Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ni Maua ya Mwituni au Magugu?

Je, Ni Maua ya Mwituni au Magugu?

Je, Ni Maua ya Mwituni au Magugu?

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Kanada

Maua ya mwituni huvutia. Tua kwa dakika chache na uchunguze maua hayo yenye umbo tata. Tazama jinsi yalivyo na rangi mbalimbali zenye kupendeza. Nusa harufu nzuri ya maua hayo. Na inatamanisha kama nini kugusa petali zake laini na nyororo! Sisi husisimuliwa na uzuri huo wa ajabu. Hata hisia zetu huchochewa na umaridadi wake. Kwa kweli, maua ya mwituni hurembesha mazingira yetu. Hufanya tufurahie zaidi maisha. Kwa hiyo tunapaswa kumshukuru Mbuni na Muumba wa maua hayo!

Ingawa sisi huvutiwa na maua kwa sababu ya rangi, umbo, na harufu yake nzuri, kusudi kuu la maua ni kutokeza mbegu ambazo ni muhimu kwa ajili ya kuzalisha mimea. Ili kutimiza hilo, maua yamebuniwa ili kuvutia wadudu, ndege, na hata popo kwa ajili ya uchavushaji. Ndege waimbaji na vipepeo hasa hutafuta maua ya mwituni. Jim Wilson, mwandishi na mkulima wa maua anasema: “Viumbe hao wanaoruka hula maua ya mwituni lakini hawali maua yaliyopandwa na watu.” Ni jambo linalopendeza kwamba kulingana na kitabu The World Book Encyclopedia, “hapo awali, maua yote yalikuwa ya mwituni.”

Kuna mimea mingi sana inayotokeza maua duniani pote. Kwa hiyo, tunawezaje kutambua ua la mwituni? Ua la mwituni ni nini? Kwa maneno rahisi, ua la mwituni ni mmea wowote unaotokeza maua ambao humea wenyewe. Huko Amerika Kaskazini pekee, kuna maua ya mwituni zaidi ya 10,000. Michael Runtz, ambaye ni mtaalamu wa viumbe na mimea na mwandishi wa kitabu Beauty and the Beasts—The Hidden World of Wildflowers, anasema: “Ingawa kwa ujumla neno hilo hurejelea mimea yenye mashina laini ambayo ina maua ya rangi nyingi, vitabu vinavyozungumzia maua ya mwituni pia vinatia ndani mimea yenye mashina magumu. Maelezo hayo mbalimbali hufanya iwe vigumu kueleza kwa usahihi mimea inayoweza kuitwa maua ya mwituni.”

Mbegu zinaweza kusafiri sana. Nyingine zinaweza kusafirishwa mbali sana na upepo au maji. Hata hivyo, mbegu nyingi hazisafirishwi mbali kwa sababu zimekusudiwa kuwa katika maeneo hususa. Mbegu ndogo sana zinaweza kupeperushwa mbali sana. Lakini mbegu zenye vitu vinavyonasa ambavyo vinafanana na parachuti kama vile mbegu za dandelion, haziwezi kusafiri mbali.

Huenda ukashangaa kujua kwamba ikiwa unaishi Amerika Kaskazini, maua mengi ya mwituni yaliyo katika eneo unamoishi yalitoka nchi mbalimbali. Kuvumbuliwa kwa meli zinazosafiri baharini na kugunduliwa kwa mabara mapya kulieneza mimea na mbegu nyingi kutoka maeneo yake ya asili. Mimea mingi kama hiyo ilitoka Ulaya au Asia. Nyingine zililetwa kimakusudi, nazo nyingine zililetwa kimakosa. Kwa kweli, mbegu za mimea mingi maridadi huko Amerika Kaskazini “zilipelekwa huko pamoja na mbegu za mazao; nyingine zikapelekwa na nafaka; nyingine katika vitu vilivyotumiwa kupakia bidhaa kama vile nyasi na majani makavu; nyingine ndani ya maji ya kuimarisha meli . . . Nyingine zikapelekwa zitumiwe kukoleza, kutia rangi, kuongeza harufu, na kutumiwa kama dawa,” chasema kitabu Wildflowers Across America. Hata hivyo, kwa nini mimea hii na mingine mingi inayotoa maua huitwa magugu?

Ua la Mwituni Linapokuwa Gugu

Kwa kawaida, mmea wowote unaokua sana mahali usipotakikana unaweza kuitwa gugu, iwe ni nyasi inayokua kwenye ua wako, katika bustani yako, au kati ya mazao yako. Kitabu cha marejeo Weeds of Canada kinasema: “Mimea mingi inayoitwa magugu haingekuwako . . . ikiwa mazingira yasiyo ya asili hayangekuwako.” Kitabu hicho kinaongeza hivi: “Tumechangia sana kuwepo kwa mazingira yanayofaa kwa ajili ya mimea ambayo sisi hutaka sana kuing’oa.” Maua fulani ya mwituni yasiyo ya eneo fulani huvamia mazingira ya mimea mingine dhaifu ambayo huota yenyewe na kubadili kabisa mazingira hayo. Katika njia hiyo, mimea isiyo ya asili inaweza kuwa magugu badala ya kuwa tu mimea inayoota yenyewe.

Ikiwa umejaribu kulima shamba dogo, utaelewa maana ya mimea isiyotakikana. Udongo wa shamba lisilolimwa unaweza kumomonyolewa upesi na upepo au maji. Wakati wote kunakuwa na mamilioni ya mbegu zisizoweza kumea za mimea mbalimbali ambazo huwa zimetawanyika kwenye udongo wa juu. Eneo lisipolimwa, magugu hukua kwa wingi katika eneo hilo ili kushikilia udongo. Ingawa huenda magugu hayo yakawatatiza wakulima, kuyaelewa hutusaidia kuona sehemu muhimu ambayo hutimizwa na magugu na maua ya mwituni.

Furahia Uumbaji Huu Unaovutia

Huwezi kukosa kuvutiwa na umaridadi wa milima iliyofunikwa na miti iliyochanua maua meupe ya trillium au chicory ya rangi ya buluu ambayo huchanua asubuhi na kufuata mwelekeo wa jua, na kujikunja wakati wa mchana kunapokuwa na jua. Maua hayo yanayochanua wakati wa majira ya kuchipua huwa mwanzo wa mfuatano wa maua maridadi yanayochanua katika majira mbalimbali miaka nenda miaka rudi. Baadhi ya maua hayo kama vile tawny daylily huchanua kwa muda mfupi tu. Mengine kama vile black-eyed Susan, huchanua kondeni au kando ya barabara mwishoni mwa majira ya kuchipua hadi majira ya kiangazi.

Kwa kweli, maua ya mwituni ni sehemu ya uumbaji inayovutia. Unapoyaona kwenye nyasi iliyo kwenye ua lako au bustanini au kando ya barabara au msituni, tua kwa dakika chache na utazame maumbo yake tata, rangi zenye kupendeza, na harufu nzuri. Tambua kwamba kwa kweli maua hayo yametokezwa na Mbuni nayo ni zawadi kutoka kwa Muumba wetu mkarimu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

Je, Ulijua?

Wakati fulani ua la kawaida la dandelion halikuwepo kamwe huko Amerika Kaskazini. Sasa ua hilo hupatikana katika sehemu nyingi za ulimwengu. Wataalamu fulani hudai kwamba lilitoka Asia Ndogo. Wazungu waliohamia Amerika ambao walilitumia kama chakula, walilipanda kwenye mashamba yao mapya. Mizizi ya dandelion imetumiwa kutengeneza dawa nyingi, nayo majani yake machanga yametumiwa katika saladi.

Maua yanayoitwa oxeye daisy ni miongoni mwa maua yanayokua sana kando ya barabara. Yalitoka Ulaya. Kwa kawaida, maua hayo hufanya mandhari iwe yenye kupendeza. Kila ua lina shada la maua ya manjano na meupe. Sehemu ya katikati ya maua hayo ina mamia ya maua madogo sana ya rangi ya dhahabu yanayoweza kuzaa ambayo yamezungukwa na petali 20 hadi 30 zisizoweza kuzaa na ambapo wadudu hupenda kutua.

Inaaminika kwamba ua la tawny daylily lilitoka Asia na kupelekwa Uingereza na mwishowe Amerika ya Kaskazini. Ingawa shina moja hutokeza maua mengi, maua hayo hudumu kwa siku moja tu. Huchanua asubuhi na kunyauka kabisa jioni.

Pia ua refu la kombetindi lilisafirishwa kutoka Ulaya hadi Amerika Kaskazini. Huko, kwa kawaida ua hilo hupatikana katika viwanja vyenye unyevu na kando ya barabara. Nyakati nyingine, ua hilo hukua na kufikia meta mbili au zaidi. Hata hivyo, ni watu wachache wanaotambua kwamba linaweza kuwa hatari. Karibu aina zote za ua hilo huwa na maji yanayowasha. Kwa karne nyingi, kombetindi fulani zimesemekana kuwa mimea inayosababisha malengelenge. Anne Pratt, mwandishi Mwingereza wa karne ya 19, alisema hivi: “Kuna visa ambavyo mtembeaji wa masafa marefu hulala karibu na maua hayo, na anapoamka shavu lake huuma na kuwasha sana kwa sababu ya umajimaji unaowasha wa maua hayo.”

[Hisani]

Dandelion: Walter Knight © California Academy of Sciences; tall buttercup: © John Crellin/www.floralimages.co.uk

[Picha katika ukurasa wa 16]

Maua ya chicory

[Picha katika ukurasa wa 16]

Tawny daylily

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Maua meupe ya trillium

[Picha katika ukurasa wa 17]

Black-eyed Susans

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Top left: www.aborea.se; top middle: Courtesy John Somerville/www.british-wild-flowers.co.uk; tawny daylily: Dan Tenaglia, www.missouriplants.com, www.ipmimages.org