Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Shomoro Aliyejeruhiwa Apata Makao Mapya

Shomoro Aliyejeruhiwa Apata Makao Mapya

Shomoro Aliyejeruhiwa Apata Makao Mapya

“JE, KWELI tunahitaji kazi ya ziada?” Hivyo ndivyo nilivyohisi mwanzoni mke wangu alipomleta nyumbani shomoro mdogo aliyeanguka kutoka kwenye kiota chake. Nilipomtazama, nilibadili maoni yangu na kumhurumia ndege huyo aliyekuwa akitetemeka. Hata hivyo, bado nilijiuliza ikiwa ndege huyo dhaifu angepona. *

Mwanzoni, ilibidi tumbembeleze mgeni wetu ale chakula kilichopondwa-pondwa ambacho tulimtengenezea. Lakini siku iliyofuata, shomoro huyo mdogo alililia chakula. Mlio wake ungeweza kusikiwa kwenye ngazi nje ya nyumba yetu yenye mlango wenye sehemu mbili!

Manyoya yake yalionyesha kwamba shomoro wetu alikuwa wa kike. Baada ya muda, alipata nguvu na akaanza kuruka. Hata hivyo, jitihada zetu za kumrudisha kwenye makao yake ya asili hazikufanikiwa! Tuliwaza, ‘Pengine bado hana ujasiri wa kuondoka nyumbani kwetu.’ Kwa hiyo tulinunua tundu la ndege na kumfanya shomoro wetu mdogo kuwa mnyama kipenzi. Tulimwita “Spatzi” neno la Kijerumani linalomaanisha “shomoro.”

Siku moja tulipika wali, mlo ambao inaonekana Spatzi alipenda. Kwa kuwa ulikuwa bado moto, mke wangu aliuweka kando na kumpa Spatzi mbegu fulani. Ndege wetu mdogo alifanya nini? Aliinamisha kichwa chake na kwa mdomo wake akazisukuma mbegu hizo zilizokuwa mezani na kuziangusha chini! Mimi na mke wangu tulitazamana kwa mshangao na kucheka. Mara moja, tulimwekea Spatzi wali uliopoa, naye akaridhika na chakula hicho!

Kumtunza ndege huyo mdogo mwenye kupendeza kulitukumbusha maneno ambayo Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Je, shomoro wawili hawauzwi kwa sarafu ya thamani ndogo? Na bado hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini bila Baba yenu kujua.” Kisha Yesu akawaambia: “Msiogope: ninyi ni bora kuliko shomoro wengi.”—Mathayo 10:29-31.

Inafariji kama nini kujua kwamba Yehova huona taabu zetu na kukumbuka uvumilivu wetu! (Isaya 63:9; Waebrania 6:10) Naam, huruma tunayomwonyesha ndege mdogo ni ndogo sana ikilinganishwa na upendo ambao Yehova Mungu huwaonyesha wale wanaomtumikia!—Tumetumiwa makala hii.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Katika visa fulani, kumtunza ndege mgonjwa au aliyejeruhiwa kunaweza kuwa hatari kwa afya au kinyume cha sheria za nchi.