Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Tunahitaji Vyanzo Vipya vya Nishati?

Kwa Nini Tunahitaji Vyanzo Vipya vya Nishati?

Kwa Nini Tunahitaji Vyanzo Vipya vya Nishati?

“Leo ukosefu wa mafuta ni tatizo, lakini miaka 20 ijayo utakuwa janga kubwa.”—Jeremy Rifkin, wa Shirika la Masuala ya Uchumi, huko Washington, D.C., Agosti 2003.

KARIBU miaka 20 ijayo, wakati ambapo Micah anayetajwa katika makala iliyotangulia atakuwa na umri wa kutosha kuendesha gari, matumizi ya nishati ulimwenguni pote “yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 58,” yasema ripoti ya serikali ya Marekani inayoitwa International Energy Outlook 2003 (IEO2003). Gazeti New Scientist linasema kwamba hilo litakuwa “ongezeko kubwa zaidi la mahitaji ya nishati katika historia.” Je, vyanzo vya nishati ambavyo vimetumiwa kwa muda mrefu vitatosheleza uhitaji huo? Fikiria mambo yafuatayo.

MAKAA YA MAWE:

▪ Kati ya vyanzo vyote vya nishati vyenye kaboni, makaa ya mawe ndiyo hupatikana kwa wingi, kwani inakadiriwa kwamba yale yaliyopo yanaweza kutumiwa kwa miaka 1,000. Vituo vinavyotokeza nishati kwa makaa ya mawe hutokeza asilimia 40 hivi ya umeme unaotumiwa ulimwenguni. Australia ndiyo nchi inayouza kiasi kikubwa zaidi cha makaa ya mawe katika nchi za nje, kwani thuluthi moja hivi ya makaa ya mawe yanayotumiwa ulimwenguni hutoka huko.

Hata hivyo, ripoti moja ya hivi majuzi ya Taasisi ya Worldwatch inasema: “Kati ya vyanzo vya nishati vyenye kaboni, makaa ya mawe ndiyo hutokeza kiasi kikubwa cha kaboni, kwani hutokeza asilimia 29 ya kaboni kuliko mafuta na asilimia 80 kuliko gesi ya asili, yanapotumiwa kutokeza kiasi kilekile cha nishati. Kila mwaka makaa ya mawe hutokeza asilimia 43 ya kaboni ulimwenguni pote, yaani, tani bilioni 2.7 hivi.” Zaidi ya kuchafua mazingira, makaa ya mawe huathirije afya ya wanadamu yanapochomwa? Ripoti moja ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa ya Global Environment Outlook ilitoa mfano mmoja iliposema hivi: “Kila mwaka nchini China, moshi na chembechembe ambazo hutokezwa wakati makaa ya mawe yanapochomwa husababisha zaidi ya vifo 50 000 vya mapema na kusababisha watu 400 000 wapate ugonjwa wa mkamba katika majiji 11 ya nchi hiyo.”

MAFUTA:

▪ Ulimwenguni pote watu hutumia karibu lita bilioni 12 za mafuta kila siku. Kati ya lita trilioni 320 hivi za mafuta zilizokadiriwa kuwepo katika hifadhi za mafuta ulimwenguni, tayari lita trilioni 144 hivi zimetumiwa. Inatarajiwa kwamba mafuta yakiendelea kutokezwa kwa kiwango cha sasa, yatadumu kwa miaka mingine 40.

Hata hivyo, wataalamu Colin J. Campbell na Jean H. Laherrère walisema hivi katika mwaka wa 1998: “Katika kipindi cha miaka kumi ijayo, kiasi cha mafuta yanayopatikana kwa urahisi hakitaweza kutosheleza mahitaji.” Wataalamu hao wa mafuta walionya hivi: “Watu wengi hufikiri kimakosa kwamba tone la mwisho la mafuta litavutwa kutoka ardhini kwa urahisi sawa na vile mafuta yanavyovutwa kwa urahisi leo. Ukweli ni kwamba kiasi cha mafuta yanayovutwa kutoka katika kisima chochote au nchi yoyote ile hupanda hadi kiwango cha juu zaidi, kisha yanapokaribia kufikia nusu, kiwango hicho huanza kushuka polepole na hatimaye mafuta huacha kutoka. Kwa upande wa uchumi, jambo kuu si wakati ambapo mafuta yatakwisha kabisa bali ni wakati ambapo kiwango cha mafuta yanayovutwa kitaanza kupungua.”

Kiwango cha uzalishaji wa mafuta kitaanza kupungua lini? Mtaalamu wa mafuta Joseph Riva anasema kwamba “ongezeko la uzalishaji wa mafuta linalopangiwa . . . halifikii nusu ya kiasi cha mafuta ambacho Shirika la Kimataifa la Nishati linakadiria kitahitajiwa ulimwenguni pote kufikia mwaka wa 2010.” Gazeti New Scientist linaonya hivi: “Ikiwa viwango vya uzalishaji wa mafuta vitashuka huku mahitaji yakiendelea kuongezeka, huenda bei za mafuta zitapanda na kushuka mara nyingi na kusababisha matatizo ya uchumi, matatizo ya kusafirisha chakula na bidhaa nyinginezo, na hata vita baina ya mataifa yanayopigania kiasi kidogo cha mafuta yaliyosalia.”

Ingawa wataalamu fulani wanafikiri kwamba kupungua kwa mafuta ni tatizo, wengine wanafikiri kwamba ni afadhali tusikawie kuacha kutegemea mafuta. Jeremiah Creedon aliandika hivi katika gazeti Utne Reader: “Tatizo kubwa zaidi ya kutokuwa na mafuta ni kuendelea kuwa nayo. Ingawa kiasi cha kaboni-dioksidi inayotokezwa tunapotumia mafuta huendelea kuongeza joto la dunia, wakati masuala ya uchumi yanapozungumziwa masuala ya mazingira hayazungumziwi.” Tume moja ya Australia ilisema hivi kuonyesha jinsi nchi moja ilivyoathiriwa kwa kutegemea sana mafuta: “Magari milioni 26 yaliyoko Uingereza hutokeza thuluthi moja ya kaboni-dioksidi inayotokezwa nchini humo (ambayo husababisha ongezeko la joto la dunia) na thuluthi moja ya uchafuzi wa hewa nchini humo (ambao husababisha vifo vya watu wapatao 10,000 kila mwaka).”

GESI YA ASILI:

Kulingana na ripoti ya IEO2003, katika kipindi cha miaka 20 hivi ijayo, “inatarajiwa kwamba gesi ya asili ndiyo itakayokuwa chanzo kikuu cha nishati ulimwenguni.” Kati ya vyanzo vya nishati vyenye kaboni, gesi ya asili ndiyo haichafui mazingira sana inapochomwa, na inasemekana dunia ina kiasi kikubwa sana cha gesi ya asili.

Hata hivyo, Shirika la Gesi ya Asili lililoko Washington, D.C., linasema kwamba “kiasi kilichopo cha gesi ya asili hakiwezi kujulikana hadi gesi hiyo inapovutwa” kutoka ardhini. Kisha linaongeza hivi: “Makadirio mbalimbali hutegemea dhana tofauti-tofauti . . . Hivyo ni vigumu sana kujua kiasi kilichopo cha gesi ya asili.”

Methani ndiyo hufanyiza sehemu kuu ya gesi ya asili, nayo ni “gesi inayosababisha sana ongezeko la joto la dunia. Kwa hakika, methani ina uwezo wa kunasa joto karibu mara 21 zaidi ya kaboni-dioksidi,” lasema shirika lililotajwa awali. Hata hivyo, shirika hilo linasema kwamba uchunguzi mkubwa uliofanywa na Shirika la Kuhifadhi Mazingira na Taasisi ya Uchunguzi wa Gesi “ulionyesha kuwa faida za kuongeza matumizi ya gesi ya asili ili kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vyanzo vingine vya nishati, ni kubwa kuliko madhara yanayotokezwa na methani.”

NISHATI YA ATOMU:

Gazeti Australian Geographic linasema kwamba “mitambo 430 hivi ya nyuklia hutumiwa kutokeza asilimia 16 hivi ya umeme unaotumiwa ulimwenguni.” Mbali na mitambo ya nyuklia iliyopo, ripoti ya IEO2003 inasema: “Kufikia Februari 2003, mitambo 17 kati ya 35 inayojengwa ulimwenguni inapatikana katika nchi zinazoendelea za Asia.”

Licha ya uwezekano wa kutokea kwa misiba, kama ule uliotokea mwaka wa 1986 huko Chernobyl katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti, bado nishati ya nyuklia hutumiwa sana. Gazeti New Scientist linaripoti kwamba “mitambo ya nyuklia ya Marekani inashika kutu na kuharibika.” Pia linaripoti kwamba katika Machi 2002, mtambo wa Davis-Besse huko Ohio “ulikuwa karibu kuungua na kutokeza msiba mkubwa” kwa sababu ya kutu.

Kwa kuwa vyanzo vya nishati vinavyotumiwa sasa vinapungua na kuna hatari nyingi zinazosababishwa na kutokezwa kwa nishati, je, wanadamu wataiharibu dunia wakijaribu kutosheleza mahitaji yao makubwa ya nishati? Ni wazi kwamba tunahitaji vyanzo vinavyotegemeka ambavyo vinaweza kutumiwa kutokeza nishati bila kuchafua mazingira. Je, tunaweza kuvipata? Na je, vinaweza kutumiwa kutokeza nishati kwa gharama ya chini?