Bonde Linalochanua Maua
Bonde Linalochanua Maua
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UKRAINIA
WAKATI wa masika, bonde dogo lenye rutuba katika Milima ya Carpathia, hujaa maua meupe. Wakati mzuri wa kutembelea bonde hilo ni mwishoni mwa masika, wakati harufu nzuri inayowavutia wageni inapotanda katika bustani hiyo iliyo milimani.
Mandhari hiyo yenye kuvutia iko wapi? Katika Bonde la Narcissi—hifadhi ya kiasili karibu na Khust, Magharibi mwa Ukrainia. Bonde hilo lina bustani kubwa sana yenye mayungiyungi ya mwituni (narcissi). Ingawa kuna zaidi ya jamii 400 za mimea katika bonde hilo, mayungiyungi hayo ya mwituni ndiyo maarufu zaidi.
Kwa kweli, hifadhi hiyo huitwa kwa jina la maua hayo, ambayo pia huitwa narrow-leaved narcissi, au daffodil. Mmea huo ulio na umbo la kitunguu, wenye majani membamba marefu, petali nyeupe au za manjano, na unaofanana na tarumbeta, hupatikana kotekote katika milima ya Alps na Balkani.
Maua ya narcissi yamesifiwa kwa karne nyingi na washairi na wanamuziki. Aina moja ya maua hayo inaitwa Narcissus poeticus, au narcissi ya washairi. Lakini watu wengine wamevutiwa na umaridadi wake mbali na washairi. Katika Roma la kale, wakati fulani watawala walitumia maua ya manjano kuwakaribisha mashujaa walioshinda. Huko Prussia, maua hayo yalikuwa ishara ya upendo na furaha. Leo, jamii mbalimbali ulimwenguni pote husifu umaridadi wa maua hayo katika sherehe na sikukuu za kila mwaka.
Hata hivyo, maua hayo yana faida nyingi mbali na kuwa maridadi. Jina narcissi linatokana na neno narkeo la Kigiriki linalomaanisha, “kupumbazwa.” Je, kweli maua hayo yanaweza kumpumbaza mtu? Maua hayo yanapochanua katika Bonde la Narcissi, harufu yake inaweza kuwapumbaza au hata kuwalewesha kidogo wageni!
Kwa sababu maua hayo yana harufu inayoweza kulewesha, watu fulani wamedai kwamba yanaweza kutumiwa kama dawa. Waarabu walitumia mafuta ya maua hayo kutibu upara, nao Wafaransa waliyatumia kutibu kifafa na ugonjwa wa akili. Leo, mafuta ya maua hayo hutumiwa kutengeneza manukato, nayo harufu ya mafuta hayo yaliyosafishwa hutumiwa kutibu magonjwa fulani.
Je, Litahifadhiwa?
Maua hayo yenye majani membamba husitawi sana katika milima mirefu. Kwa kawaida hukua kwenye kimo cha kati ya meta 1,100 na 2,060 juu ya usawa wa bahari. Lakini Bonde la Narcissi liko kwenye kimo cha meta 200 juu ya usawa wa bahari, na ndilo bonde la chini zaidi lenye maua hayo.
Ili kuhifadhi maajabu hayo ya uumbaji, Bonde la Narcissi lilitengwa kuwa hifadhi mwaka wa 1979. Miaka 20 baadaye, Baraza la Ulaya lilitangaza maua hayo yenye majani membamba kuwa jamii ya mimea inayolindwa.
Mwanzoni, ilikuwa marufuku kukata nyasi katika Bonde la Narcissi baada ya maua kuchanua. Hata hivyo, baada ya miaka michache, idadi ya maua ilipungua. Kwa nini? Wanasayansi waligundua kwamba nyasi inapokua bila kukatwa inazuia maua machanga kuchipuka. Nyasi ilipoanza kukatwa, bonde hilo lilirudia hali yake ya asili. Sasa bonde hilo ni maridadi wakati wa masika, na huandaa chakula kinacholiwa na mifugo wakati wa baridi kali.
Maua hayo yenye kupendeza sana huonyesha kwamba dunia yetu inaweza kuwa maridadi. Kwa kweli, wanafunzi wengi wa Biblia wanatazamia wakati ambapo chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, “nyika na nchi isiyo na maji itafurahi; na nchi tambarare ya jangwani itakuwa na shangwe na kuchanua maua” yenye kupendeza. (Isaya 35:1) Kisha, uzuri kama ule wa Bonde la Narcissi utaonekana dunia itakapokuwa paradiso kama bustani ya Edeni ilivyokuwa mwanzoni.—Mwanzo 2:8-15.