Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Umewahi Kuonja Beri Zinazodunda-Dunda?

Je, Umewahi Kuonja Beri Zinazodunda-Dunda?

Je, Umewahi Kuonja Beri Zinazodunda-Dunda?

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Kanada

MKULIMA ananyunyiza salfa kwenye udongo ili kuufanya uwe na asidi zaidi. Mavuno yanapokaribia, anajaza shamba lake maji. Baada ya mavuno, anaangusha tunda hilo ili kuona kama litadunda-dunda.

Je, mkulima huyo ana kichaa? La, anafanya hivyo ili kuhakikisha kwamba mazao yake ni ya hali ya juu. Zao lake ni beri aina ya cranberry. Je, ungependa kujua mengi kuhusu matunda hayo magumu?

Beri Zinazokuzwa Kwenye Kinamasi

Wazungu walipofika kwenye pwani ya kaskazini-mashariki ya Amerika Kaskazini, wenyeji wa asili waliwauzia beri nyekundu zenye ladha chungu inayopendeza. Wenyeji wa asili wa Amerika walioishi katika eneo ambalo sasa linaitwa Cape Cod, waliita tunda hilo i-bimi, au “tunda chungu.” Wakoloni Waingereza waliita tunda hilo jina la ndege fulani labda kwa sababu shina na ua la mmea huo linafanana na shingo na kichwa cha ndege huyo. Pia ndege hao walipenda kula tunda hilo, na huenda hiyo ni sababu nyingine iliyofanya tunda hilo lipewe jina la ndege huyo.

Wenyeji wa asili wa Amerika walikusanya matunda hayo katika kinamasi kilichojaa mimea iliyooza. Mimea hiyo ilifanya udongo uwe na asidi isivyo kawaida na kufanya mimea mingi isikue. Hata hivyo, cranberry husitawi katika udongo huo. Mizabibu hiyo mifupi inayofanana na stroberi ilikua sana katika sehemu za kusini za Virginia ya sasa hadi sehemu za kaskazini huko Kanada.

Mnamo 1680, Mahlon Stacy, aliyekuwa mkazi wa New Jersey, alimweleza ndugu yake aliyeishi Uingereza kuhusu tunda hilo. Aliandika hivi: “Matunda hayo yenye rangi na ukubwa kama wa cheri, yanaweza kuhifadhiwa hadi msimu mwingine wa matunda. Matunda hayo hutengeneza mchuzi wa nyama ya wanyama wa pori, bata-mzinga, na ndege wengine wakubwa na yanafaa zaidi kutengeneza pai kuliko kutumia zabibu-bata au cheri. Wenyeji wa asili wa Amerika hutuletea matunda hayo kwa wingi nyumbani mwetu.”

Ni Chakula, Dawa, na Dawa ya Kuhifadhi

Wenyeji wa asili wa Amerika walitumia cranberry kuhifadhi vitu. Walitayarisha nyama au samaki waliokaushwa na kusagwa pamoja na cranberry. Mchanganyiko huo ulitengenezwa kama keki na kukaushwa kwenye jua. Keki hizo zenye protini na vitamini zilitumiwa wakati wa majira marefu ya baridi kali. Beri hizo huhifadhi chakula vizuri kwani zina pektini nyingi. Pia zina vitamini C nyingi. Kwa hiyo, zamani mabaharia walinunua mapipa yaliyojaa beri hizo walipofunga safari ndefu ili kukabiliana na ugonjwa wa kiseyeye.

Pia wenyeji wa asili wa Amerika walitumia beri hizo kama dawa, wakizichanganya na unga wa mahindi na kupaka juu ya vidonda ili kuzuia vimelea visiingie katika damu. Uchunguzi wa kitiba wa karibuni umeonyesha kwamba kunywa maji ya cranberry kunaweza kuzuia maambukizo fulani ya mfumo wa mkojo kwa kuzuia bakteria zisishike kuta za mfumo huo.

Kwa Nini Linaitwa Beri Inayodunda-Dunda?

Ukikata cranberry iliyoiva, utaona vifuko vinne vya hewa. Vifuko hivyo huwasaidia wakulima wanaouza cranberry katika njia mbili. Kwanza, badala ya kufanya kazi ngumu ya kuchuma beri, wakulima wanaweza kujaza mashamba yao maji kisha watikise mizabibu. Hilo hufanya beri zilizoiva zianguke na kuelea kwenye maji kwa sababu ya vifuko hivyo vya hewa. * Kisha wakulima huchota beri hizo na kuzichagua.

Wakulima wa cranberry waligundua faida ya pili ya vifuko vya hewa mwishoni mwa miaka ya 1800. Hekaya zinasema kuwa mkulima fulani aliangusha ndoo ya beri kwenye ngazi bila kukusudia naye alishangaa kuona beri nzuri zaidi zikidunda-dunda hadi chini kabisa, lakini zile zilizooza na nyororo zikikwama kwenye ngazi. Vifuko vya hewa vilifanya beri nzuri zaidi zidunde-dunde kama tairi zilizojazwa hewa. Beri zisizo nzuri zilikuwa kama tairi zisizo na hewa.

Mnamo 1881 mashini za kwanza za kudundisha beri zilitengenezwa. Leo, mashini zinazotenganisha beri hutumia mbinu hiyo ya kudundisha beri nzuri kuvuka kizuizi fulani kisha hukusanywa na kuuzwa. Zile nyororo huanguka kwenye mashini na hutengeneza maji ya matunda au jeli.

Katika vinamasi vilivyotayarishwa kwa njia maalumu huko kaskazini-mashariki na kaskazini-magharibi mwa Marekani na Kanada, wakulima huvuna zaidi ya kilogramu milioni 250 za cranberry kila mwaka. Ikiwa hujawahi kuonja pai ya beri, kwa nini usifanye hivyo? Tunda hilo lina vitamini na madini mengi sana, na lina vitu vinavyozuia chembe zisiharibiwe na hilo linaweza kuzuia ugonjwa wa moyo na kansa. Hata linaweza kufanya udunde-dunde kutokana na afya nzuri.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Mbinu ya kufanya vinamasi vya cranberry vifurike wakati wa mavuno imefanya watu waamini kimakosa kwamba beri hizo hukua chini ya maji.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Je, Cranberry Hukua tu Huko Amerika Kaskazini?

Kwa kawaida, cranberry huliwa kwenye mlo wa Sikukuu ya Kutoa Shukrani, ambayo husherehekewa Alhamisi ya nne ya Novemba huko Marekani na Jumatatu ya pili ya Oktoba huko Kanada. Kulingana na hekaya, mnamo 1621, wenyeji wa asili wa Amerika walileta cranberry kwenye sherehe ya kwanza ya Sikukuu ya Kutoa Shukrani, iliyokuwa sherehe ya siku tatu ya kula na kujifurahisha, ambayo ilidhaminiwa na William Bradford, gavana wa Koloni ya Plymouth. Kwa kuwa desturi nyingi zinahusianishwa na cranberry, na tunda hilo ni mojawapo ya aina chache za beri kutoka Amerika Kaskazini zinazouzwa, wengi hufikiri tunda hilo hukua katika eneo hilo tu.

Hata hivyo, tunda hilo dogo (V. oxycoccus) la Amerika Kaskazini hukua pia katika Asia na Ulaya kaskazini na kati. Tunda hilo halipikwi tu huko Amerika Kaskazini bali linatumiwa pia kwingineko. Kichapo Encyclopædia Britannica kinasema: “Watu hufikiri mchuzi na jeli ya cranberry hutumiwa tu Amerika, lakini Waskandinavia huhusudu sana tunda lao la asili linaloitwa lingonberry (V. vitisidaea), ambalo linafanana na cranberry ya Amerika [V. macrocarpon] lakini ni chungu zaidi.”

[Picha katika ukurasa wa 15]

Maua ya cranberry

[Hisani]

Courtesy Charles Armstrong, Cranberry Professional, Univ. of Maine Cooperative Extension, USA

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kuvuna cranberry katika vinamasi vilivyofurika

[Hisani]

Keith Weller/Agricultural Research Service, USDA

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kuvuna cranberry nyeupe

[Hisani]

Inset photos: Courtesy of Ocean Spray Cranberries, Inc.