Je, Ni “Kana Kwamba Ilibuniwa”?
Je, Ni “Kana Kwamba Ilibuniwa”?
Je, umewahi kutazama anga usiku ukitumia darubini? Wengi ambao wamefanya hivyo watakuambia kwamba bado wanakumbuka mara ya kwanza walipoona sayari ya Zohali. Hiyo si sayari ya kawaida. Ikiwa imezungukwa na weusi wenye nyota nyingi zinazong’aa, sayari hiyo ina umbo la duara linalopenyeza nuru ambalo lina bangili bapa zenye kuvutia!
Bangili hizo ni nini? Huko nyuma katika mwaka wa 1610, wakati mtaalamu wa nyota Galileo alipotazama Zohali kwa mara ya kwanza kwa kutumia darubini aliyojitengenezea, sayari hiyo haikuonekana waziwazi hivi kwamba ilifikiriwa kuwa ina masikio, yaani kulikuwa na duara moja kubwa na duara mbili ndogo kando yake. Darubini zenye nguvu zilipotengenezwa, wataalamu wa nyota waliona bangili hizo waziwazi zaidi, lakini bado walibishana kuhusu jinsi zilivyotengenezwa. Wengi walidai kwamba bangili hizo zilikuwa visahani vigumu. Katika mwaka wa 1895, wataalamu wa nyota walipata uthibitisho wa kutosha kwamba bangili hizo zilifanyizwa kwa visehemu vingi vya mawe na barafu.
Kitabu The Far Planets kinasema: “Bangili za Zohali, ambazo ni vistari vilivyofanyizwa kwa vipande vingi sana vidogo vya barafu, ni mojawapo ya maajabu makuu ya Mfumo wa Jua. Bangili hizo zinazong’aa ni kubwa, kwani zinaenea umbali wa kilometa 400,000 kuanzia ukingo wa ndani ulio juu ya angahewa ya sayari hiyo hadi ukingo wa nje ambao hauonekani waziwazi. Pia bangili hizo ni nyembamba sana, meta 30 hivi kwa wastani.” Mnamo Juni, mwaka wa 2004, wakati chombo cha angani, Cassini-Huygens kilipofika sayari ya Zohali na kutuma habari na picha, wanasayansi walianza kujifunza mambo mengi zaidi kuhusu bangili hizo zenye kutatanisha.
Hivi karibuni makala moja katika gazeti Smithsonian ilisema: “Zohali inaonekana kana kwamba ilibuniwa, kwani ni kitu kikamilifu kama hisabati.” Tunaweza kukubaliana na maneno ya mwandishi huyo lakini hatukubaliani na maneno “kana kwamba.” Kwa kweli, sayari hiyo yenye kuvutia ni mojawapo ya sayari nyingine nyingi ambazo Biblia ilisema hivi kuzihusu miaka mingi iliyopita: “Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu; nalo anga linatangaza kazi ya mikono yake.”—Zaburi 19:1.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Background: NASA, ESA and E. Karkoschka (University of Arizona); insets: NASA and The Hubble Heritage Team (STScl/AURA)