Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vijana Wanakabili Hatari

Vijana Wanakabili Hatari

Vijana Wanakabili Hatari

▪ Nchini Marekani, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 awafyatulia wanadarasa wenzake risasi na kuwaua 2 kati yao na kuwajeruhi 13.

▪ Nchini Urusi, kikundi cha vijana waliolewa wanamwua kikatili msichana mwenye umri wa miaka tisa na kumpiga baba yake na binamu yake.

▪ Nchini Uingereza, mvulana mwenye umri wa miaka 17 ampiga na kumchoma kisu kijana mwingine mdogo. Anawaambia polisi hivi: “Mwanzoni, sikutaka kumwua, lakini nilipoona damu nilishindwa kujizuia.”

VISA hivi vyenye kushtua ni vya kawaida. Makala moja katika gazeti Professional School Counseling inasema “jeuri inayofanywa na vijana ni tatizo kubwa katika jamii yetu.” Takwimu zinaunga mkono jambo hilo.

Kituo cha Kitaifa cha Takwimu za Elimu cha Marekani kinasema kwamba ingawa visa vya jeuri inayofanywa shuleni vimepungua, “wanafunzi wenye umri kati ya miaka 12 hadi 18 walipatwa na visa karibu milioni 2 vya wizi au vya jeuri ambayo haikusababisha kifo wakiwa shuleni katika mwaka wa 2001.” Kudhulumiwa shuleni pia kumeongezeka.

Lakini jeuri inayofanywa na vijana nchini Marekani haiwapati wanafunzi peke yao. Ripoti hiyo inasema, “katika kipindi cha zaidi ya miaka 5 kuanzia 1997 hadi 2001, walimu walipatwa na visa milioni 1.3 hivi vya jeuri isiyosababisha kifo shuleni, kutia ndani visa 817,000 vya wizi na visa 473,000 vya jeuri ya kikatili.” Isitoshe, “asilimia 9 ya walimu wa shule za msingi na wa sekondari walitishwa kuumizwa na mwanafunzi, na asilimia 4 kati yao walishambuliwa na mwanafunzi.”

Hali ikoje katika nchi nyingine? Shirika moja la habari linaripoti kwamba, “katika mwaka wa 2003, vijana 69,780 waliovunja sheria walikamatwa nchini China, ongezeko la asilimia 12.7 zaidi ya waliokamatwa katika mwaka wa 2002.” Ripoti hiyo inasema kwamba “asilimia 70 ya vijana walivunja sheria wakiwa katika kikundi.” Pia, ripoti moja kutoka Japani katika mwaka wa 2003 ilisema kwamba vijana walihusika katika nusu ya visa vya jeuri vilivyofanywa katika miaka kumi iliyopita.

Dawa za Kulevya Zinadhuru Miili ya Vijana

Jambo jingine linaloonyesha kwamba vijana wengi wanakabili hatari ni jinsi wanavyodhuru miili yao kwa dawa za kulevya. Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya ya Marekani inasema kwamba karibu nusu ya vijana wote nchini humo wamewahi kutumia dawa fulani ya kulevya isiyo halali kabla ya kumaliza shule ya sekondari. Ripoti hiyo inaongeza hivi: “Vijana wengi sana leo hutumia vinywaji vinavyolevya. Karibu wanafunzi wanne kati ya watano (asilimia 77) wametumia vinywaji hivyo (si kuonja tu) kufikia wakati wanapomaliza shule ya sekondari; na karibu nusu yao (asilimia 46) wamevitumia kufikia wakati wanapoingia darasa la nane.”

Ngono za Ovyoovyo

Bila shaka, ngono za ovyoovyo ni hatari wakati huu ambapo UKIMWI umeenea. Hata hivyo, vijana wengi wanaona ngono kuwa mchezo usio hatari. Kwa mfano, vijana fulani nchini Marekani hutumia neno la utani “kula uroda” linalomaanisha kwamba kufanya ngono ovyoovyo ni raha isiyoweza kudhuru. Wao huzungumza kuhusu kuwa na “mshikaji,” yaani, kuwa na mtu wa kufanya ngono naye bila kuwajibika kwake.

Mwandishi Scott Walter anaeleza kuhusu karamu za ngono ambazo vijana fulani wanaoishi katika vitongoji vya miji huandaa wazazi wao wanapokuwa kazini. Kwenye karamu moja kama hiyo, msichana mmoja alitangaza kwamba “atafanya ngono na wavulana wote waliokuwapo. . . . Watoto wadogo wenye umri wa miaka 12 walihusishwa katika karamu hizo.”

Je, hilo linashangaza? Haliwashangazi wataalamu ambao wamechunguza tabia ya vijana ya kufanya ngono. Dakt Andrea Pennington anaandika hivi: “Katika zaidi ya miaka 20 ambayo imepita, tumeona umri wa wastani ambao vijana hufanya ngono ukipungua. Limekuwa jambo la kawaida kwa wavulana na wasichana wenye umri wa miaka 12 kuanza kufanya ngono.”

Ripoti ambayo hasa inatia wasiwasi ilichapishwa katika gazeti USA Today: “Vijana wadogo wengi zaidi nchini humu . . . wanafanya ngono ya kinywa. . . . Watoto hao wanaamini kwamba ‘huko si kufanya ngono.’” Kulingana na uchunguzi fulani waliofanyiwa wasichana 10,000, “asilimia 80 kati yao walisema kwamba wao ni mabikira, ijapokuwa asilimia 25 walikuwa wamefanya ngono za kinywa. Na asilimia 27 walisema kwamba hilo ni ‘jambo ambalo mtu hufanya na mshikaji wake ili kujifurahisha.’”

Mtazamo huo kuhusu ngono umeanza kuathiri maeneo mengine. Shirika la UNESCO linaripoti kwamba, “ni rahisi kwa vijana wengi wa Asia kupata virusi vya UKIMWI kwa kufanya ngono na watu wa jinsia zote kwa sababu wengi wanaanza kufanya ngono wakiwa na umri mdogo.” Ripoti hiyo inaongeza hivi: “Vijana wengi zaidi wanapuuza kanuni za wazazi wao za Kiasia kwa kufanya ngono kabla ya ndoa, mara nyingi wakifanya hivyo na watu tofauti-tofauti.”

Kuna dalili gani nyingine kwamba vijana wanataabika? Gazeti la Kanada Women’s Health Weekly linaripoti: “Asilimia 25 ya wasichana kati ya umri wa miaka 16 hadi 19 watapatwa na kisa kimoja cha kushuka moyo sana.” Hata hivyo, mshuko-moyo ni ugonjwa unaowapata watu wa jinsia zote. Kulingana na U.S.News & World Report, kila mwaka, vijana elfu tano hujiua. Kwa sababu fulani, ripoti hiyo inasema, “wavulana sita zaidi ya wasichana, hujiua.”

Bila shaka, vijana wa leo wanakabili hatari sana. Ni nini kinachosababisha hali hiyo?

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

STR/AFP/Getty Images