Tunahitaji Milima
Tunahitaji Milima
“Ukipanda milima utafurahia mambo mazuri. Utahisi utulivu wa mazingira kama miti inayopata mwangaza wa jua. Utaburudishwa na upepo unaovuma, utahisi nguvu za upepo mkali, na mahangaiko yako yatatoweka kama majani yanayopukutika.”—JOHN MUIR, MWANDISHI NA MTAALAMU WA VITU VYA ASILI WA MAREKANI.
KAMA vile John Muir alivyogundua zaidi ya karne moja iliyopita, milima inaweza kutuchochea. Ukuu wa milima hutuvutia, wanyama wanaoishi huko hutupendeza, na utulivu wake hututuliza. Kila mwaka, mamilioni ya watu hutembelea milima ili kufurahia mandhari na kujiburudisha. Klaus Toepfer, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa, anasema hivi: “Tangu kale, milima imewastaajabisha na kuwachochea watu wa jamii na utamaduni mbalimbali.”
Lakini milima inakabili matatizo. Kwa karne nyingi milima haijaharibiwa na wanadamu kwa sababu ya kuwa mbali na makao yao. Hata hivyo, sasa inakabili hatari. Kulingana na ripoti moja ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa, “baadhi ya maeneo ambayo hayajaharibiwa yanatoweka haraka kwa sababu ya kilimo, ujenzi, na mambo mengine.”
Sehemu kubwa ya dunia ni milima. Asilimia 50 ya watu ulimwenguni hutegemea mali za asili zinazopatikana milimani. Na mamilioni ya watu huishi milimani. Zaidi ya kuwawezesha watu kufurahia mandhari yenye kuvutia na yenye utulivu, milima ina faida nyingine nyingi. Hebu tuzungumzie baadhi ya faida ambazo wanadamu hupata kutokana na milima.
Umuhimu wa Milima
▪ KUHIFADHI MAJI. Milima ndiyo chanzo cha mito mikubwa na cha maji yanayoingia katika hifadhi nyingi za maji. Huko Amerika Kaskazini, Mto Colorado na Mto Rio Grande hupata karibu maji yote kutoka kwenye Milima ya Rocky. Asilimia 50 hivi ya watu ulimwenguni huishi Asia Kusini na Asia Mashariki. Wengi wa watu hao hutegemea mvua inayonyesha kwenye milima mikubwa iliyo katika maeneo ya Himalaya, Karakoram, Pamirs, na Tibet.
Toepfer anasema hivi: “Milima, ambayo ni hifadhi kubwa za maji ulimwenguni, ni muhimu kwa uhai wa viumbe wote duniani na kwa afya ya watu kila mahali.” Pia anaongeza hivi: “Mambo yanayotukia katika vilele virefu zaidi vya milima huathiri uhai katika maeneo ya chini, mito, na hata bahari.” Katika maeneo mengi, milima huhifadhi theluji wakati wa baridi kali, kisha katika majira ya kuchipua na ya kiangazi theluji hiyo huyeyuka polepole na kunywesha ardhi. Katika maeneo makavu ya ulimwengu, maji yanayotumiwa kunyunyizia mashamba hutokana na theluji inayoyeyuka
katika milima ya mbali. Milima mingi ina miinuko yenye misitu ambayo hufyonza maji ya mvua kama sifongo na kufanya maji yatiririke polepole hadi mitoni bila kusababisha mafuriko.▪ MAKAO YA WANYAMA WA PORI NA UNAMNA-NAMNA WA VIUMBE. Wanadamu hawajaiharibu milima sana kwa sababu iko mbali na makao yao na haiwezi kutumiwa sana kwa kilimo. Kwa hiyo, mimea na wanyama ambao wametoweka katika maeneo ya chini wanapatikana milimani. Kwa mfano, kuna jamii 4,500 za mimea katika Mbuga ya Kitaifa ya Kinabalu huko Malasia. Mbuga hiyo inapatikana mlimani katika eneo dogo kuliko New York City. Lakini idadi hiyo ya mimea ni zaidi ya robo ya idadi ya jamii za mimea inayopatikana huko Marekani. Wanyama fulani huko China wanaoitwa giant panda, tai fulani wa Andes, na chui fulani wanaopatikana huko Asia ya kati huishi milimani sawa na jamii nyingine nyingi za wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka.
Kulingana na gazeti National Geographic, wataalamu fulani wa mazingira wamekadiria kwamba “zaidi ya thuluthi moja ya mimea na viumbe wenye uti wa mgongo wanaoishi kwenye nchi kavu hupatikana katika eneo lisilofikia asilimia 2 ya ukubwa wa dunia.” Jamii nyingi husongamana katika maeneo yenye rutuba ambayo hayajaharibiwa. Maeneo mengi kati ya hayo yako milimani, nayo yana jamii nyingi za viumbe ambao hutunufaisha sote. Baadhi ya mimea muhimu inayoliwa ulimwenguni hukuzwa milimani. Kwa mfano, mahindi hukuzwa katika maeneo ya milimani nchini Mexico, viazi na minyanya hukuzwa katika Milima ya Andes huko Peru, na ngano hukuzwa katika milima ya Caucasus.
▪ TAFRIJA NA MANDHARI YANAYOVUTIA. Pia milimani kuna vitu vya asili vyenye kuvutia. Kuna maporomoko ya maji yanayopendeza, maziwa maridadi, na sehemu nyingi zenye kuvutia zaidi ulimwenguni. Si ajabu kwamba thuluthi moja ya maeneo ya ulimwengu yanayohifadhiwa yako milimani. Na maeneo hayo hutembelewa sana na watalii.
Mamilioni ya watalii kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu hutembelea mbuga za kitaifa zilizo mbali. Watu kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu hutembelea Mbuga ya Kitaifa ya Denali huko Alaska ili wajionee Mlima McKinley, ambao ndio mlima mrefu zaidi katika Amerika Kaskazini. Watu wengi hutembelea Bonde la Ufa ili wajionee milima mirefu ya Kilimanjaro na Meru au kuona wanyama wengi wa pori wanaoishi katika maeneo yaliyo kati ya milima hiyo. Jamii nyingi za watu wanaoishi milimani hunufaika kutokana na utalii. Hata hivyo, biashara ya utalii isipodhibitiwa inaweza kuharibu mazingira ya asili.
Ujuzi Unaopatikana Milimani
Kwa karne nyingi, watu wanaoishi milimani wamejifunza jinsi ya kusitawi katika hali ngumu za mazingira. Wamefanyiza matuta kwa ajili ya kilimo, na yangali yanatumiwa hata baada ya miaka 2,000. Wamefuga wanyama wanaopatikana milimani, kama vile llama na yak, ambao wanaweza kukabiliana na hali ngumu za milimani. Na mambo ambayo wamejifunza yanaweza kuwa muhimu sana katika kuhifadhi milima ambayo sisi sote hutegemea.
Alan Thein Durning wa Taasisi ya Worldwatch anaeleza hivi: “Katika sehemu za mbali za kila bara, wenyeji wa asili ndio hutunza maeneo makubwa ambayo hayajaharibiwa sana.” Anaongeza hivi: “Ujuzi mwingi walio nao kuhusu mazingira . . . unaweza kulinganishwa na ujuzi unaopatikana katika maktaba za sayansi ya kisasa.” Ujuzi huo mwingi unahitaji kuhifadhiwa sana sawa na mali za asili zinazopatikana milimani.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa lilidhamini Mwaka wa Milima wa Kimataifa wa 2002. Ili kukazia jinsi wanadamu wanavyotegemea milima, wasimamizi wa mradi huo walitunga msemo huu, “Sisi Sote Ni Watu wa Milimani.” Walikusudia kuwajulisha watu kuhusu matatizo yanayokabili milima ulimwenguni na kutafuta njia za kuilinda.
Hatua hiyo ilifaa. Yule aliyetoa hotuba ya msingi katika Kongamano la Ulimwengu la Milima lililofanywa huko Bishkek nchini Kyrgyzstan mwaka wa 2002, alisema: “Mara nyingi sana, milima huonwa kuwa chanzo cha mali nyingi za asili, lakini matatizo ya watu wanaoishi huko pamoja na utunzaji wa mazingira ya milima hupuuzwa.”
Ni nini baadhi ya matatizo yanayokabili milima na watu wanaoishi huko? Matatizo hayo huathirije kila mmoja wetu?