Watazamaji Wanaoweza Kuathiriwa
Watazamaji Wanaoweza Kuathiriwa
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND
NI JAMBO la kawaida kwa watoto wengi kutazama filamu, televisheni, video, DVD, kucheza michezo ya kompyuta, na kutumia Intaneti. Ripoti ya karibuni iliyochapishwa na Baraza la Kuweka Viwango vya Filamu la Finland inasema kwamba “kulingana na makadirio fulani, watoto na vijana hutazama na kuvitumia vyombo vya habari kati ya mara 20 au 30 zaidi ya wakati wanaotumia kufanya mambo na familia zao.” * Kwa kusikitisha hilo huwafanya watoto wapate habari nyingi zenye kudhuru.
Katika nchi fulani, wenye mamlaka hujaribu kuweka sheria na viwango kuhusu umri ambao mtu anaruhusiwa kuona filamu fulani. Hata hivyo, kulingana na ripoti hiyo, si nyakati zote ambazo watoto na wazazi huelewa viwango hivyo, au wao huzipuuza. Pia, inajulikana kwamba majumba mengi ya kuonyeshea filamu na maduka ya kukodi kanda za video hupuuza sheria zilizowekwa kuhusu umri. Isitoshe, programu fulani na filamu hazina viwango vya umri.
Mwalimu mmoja aliyehusika katika uchunguzi huo alisema hivi: “Ni kana kwamba wanafunzi hawawezi kutambua kwamba filamu ina jeuri, isipoonyesha umwagaji wa damu.” Michezo mingi ya video, ya kompyuta, na hata vibonzo vilivyotayarishwa hasa kwa ajili ya watoto, huwa na mambo ambayo yanaweza kudhuru.
Ripoti hiyo inasema kwamba kila familia “ina wajibu wa kuamua filamu na programu ambazo watoto watatazama.” Inamalizia kwa kuuliza swali hili muhimu: “Je, sisi watu wazima tuna nia, uwezo, na njia ya kuwalinda watoto kutokana na madhara ya vyombo vya habari?”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Ripoti hiyo yenye kichwa “Viwango vya Umri wa Watazamaji wa Filamu na Kuwalinda Watoto” ilitegemea uchunguzi uliohusisha wanafunzi wa shule za msingi 340 kutia ndani wazazi na walimu wao.