Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kuna DNA Zisizohitajiwa?

Je, Kuna DNA Zisizohitajiwa?

Je, Kuna DNA Zisizohitajiwa?

WATAFITI wengi hufanya uchunguzi kuhusu biolojia, chembe za urithi, na mambo mengine ya kisayansi kwa kutumia nadharia ya mageuzi. Mara nyingi, hilo limefanya wakate kauli za uwongo. Kwa mfano, wanasayansi wa zamani walioamini nadharia ya Darwin walisema kwamba viungo fulani kama vile kidole cha tumbo (appendix), tezi ya pituitari (pituitary gland), na mafindo (tonsils) havina kazi yoyote mwilini, huku wakidai kwamba ni viungo vilivyosalia baada ya mageuzi. Hata hivyo, baadaye watu walifahamu kazi za viungo hivyo. Hilo liliwalazimu wanamageuzi kubadili kauli zao za awali.

Jambo kama hilo lilitukia hivi majuzi kuhusiana na elimu ya chembe za urithi. Utafiti wa awali ulidokeza kwamba asilimia 98 hivi ya DNA katika mwili wa wanadamu na viumbe wengine haina kazi. Hivyo, watu wengi walioathiriwa na nadharia ya mageuzi walidhania kwamba DNA hizo hazihitajiwi eti kwa sababu ni habari za ziada zilizosalia baada ya mageuzi kukamilika. Watu wengi walikubali maoni hayo haraka.

Kwa mara nyingine tena, wazo lililotegemea nadharia ya Darwin lilithibitishwa kuwa la uwongo. Hivi majuzi, wanasayansi waligundua kwamba DNA hizo hutimiza kazi muhimu mwilini kwa kutokeza aina fulani za RNA (ribonucleic acid) ambazo ni muhimu kwa uhai. John S. Mattick, msimamizi wa Taasisi ya Sayansi ya Molekuli kwenye Chuo Kikuu cha Queensland huko Australia, anasema kwamba kwa kuwa watu wengi walikubali haraka nadharia ya DNA zisizohitajiwa “huo ndio mfano bora zaidi katika miaka 25 iliyopita unaoonyesha jinsi watu hufuata maoni yaliyotia mizizi badala ya kuchunguza mambo ya hakika.” Anaongeza kwamba “huenda hilo likawa mojawapo ya makosa makubwa zaidi katika biolojia ya molekuli.”

Je, si jambo la hekima kukubali kwamba DNA ilitokana na Mbuni mwenye akili? Muda si muda, watu wanaokubali kuwapo kwa Mbuni mwenye akili hupata majibu ya mambo yanayowatatanisha kuhusu uumbaji wa Mungu. Badala ya kuwatamausha, majibu hayo huwafanya wastaajabu hata zaidi.—Methali 1:7; Mhubiri 3:11.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

DNA: Photo: www.comstock.com; researcher: Agricultural Research Service, USDA