Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kahawa ya Kona Yenye Ladha Nzuri

Kahawa ya Kona Yenye Ladha Nzuri

Kahawa ya Kona Yenye Ladha Nzuri

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hawaii

WATU wanaotembelea wilaya ya Kona kwenye kisiwa cha Big Island cha Hawaii hupata fursa ya kuonja mojawapo ya kahawa bora zaidi ulimwenguni, yaani, kahawa ya Kona, ambayo huonwa na watu wengi kuwa kahawa yenye ladha nzuri.

Katika eneo la mauka (mlimani) lenye barabara nyembamba zinazojipinda-pinda, kuna maelfu ya ekari za kahawa zilizopandwa kwenye miteremko ya milima. Miti hiyo ina majani yenye kung’aa inayovutia, na nyakati fulani katika mwaka, maua meupe madogo yenye kunukia huchanua. Mwishowe, maua hayo huzaa matunda ambayo wakulima na watengenezaji wa kahawa huyaita buni.

Mashamba makubwa na madogo—zaidi ya 600—yaliyo karibu-karibu humilikiwa na familia, na baadhi ya mashamba hayo yamerithishwa kutoka kizazi hadi kizazi! Ukanda unaolimwa kahawa katika kisiwa cha Big Island ni mkubwa sana kwani unakadiriwa kuwa na upana wa kilometa moja na nusu na urefu wa kilometa 50 hivi. Ukanda huo uko kwenye miteremko ya milima miwili ya volkeno ya kale, Hualalai na Mauna Loa. Kahawa hukua vizuri katika maeneo yenye mwinuko wa meta 150 na 750.

Sehemu maarufu za kutalii, maduka makubwa, maduka madogo ya mashambani, na mikahawa ya vijijini iliyo kando ya barabara huko Hawaii huuza kahawa hiyo yenye ladha nzuri. Wanywaji wa kahawa wa muda mrefu huipenda kwa sababu ya harufu yake nzuri na ladha yake tamu. Lakini kahawa ilianzaje kukuzwa katika eneo hilo ambalo wakati mmoja lilitawaliwa na ukoo fulani wa kifalme, nayo ilipataje kuwa biashara yenye kuleta faida kubwa sana?

Inasemekana kwamba Francisco de Paula Marín, daktari na msaidizi wa Mfalme Kamehameha wa Kwanza, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuleta na kupanda kahawa katika kisiwa cha Oahu katika mwaka wa 1813. Hatimaye, yapata mwaka wa 1828, vipandikizi vya mibuni ya Oahu vilipandwa katika wilaya ya Kona ya Big Island. Vipandikizi hivyo vilikuwa vya kahawa aina ya arabica, ambayo bado hukuzwa huko Kona. Kufikia miaka ya 1830, kahawa ilikuwa ikikuzwa sana huko Kona na kuuzwa.

Kwa Nini Kahawa Husitawi Katika Wilaya ya Kona?

Ingawa umeainishwa kuwa kichaka, mbuni (1) unaweza kukua kufikia kimo cha meta 10. Hivyo, watu wengi huuita mti. Wilaya ya Kona ina mazingira mazuri ya ukuzaji wa kahawa. Hii ni kwa sababu pepo za msimu huvuma kutoka upande wa mashariki wa kisiwa hicho. Zinapopiga upande wa mashariki wa mlima Mauna Loa, ambao una urefu wa meta zaidi ya 4,000, pepo hizo huwa zenye uanana. Kisha pepo hizo huvuma kwenye mlima kuelekea eneo la Kona kwa utaratibu hivi kwamba haziharibu maua madogo ya mibuni yanayochanua.

Jua huangaza vizuri kwenye miteremko ya Kona, na mara nyingi wakati wa alasiri, mawingu hutokeza kivuli ambacho hukinga mibuni kutokana na jua kali. Kisha wakati wa alasiri mawingu hayo hutokeza rasharasha za kutosha mibuni hiyo. Kwa kuwa hali ya hewa ni ya kadiri mwaka mzima, hakuna hatari ya buni kuganda.

Kuvuna na Kutayarisha Kahawa

Inachukua muda gani kupanda kahawa, kuivuna na kuiuza? Kwa kawaida, angalau miaka mitatu hupita kabla mmea wa kahawa haujaanza kuzaa vizuri. Mibuni huchanua maua mara nyingi katika mwaka. Kwa hiyo, kila mwaka lazima mkulima wa kahawa avune kwa mikono mara nane au zaidi!

Kwa kawaida, tunda lenye nyama huwa na mbegu mbili, au buni za kahawa. Kwa kuwa buni hizo huwa zimefunikwa na ngozi nyembamba, ni lazima zisafishwe ili kuondoa nyama na ngozi hiyo (2). Kisha hulowekwa kwenye maji (3) na kukaushwa (4). Baada ya hatua hizo, buni zilizobaki huwa chache kuliko zilizovunwa. Ikitegemea ubora wa kahawa, magunia manane ya buni yanaweza kutokeza gunia moja tu la kahawa iliyokaangwa.

Kukaanga (5) buni ni ufundi unaohitaji vifaa bora na pia ustadi mkubwa. Mambo kama vile unyevunyevu, uzito, gredi, ubora wa buni, weusi unaotakiwa wa buni, na hali ya hewa ndiyo huamua kahawa itakaangwa kwa muda gani.

Mashamba na viwanda vingi vya kahawa huko Big Island hutumia mbinu za kisasa za kuuza kahawa. Viwanda hivyo hualika watu watembelee mashamba hayo, watazame jinsi kahawa ya Kona inavyotayarishwa, na waionje. Ishara maridadi za barabarani na viwanda vya zamani vyenye kuvutia pamoja na mikahawa na hoteli za zamani bado zipo. Bila shaka, zote huuza kahawa ya Kona!

Hapo awali punda ambao ni wanyama wapole walitumiwa kubeba magunia ya kahawa. Baadaye magari ya jeshi aina ya jeep yalitumiwa, na mwishowe watu wakaacha kuyatumia. Lakini bado kuna punda wachache wanaoishi mwituni ambao wanalindwa na sheria. Na bado kuna magari aina ya jeep yaliyoharibika kwenye nyua za wakulima.

Kuboreshwa kwa Soko la Kahawa ya Kona

Kwa miaka mingi kahawa ya Kona ilichanganywa na kahawa za gredi ya chini na kuuzwa ikiwa hivyo. Hata hivyo, katikati ya miaka ya 1950 kulikuwa na badiliko kubwa. Bei ya kahawa ulimwenguni ilipanda, na mazao ya kahawa ya Kona kwa ekari yalikuwa ya juu. Kupitia Mradi wa Chuo Kikuu cha Hawaii, wakulima walitiwa moyo wakuze kahawa zaidi, na wakulima, watengenezaji, watafiti, na walimu kutoka chuo hicho kikuu walibadilishana maoni kuhusu ukuzaji wa kahawa.

Kulikuwa na matokeo mazuri sana. Tangu mwaka wa 1970, polepole kahawa ya Kona iliacha kuwa kahawa iliyochanganywa na kahawa za gredi ya chini na kuwa kahawa bora yenye ladha nzuri sana iliyouzwa nchini humo na pia kimataifa. Hilo limefanya kahawa hiyo iwe ya bei ghali. Mikataba kuhusu bidhaa zinazouzwa ulimwenguni pote imewasaidia wakulima kwa kuwa imefanya bei ya kahawa kuwa imara na kuzuia isibadilike-badilike. Sheria inayolinda kuzalisha na kuuzwa kwa kahawa yenye kibandiko, “Kahawa ya Kona” imesaidia kuuzwa kwa bidhaa hiyo, na sasa wakulima wengi wa kahawa hiyo hupata faida nyingi kwa kuuza kahawa yao kupitia Intaneti.

Maonyesho ya Kahawa ya Kona

Sasa, kila mwaka Maonyesho ya Kitamaduni ya Kahawa ya Kona huwaalika watu washiriki katika maonyesho yenye kuvutia ya kahawa. Kuna mashindano ya mapishi mbalimbali ya kahawa ya Kona, mashindano ya gofu, na tamasha nyingine nyingi. Tamasha kuu katika maonyesho hayo huwa mashindano ya kuonja kahawa, ambapo wataalamu huonja na kuamua kahawa yenye ladha bora. Mashindano hayo huwa makali sana kwa kuwa tuzo zinazotolewa zaweza kuchangia sana kuongeza mauzo ya kahawa za washindi.

Yafuatayo ni maelezo kutoka kwenye maonyesho hayo kuhusu jinsi ya kutayarisha “kikombe murua cha kahawa ya Kona”: “Njia bora zaidi ya kupika kahawa ni kutumia mashini maalumu yenye kichujio cha karatasi. Tumia maji safi, baridi. Ongeza kijiko kikubwa cha kulia cha Kahawa ya Kona kwenye mililita 178 za maji. Ili kupata ladha bora zaidi, weka kahawa iliyochemshwa ikiwa vuguvugu na inywe katika muda wa saa moja.”

Je, ungependa kuionja? Ikiwa ungependa, utakuwa ukinywa kahawa ambayo wengi huiona kuwa bora zaidi ulimwenguni, yaani, kahawa ya Kona yenye ladha nzuri!

[Ramani katika ukurasa wa 25]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kona

[Hisani]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Wilaya ya Kona

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mbuni wachanua maua

[Picha katika ukurasa wa 26]

Tunda

[Picha katika ukurasa wa 26]

Buni

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ngozi imetolewa

[Picha katika ukurasa wa 26]

Iliyokaangwa