Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kutumia Mtandao Kuwaonea Wengine

Vijana wengi hutumia simu za mkononi na Intaneti kuwasiliana. Kwa kuwa watu wanaotumia mtandao kuwaonea wengine wanaweza kutumia barua-pepe, au watume ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi au kupitia mfumo wa kompyuta wa kuwasiliana haraka, gazeti Maclean’s la Kanada linasema hivi: “Vifaa hivyo vinaweza kuharibu uhusiano wao pamoja na wengine. Robo ya vijana wa Kanada wanaotumia Intaneti wanaripoti kwamba wamepokea habari zilizosema mambo yenye chuki kuhusu wengine.” Kuwaonea wengine katika njia hiyo kumefanya polisi wawakumbushe watu kwamba ni hatia kutisha kuwaua wengine kupitia maandishi. Gazeti Maclean’s linawashauri wazazi wazungumze na watoto wao kuhusu watu wanaowasiliana nao kwenye Intaneti au vituo wanavyofungua na waweke kompyuta mahali palipo wazi ambapo wanaweza kuona watoto wanasoma au kutuma ujumbe gani. Ripoti hiyo inawaonya watoto wasijibu kamwe ujumbe kutoka kwa watu wanaowaonea wengine na “wasimpe yeyote neno lao la siri wanalotumia kufungua kompyuta, hata ikiwa ni marafiki wao wa karibu zaidi,” ili kuzuia watu wengine wasipate habari zao za kibinafsi.

Magari Mengi—Matatizo Mengi

Gazeti China Daily linasema kwamba, “China inaacha kutumia baiskeli na kuanza kutumia magari.” Kwa sasa, kuna magari 20 kwa watu 1,000 nchini China, ikilinganishwa na uwiano wa ulimwenguni pote wa watu 120 kwa magari 1,000. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka sana. Chen Qingtai, naibu mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo cha Baraza la Kitaifa, anaamini kwamba maisha ya watu wengi yataboreka wakiwa na magari. Lakini pia Chen anaona kwamba kutakuwa na matatizo haya: “Ikiwa hatutaweza kuzuia kabisa moshi wa magari, moshi huo ndio utakaochafua majiji bali si makaa ya mawe.” Katika baadhi ya majiji nchini China, magari ndiyo yanayotoa kiwango kikubwa zaidi cha kaboni monoksidi na nitrojeni oksidi. Jitihada zinafanywa ili kupunguza uchafuzi kabla ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2008 itakayofanywa Beijing.

Ndoa Bandia

Gazeti Sowetan la Johannesburg linaripoti kwamba zaidi ya wanawake 3,000 nchini Afrika Kusini wameingia katika “ndoa” bila kujua. Katika kisa kimoja, wanawake walifikiri kwamba walikuwa wakitia sahihi mkataba wa kazi, lakini kwa kweli walikuwa wakitia sahihi cheti cha ndoa. Cheti hicho kinampa “bwana harusi” ambaye si raia wa nchi hiyo kibali cha kuishi nchini humo. Huenda “bibi harusi” akagundua udanganyifu huo anapoenda kutafuta vitambulisho vilivyopotea na kugundua kwamba ana jina tofauti la familia, au katika siku anayofunga ndoa halisi, anagundua kwamba tayari ameandikishwa kuwa ameolewa! Inaweza kuwa vigumu kuvunja “ndoa” hiyo. Hata hivyo, wanawake 2,000 hivi wamefanikiwa kuvunja ndoa hizo bandia. Ili kuzuia jambo hilo, sheria mpya inamtaka mwenzi ambaye si raia wa nchi hiyo asubiri kwa miaka mitano kabla ya kuomba uraia.

Uvumbuzi Usio wa Kawaida

Wavumbuzi wa vitu vya kale wanaochunguza mapango karibu na Bahari ya Chumvi walivumbua vito na vitu vingine vinavyofikiriwa kuwa vya miaka 2,500 iliyopita, kipindi ambacho Wayahudi walirudi katika nchi yao kutoka utekwani Babiloni. Wavumbuzi hao kutoka Chuo Kikuu cha Hebrew huko Jerusalem na wa Chuo Kikuu cha Bar Ilan huko Ramat Gan, walipata vitu hivyo kwa kutumia chombo cha kunasia vyuma. Kati ya hazina zilizogunduliwa ni kioo kidogo cha shaba, kidani cha fedha, mkufu wa dhahabu, shanga zenye mawe ya thamani ya kadiri, nishani ya ageti ya Babiloni, na stempu yenye picha ya kuhani Mbabiloni akisujudia mwezi, linasema shirika la habari la Associated Press. Tsvika Tsuk ambaye ni mvumbuzi mkuu wa Halmashauri ya Kulinda Mbuga za Kitaifa na Mazingira ya Israeli alisema hivi: “Uvumbuzi huo si wa kawaida. Ni vigumu sana kwa wavumbuzi kupata vitu vingi hivyo vya kale vyenye thamani hasa vya kipindi hicho.”

Watoto Wanaweza Kupatwa na Kiharusi

Gazeti Vancouver Sun linaripoti kwamba “angalau mtoto mmoja hupatwa na kiharusi kila siku nchini Kanada.” Mtaalamu wa mfumo wa neva Gabrielle deVeber ambaye pia ni mkurugenzi wa Usajili wa Watoto Wenye Ugonjwa wa Moyo nchini Kanada anasema kwamba watoto wanaopatwa na kiharusi wanapaswa kutibiwa mara moja la sivyo, “watapatwa na matatizo makubwa ya ugonjwa huo na madhara ya mfumo wa neva.” Kulingana na gazeti hilo, “lazima mtu apewe dawa zinazoondoa tatizo la kuganda kwa damu kabla ya muda wa saa tatu baada ya kupatwa na kiharusi.” Lakini ‘mara nyingi kiharusi kinachowapata watoto hudhaniwa kuwa kifafa au kipandauso.’ Gazeti hilo linasema kwamba dalili za kiharusi zinatia ndani “kufa ganzi au kudhoofika, hasa upande mmoja wa mwili, kuchanganyikiwa, tatizo la kuongea, kutoona, kizunguzungu, na kuumwa na kichwa sana ghafula.” Kiharusi cha watoto kinaweza kusababishwa na matibabu fulani ya ugonjwa wa moyo na kansa, na wataalamu fulani wanashuku kwamba “kunenepa kwa watoto kupita kiasi na kula vyakula vyenye mafuta mengi” kunaweza kutokeza hatari hizo.

Vyakula na Vinywaji Vyenye Sumu

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na shirika la mazingira la Toxics Link, watu wanaoishi Asia Kusini wanakula vichafuzi hatari katika vyakula vyao vya kawaida, linaripoti gazeti la India, The Hindu. Uchunguzi huo uligundua vitu vilivyopigwa marufuku au vilivyodhibitiwa katika vyakula vya kawaida kama vile nyama, vikolezo, na mafuta. Vitu vyenye kuchafua mazingira ambavyo haviwezi kuondolewa kwa urahisi kama vile kemikali ya polychlorinated biphenyls (PCB) vimeingia kwenye mazingira ‘pengine kupitia transfoma na kapasita zilizotupwa ovyoovyo kabla ya PCB kupigwa marufuku’ au kemikali hizo hutokezwa kwenye maeneo ya kuharibia meli, yasema ripoti hiyo. Uchunguzi mwingine uligundua dawa ya DDT kwenye mboga na samaki waliokaushwa. Ripoti hiyo inasema kwamba licha ya mikataba ya kimataifa ya kudhibiti hatari hizo, ‘viwango vikubwa vya kemikali za DDT, HCB, Aldrin, Dieldrin, [Dioxin], Furan na PCB vimepatikana katika maziwa ya mama, mafuta na damu ya wanadamu.’

Bunduki Zinabadili Jamii

Gazeti la London, The Independent linasema kwamba, “kuenea kwa silaha, hasa silaha ndogo, ndiko husababisha kifo cha mtu mmoja kila dakika na vifo vya watu zaidi ya 500,000 kila mwaka [ulimwenguni pote]. Katika mwaka wa 2001, silaha za kijeshi bilioni 16 zilitengenezwa, nazo zinatosha kuua kila mtu duniani mara mbili.” Karibu silaha milioni nane hutengenezwa kila mwaka, na nyingi kati ya silaha hizo kwa ajili ya kutumiwa na raia. Kama utafiti uliofanywa na mashirika ya Amnesty International, Oxfam, na Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Silaha Ndogo unavyoonyesha, “jamii ambazo hapo awali zilikuwa zenye amani na zilizosuluhisha mabishano yao kwa ngumi na visu sasa zinatumia bunduki.” Katika nchi moja, bunduki za rashasha zinatumiwa kama pesa. Katika nchi nyingine, mwalimu mmoja aliyekuwa akimfundisha mwanamke mmoja mzee Kiingereza alipewa gruneti kama mshahara. Na bado katika nchi nyingine, “watoto hupewa majina ya bunduki za rashasha wanazopenda baba zao kama vile ‘Uzi’ na ‘AK,’” gazeti hilo lilisema.