Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unamjua “Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle”?

Unamjua “Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle”?

Unamjua “Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle”?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

KUTA kubwa zisizo na madirisha huzunguka makao yake ya kifahari. Walinzi waliovaa makoti ya mkia ya rangi ya waridi, vizibao vyekundu, na kofia ndefu nyeusi za hariri wanalinda malango yake. Kamera za ulinzi zilizofichwa huwachunguza wageni wake. “Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle” ni nani, na kwa nini anahitaji kulindwa?

“Bibi Kizee” huyo ni Benki ya Uingereza ambayo ni mojawapo ya vituo vikuu vya biashara ulimwenguni. Lakini kwa nini benki hiyo ikaitwa jina la ajabu hivyo? Barabara ya Threadneedle iko katika sehemu ya London iliyokuwa na wafanyabiashara wengi au wasanii, na yaelekea jina lake linatokana na sindano tatu zilizo katika nembo ya Kampuni ya Kutengeneza Sindano. Miaka mia moja hivi baada ya benki hiyo kuanzishwa, mwanasiasa na mwandishi wa riwaya Richard Sheridan akiwa bungeni alirejelea benki hiyo kuwa “bibi kizee katika jiji lenye sifa nzuri na ambalo limekuwepo kwa muda mrefu.” Mchoraji wa vibonzo James Gillray, alitumia wazo hilo kwamba benki yaweza kuwa kama bibi kizee, na kuanzia wakati huo, benki hiyo ikajulikana kama Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle.

Uhitaji wa Kuwa na Benki ya Taifa

Katika karne ya 17, wafuaji wa dhahabu waliendesha benki nyingi huko London. Mpango huo ulifaulu hadi wafalme wa ukoo wa Stuart walipoanza kukopa pesa bila kulipa. Hatimaye wafuaji mashuhuri wa dhahabu walioendesha benki walifilisika, nayo serikali ikahitaji pesa nyingi ili kutegemeza vita kati yake na Ufaransa.

Kufikia wakati William wa Tatu na Mary wa Pili walipoanza kutawala mnamo mwaka wa 1689, mapendekezo yalikuwa yamefanywa kuwe na benki ya taifa ambayo ingekuwa benki ya serikali na ambayo ingekusanya pesa. Kati ya mapendekezo mengi yaliyotolewa, mwishowe Bunge lilikubali pendekezo la mfanyabiashara Mskoti aliyeitwa William Paterson licha ya upinzani mkali. Wakaaji wa London waliombwa waikopeshe benki hiyo pesa ambazo ilitumainiwa zingekuwa pauni 1,200,000. Nayo serikali ingewalipa wakopeshaji hao riba ya asilimia 8 na kuwafanya Gavana na Msimamizi wa Benki ya Uingereza. Katika majuma mawili, pesa hizo zilipatikana, na mnamo 1694, Benki ya Uingereza ikaanza kazi.

Miaka 40 baadaye, benki hiyo ilihamia Barabara ya Threadneedle. Jengo la sasa, lililoanza kutumika katika miaka ya 1930, lina orofa saba, na maeneo ya kuhifadhi vitu yaliyo chini ya ardhi, nalo limejengwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari tatu.

Nyakati Nzuri na Mbaya

Mwanzoni, benki hiyo ilitoa risiti zilizoandikwa kwa mkono juu ya karatasi ya benki kwa ajili ya wateja walioweka pauni zao, shilingi, na senti. Mtu yeyote angeweza kubadilishiwa noti hizo ziwe dhahabu au sarafu ikiwa angezileta kwenye benki. Bila shaka, ikiwa kila mtu angeitisha pesa zake wakati uleule, benki hiyo ingefilisika. Benki hiyo ilikuwa karibu kufilisika mara kadhaa. Kwa mfano, kufikia mwaka wa 1797, vita vingine kati ya Uingereza na Ufaransa vilikaribia kuifilisi nchi. Wawekezaji walipoondoa akiba zao kwa sababu ya kuwa na wasiwasi, pesa zilizokuwa katika benki hiyo zilikwisha na ikalazimika kutumia noti zenye thamani ya chini badala ya dhahabu kwa miaka 24 iliyofuata. Ilikuwa katika kipindi hiki cha kuzuia dhahabu isitolewe kwamba benki hiyo ilipewa jina la utani Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle. Noti hizo za benki zilizotengenezwa harakaharaka zilifanya iwe rahisi kutokeza noti bandia, lakini siku hizo adhabu ya kufanya hivyo ilikuwa kali sana. Zaidi ya watu 300 walinyongwa kwa sababu ya kutengeneza noti bandia.

Benki hiyo pia iliponea chupuchupu tatizo la aina nyingine. Mnamo 1780, watu wenye fujo jijini London walijaribu kuvamia jengo hilo. Baada ya hapo, kila usiku hadi mwaka wa 1973, askari walilinda jengo hilo na kuhakikisha kwamba dhahabu ya nchi ilikuwa salama.

Katika karne ya 19, pauni ya Uingereza na noti za Benki ya Uingereza zilikuwa pesa zenye thamani zaidi ulimwenguni. Hata hivyo, Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilibadili hali hiyo. Gharama kubwa ya vita hivyo iliharibu nchi vibaya sana. Wawekezaji wengi waliharakisha kubadili noti zao kwa dhahabu hivi kwamba sarafu za dhahabu zikatoweka. Mahali pake pakachukuliwa na noti za benki zenye thamani ndogo. Sarafu za dhahabu zilizotumiwa kila siku zilipotelea mbali. Mnamo 1931, Uingereza iliacha kabisa kutumia dhahabu kuwa kiwango, na hiyo ilimaanisha kwamba pesa za Uingereza hazingeweza kulinganishwa na kiasi fulani hususa cha dhahabu.

Tangu kuanzishwa kwake, benki hiyo ilikuwa kampuni iliyomilikiwa na watu binafsi. Hata hivyo, mnamo 1946, benki hiyo ilitwaliwa na serikali.

“Bibi Kizee” Aendelea Kuwa na Shughuli Nyingi

Benki ya Uingereza ni benki kuu. Hiyo hutenda kama benki ya serikali, ikiishauri kuhusu sera za kifedha na kuhakikisha kwa kadiri iwezavyo kwamba pesa zinadumisha thamani yake kwa kutoza viwango vya riba vinavyofaa. Wateja wake wengine ni benki za biashara na benki kuu za nchi nyingine. Akiba ya dhahabu ya nchi hulindwa katika sehemu za kuhifadhia pesa zilizo chini ya ardhi katika benki hiyo. Benki hiyo husimamia kuchapishwa kwa noti mpya nje ya jiji la London, katika sehemu nyingine yenye usalama.

Jiji la London ambalo liko katikati ya kanda za wakati za ulimwengu huwa na shughuli nyingi kila wakati. Benki hiyo hutimiza fungu muhimu katika jiji hilo. Shughuli ambazo huendeshwa ndani ya jengo hilo lisilo na madirisha huathiri vituo vingine vya kibiashara ulimwenguni pote. Naam, “Bibi Kizee wa Barabara ya Threadneedle” anaendelea kuwa na shughuli nyingi, huku akidhibiti daima uchumi wa taifa hilo.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Idhini ya kwanza ya benki, 1694

[Picha katika ukurasa wa 24]

Noti ya pauni tano iliyoandikwa kwa mkono, 1793

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kwenya Barabara ya Threadneedle, 1794

[Picha katika ukurasa wa 24]

Sarafu ya dhahabu ya pauni moja, 1911

[Picha katika ukurasa wa 24]

Sehemu ya kibonzo cha kwanza cha James Gillray, 1797

[Picha katika ukurasa wa 25]

Noti ya shilingi kumi, 1928

[Picha katika ukurasa wa 25]

Jengo la sasa, tangu 1939