Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukabiliana na Kansa ya Ngozi

Kukabiliana na Kansa ya Ngozi

Kukabiliana na Kansa ya Ngozi

JEREMIAH mwenye umri wa miaka 51 ni Mwaustralia wa asili ya Ireland, ambaye ana nywele nyekundu na ngozi nyeupe. Anasema hivi: “Kama Waaustralia wengi, mara nyingi familia yetu ilikuwa nje hasa miisho-juma na wakati wa likizo msimu wa kiangazi. Nilipokuwa mtoto, niliogelea kwenye kidimbwi kilichokuwa nyuma ya nyumba yetu kwa saa nyingi na nikateleza na kucheza kriketi kwenye fuo za Gold Coast, kusini ya Brisbane. Mara nyingi, nilivalia tu kaptura ya kuogelea.”

Jeremiah anaendelea kusema: “Losheni zenye nguvu za kutosha kukinga miale ya jua hazikubuniwa hadi nilipokuwa kijana. Siku hizo, matangazo ya biashara yaliwatia watu moyo watumie mafuta ya nazi ili wawe na ngozi nyeusi kama ile ya Waaustralia waliofanya kazi ya uokoaji katika sehemu za kuogelea. Wakati huo hatukujua sana jinsi ambavyo jua linaweza kudhuru ngozi. Nilianza tu kujikinga na kuepuka kukaa sana kwenye jua baada ya kupata maumivu ya kuunguzwa na jua mara kadhaa.” Lakini tayari alikuwa amepatwa na madhara. “Kwa sababu ya kuogelea na kuteleza kwa miaka mingi bila shati, nilipatwa na mabaka mengi ambayo yalianza kuwa meusi na makubwa hasa kifuani.”

Kufikia sasa Jeremiah amefanyiwa upasuaji mara tatu ili kuondoa uvimbe wa kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi na pia upasuaji mwingi wa kuondoa kansa inayoathiri chembe za juu. Kwa sababu ya hilo, amebadili mazoea yake. Anasema: “Kila siku, kabla ya kutoka nje, mimi hujipaka losheni ya ngozi. Kisha mimi hujipaka losheni ya kujikinga na jua. Siku hizi mimi huvaa kofia mara nyingi wakati wa kiangazi kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.” Yeye pia huenda kumwona mtaalamu wa ngozi baada ya kila miezi mitatu.

Jeremiah anaeleza kile ambacho kimemsaidia kukabiliana na hali hiyo ngumu: “Yehova Mungu amenipa usadikisho wenye nguvu wa kutazamia kupona wakati wengine walitazamia kwamba nitakufa mwaka wowote ule. Kwa kutegemea makadirio yaliyofanywa miaka 20 hivi iliyopita kuhusu watu wengi wenye kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi, watu wengi huona kwamba nitakufa hivi karibuni. Nimeona ukweli wa maneno ya Mfalme Daudi aliyesema: ‘Yehova mwenyewe atanitegemeza katika kitanda cha ugonjwa; kitanda changu chote hakika utakibadilisha wakati wa ugonjwa wangu.’”—Zaburi 41:3.

Mwingine ambaye amegua kansa ya ngozi ni Maxine. Alipokuwa bado na ngozi yake nzuri ya ujana, Maxine alitumwa kwenye nchi za Tropiki akiwa mmishonari, kwanza katika Jamhuri ya Dominika kisha Puerto Riko. Kwa miaka 20, kazi yake ya umishonari ilitia ndani kwenda nyumba kwa nyumba katika utumishi kwenye jua kwa muda mrefu. Pia, alipenda kujianika juani wakati wake wa mapumziko. Kisha, mnamo mwaka wa 1971 iligunduliwa kwamba alikuwa na kansa inayoathiri chembe za katikati za ngozi usoni. Alitibiwa kwa mnururisho, akafanyiwa upasuaji, kisha akapandikizwa ngozi kutoka sehemu nyingine mwilini. Hata hivyo, chembe za kansa ziliendelea kuongezeka.

Maxine anaeleza hivi: “Tatizo lilikuwa kwamba mara nyingi chembe zenye kansa hazikugunduliwa, kwa hiyo ziliendelea kuongezeka. Kimekuwa kipindi kirefu na chenye kufadhaisha, karibu miaka 30 ya kuwaona madaktari, kwenda kliniki, na hospitali. Nimefanyiwa upasuaji angalau mara kumi usoni, mbali na kwenda kliniki mara kadhaa kupata matibabu mengine ya kansa.” Sasa, Maxine aliye na umri wa miaka 80 amefanyiwa upasuaji wa Mohs ambao umefaulu kuondoa chembe zenye kansa.

Kwa sababu kansa yake ya ngozi inatokea mara kwa mara, imembidi Maxine abadili njia yake ya kufanya utumishi wa umishonari, kwa kuhubiri jioni ili kuepuka jua. Ni nini kimemsaidia Maxine kukabiliana na hali hiyo? “Jambo moja ni kudumisha mtazamo unaofaa. Ninajua kwamba chembe za kansa zitaendelea kutokea na kwamba nitalazimika kumwona daktari tena. Ninakubali hali hiyo. Sijisikitikii wala kulalamika kwa sababu ya matatizo yangu. Matatizo hayo hayafanyi nikose furaha katika huduma. Bado ninaweza kuzungumza na wengine kuhusu Ufalme wa Yehova. Na nina tumaini kwamba nitapona kabisa hivi karibuni katika ulimwengu mpya. Wakati huo nitakuwa na uso wenye kupendeza na usio na kasoro.”

Naam, watu walio na kansa ya ngozi na wenye magonjwa mengine wanaweza kutazamia wakati ambapo maneno haya yaliyoandikwa katika kitabu cha Ayubu yatatimia: “Nyama yake na iwe laini kuliko wakati wa ujana; na arudi kwenye siku za nguvu za ujana wake.” (Ayubu 33:25) Hadi wakati huo, sote na tutambue hatari zinazotokana na kupigwa na jua kwa muda mrefu na acheni tujitahidi kulinda ngozi zetu.

[Picha katika ukurasa wa 9]

Jeremiah amefanyiwa upasuaji wa kuondoa kansa mbalimbali za ngozi, kutia ndani kufanyiwa upasuaji mara tatu kuondoa kansa inayoathiri chembe za ndani za ngozi. Hata hivyo, bado ana matumaini na mtazamo mzuri

[Picha katika ukurasa wa 10]

“Katika ulimwengu mpya . . . , nitakuwa na uso wenye kupendeza na usio na kasoro.”—Maxine