Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Labda Ndicho Chuo Kikuu cha Kale Zaidi

Kikundi cha wanaakiolojia Wapolandi na Wamisri wamefukua eneo la chuo kikuu cha kale cha Alexandria, Misri. Kulingana na gazeti Los Angeles Times, kikundi hicho kilipata kumbi 13 zinazotoshana za mihadhara ambazo zingeweza kutoshea wanafunzi 5,000 hivi. Gazeti hilo linasema kwamba kumbi hizo “zina safu za mabenchi ya mawe yaliyopangwa kama ngazi kwenye kuta tatu za majumba hayo na nyakati nyingine yakiungana kufanyiza herufi ‘U.’” Katikati kuna kiti kilichoinuka ambacho huenda kilikuwa cha mhadhiri. Mwanaakiolojia Zahi Hawass, ambaye ni msimamizi wa Baraza Kuu la Vitu vya Kale la Misri anasema: “Ni mara ya kwanza kabisa kwa jengo lenye kumbi za mihadhara kufukuliwa katika eneo lolote lililotawaliwa na Wagiriki na Waroma katika eneo lote la Mediterania.” Hawass anasema “labda hicho ndicho chuo kikuu cha kale zaidi ulimwenguni.”

Ungependa Aiskrimu ya Kitunguu Saumu?

Kwa muda mrefu imesemwa kitunguu saumu ni dawa. Gazeti Philippine Star linaripoti kwamba Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Mariano Marcos huko kaskazini mwa Filipino kimetengeneza aiskrimu ya kitunguu saumu kwa sababu za “kiafya.” Inatazamiwa kwamba huenda bidhaa hiyo mpya ikawasaidia wale wenye magonjwa ambayo hutibiwa kwa kitunguu saumu. Baadhi ya magonjwa hayo ni, mafua, homa, kupanda kwa shinikizo la damu, matatizo ya kupumua, baridi yabisi, kuumwa na nyoka, maumivu ya meno, kifua-kikuu, kifaduro, vidonda, na hata upara. Kwa hiyo, ungependa aiskrimu ya kitunguu saumu?

Aktiki Ilikuwa na Joto

Kikundi cha kimataifa cha wanasayansi ambao wamekuwa wakichimba sakafu ya Bahari ya Aktiki kati ya Siberia na Greenland wanasema kuwa eneo hilo lilikuwa na joto. Shirika la Arctic Coring Expedition lilitumia meli tatu za kuvunja barafu kufanya kazi hiyo na walipata vipande vya miamba kutoka meta 400 hivi chini ya sakafu ya bahari. Visukuku vidogo vya mimea na wanyama wa baharini vilivyopatikana katika vipande hivyo vinaonyesha kwamba wakati mmoja halijoto ya bahari ilikuwa digrii 20 Selsiasi hivi, badala ya digrii -1.5 Selsiasi iliyopo leo. Kulingana na Profesa Jan Backman wa Chuo Kikuu cha Stockholm aliyenukuliwa na Shirika la Habari la BBC, “hali ya zamani ya Sakafu ya Aktiki itachunguzwa upya kwa kutegemea matokeo ya kisayansi yaliyopatikana katika uchunguzi huo.”

Ubao wa Elektroni Watumiwa Shuleni

Gazeti El Universal la Mexico City linaripoti kwamba madarasa zaidi ya 21,000 ya shule za msingi nchini Mexico, sasa yanatumia ubao wa elektroni uliounganishwa na kompyuta badala ya ubao wa rangi ya kijani, chaki, na kifutio ambavyo vimetumiwa kwa muda mrefu. Kwa sasa, ubao huo wenye upana wa karibu meta mbili na urefu wa meta moja unatumiwa katika darasa la tano na sita. Kuna vitabu saba vya kielektroni vinavyotumiwa kufundisha historia, sayansi, hisabati, jiografia, na masomo mengine. Pia video zinaweza kuonyeshwa kwenye ubao huo. Kwa sababu hiyo, wanafunzi katika darasa la mwalimu mmoja “wameona piramidi za Tikal na Palenque, wameona utamaduni wa Wamaya, na kusikiliza muziki [wao].” Kumekuwa na faida gani? Mwalimu huyo anasema kwamba, “watoto huwa makini zaidi, hujifunza, na kushiriki zaidi katika mazungumzo.”

Watu Milioni Moja Hujiua Kila Mwaka

Karibu nusu ya vifo vyote vyenye jeuri ulimwenguni hutokana na kujiua. Watu wapatao milioni moja hujiua kila mwaka, idadi iliyozidi vifo vyote vilivyotokana na kuuawa kimakusudi na vita mwaka wa 2001. Mtu mmoja anapojiua, kuna wengine kati ya 10 na 20 walioshindwa kujiua. Takwimu hizo zilichapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lililoko Geneva, Uswisi. Shirika hilo linasema kwamba katika kila kisa cha kujiua, “familia nyingi na marafiki huathiriwa kihisia, kijamii, na kifedha.” Ripoti hiyo inasema kwamba mambo yanayozuia watu wasijiue yanatia ndani “kujiheshimu sana,” utegemezo wa kihisia kutoka kwa marafiki na familia, mahusiano imara, na kuwa mtu wa kidini au wa kiroho sana.

Maonyo ya Dhoruba za Vumbi

Gazeti The Times la London linasema kwamba kutumia magari yanayoendeshwa kwa magurudumu yote manne jangwani “kumezidisha mara kumi dhoruba za vumbi ulimwenguni na kunaharibu mazingira na afya ya wanadamu.” Magari hayo huvunja-vunja tabaka la juu la udongo na kutifua vumbi. Profesa Andrew Goudie wa Chuo Kikuu cha Oxford anasema: “Kuna magari mengi sana ya aina hiyo jangwani leo. Huko Mashariki ya Kati, wahamaji waliochunga mifugo yao wakiwa juu ya ngamia sasa hutumia magari hayo.” Goudie anaonya kwamba mbali na kutifua vumbi jangwani, “dhoruba za vumbi hupeperusha dawa za kuua magugu na wadudu kutoka kwenye mashamba na sakafu ya maziwa yaliyokauka na kuzisambaza hewani.” Chembechembe hizo zinazopeperushwa pia huwa na mizio na bakteria zinazoweza kusababisha matatizo makubwa ya afya. Wanamazingira wanahofu kwamba sehemu fulani za Afrika zinaweza kukumbwa na dhoruba ya vumbi kama ile iliyotokea miaka ya 1930 iliyosababishwa na kulima kupita kiasi na ukame na ikaharibu mashamba huko Marekani.

Wapanda Milima Waumia kwa Kutokuwa Waangalifu

Kila mwaka, mamia ya watu hufa wanapopanda milima. Wengine hufa kwa sababu ya kuangukiwa na mawe au matatizo yasiyotarajiwa ya afya, kama vile mshtuko wa moyo. Hata hivyo, kulingana na gazeti la Ujerumani Leipziger Volkszeitung, sababu moja kuu ya vifo milimani ni kutokuwa waangalifu. Tatizo hilo haliwapati tu vijana na watu wasio na uzoefu. Kulingana na Miggi Biner, msimamizi wa shirika la Mountain Guides’ la Zermatt, Uswisi, “iwe mtu ni mzoefu au sivyo—mara nyingi tatizo hutokea kwa sababu watu hujiamini kupita kiasi au kupuuza hali ya hewa na hali nyingine.” Wengine wanaokuwa na simu za mkononi hujidanganya kuwa wako salama kwani wakati wowote hali ya dharura inapotokea helikopta itawaokoa.

Mawimbi Makubwa Yasiyotarajiwa

Inasemekana kwamba kwa wastani meli mbili kubwa huzama mahali fulani ulimwenguni kila juma. Hata meli kubwa sana za kubeba mafuta na kontena zenye urefu unaozidi meta 200 zimezama. Inaaminika misiba mingi kama hiyo imesababishwa na mawimbi makubwa yasiyotarajiwa. Ripoti kuhusu mawimbi makubwa sana yanayoweza kuzamisha meli kubwa zimepuuzwa kwa muda mrefu zikifikiriwa kuwa ni hekaya tu za mabaharia. Hata hivyo, mradi wa utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Ulaya unathibitisha ukweli wa hadithi hizo. Picha za bahari zilizopigwa kwa setilaiti zilichunguzwa ili kuonyesha mawimbi hayo. Kulingana na Süddeutsche Zeitung, kiongozi wa mradi huo Wolfgang Rosenthal anasema: “Tumethibitisha kwamba mawimbi makubwa sana ni ya kawaida kuliko ilivyofikiriwa.” Katika kipindi cha majuma matatu, kikundi chake kiliona angalau mawimbi kumi kama hayo. Ni kama mawimbi hayo husimama wima, yanaweza kuwa na urefu wa meta 40, na yanaweza kuipiga meli na kuiharibu vibaya au hata kuizamisha. Ni meli chache tu zinaweza kuyahimili. Rosenthal anasema, “Sasa tunapaswa kuchunguza kama mawimbi hayo yanaweza kutabiriwa.”