Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magumu Ambayo Mama Hukabili

Magumu Ambayo Mama Hukabili

Magumu Ambayo Mama Hukabili

“Kazi za nyumbani ndizo kazi za wanadamu zilizo muhimu zaidi. . . . Mama asipotimiza daraka lake, hakutakuwa na kizazi kingine, au kutakuwa na kizazi kiovu sana hivi kwamba ni afadhali kisiwepo.”—Theodore Roosevelt, rais wa 26 wa Marekani.

NI WAZI kwamba mama ni mtu muhimu maishani mwetu, na daraka lake linahusisha mengi zaidi ya kuzaa watoto. Mwandishi mmoja alisema hivi kuhusu daraka la mama katika sehemu nyingi za ulimwengu: “Yeye ndiye mtunzaji mkuu wa afya, elimu, akili, utu, sifa, na hisia za mtoto.”

Mojawapo ya madaraka mengi ya mama ni kuwafundisha watoto wake. Mtoto hujifunza maneno yake ya kwanza na njia ya kuyatamka kutoka kwa mama yake. Hivyo, lugha ya kwanza ya mtu huitwa lugha ya mama. Kwa kuwa mama hutumia wakati mwingi pamoja na watoto kuliko baba, yeye huwa mwalimu wao mkuu na ndiye hasa anayewatia nidhamu. Hivyo, methali ya Mexico inayosema, “Mtoto hunyonyeshwa elimu” huonyesha jinsi daraka la akina mama lilivyo muhimu.

Pia, Muumba wetu, Yehova Mungu, huwaheshimu akina mama. Kwa hakika, moja kati ya zile Amri Kumi, zilizoandikwa kwenye mabamba ya mawe kwa “kidole cha Mungu,” huwahimiza watoto hivi: “Mheshimu baba yako na mama yako.” (Kutoka 20:12; 31:18; Kumbukumbu la Torati 9:10) Isitoshe, methali moja ya Biblia inataja “sheria ya mama yako.” (Methali 1:8) Watu wengi leo wanatambua umuhimu wa kuwafundisha watoto katika miaka yao mitatu ya kwanza, wakati ambapo watoto wengi bado wanatunzwa na mama zao.

Baadhi ya Magumu

Ni vigumu kwa akina mama wengi kuwafundisha watoto wao katika miaka yao ya mapema kwa sababu wao hulazimika kufanya kazi ili kuruzuku familia. Habari zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba katika nchi nyingi zilizoendelea zaidi ya nusu ya akina mama wenye watoto walio chini ya umri wa miaka mitatu wameajiriwa.

Isitoshe, mama wengi hukabili ugumu wa kuwalea watoto wakiwa peke yao kwa kuwa waume wao huhamia majiji mengine au nchi nyingine ili kutafuta kazi. Kwa mfano, inaripotiwa kwamba katika maeneo fulani ya Armenia, thuluthi moja hivi ya wanaume wamehamia nchi nyingine ili kutafuta kazi. Mama wengine huwalea watoto wakiwa peke yao kwa sababu waume wao wamewaacha au wamekufa.

Pia akina mama katika nchi fulani hukabili tatizo la kutokuwa na elimu. Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Uchumi na Jamii inakadiria kwamba thuluthi mbili ya watu milioni 876 ulimwenguni ambao hawajui kusoma na kuandika ni wanawake. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, zaidi ya asilimia 60 ya wanawake katika Afrika, nchi za Kiarabu, na nchi za Asia Mashariki na Kusini, hawajui kusoma na kuandika. Zaidi ya hayo, wanaume wengi sana wanaamini kwamba haifai kuwaelimisha wanawake na kwamba wakielimishwa hawatastahili kuzaa.

Gazeti Outlook linasema kwamba katika wilaya moja ya jimbo la Kerala nchini India, ambako wasichana hupata watoto wakiwa na umri wa miaka 15, wanaume hawataki kuoa wanawake walioelimishwa. Katika nchi jirani ya Pakistan, wavulana hasa ndio wanaoelimishwa. Hilo huwawezesha wavulana kupata kazi zenye mshahara mkubwa ili wawategemeze wazazi wao wanapozeeka. Kwa upande mwingine, kitabu Women’s Education in Developing Countries kinasema kwamba “wazazi hawatumii pesa zao kuwaelimisha binti zao kwa sababu hawatarajii waifaidi familia kifedha.”

Tatizo lingine ambalo akina mama hukabili ni mila. Kwa mfano, katika nchi fulani mama hutarajiwa kuunga mkono mila zinazohusisha kuwaoza wasichana wakiwa wadogo na kuwapasha tohara. Pia ni mwiko kwa akina mama kuwafundisha na kuwaadhibu wana wao. Je, mama anapaswa kufuata mila hizo na kuacha wana wake wafundishwe na watu wengine?

Katika makala zinazofuata, tutaona jinsi akina mama fulani wanavyokabiliana na magumu hayo. Pia tutaona umuhimu wa akina mama na wa madaraka wanayotimiza, na jinsi tunavyoweza kuwa na maoni yanayofaa kuhusu daraka lao la kuwafundisha watoto wao.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

“Mama hutimiza daraka muhimu katika kuchochea akili, tamaa ya kujifunza, na uwezo wa mtoto wa kubuni mambo.”—Kongamano la Haki za Watoto, Burkina Faso, 1997.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Akina mama huchangia sana afya, elimu, utu, na hisia za mtoto