Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Venice—‘Jiji Lililo Baharini’

Venice—‘Jiji Lililo Baharini’

Venice—‘Jiji Lililo Baharini’

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Italia

“Kuna Jiji tukufu lililo Baharini. Bahari ndiyo barabara zake pana na nyembamba, maji yake yanaongezeka na kupungua; na magugu-maji yameshikamana na mawe ya marumaru ya makasri yake.”—Samuel Rogers, mshairi Mwingereza, 1822.

‘JIJI hilo tukufu’ linaitwa Venice. Wakati mmoja Venice lilikuwa jiji kuu la jamhuri yenye mamlaka kubwa ambayo ilimiliki kwa karne nyingi maeneo makubwa ya bahari na nchi kavu. Kwa nini jiji hilo lilijengwa “baharini”? Nalo lilijengwaje? Kwa nini lilionwa kuwa tukufu? Milki hiyo iliangukaje, na ni mambo gani kuhusu fahari ya jiji la Venice yaliyobaki?

Eneo Lisilopendeza

Venice liko katikati ya wangwa ulio kaskazini-magharibi mwa Bahari ya Adriatiki, na linaunganisha visiwa 118. Mito inayotiririka hadi baharini huingiza kiasi kikubwa cha mchanga-tope katika maji ya pwani. Mikondo ya maji na mawimbi yamefanyiza mafungu ya mchanga yaliyozingira wangwa wenye urefu wa kilometa 51 hivi na upana wa kilometa 14. Vijia vitatu vyembamba vinavyoingia baharini huwezesha mawimbi yenye urefu wa meta moja na mashua kufika baharini. Chanzo kimoja kinasema hivi: “Kwa karne nyingi wangwa huo ulikuwa kituo kikuu cha meli nyingi za kibiashara zilizosafiri kwenye Bahari ya Adriatiki au zilizotoka katikati au kaskazini mwa Ulaya kupitia mito au njia nyingine.”

Wasomi wanasema kwamba jiji hilo lilianza kati ya karne ya tano na ya saba W.K., wakati ambapo wavamizi waliotoka kaskazini waliteketeza na kupora watu walioishi kwenye nchi kavu. Wakaaji wa eneo hilo waliwatoroka wavamizi hao, na wengi wao wakakimbilia visiwa visivyofikika kwa urahisi, lakini vyenye usalama.

Maandishi ya kale yanaonyesha kwamba misingi ya majengo ya kwanza ya jiji hilo ilijengwa juu ya nguzo zilizoingizwa matopeni na kuunganishwa kwa matawi membamba au matete. Baadaye wakaaji wa jiji hilo walijenga majengo ya mawe juu ya misingi iliyojengwa juu ya maelfu ya mihimili ya mbao. Wakati huohuo, visiwa vya Rialto ambavyo baadaye vilikuwa kitovu cha jiji hilo, mara nyingi vilifurika na havikuwa imara wala havikutosha kuhimili uzito wa idadi kubwa ya watu waliohamia huko. Ilibidi maji yaondolewe na visiwa hivyo vipanuliwe kwa kutumia mbinu duni. Kwa hiyo, wakaaji walichimba mifereji kwa ajili ya mashua zao na kuimarisha visiwa hivyo ili wapate mahali panapofaa zaidi kwa ujenzi. Mifereji ikawa barabara za jiji hilo na madaraja yakajengwa juu ya mifereji hiyo ili kuwawezesha watu waliotembea kwa miguu kuvuka kutoka kisiwa kimoja hadi kingine.

Jinsi Jamhuri Hiyo Ilivyoanza na Kusitawi

Baada ya kuanguka kwa Milki ya Roma huko Magharibi, visiwa hivyo vilianza kumilikiwa na Milki ya Bizantiamu. Makao makuu ya milki hiyo yalikuwa huko Constantinople, ambayo sasa ni Istanbul. Hata hivyo, wakaaji wa visiwa hivyo waliasi na kupigania uhuru. Hivyo, Venice lilibaki katika hali ya pekee likiwa “jimbo huru . . . katikati ya milki mbili kuu,” yaani, Jamii ya Frank na Milki ya Bizantiamu. Hali hiyo ya pekee iliwezesha jiji hilo kusitawi na kuwa “kituo [kikubwa] cha kibiashara.”

Katika karne zilizofuata, jiji la Venice lilipigana na majeshi mengine katika eneo la Mediterania, kama vile majeshi ya Wasaracen, Wanorman, na Wabizantiamu. Baada ya kutumia krusedi ya nne katika mwaka wa 1204 kuharibu jiji la Constantinople ambalo lilikuwa adui mkubwa zaidi, Venice likawa jiji lenye nguvu kuliko majiji hayo mengine. Venice lilifanya vituo vingi vya kibiashara katika Bahari Nyeusi, Bahari ya Aegea, Ugiriki, Constantinople, Siria, Palestina, Saiprasi, na Krete. Milki ya Bizantiamu ilipoanguka, Venice lilifanya baadhi ya sehemu hizo ziwe koloni zake.

“Bimkubwa wa Mediterania”

Mapema katika karne ya 12, viwanda vya kutengenezea meli vya Venice vilikuwa vikitokeza meli nzima yenye vifaa kamili kwa saa chache tu. Viwanda vya jiji hilo vilitengeneza glasi na vitambaa vya hali ya juu kama vile lesi, hariri iliyotariziwa, na mahameli. Wafanyabiashara wa Venice na wa maeneo mengine walileta silaha, farasi, kaharabu, manyoya, mbao, sufu, asali, nta, na watumwa kutoka maeneo ya Magharibi. Bidhaa zilizoingizwa Venice kutoka nchi za mashariki mwa Mediterania zilitia ndani dhahabu, fedha, hariri, vikolezo, pamba, rangi, pembe za tembo, manukato, na bidhaa nyingine nyingi. Wakuu wa jiji walihakikisha kwamba bidhaa zote zilizoingia na kutoka katika masoko ya jiji hilo zilitozwa ushuru.

Kwa kuwa lilipambwa na wasanii wa ujenzi na wachoraji maarufu kama vile Palladio, Titian, na Tintoretto, jiji la Venice liliitwa la serenissima, yaani, “lenye utulivu zaidi” au “maridadi.” Hivyo, ilifaa kwamba jiji hilo lilirejelewa kuwa “bimkubwa wa Mediterania, . . . kituo cha kibiashara chenye utajiri na ufanisi mwingi zaidi katika maeneo yaliyostaarabika.” Lilibaki hivyo kwa karne nyingi. Hata hivyo, katika karne ya 16 mamlaka yake ilianza kupungua kwani wakati huo vituo vikuu vya biashara vilihamia maeneo ya Atlantiki na mabara ya Amerika.

Koloni za Venice, zilizokuwa kotekote katika eneo la Mediterania, zilikuwa zimetengana, hazikuwa na serikali moja, wala hazikuwa na umoja. Hivyo, Venice halingeweza kuendelea kushikilia koloni zake. Pole kwa pole, milki jirani zilinyakua koloni za Venice na hatimaye mwaka wa 1797 Napoléon wa Kwanza akashinda jiji hilo na kulifanya liwe chini ya Austria. Mnamo mwaka wa 1866, Venice likawa chini ya Italia.

Jiji la Kustaajabisha

Wengi wanapotembelea Venice wao huhisi ni kana kwamba wamerudi nyuma miaka mia mbili au mia tatu. Jiji hilo lina mazingira ya pekee.

Jambo moja la pekee ni utulivu wa jiji hilo. Kwa kawaida, watu wanaotembea kwa miguu hupita katika njia nyembamba zilizotengwa na njia za mashua, isipokuwa mahali ambapo njia hizo huwa sambamba na mifereji au wanapoivuka kupitia madaraja ya mawe. Magari ya jiji hilo ni mashua kwani maji ndiyo “barabara” zake. Jiji hilo ni maridadi sana. Ua wa St. Mark huwavutia wachoraji kwa kuwa una kanisa, mnara wa kengele, na bandari yenye kustaajabisha ambayo huvutia sana wakati jua linapoangaza wangwa wake wa kijani.

Watalii na wenyeji huenda kwenye mikahawa iliyo katika ua huo. Ukiwa huko unaweza kufurahia kinywaji au aiskrimu huku ukisikiliza muziki mtamu. Ukiwa umeketi ukiwatazama wapita-njia na majengo yenye kuvutia pande zote bila kuona magari yoyote, utahisi kana kwamba uko katika enzi za zamani.

Jiji hilo huwavutia wale wanaopenda sanaa. Kuna michoro ya wasanii wengi maarufu katika makasri, majumba ya ukumbusho, na makanisa ya Venice. Hata hivyo, wageni fulani hufurahia tu kutembea katika njia zake nyembamba na kutazama mandhari za pekee. Maduka mengi huwauzia watalii bidhaa maarufu za jiji hilo kama vile lesi na matarizi yaliyotengenezewa katika kisiwa cha Burano na vyombo bora vya fuwele na vya glasi kutoka Murano. Huenda ukafurahia kusafiri kwa mashua yenye injini hadi visiwa hivyo, na unaweza kujionea jinsi bidhaa hizo zinavyotengenezwa.

Makasri makubwa yenye madirisha na mapaa ya matao yamejengwa kwa mitindo ya watu wa kale wa Mashariki. Wageni huvutiwa na daraja maarufu la Rialto linalovuka Mfereji wa Grand, ambayo ndiyo njia kuu ya jiji hilo, kwani mashua nyeusi zinazoitwa gondola husafiri kwa utulivu chini ya daraja hilo.

Linaendelea Kukabiliana na Matatizo

Karne mbili baada ya ‘Jamhuri hiyo maridadi’ kuanguka, jiji la Venice linaendelea kukabiliana na matatizo mengine. Idadi ya wakaaji wa jiji hilo la kihistoria ilipungua kutoka watu 175,000 katika mwaka wa 1951 hadi watu 64,000 katika mwaka wa 2003 kwa sababu ya kupanda kwa bei za ardhi, ukosefu wa kazi, na uhaba wa vifaa vya kisasa. Kuna matatizo makubwa ya kijamii na ya kiuchumi yanayohitaji kushughulikiwa. Kwa mfano inahitaji kuamuliwa ikiwa jiji hilo linalozorota linahitaji kujengwa upya na jinsi ya kufanya hivyo.

Katika miaka ya 1920, eneo jipya la viwanda lilisitawishwa kwenye nchi kavu na ilitarajiwa kwamba mradi huo utaboresha uchumi wa jiji hilo. Pia, mfereji wenye kina kirefu ulichimbwa katika wangwa huo ili kuwezesha meli za mafuta zifike kwenye viwanda vya kusafisha mafuta. Ijapokuwa viwanda hivyo viliwawezesha watu kupata kazi, inasemekana vimesababisha uchafuzi na kuwapo kwa mawimbi hatari yanayoitwa acqua alta (maji yaliyoinuka), ambayo mara nyingi hufunika sehemu kubwa ya kitovu cha jiji hilo.

Tangu zamani, mazingira ya wangwa huo na nguvu za maji zimezuia jiji hilo lisitokomee. Kuanzia mwaka wa 1324, wakaaji wa Venice walianzisha miradi mikubwa ya uhandisi ili kugeuza mito iliyokuwa karibu kufunika wangwa huo kwa mchanga-tope. Katika karne ya 18, walijenga kuta za maji ili kuzuia maji ya Bahari ya Adriatiki yasiharibu wangwa huo.

Sasa hali ni mbaya zaidi. Inaaminiwa kwamba tatizo la kushuka kwa ardhi linalosababishwa na matumizi makubwa ya maji yaliyomo ardhini katika viwanda limekomeshwa. Hata hivyo, ulimwenguni pote viwango vya maji ya bahari vinazidi kupanda. Isitoshe, ukubwa wa wangwa huo umepungua kutokana na mbinu za kuondoa maji ili kupata mashamba, na watu wamevuruga usawaziko kati ya maji na ardhi. Kwa muda mrefu maji yaliyoinuka yamekuwa tishio lakini sasa hali ni mbaya zaidi. Mwanzoni mwa karne ya 20, Ua wa St. Mark ulikuwa ukikumbwa na mafuriko mara tano hadi saba kwa mwaka. Karne moja baadaye, ua huo ulikumbwa na mafuriko mara 80 katika kipindi cha mwaka mmoja tu.

Mataifa yameanza kuhangaikia jiji la Venice kwa sababu ya historia yake ya pekee, sanaa yake, na pia matatizo yanayolikabili. Sheria mbalimbali zimetungwa ili kuhifadhi mazingira ya jiji hilo na kuzuia maji yanayoinuka yasiliharibu. Sheria hizo pia zitahakikisha kwamba shughuli za bandari yake au maisha ya wakaaji wake hayaathiriwi. Njia bora ya kufanya hivyo bado haijulikani.

Jitihada zinafanywa kuinua kingo za mfereji, kuzuia maji yaliyo ardhini yasiinuke, na kuzuia maji machafu yasirudi jijini wakati maji ya bahari yanapoinuka. Mradi ambao umebishaniwa sana ni ule wa ujenzi wa vizuizi, ambavyo vinaweza kuinuliwa maji yanapoinuka, kwenye milango ya wangwa huo.

Jitihada nyingi zinahitajiwa ili kutimiza miradi hiyo. “Jiji [hilo] tukufu lililo Baharini” lina historia ya ajabu, lakini waandishi kadhaa wanasema linakabili hatari ya kubadilishwa “na wageni kuwa jiji la ukumbusho huku mahitaji ya wenyeji yakipuuzwa na kuwalazimu kuhama.” Kwa muda mrefu jiji la Venice limekabili hali ngumu za mazingira. Hata hivyo, “miradi ya kulinda jiji hilo lisiharibiwe na maji haitakuwa na faida yoyote ikiwa halitaimarishwa kijamii na kiuchumi, na ikiwa halitakuwa na wakaaji wala utendaji mwingi.”

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Venice

[Picha katika ukurasa wa 16]

Daraja la Rialto linalovuka Mfereji wa Grand

[Picha katika ukurasa wa 17]

San Giorgio Maggiore

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kanisa la Santa Maria della Salute

[Picha katika ukurasa wa 18]

Mikahawa iliyo kwenye Mfereji wa Grand

[Picha katika ukurasa wa 19]

Furiko katika Ua wa St. Mark

[Hisani]

Lepetit Christophe/GAMMA

[Picha katika ukurasa wa 16 zimeandaliwa na]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.; background photo: © Medioimages