Faida za Kutembelea Majumba ya Ukumbusho
Faida za Kutembelea Majumba ya Ukumbusho
JIJI kuu la Marekani, Washington, D.C., huwavutia watalii wengi sana. * Wao huvutiwa na nini? Mojawapo ya vitu vinavyowavutia watu ni Jumba la White House, makao rasmi ya rais yaliyo katika barabara ya 1600 Pennsylvania. Watu zaidi ya milioni moja na nusu hutembelea makao hayo kila mwaka. Watu huruhusiwa kutembea katika vyumba fulani vya White House vilivyopambwa kwa mitindo ya enzi mbalimbali. Vyumba hivyo vina vyombo vya kale vilivyotengenezwa kwa mbao, kauri, na fedha.
Jengo lingine linalovutia ni Capitol. Hicho ndicho kituo cha serikali ya nchi ya Marekani iliyo na raia wapatao milioni 300. Unapotembea katika majumba na vijia vya jengo hilo, utaona sanamu za viongozi maarufu wa kale. Ukiwa makini unaweza kumwona mwanasiasa fulani maarufu. Hata hivyo, si watalii wote wanaovutiwa na majengo hayo. Wengi wao huvutiwa na vituo vya utamaduni vinavyopatikana katika jiji hilo, yaani, majumba ya ukumbusho na ya maonyesho ya sanaa.
Kuna majumba mengi sana ya ukumbusho na ya maonyesho jijini Washington, D.C., hivi kwamba kwa sasa hatuwezi kuyatembelea yote. Mtu anahitaji kukaa katika jiji hilo kwa muda mrefu ili ayatembelee yote. Hebu tuone tunaweza kutembelea majumba mangapi kwa siku chache.
Jumba la Ukumbusho la Pekee
Bila shaka, watalii wengi huvutiwa hasa na Taasisi ya Smithsonian. Kwa nini? Ni kwa sababu taasisi hiyo ina majumba kadhaa ya ukumbusho na vituo vya elimu. Unaweza kuona kwa urahisi Kasri ya Smithsonian iliyo katika National Mall, ambalo ni eneo lenye nyasi na lenye urefu wa kilometa 1.5. Jengo
la Capitol liko mwanzoni mwa eneo hilo huku Nguzo ya Washington ikiwa mwishoni mwake. Ikiwa utasimama kuelekeana na Nguzo ya Washington, unaweza kuona Kasri ya Smithsonian, ambalo ni jengo muhimu la mawe lenye rangi nyekundu lililoko upande wa kushoto wa eneo hilo maarufu.Ni jengo gani lililo muhimu zaidi katika Taasisi ya Smithsonian? Katika enzi hii ya sayansi, jengo muhimu zaidi ni Jumba la Ukumbusho la Kitaifa la Usafiri wa Anga, ambalo kulingana na kitabu kimoja cha wasafiri, “ndilo jumba la ukumbusho linalotembelewa sana ulimwenguni.” Kwa nini watu wengi huvutiwa na jumba hilo? Jumba hilo lina sehemu 23 za maonyesho. Vitu vilivyomo huonyesha mambo yanayosisimua kuhusu historia ya usafiri wa anga. Vitu vingi katika jumba hilo vimening’inizwa darini. Katika sehemu ya maonyesho inayoitwa Milestones of Flight kuna ndege inayoitwa Flyer, ambayo Orville Wright alitumia katika safari yake maarufu ya mwaka wa 1903 huko Kitty Hawk, North Carolina. Karibu nayo, kuna ndege inayoitwa Spirit of St. Louis, ambayo Charles Lindbergh alitengeneza ili ashinde tuzo ya kuwa mtu wa kwanza kuvuka Bahari ya Atlantiki kwa ndege akiwa peke yake katika mwaka wa 1927. Isitoshe, katika jumba hilo la ukumbusho kuna vyombo vya angani vilivyo maarufu ambavyo vimetumiwa karibuni na vilevile mawe yaliyotolewa mwezini.
Je, Pesa Hukuvutia?
Ukitembea hatua chache kutoka katika Jumba la Ukumbusho la Washington utafika kwenye jengo linalovutia maelfu ya raia walio na hamu ya kupashwa habari, na huenda baadhi yao wana vitu vinavyotengenezwa katika jengo hilo, yaani, noti za benki! Hilo ni jengo la Shirika la Kuchora na Kuchapa. Ukitumia dakika 40 kutembea katika jumba hilo utaona jinsi noti huchorwa na kuchapwa. Zaidi ya dola bilioni 140 huchapiwa hapa kila mwaka. Je, serikali huficha habari kuhusu karatasi inayotumiwa kuchapa noti? Noti hutumiwa na umma kwa muda gani? Ni mambo gani hufanywa ili kuzuia uchapaji wa noti bandia? Ukitembelea jengo hilo utapata majibu ya maswali hayo yote.
Kando ya jengo hilo, kuna jengo lingine la pekee linalowavutia watalii wengi kutoka sehemu zote za ulimwengu. Jengo hilo lilifunguliwa katika mwaka wa 1993. Hilo ni Jumba la Ukumbusho la Maangamizi Makubwa la Marekani.
Jumba la Ukumbusho la Maangamizi Makubwa
Jina la jumba hilo, yaani Holocaust, linatokana na neno la Kigiriki linalotumiwa katika Biblia na linalomaanisha toleo zima la kuteketezwa. (Waebrania 10:6) Hata hivyo, kuhusiana na jumba hilo la ukumbusho, neno Holocaust hutumiwa kurejelea “mateso na mauaji ya Wayahudi wa Ulaya yaliyopangwa na kutekelezwa na serikali ya Nazi ya Ujerumani na washiriki wake katika mwaka wa 1933 hadi 1945.” Wayahudi hasa ndio walioshambuliwa, hata hivyo, sera ya serikali ilihusisha kuangamiza makabila mawili ya Wagypsy, yaani Roma na Sinti, kuangamiza wasiojiweza, Wapoland, wafungwa wa vita wa Sovieti, walawiti, Mashahidi wa Yehova, na waasi wa kisiasa.
Huwezi kuvutiwa na chochote uingiapo katika jumba hilo. Kambi za mateso za Nazi zilikusudiwa kuwatisha watu. Jumba hilo la ukumbusho linaonyesha jinsi hali ilivyokuwa katika kambi hizo. Jumba hilo ni jengo refu linalotisha lililojengwa kwa chuma na matofali nalo hufanana na kiwanda. Ukiwa katika Jumba la Ushahidi, ambalo liko kwenye orofa ya kwanza, unaweza kuona paa ya chuma na kioo iliyo juu ya orofa ya tatu. Broshua moja husema kuwa mtu akitazama juu anaweza kufikiri kwamba vitu vilivyomo “vimepindika, vimekunjamana, na kuegemea upande.” Mhandisi wa jumba hilo alitaka watalii wahisi kwamba “kuna kasoro fulani humo.”
Jumba hilo la ukumbusho lina orofa tano, lakini watu hutembelea hasa orofa ya pili, ya tatu, na ya nne. Inapendekezwa uanze matembezi yako kwenye orofa ya nne. Huenda ukachukua saa mbili au tatu kutembea katika jumba hilo na huhitaji kuongozwa na mtu. Kwa kuwa kuna picha za kushtua zinazoonyesha jinsi watu walivyonyanyaswa na kuuawa, inapendekezwa watoto walio chini ya umri wa miaka 11 wasitembelee sehemu inayoitwa Permanent Exhibition. Katika orofa ya kwanza,
kuna eneo lililotengewa watoto ambalo huitwa Hadithi ya Daniel. Linaonyesha jinsi mtoto aliyeishi huko Ujerumani wakati wa utawala wa Nazi alivyoyaona hayo Maangamizi Makubwa.Lifti zinazoenda kwenye orofa ya nne ni kama vyombo baridi vya chuma vinavyotisha. Historia ya Maangamizi Makubwa huonyeshwa kuanzia kwenye orofa hiyo nayo huhusisha “Mashambulizi ya Wanazi” ya mwaka wa 1933 hadi 1939. Ukiwa huko utaona jinsi habari za uwongo ambazo zilienezwa na Wanazi zilivyowaathiri raia wa Ujerumani na kuwaogopesha hasa Wayahudi wa Ujerumani. Kuna nini kwenye orofa ya tatu?
Kwenye orofa hiyo utaona kichwa hiki chenye kushtua, “Final Solution” (“Suluhisho la Mwisho”)—1940-1945. Kitabu kimoja cha kuwaongoza wageni kinasema kwamba sehemu hiyo “inaonyesha makao ya Wayahudi, uhamisho, kazi ngumu, kambi za mateso, na jinsi ‘Suluhisho la Mwisho’ [kuangamizwa kwa Wayahudi na watu wengine] lilivyotekelezwa kwa kutumia njia mbalimbali kama vile vikosi vya wauaji waliosafiri na kambi za vifo.”
Orofa ya pili ina kichwa kinachopendeza, yaani, “Last Chapter” (“Sura ya Mwisho”). Inaonyesha historia ya “uokoaji, upinzani, kuwekwa huru, na jitihada za waokokaji za kuanza upya maisha yao.” Kwenye upande mmoja wa orofa hiyo kuna Kituo cha Kujifunzia cha Wexner, kilicho na jambo fulani linalowapendeza Mashahidi wa Yehova. Kwa kutumia kompyuta watalii wanaweza kuchunguza historia ya baadhi ya Mashahidi walioteswa au kuuawa.
Kwa mfano, unaweza kuchunguza yaliyompata Helene Gotthold, aliyeishi Dortmund, Ujerumani. Mama huyo aliyekuwa na watoto wawili, aliendelea kuhudhuria mikutano ya Kikristo licha ya Wanazi kupiga marufuku mikutano hiyo. Aliuawa kwa kukatwa kichwa mnamo Desemba 1944. Unaweza kuchunguza masimulizi ya watu wengine wengi ambao walinyanyaswa na kuuawa katika kambi za mateso.
Vilevile katika orofa hiyo kuna Tower of Life (Mnara wa Uhai) ambao pia huitwa Tower of Faces (Mnara wa Nyuso) ambao huinuka hadi kwenye orofa ya nne. Mnara huo hufanyizwa kwa mamia ya picha za Wayahudi walioishi Eishyshok, mji mdogo nchini Lithuania ambao sasa unaitwa Eisiskes. Picha hizo zilipigwa kati ya mwaka wa 1890 na 1941. Hizo ni picha za jamii fulani ya Wayahudi iliyokuwa na ufanisi kwa kipindi cha miaka 900. Katika mwaka wa 1941, kwa siku mbili tu, wauaji wanaosafiri wa kikosi cha SS (Einsatzkommando) waliua jamii hiyo nzima ya Wayahudi! Kulingana na rekodi za serikali ya Nazi, jumla ya Wayahudi 3,446 waliuawa, wakiwemo wanaume 989, wanawake 1,636, na watoto 821. Wanazi waliangamiza jamii nzima.
Vilevile kwenye orofa ya pili kuna Hall of Remembrance (Jumba la Kumbukumbu), na katika Kumbukumbu la Torati 30:19 na Mwanzo 4:9, 10. Pia kuna vitu mbalimbali vinavyoonyesha kwamba Mashahidi wa Yehova waliteswa kama vile pembe tatu ya rangi ya zambarau ambayo walihitaji kuwa nayo ili kuwatambulisha. Ukiwa makini utaona vitu hivyo unapotembea. Kuna vitu vingi unavyoweza kuchunguza kutia ndani sehemu kubwa ya kufanya utafiti iliyo kwenye orofa ya tano.
kuta zake za marumaru kuna maandiko fulani ya Biblia, kama vileMoyo wako utatulia ukitoka nje ya jumba hilo la ukumbusho. Hebu sasa tutembelee jumba jipya zaidi kati ya majumba ya ukumbusho ya Washington. Jumba hilo linatukumbusha jambo tofauti sana na pia jitihada ya kuangamiza jamii nzima.
Jumba la Ukumbusho la Utamaduni wa Waamerika
Jumba hilo jipya zaidi kati ya majumba ya ukumbusho ya Taasisi ya Smithsonian linawakumbusha watu kuhusu wakaaji wa zamani zaidi wa mabara ya Amerika. Jamii zaidi ya 500 za Wenyeji wa Asili wa Amerika waliishi katika mabara hayo kabla Wazungu na Waafrika hawajafika huko. Hilo huitwa Jumba la Ukumbusho la Kitaifa la Wahindi Waamerika nalo liko katika eneo la National Mall, karibu na Jumba la Ukumbusho la Usafiri wa Anga. Jumba hilo lilifunguliwa mnamo Septemba 21, 2004. Ni rahisi kulitambua jengo hilo kwani lina mistari ya pekee iliyopindika. Kuta za nje za jengo hilo lenye ukubwa wa meta 23,000 za mraba, zimefunikwa kwa chokaa ya Kasota kutoka Minnesota. Jengo hilo linafanana na “mwamba wenye matabaka mengi uliochongwa kwa pepo na maji.”
Unafikiri kuna nini humo? Sehemu tano kuu za maonyesho zina “vitu 7,000 hivi kati ya vitu
800,000 vya kiakiolojia na kitamaduni vinavyopatikana katika Jumba la Ukumbusho la Kitaifa la Wahindi Waamerika.” (Insight, gazeti la Smithsonian) Kuna vikapu, vyombo vya udongo, na shanga zilizotengenezwa na kabila la Mapuche nchini Chile, kabila la Quechua nchini Peru, kabila la Lakota nchini Marekani, na kabila la Anishinabe nchini Kanada.Mwanzilishi wa jumba hilo, W. Richard West, Jr., ambaye ni Mcheyenne wa Kusini, anasema kwamba kusudi la jumba hilo ni “kurekebisha maoni mabaya na kuwasaidia watu wote, yaani wenyeji na wale ambao si wenyeji, kuelewa maisha na utamaduni wa wenyeji wa mabara hayo.” Inachukua saa mbili hivi kutembea na kuona vitu vya utamaduni wa Wahindi Waamerika. Tunaweza kutembelea jumba gani lingine kati ya majumba ya maonyesho yanayopatikana Washington?
Vitu vya Sanaa vya Karne Mbalimbali
Hebu twende kwenye Jumba la Kitaifa la Maonyesho ya Sanaa. Jumba hilo lilifunguliwa mwaka wa 1941. Humo utaona vitu vya sanaa vya karne nane. Ikiwa unapenda sanaa, itafaa uanze matembezi asubuhi kwani itakuchukua saa kadhaa kutembea, kutazama, na kufikiria vitu hivyo vya kustaajabisha ikitegemea unapenda sanaa ya kipindi gani. Kwa kuwa kuna viti vingi, unaweza kuketi ili kuchunguza vitu hivyo au kupumzika.
Kwa kuwa Kanisa Katoliki hasa ndilo lililodhamini vitu vingi vya sanaa vya karne ya 13 hadi ya 15, michoro mingi ni ya kidini. Utaona mchoro wa Giotto unaoitwa “Madonna na Mtoto,” mchoro wa Raphael unaoitwa “The Alba Madonna” (1508), na michoro ya Leonardo da Vinci. Kazi za sanaa za karne ya 16 zinatia ndani zile za Tintoretto, Titian, na wengineo. Wanafunzi wa Biblia wanaweza kufurahia mchoro wa Tintoretto “Kristo Kwenye Bahari ya Galilaya” (karibu mwaka wa 1575/1580), unaoonyesha wanafunzi wa Kristo wakiwa ndani ya mashua ya kuvua samaki inayopigwa na dhoruba. Mchoro mwingine unaohusiana na Biblia ni ule wa El Greco unaoitwa “Kristo Akisafisha Hekalu.” Linganisha njia tofauti-tofauti za uchoraji za wasanii hao. Hebu tazama mchoro wa El Greco ulio na rangi nyingi unaoonyesha utendaji mbalimbali.
Vitu vya sanaa vya karne ya 17 vinatia ndani vile vya Rubens, Rembrandt, na wasanii wengine. Wanafunzi wa Biblia watavutiwa na Mchoro wa Rubens unaoitwa “Danieli Katika Tundu la Simba,” uliochorwa wapata mwaka wa 1615. Mwone Danieli akiwa mtulivu huku akimshukuru Mungu kwa kuokoa uhai wake. Sasa hebu tuchunguze vitu vilivyotengenezwa na wasanii Wafaransa katika karne ya 19.
Jumba la Kitaifa la Maonyesho ya Sanaa lina baadhi ya michoro bora zaidi ya wasanii Wafaransa mbali na ile inayopatikana huko Paris. Ikiwa umeona tu michoro iliyotokezwa kwa kuiga sanaa za awali, utasisimuka sana kuona michoro ya awali ya wasanii mbalimbali. Utavutiwa sana na ustadi wa wasanii maarufu kama vile Cézanne, Manet, Renoir, Degas, na Monet. Pia kuna michoro ya pekee ya wasanii wa Marekani kama ile ya Mary Cassatt (“Watoto Wakicheza Ufuoni”), James Abbott McNeill Whistler (“Msichana Mweupe”), na Winslow Homer (“Kubebwa na Upepo”).
Huenda ungependa kutembelea jumba la maonyesho liitwalo East Building, ambalo lina vitu vya sanaa ya kisasa. Kuna michongo mikubwa ndani ya ua wa jengo hilo ambayo ilichongwa na Alexander Calder, Henry Moore, na wasanii wengine. Pia utaona kitambaa kilichofumwa na msanii wa Catalonia anayeitwa Joan Miró.
Ni wazi kwamba itakuchukua muda mrefu kutembelea sehemu zote za jumba hilo la maonyesho. Bila shaka, kuna majumba mengine mengi ya maonyesho ya sanaa unayoweza kutembelea, kama vile Jumba la Maonyesho ya Sanaa la Corcoran ambalo lina vitu bora vya sanaa vilivyotengenezwa na wasanii stadi wa Ulaya na Marekani, kutia ndani michoro ya Monet na Renoir. Pia lina vitu vingi zaidi vya sanaa ambavyo vilitengenezwa na Jean-Baptiste Camille Corot mbali na vile vinavyopatikana Ufaransa. Je, bado una wakati na nguvu za kutosha? Ikiwa ndivyo, unaweza kutembelea majumba mengine.
Ziara yako ya Washington itakuwezesha kufahamu na kuthamini utamaduni. Huenda ukafahamu sababu iliyomfanya mwandishi Mfaransa Destouches aseme hivi: “Uchambuzi ni jambo rahisi, lakini kazi ya sanaa ni ngumu.” Huenda ziara hii itakuchochea kutembelea majumba ya ukumbusho na ya maonyesho ya sanaa yanayopatikana kwenu. Yatembelee na uchunguze uhusiano uliopo kati ya vitu vilivyomo, dini, na Biblia.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Kwa nini jiji hilo linaitwa “D.C.” (District of Columbia)? Linaitwa hivyo kwa sababu halimilikiwi na jimbo lolote kwani liko katika ardhi ya serikali yenye ukubwa wa kilometa 177 za mraba. Pia jina “D.C.” hulitofautisha na jimbo la Washington, lililo kwenye Pwani ya Magharibi, kilometa 3,000 hivi kutoka katika jiji hilo.
[Picha katika ukurasa wa 14]
Kasri ya Smithsonian
[Hisani]
Smithsonian photo by Eric Long
[Picha katika ukurasa wa 14, 15]
Jumba la Ukumbusho la Kitaifa la Usafiri wa Anga lina ndege ya “Flyer” ya mwaka wa 1903 (kulia) na ndege ya Lindbergh inayoitwa “Spirit of Saint Louis” (chini)
[Picha katika ukurasa wa 15]
Shirika la Kuchora na Kuchapa huvutia watalii wengi
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mnara wa Uhai una orofa tatu
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mavazi ya kambi ya mateso yaliyovaliwa na Shahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 17]
Jumba la Ukumbusho la Maangamizi Makubwa la Marekani
[Picha katika ukurasa wa 17]
Helene Gotthold
[Hisani]
USHMM, courtesy of Martin Tillmans
[Picha katika ukurasa wa 18]
Jumba la Ukumbusho la Kitaifa la Wahindi Waamerika lina muundo wa pekee wa mistari iliyopindika
[Hisani]
Photo by Robert C. Lautman
[Picha katika ukurasa wa 18]
Chombo cha glasi kilichotengenezwa na msanii wa kisasa ambaye ni Mhindi Mwamerika
[Hisani]
Photo by Ernest Amoroso, © Smithsonian Institution/National Museum of the American Indian
[Picha katika ukurasa wa 18]
Mchoro wa Winslow Homer unaoitwa “Kubebwa na Upepo,” unaopatikana katika Jumba la Kitaifa la Maonyesho ya Sanaa
[Hisani]
Winslow Homer, Breezing Up (A Fair Wind), Gift of the W. L. and May T. Mellon Foundation, Image © Board of Trustees, National Gallery of Art, Washington
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Top: Background: Smithsonian photo by Dane Penland; plane: © Mark Polott/Index Stock Imagery; tour: Photo by Carolyn Russo/NASM; bottom three photos: Courtesy of the Department of the Treasury, Bureau of Engraving and Printing