Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Pango la Marumaru

Pango la Marumaru

Pango la Marumaru

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

AKIWA amesimama juu ya “marumaru” yaliyotapakaa katika pango, Mmarekani fulani ambaye ni mtaalamu wa kuchunguza mapango alisema hivi: “Asante sana Mungu, kwa kunipa uhai ili niweze kuona maajabu haya!” Mtaalamu huyu alikuwa ametembelea Pango la Marumaru lenye urefu wa meta 529 na kina cha meta 17 ambalo liko kusini-mashariki mwa Mexico. Mtu akiwa ndani ya pango hilo anaweza kuona miamba iliyo na maumbo mbalimbali yenye kuvutia. Tuliposikia kuhusu pango hilo, tulitaka kuliona.

Pango hilo liko katika shamba la mtu fulani, kwa hiyo ni vema kwamba tulikuwa tunafahamiana na mke wake. Tunapoingia kwenye pango hilo lenye marumaru, tunaona zaidi ya vipande milioni 200 hivi vya marumaru vilivyo kama mipira. Marumaru yamefunika eneo la urefu wa meta 50 hivi na kina cha sentimeta 12. Hakuna anayeweza kujizuia kuchota vito hivyo kwa mkono na kuacha vile vidogo kama dengu vinyiririke kupitia vidole vyake. Vipande vikubwa vya marumaru vinatoshana na chungwa dogo. Unapoondoa vipande hivyo vya marumaru ili uguse sakafu utatambua kwamba imefunikwa kabisa kwa marumaru yaliyoungana vizuri.

Marumaru yanayopatikana katika mapango hufanyizwaje? Maji hutiririka kwa nguvu na kukusanyika kwenye vidimbwi. Maji hayo hufanya kemikali ya calcite iliyo katika paa na kuta za pango igandamane na kufunika vitu kama vile mchanga, vipande vidogo vya mfupa, au hata mirija ya kunywa soda. Kemikali hiyo inapoongezeka, marumaru hutokezwa.

Ingawa wakazi wa eneo hilo wamelifahamu pango hilo kwa muda mrefu, wataalamu kutoka nchi nyingine ambao wamevutiwa na wingi wa marumaru katika pango hilo wamelitembelea hivi majuzi. Kwa sasa, jitihada zinaendelea ili kuchunguza na kuhifadhi pango hili.

Maeneo kama vile Pango hilo la Marumaru hutukumbusha maneno ya Zaburi 111:2: “Kazi za Yehova ni kuu, zinazotafutwa na wale wote wanaopendezwa nazo.”