Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mamba Weupe Wapatikana

Gazeti la India The Hindu linasema kwamba, “maofisa wa msitu katika Mbuga ya Kitaifa ya Bhitarkanika huko Orissa, wamewapata mamba weupe 15 wasiopatikana kwa urahisi . . . wakati wa kuhesabu idadi ya mamba kila mwaka.” Ni nadra sana kuwapata mamba weupe nao “hawapatikani mahali pengine popote ulimwenguni.” Kwa sababu ya uwindaji haramu, mamba hao wa maji ya chumvi walikuwa karibu kutoweka katika miaka ya 1970, lakini serikali ya jimbo ikisaidiwa na programu za Umoja wa Mataifa, ilianzisha miradi ya kufuga mamba katika mbuga hiyo. Programu hiyo ya kuzalisha mamba imefanikiwa sana kwa sababu ya kuwepo kwa mikoko mingi, maji yasiyochafuliwa, chakula kingi, na kwa sababu ni watu wachache tu huingia humo. Kulingana na gazeti The Hindu, sasa kuna mamba 1,500 hivi wenye rangi za kawaida katika mbuga hiyo kwa kuongezea wale wenye rangi nyeupe ambao hawapatikani kwa urahisi.

Tumbaku, Umaskini, na Magonjwa

Gazeti Diario Medico la Kihispania linasema hivi: “Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linaonya kwamba asilimia 84 hivi ya wavutaji-sigara huishi katika nchi maskini ambako kuvuta tumbaku husababisha umaskini, nao umaskini huwafanya watu wavute tumbaku.” Kwa kuongezea, katika kila nchi “wale ambao huvuta sigara sana na kupatwa na matatizo mengi zaidi yanayohusiana na kuvuta tumbaku ni wale walio maskini zaidi.” Ingawa idadi ya watu wanaovuta sigara imepungua katika nchi nyingi zilizoendelea, gazeti hilo linaripoti kwamba ulimwenguni pote, uvutaji wa sigara umekuwa “sababu ya nne kubwa inayotokeza hatari ya kupata magonjwa.” Nchini Hispania ambako kila mwaka watu wapatao 60,000 hufa kutokana na uvutaji tumbaku, zoea hilo limekuwa “kisababishi kikuu cha magonjwa, ulemavu, na vifo vinavyoweza kuepukwa.”

Kondoo Hukumbuka Nyuso

Mtaalamu wa mfumo wa neva Keith Kendrick anaandika hivi katika jarida New Scientist: “Tumegundua kwamba kondoo wanaweza kutambua nyuso za angalau kondoo wengine 50 na za wanadamu 10.” Kendrick na kikundi chake waligundua kwamba baada ya kuona nyuso hizo 60 kwa majuma machache, kondoo walikumbuka nyuso zote “kwa miaka miwili hivi.” Kondoo hao hawakutambua tu nyuso bali sawa na wanadamu waliweza pia “kutambua hisia zilizoonyeshwa na nyuso.” Jarida hilo linaripoti kwamba kondoo “wanaweza kutofautisha kati ya hisia mbalimbali zinazoonyeshwa na wanadamu, na wanaweza kutambua mabadiliko kwenye nyuso za kondoo wenye wasiwasi. Pia wao hupendezwa zaidi na nyuso za wanadamu wanaotabasamu kuliko wale waliokasirika.” Watafiti hao waligundua kwamba kondoo “wanaweza kulinganisha nyuso za wanadamu ambao huwachunga katika njia ileile na za mshiriki mwingine wa kundi la kondoo.” Kendrick anasema: “Kondoo huwaona wanadamu wenye urafiki kama kondoo wenzao. Hilo linaonyesha kwamba kondoo huhisi wana uhusiano wa karibu pamoja na wachungaji wao.”

Uchafuzi wa Australia Unaotokana na Gesi Zinazoongeza Joto

Taasisi ya Australia inasema kwamba, “kati ya nchi zote zilizositawi kiviwanda, watu wa Australia ndio hutokeza gesi nyingi zaidi zinazoongeza joto duniani.” Katika mwaka wa 2001, kila mtu mmoja huko Australia alitokeza wastani wa tani 27.2 za kaboni dioksidi na gesi nyingine zinazoongeza joto duniani. Ripoti kutoka kituo hicho cha utafiti inasema kwamba idadi hiyo kubwa inasababishwa na Australia kutumia sana umeme unaotokezwa kwa kuchoma makaa ya mawe na kupitia magari, kutia ndani utokezaji wa alumini. Nchi zinazoifuata Australia katika kutokeza gesi zinazoongeza joto duniani ni Kanada (tani 22) na Marekani (tani 21.4). Nchi iliyokuwa na kiwango cha chini zaidi katika mwaka wa 2001 ni Latvia kwani mtu mmoja alitokeza tani 0.95 za gesi hizo. Licha ya kwamba Australia ina idadi ndogo ya watu kwa kulinganisha, ripoti hiyo ilisema kwamba nchi hiyo hutokeza gesi zinazoongeza joto duniani “kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko nchi kubwa za Ulaya kama vile Ufaransa na Italia (kila moja ina idadi ya watu mara tatu hivi zaidi ya Australia).”

Nyimbo za Kinega Zashindana na Kelele za Magari

Gazeti la Ujerumani Berliner Zeitung linasema kwamba, “kelele zinapoongezeka, ndege aina ya kinega huimba kwa sauti ya juu zaidi.” Uchunguzi uliofanywa na Henrik Brumm wa Taasisi ya Biolojia kwenye Chuo Kikuu cha Free cha Berlin, ulionyesha kwamba kiasi cha sauti za nyimbo hizo, ambazo hukusudiwa kuonyesha eneo la ndege na kuwavutia ndege wa kike, kilitofautiana kwa desibeli 14 ikitegemea kiasi cha kelele katika eneo hilo. Brumm anasema kwamba “ingawa kiasi hicho kinaonekana kuwa kidogo, kinalingana na ongezeko la mara tano katika mvumo wa sauti, jambo linalomaanisha kwamba lazima mkazo katika mapafu ya ndege uzidishwe mara tano zaidi.” Katika maeneo matulivu, nyimbo za ndege hao zilirekodiwa kuwa desibeli 75. Lakini kwenye maeneo yenye kelele nyingi za magari, ndege hao waliimba kwa desibeli 89. Gazeti hilo lilisema kwamba, “jambo ambalo lilimshangaza hasa mtafiti huyo ni kwamba ndege hao walibadilikana kila siku ikitegemea kelele za magari. Katika miisho-juma, wakati ambapo hakukuwa na magari mengi, kwa kawaida ndege hao waliimba kwa sauti nyororo zaidi kuliko katikati ya juma.”

Jeuri Katika Shule za Poland

Jarida la Poland Zwierciadło, linaripoti kwamba katika mwaka wa 2003, “visa elfu ishirini vya unyang’anyi vilifanywa katika shule [nchini Poland]. Gazeti hilo linaongeza hivi: “Asilimia 80 ya wanafunzi [nchini Poland] hawapendi shule yao kwa sababu wanajihisi upweke na hawana uhusiano mzuri pamoja na walimu na wanafunzi wenzao.” Kwa nini kuna matatizo mengi hivyo? Mtaalamu wa magonjwa ya akili Wojciech Eichelberger anasema hivi: “Shule hazijakingwa na matatizo yaliyo nje, kwani hizo huathiriwa pia na mambo mabaya yanayotendeka katika jamii. Jamii ndiyo huweka viwango vya tabia na kanuni zinazopaswa kufuatwa shuleni.” Eichelberger anapendekeza kwamba ili kutatua tatizo hilo, wazazi wanapaswa kutumia wakati pamoja na watoto wao na hivyo wawafundishe kwamba wanawaona watoto wao kuwa watu muhimu.

Kupambana na Maoni ya Kibinafsi Kuhusu Sura

Gazeti Globe and Mail la Kanada linasema kwamba, “vijana, hasa wasichana, wanapambana na maoni yao kuhusu sura wanapokuwa na umri mdogo sana na hilo linaweza kufanya wapatwe na madhara mabaya sana ya afya.” Wasichana walio na umri wa kati ya miaka 10 hadi 14 walichunguzwa kuhusiana na maoni yao kuelekea kula, na zaidi ya 2,200 wakatoa majibu yao. Gazeti Globe linaripoti hivi: “Asilimia 7 hivi ya wasichana walikuwa wanene kupita kiasi, lakini zaidi ya asilimia 31 walisema kwamba wao ni ‘wanene sana’ na asilimia 29 walisema kwamba wanakula kiasi kidogo ili wapunguze uzito.” Kwa nini wasichana wenye afya nzuri wanataka kupunguza uzito? Kulingana na gazeti hilo, kielelezo kinachowekwa na watu wazima ndicho huwafanya wahisi hivyo, kwani kila mara wao hula chakula kidogo ili kupunguza uzito, nao huwatania watu wanene kupita kiasi. Gazeti Globe linasema, “vyombo vya habari pia huchangia katika kuathiri tabia ya vijana, kwani daima huonyesha kwamba wasichana wenye umbo zuri ni wale wembamba.” Dakt. Gail McVey ambaye ni mwanasayansi wa utafiti katika Hospitali ya Watoto Wagonjwa katika jimbo la Toronto, anasema kwamba watoto, wazazi, na walimu wanapaswa kutambua kwamba “ni jambo la kawaida na linalofaa kwa watoto kuongeza uzito wanapobalehe.”