Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Capoeira”—Je, Ni Dansi, Mchezo, au Mafunzo ya Kujihami?

“Capoeira”—Je, Ni Dansi, Mchezo, au Mafunzo ya Kujihami?

“Capoeira”—Je, Ni Dansi, Mchezo, au Mafunzo ya Kujihami?

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Brazili

“Kunyumbulika na kuonyesha usawaziko kama wanasarakasi, madaha na nguvu za dansi, ustadi na mwendo wa kasi wa pigano, na mdundo wa muziki.”

HIVYO ndivyo mwandishi mmoja alivyoelezea sanaa ya Brazili inayoitwa capoeira. Kulingana na mwandishi mmoja, capoeira imekuwa “sanaa ya ulimwenguni pote.”

Mpangaji-dansi na mtafiti anayeitwa Edward Lunda anaita sanaa hiyo “mchanganyiko wa kipekee wa dansi, mafunzo ya kujihami, mchezo, na mila.” Kichapo The New Encyclopædia Britannica kinaifafanua kuwa “dansi ya kitamaduni.” Inachezwaje? Wachezaji na watazamaji hufanyiza duara, na ndani ya duara hiyo “wanaume wawili hukabiliana, wakiiga ngumi na mbinu za kukwepa ambazo hufanywa katika pigano halisi kupatana na midundo ya berimbau, au uta wa kupigia zeze.”

Ingawa kuna mjadala mkali kuhusu chanzo cha sanaa ya capoeira, watafiti wengi wanaamini kwamba inatokana na dansi za kitamaduni na mila za Kiafrika. Inaonekana kwamba sanaa hiyo iliingia Brazili wakati wa biashara ya utumwa. Kwa miaka mingi, dansi hiyo ilichezwa na watumwa, licha ya kwamba watu waliomiliki watumwa walikandamiza utamaduni wa Kiafrika.

Kulingana na mwandishi mmoja wa Brazili, biashara ya utumwa ilipokomeshwa nchini Brazili mnamo 1888, “watumwa walioachiliwa hawakuweza kuchangamana na jamii wala kujitegemeza kiuchumi.” Kwa sababu hiyo, watu wengi waliokuwa watumwa walijiunga na magenge ya wahalifu. Sanaa ya capoeira ikawa aina fulani ya mapigano ya mtaani. Magenge hayo yaliyojihami kwa visu na fimbo yaliwahangaisha watu.

Jarida Planet Capoeira linasema kwamba dansi hiyo iliyochezewa mitaani ilikuwa yenye jeuri. Linaeleza hivi: “Walimu wa dansi hiyo waliondoa miondoko yote yenye madaha kwa sababu haingemsaidia mtu wakati wa pigano. Kwa mfano, mateke yalipaswa kuwa ya chini yakielekezwa kwenye mwili wala si kichwani. Mikono ilitumiwa katika njia mbalimbali ili kudanganya au kuupiga mwili ngumi au kudunga macho kwa vidole. Hakukuwa na muziki, wala kuvingirika kisarakasi, na sarakasi hazikufanywa ila tu zile ambazo zingeweza kutumiwa kwa mapigano.” Basi haishangazi kwamba sanaa ya capoeira ilipigwa marufuku nchini kote mnamo 1890. Macapoeira waliokamatwa wangefungwa gerezani, wachapwe viboko 300 hivi, au hata wafukuzwe nchini. *

Katika miaka ya 1930, Manuel dos Reis Machado, aliyejulikana kati ya macapoeira kama Mestre Bimba, alifungua shule ya kufundisha sanaa hiyo. Bila shaka, kwa kuwa sanaa hiyo ilikuwa haramu, alikuwa mwangalifu asiseme waziwazi kwamba alikuwa akifundisha capoeira. Mnamo 1937, baada ya kupewa kibali na Rais Getúlio Vargas, wa Brazili, sanaa ya capoeira ilianza kuonwa kuwa mchezo halisi wa Brazili. Leo, inakadiriwa kwamba Wabrazili 2,500,000 hucheza capoeira, na sanaa hiyo hufundishwa katika shule nyingi za umma, vyuo vikuu, na shule za kijeshi.

Je, Ni Dansi ya Kitamaduni au Ni Mafunzo ya Kujihami?

Ingawa watu hucheza capoeira kama dansi, wengi husema kwamba ni mafunzo ya kujihami. Augusto, ambaye alijifunza capoeira na baba yake, anasadiki kwamba “licha ya kuwa aina ya dansi, inachochea jeuri na inapingana na kanuni za amani na upendo.” Anasema: “Ni rahisi kumwumiza mtu kwa kutumia capoeira unapokuwa na hasira.” Hata wakati wachezaji wanapoepuka kugusana, mwondoko fulani usiokusudiwa unaweza kutokeza majeraha mabaya.

Pia wengi huhisi kwamba sanaa ya capoeira ina mambo ya kidini. Pedro Moraes Trindade, ambaye ni gwiji wa capoeira kutoka Jimbo la Bahia, nchini Brazili, anasema kwamba sanaa hiyo “huhusisha mwili na akili.” Anaongeza hivi: “Kwa kusema kwamba capoeira ni mchezo tu, unapunguza mambo yanayohusika katika historia na imani yake.” Edmilson, aliyecheza capoeira kwa miaka minane katika jiji la Niterói, Rio de Janeiro, anasema hivi: “Baadhi ya chulas [nyimbo za kufungua] na mila zinazohusiana na capoeira, zinahusishwa moja kwa moja na kuwasiliana na roho.”

Edmilson na Augusto, waliotajwa awali, walipochunguza kanuni za Biblia kwa uangalifu, waliacha kucheza capoeira. Waliamua kwamba afya yao ya kiroho na ya kimwili ilikuwa yenye thamani sana wasiweze kuihatarisha. Ingawa hapo awali walifurahia midundo na miondoko yenye madaha ya capoeira, wameamua kwamba haipatani na Biblia ambayo huwafundisha watu ‘wasijifunze vita tena.’—Isaya 2:4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Neno la Kireno “capoeira” linarejelea sanaa hiyo au mtu anayeicheza.

[Picha katika ukurasa wa 23]

“Capoeira” huchezwa kulingana na midundo ya ala za kitamaduni za Brazili zinazoitwa “berimbau” na “atabaque”