Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Chokoleti Inavyotengenezwa

Jinsi Chokoleti Inavyotengenezwa

Jinsi Chokoleti Inavyotengenezwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI CÔTE D’IVOIRE

Watu ulimwenguni pote hufurahia ladha ya pekee ya chokoleti. Chokoleti hutoka wapi, nayo hutengenezwaje? Tafadhali soma makala hii inayozungumzia historia ya chokoleti.

WATAALAMU wa mimea wanasema kwamba huenda maelfu ya miaka iliyopita mikakao ilikua katika mabonde ya Amazon na Orinoco huko Amerika Kusini. Huenda Wamaya ndio waliokuwa wa kwanza kupanda kakao na kuipeleka Yucatán walipohamia huko. Familia ya kifalme ya Waazteki ilifurahia kunywa kinywaji kichungu cha chokoleti kilichotayarishwa kwa kuchanganya mbegu zilizosagwa za kakao na mahindi yaliyochachushwa au divai. Walitumia vikombe vya dhahabu kunywa kinywaji hicho. Inasemekana kwamba Montezuma, Maliki wa Waazteki, alikunywa zaidi ya vikombe 50 vya chokoleti kwa siku.

Shujaa Mhispania Hernán Cortés, (1485-1547) alivutiwa hasa na vikombe hivyo vya dhahabu kuliko kinywaji chenyewe. Hata hivyo, Cortés alitambua kwamba Waazteki walitumia mbegu za kakao kama pesa. Bila kukawia, alipanda mashamba ya kakao. Mashamba hayo ya kakao yalileta faida kubwa, na Hispania ikadhibiti sehemu kubwa ya biashara ya kakao hadi karne ya 18.

Wahispania walipeleka kakao huko Haiti, Trinidad, na kisiwa cha Bioko cha Afrika Magharibi. Ganda moja la mbegu za kakao lilitolewa katika kisiwa hicho na kupelekwa barani Afrika, na kufikia sasa kuna biashara kubwa ya kakao katika nchi nne za Afrika Magharibi.

Chokoleti Huko Ulaya

Katika karne ya 16, Cortés alifanya maofisa wa baraza la Hispania waanze kunywa kinywaji cha chokoleti cha Waazteki. Wanawake wa familia ya kifalme ya Hispania walikunywa kwa kiasi kinywaji hicho kikiwa na vikolezo na nyakati nyingine kikiwa kimetiwa pilipili. Muda si muda, watu wenye cheo cha juu huko Ulaya walianza kunywa kinywaji hicho.

Wazungu walivutiwa sana na ladha ya pekee ya chokoleti na wazo la kwamba ingeweza kuponya magonjwa. Katika mwaka wa 1763, watengenezaji wa pombe huko Uingereza walihangaishwa kuona jinsi idadi ya watu wanaopenda chokoleti ilivyoendelea kuongezeka, hivyo wakaomba sheria itungwe ili kudhibiti utengenezaji wa chokoleti. Kwa sababu ya mashindano makali katika biashara ya chokoleti, watu fulani waliongeza wanga ili kutengeneza chokoleti kwa wingi zaidi. Ili kuongeza rangi ya chokoleti, Waingereza walitia kiasi kidogo cha unga wa matofali! Idadi ya watu waliotaka chokoleti bora zaidi na yenye ladha tamu zaidi iliendelea kukua.

Chokoleti ilianza kutokezwa viwandani wakati wa ule mvuvumko wa kiviwanda. Injini za mvuke zilipoanza kutumiwa kuendesha vinu vya kakao, mbegu za kakao zilisagwa kwa mashine badala ya mikono. Chokoleti iliboreshwa mwaka wa 1828, wakati mwanakemia Mholanzi Coenraad van Houten, alipogundua njia ya kutenganisha unga na siagi katika ute uliotokezwa kwa kusaga mbegu za kakao. Hivyo, baadaye watu walitengeneza “chokoleti za kuliwa” kwa kuchanganya majimaji ya chokoleti, siagi ya kakao, na sukari.

Katika nusu ya pili ya miaka ya 1800, Waswisi walivumbua mbinu iliyoboresha chokoleti. Katika mbinu hiyo, ute wa mbegu zilizosagwa za kakao hupitishwa katikati ya sahani za kauri kwa saa nyingi na kutokeza chokoleti nyepesi ambayo huyeyuka mdomoni. Wataalamu wa kukagua ubora wa chokoleti wanasema kwamba chokoleti bora ni ile iliyopitishwa katikati ya sahani hizo kwa angalau saa 72.

Huenda umeona majina ya wafanyabiashara wengi wenye ujuzi kama vile Hershey, Kohler, Lindt, Nestlé, Peter, Suchard, na Tobler kwenye pakiti za chokoleti. Watu hao walichangia kusitawi kwa biashara ya chokoleti kwa kuvumbua mashine bora zaidi au kuboresha njia za kutengeneza chokoleti.

Chanzo cha Chokoleti

Mkakao wa Tropiki hukua vizuri katika maeneo yaliyo kati ya nyuzi 20 kaskazini au kusini mwa ikweta. Mti huo husitawi vizuri katika maeneo yenye miti na anganyevu. Mikakao huchanua maua na huzaa matunda muda wote wa mwaka. Tunda lake ni ganda (1) ambalo hukua kutoka kwenye shina na matawi ya chini.

Kakao huvunwaje? Maganda mabivu hukatwa kutoka kwenye mti kwa panga au kwa mianzi iliyo na visu vikali. Maganda hayo hupasuliwa (2) ili kutoa mbegu 20 hadi 50 zilizoshikamana na sehemu nyeupe ya ndani ambayo ina ladha chungu na tamu. Kisha mbegu hizo hutolewa kwa mkono. Wakati wa mavuno, wavunaji hufanya kazi mchana kutwa wakipasua maganda na kuondoa mbegu. Kisha mbegu hizo hufunikwa na kuachwa kwa siku kadhaa. Wakati huo, sehemu ya ndani ya ganda huchachuka na mbegu za kakao hupata rangi ya kahawia. Kisha, mbegu hizo hukaushwa (3) kwa kuanikwa kwenye jua au kwa kutumia mashine za kutokeza hewa yenye joto. Mbegu hizo hukaushwa ili zisiharibike zinaposafirishwa na kuhifadhiwa.

Hasa kuna aina mbili za mbegu za kakao, yaani, Forastero na Criollo. Mbegu za Forastero ndizo hutumiwa zaidi katika viwanda vingi ulimwenguni. Kakao hiyo hukuzwa hasa huko Afrika Magharibi, Brazili, na Kusini-Mashariki mwa Asia. Kakao ya Criollo ina ladha nzuri sana. Inakuzwa kwa kiwango kidogo katika Amerika ya Kati, Ekuado, na Venezuela. Chembe zake hutiwa katika chokoleti ili kuiboresha.

Baada ya kukaushwa, mbegu za kakao hupakiwa kwenye magunia (4) na kusafirishwa hadi viwandani katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, hasa Ulaya na Amerika Kaskazini. Mbegu za kakao zilizokaushwa (5) zinazoweza kutoshea ndani ya mikono ya mtu zinaweza kutumiwa kutokeza karibu nusu kilo ya peremende za chokoleti. Si rahisi kusadiki kwamba mbegu chungu za kakao zinaweza kugeuzwa na kuwa chokoleti tamu. Hata hivyo, kwa karne kadhaa, njia za kutengeneza chokoleti hazijabadilika.

Kutengeneza Chokoleti

Zinapofika viwandani, kakao hizo huoshwa na kutenganishwa. Sawa na vile mbegu za kahawa zinavyookwa ili kutokeza ladha yake nzuri, ndivyo kakao zinavyookwa ili kutokeza ladha halisi ya chokoleti. Baada ya kuokwa mbegu hizo hupasuliwa (6). Chembe za rangi ya kahawia zilizo ndani ya mbegu ndizo hutumiwa kutengeneza kakao na chokoleti.

Chembe hizo husagwa ili kutokeza ute mzito au majimaji ya chokoleti (7). Ute huo hufanywa kuwa mgumu kisha huuzwa ili utumiwe kuoka. Majimaji ya chokoleti hushinikizwa ili kutokeza siagi na unga wa kakao. Mbinu hiyo ilivumbuliwa na Van Houten. Siagi ya kakao huchanganywa na majimaji ya kakao ili kutengeneza zile chokoleti tunazozijua, yaani, chokoleti za kuliwa. Mbinu ya kupitisha ute wa kakao katikati ya sahani za kauri (8) na mbinu nyingine za kuboresha chokoleti hutumiwa kutengeneza chokoleti zinazopendwa na watu wengi leo (9).

Utakapokuwa ukifurahia kula chokoleti laini, kumbuka kazi nyingi iliyohusika ya kufanya kakao chungu za maeneo ya Tropiki ziwe chokoleti tamu iliyo mkononi mwako.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Photos 2, 3, and 4 (except top sack): © CHOCOSUISSE, Münzgraben 6, 3011 Berne

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Photos 6, 7, and 8: © CHOCOSUISSE, Münzgraben 6, 3011 Berne