jiji la Bagamoyo lililo kwenye pwani ya mashariki wakiwa na tani sita za chakula na vitu vingine. Ilikuwa hatari sana kusafiri kilometa 1,500 bila ramani! Mvua kubwa ilifanya mito ifurike. Stanley na wenzake waliugua malaria na magonjwa mengine na pia walichoka sana. Mito yote ya eneo hilo ilikuwa na mamba; Stanley alitazama kwa hofu huku mamba akimburuta na kumuua mmoja wa punda wake waliosalia. Pindi nyingine, Stanley mwenyewe aliponea chupuchupu kutafunwa na mamba! Licha ya magumu hayo yote,
Stanley hakukata tamaa. Alisisimuka aliposikia kwamba mzungu fulani mzee sana anaishi huko Ujiji.Stanley alipokaribia Ujiji, alijitayarisha kukutana na mzee huyo. Kitabu Stanley kilichoandikwa na Richard Hall kinasema hivi: “Stanley alikuwa amekonda na kuchoka, hata hivyo, alihisi kwamba angeweza kuingia mjini akionekana kuwa hodari kuliko [wavumbuzi waliomtangulia].” Bila shaka, hii ingekuwa pindi muhimu sana, naye hangehusika tu bali pia angeirekodi. Wote waliosafiri naye walivalia mavazi bora zaidi waliyokuwa nayo. Stanley alifunga utepe mpya kwenye kofia yake, akavalia suruali safi nyeupe, na kung’arisha viatu vyake kwa rangi.”
Stanley anaelezea mambo yaliyofuata: “Hatimaye safari inafikia mwisho wake . . . Pale nawaona Waarabu fulani wenye kuheshimika; na ninapokaribia, namwona mzungu fulani mzee. . . . Tunavuliana kofia, kisha ninasema, ‘Nafikiri wewe ndiwe Dakt. Livingstone,’ naye anasema ‘Naam.’”
Mambo Yaliyofuata
Mwanzoni Stanley alikusudia kukaa kwa muda wa kutosha ili amhoji Livingstone na kuandika habari kumhusu. Lakini, muda si muda, Livingstone na Stanley wakawa marafiki. Yule anayetutembeza anasema: “Stanley alikaa na Livingstone kwa majuma kadhaa, nao wakalichunguza Ziwa Tanganyika. Stanley alijaribu kumshawishi Livingstone arudi Ulaya, lakini Livingstone alinuia kubaki na kutafuta chanzo cha Nile. Hivyo, mnamo Machi 14, 1872, Stanley na Livingstone waliagana kwa majonzi. Kisha Stanley akasafiri hadi pwani ambako alinunua chakula na vitu vingine na kumtumia Livingstone. Halafu, Stanley akaanza safari yake ya kurudi Ulaya.”
Ni nini kilichompata Livingstone? Yule anayetutembeza anaeleza hivi: “Katika Agosti 1872, Livingstone alianza tena jitihada yake ya kutafuta chanzo cha Mto Nile. Alisafiri kuelekea kusini huko Zambia. Hata hivyo, alikuwa amedhoofishwa sana na uchovu na ugonjwa. Mnamo Mei 1, 1873, alipatikana amekufa. Watumishi wake . . . waliupaka mwili wake dawa ya kuuzuia usioze, na kuzika moyo na matumbo yake katika ardhi ya Afrika. Mwili wa Livingstone ulisafirishwa kilometa 2,000 hivi hadi Bagamoyo, ambako ulipokewa na wamishonari. Mipango ilifanywa ili kuusafirisha mwili huo hadi Zanzibar, kisha kuupeleka Uingereza. Mwili wa Livingstone ulifikishwa London mnamo Aprili 15, 1874, na kuzikwa huko Westminster Abbey siku tatu baadaye. Ilichukua kipindi cha mwaka mzima hivi kufikisha mwili wa Livingstone mahali ambapo ungezikwa.”
Stanley alirudi Afrika ili kuendeleza mradi uliokuwa umeanzishwa na Livingstone. Stanley aliongoza kundi la wavumbuzi kuchunguza maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, na mto mkubwa wa Kongo.
Bila shaka tunavutiwa na ujasiri na azimio la watu kama Livingstone na Stanley. Kichapo Britannica kinasema hivi kumhusu Livingstone: “Uvumbuzi wake kuhusu mambo ya kijiografia, kiteknolojia, kitiba, na kijamii, umewawezesha watu kujua mambo mengi ambayo bado yanafanyiwa utafiti.” Watu hawawaoni Livingstone na Stanley kama mhubiri na ripota, bali huwaona kuwa wavumbuzi. Hata hivyo, jitihada zao ziliwezesha ujuzi wa Biblia uenezwe sana miaka mingi baadaye.
Hivyo, wamishonari ambao ni Mashahidi wa Yehova, wameweza kuwasaidia Waafrika wengi kukubali kweli za Biblia. Ama kweli, huko Ujiji, mahali ambapo Stanley na Livingstone walikutana kwa mara ya kwanza, kazi ya Mashahidi wa Yehova ya kuhubiri kweli za Biblia inajulikana sana hivi kwamba si ajabu kwa wakaaji kusema hivi wanapowaona Mashahidi wa Yehova wakitembelea eneo hilo: “Nafikiri ninyi ni Mashahidi wa Yehova.”
[Ramani katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Ziwa Victoria
Safari za Livingstone
Cape Town
Port Elizabeth
Kuruman
Ziwa Ngami
Linyanti
Luanda
Maporomoko ya Victoria
Quelimane
Msumbiji
Mikindani
Zanzibar
Chitambo
Ziwa Tanganyika
Nyangwe
Ujiji, mahali ambapo wanaume hao wawili walikutana
Safari ya Stanley ya kumtafuta Livingstone katika mwaka wa 1871
Zanzibar
Bagamoyo
Ujiji, mahali ambapo wanaume hao wawili walikutana
[Hisani]
Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
David Livingstone
[Hisani]
Livingstone: From the book Missionary Travels and Researches in South Africa, 1858
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
Henry M. Stanley
[Picha katika ukurasa wa 23]
Maporomoko ya Victoria
[Picha katika ukurasa wa 24]
Shahidi wa Yehova akihubiri kweli za Biblia huko Ujiji