Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mahali Ambapo Mabara Sita Huungana

Mahali Ambapo Mabara Sita Huungana

Mahali Ambapo Mabara Sita Huungana

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Ukrainia

JE, WEWE hufurahia kuwatazama wanyama wakiwa katika makao yao ya asili? Ikiwa ndivyo, unaweza kufurahia sana kutembelea bara la Afrika, Asia, Australia, Ulaya, Amerika Kaskazini, na la Amerika Kusini kwa wakati uleule. Je, kweli inawezekana? Unaweza kufanya hivyo kwa kutembelea Hifadhi ya Viumbe ya Askaniya-Nova, kusini mwa Ukrainia. Wanyama wa pori kutoka katika mabara sita huishi kwa amani katika hifadhi hiyo.

Hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka wa 1883. Katika mwaka huo, mhamiaji mmoja kutoka Ujerumani aliyeitwa Friedrich Pfalz-Pfein alitenga eneo lisilotumiwa ili liwe hifadhi. Tayari alikuwa amefuga zaidi ya jamii 50 za ndege na wanyama katika eneo hilo. Kisha, katika mwaka wa 1887, bustani ilipandwa katika hifadhi hiyo. Kwa sasa, Hifadhi ya Viumbe ya Askaniya-Nova ina bustani ya mimea, eneo lisilo na miti la zaidi ya ekari 27,000, na eneo la kufugia wanyama.

Kitu cha kwanza utakachoona unapokaribia hifadhi hiyo ni bustani ya mimea. Wanasayansi walipeleka aina tofauti-tofauti za miti kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu katika eneo hilo. Miti hiyo imepandwa katika eneo la ekari 500. Kwa kuwa hifadhi hiyo iko katika eneo kavu la Ukrainia, visima vya maji na mitaro imechimbwa ili kunywesha miti na mimea. Katika mwaka wa 1889, hifadhi hiyo ilitunukiwa medali ya dhahabu katika Maonyesho ya Ulimwengu ya Paris kwa sababu ya mandhari yake ya awali na mfumo wa kunyunyiza maji.

Wanyama Kutoka Mabara Sita

Tunapotoka katika bustani hiyo, tunaelekea kwenye eneo lisilo na miti. Jamii 50 hivi za wanyama huishi huko katika eneo la ekari 6,000 hivi ambalo limezungushiwa ua. Kwanza, acha tuwatazame wanyama fulani kutoka Afrika.

Nyati ndiye mnyama maarufu na hatari zaidi kati ya wanyama wakubwa wa hifadhi hiyo. Mnyama huyo anastaajabisha kwa sababu ya ukubwa wake kwani ana kimo cha meta 1.7 kufikia mabegani, na ana pembe zenye urefu wa meta 1. Si vizuri kuwakaribia nyati-dume kwa kuwa wanaweza kushambulia wakati wowote.

Tunavutiwa pia na pofu, ambaye ni paa kutoka kusini-mashariki mwa Afrika. Kwa kuwa uwindaji hauruhusiwi katika hifadhi hiyo, pofu wameishi kwa amani tangu walipopelekwa huko mwaka wa 1892. Hata wanapotazamwa na wageni, wao huendelea kula bila wasiwasi. Pofu wengine hufugwa na kukamuliwa kama ng’ombe wa maziwa. Maziwa yao yenye lishe huwa na mafuta mengi, na hutumiwa kutibu magonjwa mbalimbali kama vile vidonda vya tumbo.

Emu ni ndege mkubwa asiyeweza kuruka kutoka Australia. Yeye ndiye ndege wa pili kwa ukubwa, kwani mbuni tu ndiye anayemzidi. Emu fulani huwa na kimo cha meta 1.8, nao huwa na uzani wa kilo 59. Ijapokuwa ua limewatenganisha na wanyama, wana nafasi kubwa ya kukimbia huku na huku.

Emu ni ndege wa pekee kwani vifaranga wake huitikia sauti ya emu wa kiume wanapokuwa ndani ya mayai. Kwa mfano, inasemekana kwamba sauti ya emu wa kiume inapochezwa kabla tu ya mayai kuanguliwa, vifaranga walio ndani ya mayai husongasonga na kufanya mayai yatikisike. Hata hivyo, vifaranga wanapokuwa ndani ya mayai hawaitikii sauti ya emu wa kike. Kwa nini?

Ijapokuwa emu wa kike hutaga mayai, emu wa kiume ndiye huyalalia. Yeye huyatunza kwa siku 50 hivi hadi yanapoanguliwa, kisha huwatunza vifaranga. Kwa hiyo, hata kabla ya mayai kuanguliwa, vifaranga hutambua yule anayewatunza. Hayo si mayai ya kawaida kwani yana rangi ya kijani kibichi, ni makubwa sana, na yana uzani wa gramu 700 hivi!

Hifadhi hiyo ina makundi ya farasi wa Przewalski. Katika mwaka wa 1899, farasi hao walitolewa Mongolia na kupelekwa katika hifadhi ya Askaniya-Nova. Inasemekana kwamba farasi hao walitoweka msituni katika miaka ya 1960 kwa sababu ya kuwindwa na kukosa chakula.

Kwa sasa kuna farasi 1,100 hivi wa Przewalski katika hifadhi mbalimbali. Farasi mia moja kati yao wako katika Hifadhi ya Askaniya-Nova. Wanasayansi wanajaribu kuwarudisha wanyama hao msituni. Katika mwaka wa 1992 na 1993, farasi 21 wa Przewalski walipelekwa Mongolia.

Jamii kubwa zaidi ya wanyama katika hifadhi hiyo ni ya mbawala mwenye madoa ambaye alitolewa China na Japani. Watu humwita mbawala mwenye maua kwa sababu ya madoadoa yaliyo mgongoni mwake. Yeye ni mnyama anayependeza kwani ni mwembamba na ana pembe za fahari juu ya kichwa chake kidogo.

Pia unaweza kuwaona mafahali wakubwa wa India wanaoitwa gayal wakila kwa amani. Nyakati nyingine wanyama hao hufugwa. Huko India, mafahali hao hurandaranda peke yao msituni wakati wa mchana, kisha wao hurudi vijijini usiku. Japo hakuna msitu wala kijiji katika Hifadhi ya Askaniya-Nova, mafahali hao hufurahia kuishi na wanyama wengine katika maeneo yenye nyasi.

Nyati wa Amerika, ambaye pia huitwa baisani, anastaajabisha kwani ni mkubwa na mwenye nguvu. Miaka 150 hivi iliyopita, mamilioni ya nyati hao waliishi Amerika Kaskazini, lakini waliwindwa na walikuwa karibu kutoweka. Nyati wa Amerika walio katika hifadhi hiyo ndio wanaopatikana tu Ulaya. Nyati hao hustarehe katika maeneo yenye nyasi wakati wa kiangazi na baridi kali.

Bara la Amerika Kusini linawakilishwa na ndege mkubwa asiyeweza kuruka anayeitwa rhea (au nandu). Ndege huyo anafanana na emu wa Australia, naye ana kimo cha meta 1.5 na uzani wa kilo 50. Sawa na emu wa kiume, ndege wa kiume wa rhea ndiye hulalia mayai. Tofauti ni kwamba emu huwa na mwenzi mmoja tu, lakini rhea huwa na wenzi wengi. Hivyo, huenda rhea watatu hadi watano wa kike wakataga mayai yao ndani ya kiota kimoja.

Mbawala mwekundu na mbawala aina ya roe wanawakilisha Ulaya. Mbawala hao hula nyasi na wanaweza kustahimili baridi na joto. Mbawala hao hupelekwa katika hifadhi mbalimbali za Ulaya na maeneo ya kuwawindia wanyama. Farasi wa Shetland walipelekwa kwenye Hifadhi ya Askaniya-Nova kutoka Ulaya Kaskazini katika mwaka wa 1960. Tangu wakati huo, wameongezeka sana.

Pia kuna makundi ya pundamilia, nyumbu-kusi (paa wakubwa wa Afrika), punda-mwitu wa Asia, na saiga (paa wa Ulaya na Asia), na vilevile aina nyingi sana za ndege. Wanyama wengine huishi nje mwaka mzima, huku wengine wakihamishiwa kwenye mabanda wakati wa baridi kali.

Kutunza Hifadhi Hiyo

Leo, Hifadhi ya Askaniya-Nova ni kituo cha utafiti cha taasisi ya uchunguzi wa sayansi ya Ukrainia. Wafanyakazi wa taasisi hiyo hujitahidi sana kuhifadhi mazingira ya kiasili ya hifadhi hiyo na kuwasaidia wanyama kuzoea mazingira yao mapya. Pia, wanasayansi wanajitahidi kufanya wanyama waliopelekwa huko na wale wasiopatikana kwa wingi wazalishe wanyama bora zaidi.

Hifadhi za kiasili hupatikana katika maeneo mbalimbali duniani. Hifadhi hizo hupatikana Amerika Kaskazini na Amerika Kusini, katika nyika za Afrika, katika Australia, na katika Asia na Ulaya. Hifadhi hizo hutofautiana, na zina mimea na wanyama wa jamii mbalimbali. Kwa kuwa wanyama wanaopatikana katika Hifadhi ya Askaniya-Nova wametoka katika mabara tofauti-tofauti, hilo linaonyesha kwamba viumbe wanaweza kuzoea mazingira mapya na kuishi pamoja kwa amani.

Watu wengi wanatazamia kwa hamu wakati uliotabiriwa na Biblia, ambapo Ufalme wa Mungu utaleta amani kati ya wanadamu na vilevile kati ya jamii za wanyama wanaoishi duniani.—Isaya 11:6-9; Hosea 2:18; Matendo 10:34-35.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Hifadhi ya Viumbe ya Askaniya-Nova

[Picha katika ukurasa wa 15]

Pofu

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nyati

[Picha katika ukurasa wa 15]

Emu

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mbawala mwenye madoa

[Picha katika ukurasa wa 16]

Farasi wa Przewalski

[Picha katika ukurasa wa 16]

Nyati wa Amerika

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Ndege wa aina nyingi hupatikana katika hifadhi hiyo

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Rhea”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mbawala aina ya “roe”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mbawala mwekundu

[Picha katika ukurasa wa 17]

Bustani ya mimea

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Eland and emu: Biosphere Reserve “Askaniya-Nova,” Ukraine; globes: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Deer: Biosphere Reserve “Askaniya-Nova,” Ukraine; globes: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Birds: Biosphere Reserve “Askaniya-Nova,” Ukraine; flowers and park: Olha Dvorna/ Biosphere Reserve “Askaniya-Nova,” Ukraine; globes: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.