Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuiba Vitu Dukani—Je, Ni Msisimuko Usiodhuru Au Ni Uhalifu Mbaya?

Kuiba Vitu Dukani—Je, Ni Msisimuko Usiodhuru Au Ni Uhalifu Mbaya?

Kuiba Vitu Dukani—Je, Ni Msisimuko Usiodhuru Au Ni Uhalifu Mbaya?

WAZIA tukio hili. Mlango wa duka kubwa unafunguliwa na wasichana wawili waliovalia vizuri wanaingia. Wanatembea kuelekea mahali ambapo vipodozi huwekwa. Mlinzi aliyevalia mavazi rasmi anawafuata na kusimama meta 10 hivi kutoka mahali walipo akiwa ameweka mikono nyuma. Anawatazama wasichana hao wanaposhika-shika lipstiki na wanja.

Wanamtazama mlinzi ambaye anawakazia macho. Wanasisimuka sana. Msichana mmoja anasogea karibu na rangi za kucha na kuchukua chupa kadhaa. Anasitasita huku akijifanya kuwa anachunguza rangi mbili nyekundu zinazokaribiana. Anaweka chupa moja chini na kuchukua nyingine ambayo ni nyekundu zaidi.

Mlinzi anatazama chini na kugeuka kutazama upande mwingine. Mara moja, wasichana hao wanaweka lipstiki na chupa za rangi za kucha katika vibeti vyao. Wanaonekana kuwa watulivu, lakini ndani wamesisimuka sana. Wanasimama mahali hapo kwa dakika chache, mmoja anaangalia tupa za kusugua kucha huku mwingine akitazama wanja.

Wasichana hao wanatazamana kisha wanatoleana ishara, na kuanza kutembea kuelekea mlangoni. Mlinzi anawapisha, nao wanamtazama na kutabasamu wanapompita. Wanapopita karibu na vifaa vya simu za mkononi kando ya keshia, wanavitazama. Wananong’onezeana kuhusu mifuko ya ngozi ya simu za mkononi. Kisha wanatembea kuelekea mlangoni.

Kila hatua wanayopiga inawafanya wasisimuke zaidi na kujawa na woga. Wasichana hao wanapopita mlangoni, wanataka kupiga mayowe, lakini wanajizuia. Wakiwa nje, joto linawapanda. Msisimuko waliokuwa nao unapungua, nao wanashusha pumzi. Wasichana hao wanatembea haraka huku wakicheka-cheka. Wote wanafikiria jambo moja:‘Hatukukamatwa!’

Wasichana hao wawili si watu halisi lakini kwa kusikitisha, tukio hilo linaonyesha mambo halisi. Nchini Marekani pekee, kuna visa karibu milioni moja vya wizi wa aina hiyo, hata hivyo hilo ni tatizo la ulimwenguni pote. Kama tutakavyoona, tatizo hilo linatokeza madhara makubwa sana. Lakini watu wengi wanaoiba vitu dukani hawafikirii hasara wanayotokeza. Hata watu wengi wenye pesa huiba. Kwa nini?