Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Milima Imo Hatarini

Milima Imo Hatarini

Milima Imo Hatarini

“Kila mtu anaweza kufaidika kwa kuhakikisha kwamba maeneo ya milimani yanaendelea kutokeza mali za asili kwa ajili ya vizazi vingi vya wakati ujao.”—KOFI ANNAN, KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA.

MILIMA humfanya mtu afikirie kuhusu ukuu, uthabiti, na nguvu. Je, kweli milima inaweza kuhatarishwa? Huenda watu fulani wakashindwa kuwazia kwamba milima inaweza kuwa hatarini. Lakini, kwa hakika milima imo hatarini. Wahifadhi wa mazingira hutaja baadhi ya matatizo hususa yanayokabili mazingira ya milimani. Matatizo yote hayo ni makubwa na hali inazidi kuwa mbaya. Hebu ona baadhi ya matatizo yanayoikumba milima.

MIRADI YA MAENDELEO. Asilimia 25 hivi ya maeneo ya milimani yanahatarishwa na barabara, uchimbaji wa migodi, mabomba, mabwawa, na miradi mingine ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika miaka 30 ijayo. Ujenzi wa barabara unaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo kwenye miinuko mikali, na barabara hizo hutumiwa na wakataji wa miti ambao husababisha madhara zaidi. Kila mwaka, tani bilioni kumi hivi za madini huchimbuliwa hasa kwenye milima, na takataka nyingi sana hutokezwa. *

ONGEZEKO LA JOTO LA DUNIA. Taasisi ya Worldwatch inasema hivi: “Miaka tisa yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa imekuwepo tangu 1990.” Na hasa maeneo ya milimani ndiyo yameathiriwa. Mito ya barafu imekuwa ikiyeyuka, na vilele vyenye theluji vinapungua, na kulingana na wanasayansi fulani jambo hilo litaathiri hifadhi za maji na kusababisha maporomoko hatari ya ardhi. Sasa maziwa mengi ya barafu huko Himalaya yanakaribia kufurika na kusababisha msiba. Jambo hilo limetukia mara kadhaa katika miaka iliyopita.

KILIMO CHA KIWANGO KIDOGO. Ongezeko la idadi ya watu linawafanya wanadamu kulima katika maeneo yasiyo na rutuba. Kulingana na uchunguzi mmoja, karibu nusu ya maeneo ya milimani barani Afrika yanatumiwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji, yaani, asilimia 10 kwa ajili ya mazao na asilimia 34 kwa ajili ya malisho. Mara nyingi, kilimo hicho hakileti faida kubwa, kwani maeneo hayo hayafai kwa ukuzaji wa mimea. * Na mimea huharibiwa wakati maeneo yaleyale yanapotumiwa kupita kiasi kuwalisha ng’ombe. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba asilimia 3 tu ya maeneo ya milimani ndiyo yanayoweza kulimwa bila kuharibu mazingira.

VITA. Ongezeko la vita vya wenyewe kwa wenyewe limesababisha uharibifu wa mazingira ya milimani. Vituo vya waasi huwa milimani. Ripoti moja ya Umoja wa Mataifa inakadiria kwamba asilimia 67 ya maeneo ya milimani ya Afrika yameathiriwa na “mapambano ya wanadamu yenye jeuri.” Isitoshe, maeneo fulani ya milimani hutumiwa kutokeza dawa za kulevya, na mara nyingi hilo husababisha uharibifu wa mazingira na mapambano makali kwa kutumia silaha.

Je, Jitihada Zaidi Zinahitajiwa?

Matokeo ya uharibifu wa milima unaosababishwa na wanadamu yanaonekana. Mafuriko, maporomoko ya ardhi, na ukosefu wa maji ni baadhi ya mambo yanayoonyesha kuna matatizo. Serikali zimeanza kuchukua hatua. Miti inapandwa, na ukataji wa miti umepigwa marufuku katika sehemu fulani. Mbuga za kitaifa zimeanzishwa ili kulinda maeneo yanayovutia sana na makao ya wanyama wa pori yanayokabili hatari kubwa zaidi.

Lakini hata maeneo yanayolindwa huathiriwa na uharibifu wa mazingira. (Ona sanduku lenye kichwa “Baadhi ya Maeneo ya Pekee ya Asili.”) Kutoweka haraka kwa jamii za viumbe kunaonyesha kwamba jitihada za kulinda maeneo ya milimani hazijafanikiwa kabisa. Wataalamu wanajua matatizo yanayokabili milima, lakini jitihada kubwa hazijafanywa ili kuhifadhi maeneo ambayo bado hayajaharibiwa. Mwanabiolojia maarufu E. O. Wilson, anasema hivi: “Ujuzi wetu wa kisayansi unanitia moyo, lakini ninavunjika moyo kwa sababu ya kuharibiwa kwa maeneo muhimu yaliyo na jamii nyingi za viumbe.”

Je, kutoweka kwa jamii za viumbe ni tatizo kubwa? Kulingana na wanabiolojia wengi, wanadamu hufaidika sana wanyama na mimea inapohifadhiwa. Wanabiolojia hutaja mfano wa mmea unaoitwa rosy periwinkle unaopatikana huko Madagaska kwenye maeneo ya milimani yenye jamii nyingi za viumbe. Mmea huo umetumiwa kutokeza dawa muhimu ya ugonjwa wa lukemia. Isitoshe, kwa miaka mingi, mti wa cinchona unaopatikana katika Milima ya Andes umetumiwa kutengeneza kwinini na dawa nyingine za malaria. Mimea mingi inayokua katika maeneo ya milimani imetumiwa kuokoa uhai wa mamilioni ya watu. Ni kweli kwamba baadhi ya mimea hiyo inayokua milimani imepandwa na kusitawi pia katika maeneo yasiyo na milima. Hata hivyo, jambo linalohangaisha ni kwamba uharibifu mkubwa wa mimea inayopatikana milimani huenda ukasababisha kutoweka kwa mimea muhimu ambayo bado haijagunduliwa. Na huenda mimea hiyo ni muhimu kwa afya na inaweza kutumiwa kutengeneza dawa.

Je, uharibifu huo unaweza kukomeshwa? Je, maeneo yaliyoharibiwa yanaweza kurekebishwa? Je, milima itaendelea kuvutia na kuhifadhi jamii nyingi za viumbe?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Kwa wastani, tani tatu za takataka hutokezwa wakati pete moja tu ya dhahabu inapotengenezwa.

^ fu. 6 Kwa upande mwingine, kwa karne nyingi watu wanaoishi milimani wamejifunza kulima katika maeneo hayo bila kuharibu mazingira.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

Viumbe wa Milimani

Puma hupatikana hasa milimani. Mnyama huyo hupatikana hasa katika Milima ya Rocky na ya Andes. Sawa na wanyama wengi wakubwa wanaowinda, puma amehamia maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa sababu ya kuhatarishwa na wanadamu.

Dubu anayeitwa red panda anapatikana tu katika Milima ya Himalaya (hata katika maeneo ya chini ya Mlima Everest). Ijapokuwa anaishi mbali, mnyama huyo anakabili hatari ya kutoweka kwa sababu ya uharibifu wa misitu ya mianzi ambayo ndiyo chakula chake.

[Hisani]

Cortesía del Zoo de la Casa de Campo, Madrid

Dubu anayeitwa brown bear alipatikana katika sehemu nyingi za Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini. Huko Ulaya, anapatikana tu katika maeneo machache ya milimani, ingawa anapatikana zaidi huko Alaska, Siberia, na kwenye Milima ya Rocky nchini Kanada. Katika karne iliyopita, idadi ya dubu hao ilipungua kwa asilimia 99 huko Marekani.

Tai aina ya golden eagle hupatikana sana katika maeneo mengi ya milimani ya Kizio cha Kaskazini. Inasikitisha kwamba huko Ulaya idadi yao imepungua kufikia chini ya vikundi 5000 vya ndege wawili wawili wa kiume na wa kike kwa sababu hapo zamani ‘walichukiwa.’

Mtaalamu wa vitu vya asili wa China anayeitwa Tang Xiyang anasema kwamba dubu anayeitwa giant panda “hutegemea hasa vitu vitatu.” Vitu hivyo ni “milima mirefu na mabonde yenye kina kirefu, misitu mikubwa ya mianzi, na vijito.” Kulingana na kadirio moja, idadi ya panda waliosalia porini haizidi 1,600.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Baadhi ya Maeneo ya Pekee ya Asili

Mbuga ya Kitaifa ya Yosemite (California, Marekani) ilianzishwa katika mwaka wa 1890 kutokana na jitihada kubwa za mtaalamu wa vitu vya asili John Muir. Mandhari yake yanayopendeza huwavutia watalii milioni nne kila mwaka. Hata hivyo, wasimamizi wa mbuga hiyo hukabili matatizo wanapojitahidi kuilinda, huku wakitosheleza mahitaji ya watu wanaovutiwa na viumbe.

Mbuga ya Kitaifa ya Podocarpus (Ekuado) ni hifadhi ya msitu unaofunikwa na mawingu katika Milima ya Andes. Msitu huo una jamii nyingi za wanyama na za mimea kwani kuna zaidi ya aina 600 za ndege na jamii 4,000 hivi za mimea. Dawa ya kwinini, ambayo imeokoa uhai wa watu wengi sana, iligunduliwa katika eneo hilo. Sawa na mbuga nyingi, mbuga hiyo inahatarishwa na ukataji wa miti na uwindaji haramu.

Mlima Kilimanjaro (Tanzania) ni mmojawapo wa milima mikubwa zaidi ya volkeno ulimwenguni na ndio mlima mrefu zaidi barani Afrika. Tembo hulisha katika maeneo ya chini, huku mimea ya pekee kama vile giant lobelia na giant groundsel ikikua katika maeneo ya juu. Mlima huo unahatarishwa hasa na uwindaji haramu, ukataji wa miti, na ulishaji wa ng’ombe.

Mbuga ya Kitaifa ya Teide (Visiwa vya Canary) ni hifadhi ya mimea ya pekee ambayo hupamba eneo hilo lenye milima ya volkeno. Mazingira ya visiwa vilivyo na milima ya volkeno yanaweza kuharibiwa kwa urahisi na jamii mpya za viumbe.

Mbuga za kitaifa za Pyrenees na Ordesa (Ufaransa na Hispania) ni hifadhi za milimani zilizo na mandhari yanayovutia, mimea, na wanyama wengi. Sawa na safu nyingine za milima huko Ulaya, Milima ya Pyrenees imeathiriwa na ongezeko la sehemu za kuteleza kwenye theluji na za kuwahudumia watalii. Pia, mazingira ya eneo hilo yameathiriwa sana kwa sababu ya kubadili mbinu za kilimo zilizotumiwa kwa muda mrefu.

Mbuga ya Kitaifa ya Sǒraksan ndiyo mbuga inayotembelewa zaidi katika Jamhuri ya Korea. Vilele vyake vyenye kupendeza na miinuko yake yenye misitu huvutia sana katika majira ya kupukutika kwa majani. Hata hivyo, kwa kuwa watu wengi hutembelea mbuga hiyo, mwishoni mwa juma vijia vyake hujaa watu kama vile barabara za jiji.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Mimea ya Milimani

Tower of jewels. Kwa muda wa majuma machache katika majira ya kuchipua, mmea huo wenye kustaajabisha hukua kufikia urefu wa mtu. Mmea huo hupatikana tu kwenye vilele vya milima miwili ya volkeno iliyo meta 1,800 hivi juu ya usawa wa bahari katika Visiwa vya Canary. Jamii nyingi za mimea ya milimani hupatikana tu katika maeneo ya juu kama hayo.

Carline thistle hukua katika Milima ya Alps na Pyrenees. Rangi yake nyangavu hung’aa majira ya kiangazi yanapokaribia kwisha na wadudu hula maua yake sana.

English iris. Jamii za mmea huo zilizopatikana kwa kuchavushwa pamoja na mimea mingine hukuzwa kwenye bustani. Maua mengi yanayokuzwa kwenye bustani yalitolewa milimani.

Mountain houseleek ni mmojawapo wa mimea mingi ya milimani ambayo hushikamana na nyufa za miamba. Mmea huo, ambao hupatikana katika milima ya Ulaya Kusini, unaitwa pia “ishi milele” kwa sababu unastahimili hali ngumu na unaishi kwa muda mrefu.

Bromeliad. Aina nyingi za mmea huo na za mmea wa okidi husitawi kwenye maeneo ya Tropiki katika misitu ya milimani ambayo hufunikwa na mawingu. Mimea hiyo hukua hata kwenye maeneo yaliyo meta 4,500 juu ya usawa wa bahari.

Algerian iris unapatikana katika Mlima wa Er Rif na wa Atlas, kaskazini mwa Afrika, na eneo hilo la Mediterania lina jamii nyingi za mimea inayokabili hatari ya kutoweka.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Kuchimbua shaba na dhahabu karibu na Milima ya Maoke, huko Indonesia

[Hisani]

© Rob Huibers/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 8]

Rosy periwinkle