Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Makaa ya Mawe—Mawe Meusi Kutoka Shimo Jeusi

Makaa ya Mawe—Mawe Meusi Kutoka Shimo Jeusi

Makaa ya Mawe—Mawe Meusi Kutoka Shimo Jeusi

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Australia

“HUWEZI kuelewa weusi ni nini hadi uteremke kwenye mgodi wa makaa ya mawe,” akasema rafiki yangu Bernie kwa sauti kubwa kwa sababu mashini zilikuwa zikipiga kelele. Ninapoangalia shimo lenye kina kirefu lililo mbele yangu, ninaanza kujiuliza ikiwa kweli ninataka kujua Bernie anamaanisha nini. Tunaelekea kwenye tabaka la makaa ya mawe lililo nusu kilometa chini ya ardhi.

Tunapita kikundi cha wachimba migodi wanaojikokota kuelekea kwenye bafu. Watu hao wana mabega mapana na lafudhi nzito ya Kiaustralia. Wanapotabasamu, macho na meno yao yanang’aa kwa sababu vumbi ya makaa ya mawe imefanya nyuso zao ziwe nyeusi.

Tunapanda treni ndogo inayotuteremsha kwenye mgodi wa makaa ya mawe. Mteremko huo ni mkali sana hivi kwamba kiti cha dereva kimeundwa ili kiweze kuzunguka, kikining’inia kwenye paa ya treni. Nimefungwa betri isiyoweza kutoa cheche kiunoni ambayo huwasha taa iliyo kwenye kofia yangu, pia nina kifaa cha kutoa hewa safi wakati wa dharura. Treni hiyo inapoteremka, anga linafifia na kuwa ndogo na mwishowe linaonekana kama doa dogo la buluu lililozungukwa na rangi nyeusi.

Wafanyakazi Wachache Wachimba Makaa ya Mawe Mengi Zaidi

Mgodi huu ni mojawapo ya migodi mingi iliyoko kusini-mashariki mwa Australia. Bernie, anayenitembeza ni kati ya wachimba migodi 25,000 ambao huchimba makaa ya mawe yenye thamani ya dola milioni elfu nane [za Australia] kila mwaka kutoka kwenye migodi ya Australia. Ulimwenguni pote, wachimba makaa ya mawe milioni kumi hufanya kazi kwenye migodi iliyo chini au juu ya ardhi. Lakini idadi hiyo inapungua. Huko Uingereza, idadi ya wachimba migodi ilipungua kutoka milioni 1.2 mwaka wa 1978 kufikia 13,000 hivi mwanzoni mwa karne hii. Nchini Marekani, idadi ya wachimba migodi ilipungua kutoka 705,000 mwaka wa 1924 kufikia chini ya 82,000. China ilipunguza wachimba migodi 870,000 katika kipindi cha miaka mitano hivi karibuni.

Hata hivyo, kupungua kwa wachimba migodi hakumaanishi matumizi ya makaa ya mawe yamepungua. Kwa kweli, inatabiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2020, matumizi ya makaa ya mawe yataongezeka kwa asilimia 11 katika nchi zilizoendelea kiviwanda, na China na India zinatazamiwa kujenga stesheni mpya zaidi ya 750 za kutokeza umeme kwa kutumia makaa ya mawe katika kipindi hichohicho. Idadi ya wafanyakazi imepungua hasa kwa sababu ya teknolojia mpya, inayowezesha kampuni zitumie watu wachache kutokeza makaa ya mawe mengi zaidi. Mashini kubwa ambayo Bernie anataka kunionyesha ni mojawapo ya teknolojia hiyo ya hali ya juu.

Ndani ya Mgodi Wenye Giza

“Hii ndiyo sakafu ya mgodi,” anasema Bernie tunapotoka kwenye treni. “Mashimo yote ya chini ya ardhi huanzia hapa.” Kuna taa za mmemeto kwenye dari. Magogo madogo yaliyowekwa katikati ya sakafu na paa hutegemeza maboriti membamba yanayoshikilia paa. Bolti nyingi sana zimefungwa kwenye dari. Bolti hizo zimeshindiliwa meta mbili ndani ya paa na kushikilia mwamba ulio juu ili kuzuia mgodi usiporomoke.

Ninashangaa kuona kuta si nyeusi bali nyeupe. Bernie anaeleza: “Kuta zimepakwa chokaa. Chokaa hupunguza hatari ya kutokea kwa mlipuko unaosababishwa na gesi ya methani na vumbi ya makaa ya mawe. Cheche inaweza kuwasha methani. Nayo gesi ya methani inaweza kusababisha mlipuko mkubwa kwa sababu ya vumbi ya makaa ya mawe iliyo hewani. Kila dakika, karibu lita 2,000 za methani hutolewa nje ya mgodi huu na hutumiwa kutokeza umeme katika mgodi.” Ili kuepuka uwezekano wa cheche kuwasha gesi zozote zinazovuja, niliacha nje kamera, redio, na hata saa yangu ya betri.

Ndani ya mojawapo ya miingilio ya mashimo hayo mengi yanayoelekea sehemu mbalimbali za mgodi, kuna gari dogo lenye nguvu, la diseli. Mota inapowashwa, tunaelekea katika mojawapo ya mashimo yaliyo chini ya ardhi. Nuru inafifia, lakini taa iliyo kwenye kofia yangu inamulika dari lililo sentimeta chache tu juu ya kichwa changu. Tunapopita mashimo mengine mengi, ninaona taa nyingine za kofia zikimweka kama vimulimuli gizani. Kwenye shimo jingine kando yetu, mkanda wa kusafirishia vitu wenye urefu wa kilometa tano unavuta makaa ya mawe kutoka kwenye mgodi.

Mashini ya Kuchimba Inayoitwa Longwall

Tunapofika kwenye mgodi wenyewe, ingawa kuna ukungu unaotokezwa na maji na vumbi ya makaa ya mawe, ninaona watu watatu wakiwa wamevalia mavazi maalumu, vifuniko vya kichwa, na vifaa vya kujikinga na vumbi. Wanaume hawa hufanya kazi pamoja wakitumia mashini kubwa yenye upana wa meta 250 inayoitwa longwall miner. Silinda mbili zinazozunguka, kila moja yenye kipenyo cha meta mbili, husonga polepole juu ya mgodi kutoka upande mmoja wa mashini hadi mwingine. Silinda hizo zina misumari ambayo hukata ukuta wa mgodi kwa kina cha nusu meta zinapozunguka. Mashini hiyo ina mkanda wa kusafirishia vitu ambao huvuta makaa ya mawe kupitia shimo lililo kando, ambako mawe hayo huvunjwa-vunjwa katika vipande vinavyotoshana na kubwagwa kwenye mkanda mkubwa wa kusafirishia vitu.

Nguzo nene za haidroli ambazo hushikilia mabamba makubwa ya chuma yaliyo juu ya vichwa vya waendeshaji huzuia mwamba ulio juu usiporomoke. Silinda hizo zinapomaliza kukata, mashini yote, yaani, silinda, nguzo za haidroli, na paa ya mabamba ya chuma, hujisongeza mbele nusu meta. Mashini hiyo inaposonga mbele, inaacha mwamba ukiwa umening’inia. Mwamba huo huning’inia kwa muda mfupi. Kisha unaporomoka kwa kishindo chenye kuogofya! “Kwa njia hii tunachimba tani elfu moja za makaa ya mawe kwa saa,” anasema Bernie. “Sehemu kubwa ya makaa ya mawe ikiondolewa, mashini hiyo hufunguliwa na kupelekwa sehemu nyingine.”

Mwishowe, Twaona Nuru!

Mimi na Bernie tunarudi kwenye lile gari dogo na kusafiri kilometa tano kupitia mashimo yaliyo chini ya ardhi kabla ya kusimama kwenye pango kubwa. Shimo linaloelekea juu lenye kipenyo cha meta kumi, hutokea kwenye uso wa dunia kutoka kwenye pango hilo. “Ule mkanda mkubwa wa kusafirishia vitu humwaga makaa ya mawe hapa,” anasema Bernie kwa sauti kubwa kwa sababu ya kelele za makaa ya mawe yanayoanguka ndani ya pipa kubwa la chuma. “Pipa unaloona linaweza kubeba tani 18 za makaa ya mawe.” Bernie anapozungumza, pipa lililojaa linavutwa juu kwa waya. Pipa jingine linateremshwa kutoka kwenye shimo lililo katika dari na kuanza kujazwa tena.

Tunapomaliza matembezi, tunapanda treni inayojikokota hadi kwenye mwingilio wa mgodi huku nikifikiri tutatokea kwenye mwangaza wa jua linalovutia. Hata hivyo, tumekaa ndani ya mgodi kwa muda mrefu hivi kwamba jua limetua na giza likaingia. Ingawa nje kuna giza nzito, sasa ninaelewa kwa nini Bernie alisema: “Huwezi kuelewa weusi ni nini hadi uteremke kwenye mgodi wa makaa ya mawe.”

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Mjadala Mkali Kuhusu Makaa ya Mawe

Makaa ya Mawe na Uchafuzi: Ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa inasema: “Moshi na chembe ndogo za makaa ya mawe husababisha vifo zaidi ya 50 000 vya mapema na visa vipya 400 000 vya ugonjwa wa mkamba kila mwaka katika majiji makubwa 11 [ya China].” Taasisi ya Worldwatch inasema kwamba kila mwaka, zaidi ya vifo milioni moja na nusu ulimwenguni husababishwa na uchafuzi wa makaa ya mawe. Kuna mbinu ya kisasa ya kuondoa uchafuzi huo lakini ni ghali sana hivi kwamba nchi nyingi zinazohitaji sana umeme haziwezi kuigharimia.

Makaa ya Mawe na Badiliko la Hali ya hewa: Kuchoma makaa ya mawe hutokeza zaidi ya tani milioni elfu mbili za gesi ya kaboni dioksidi kila mwaka. Na inatabiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2020, makaa ya mawe yatakuwa ya pili katika kutokeza moshi wenye kaboni, kwa kiwango cha asilimia 34 hivi. Wengi wanashtuliwa sana na takwimu hizo.

Seth Dunn, mtafiti msaidizi wa Taasisi ya Worldwatch anasema: “Tunapaswa kupunguza haraka matumizi ya makaa ya mawe ili kupunguza mabadiliko ya hali ya hewa katika karne inayofuata.”

[SandukuPicha katika ukurasa wa 14]

Kutegemea Sana Makaa ya Mawe

▪ Zaidi ya asilimia 70 ya chuma inayotokezwa ulimwenguni husafishwa kwa tanuri ya makaa ya mawe. Zaidi ya hayo, wanaotengeneza matofali, vigae, saruji, plastiki, rangi, na baruti hutumia kemikali zinazotokana na makaa ya mawe.

▪ Hata hivyo, viwanda vya kutokeza umeme ndivyo hutumia makaa ya mawe mengi zaidi. Asilimia 84 ya umeme nchini Australia hutokezwa na viwanda vinavyotumia makaa ya mawe. Angalau robo tatu ya umeme unaotumiwa nchini China, Afrika Kusini, na Denmark, hutokezwa kwa makaa ya mawe. Marekani hutegemea makaa ya mawe kutokeza zaidi ya nusu ya umeme wake. Makaa ya mawe hutumiwa kutokeza zaidi ya thuluthi moja ya umeme unaotumiwa ulimwenguni.

▪ Yaani, ikiwa una jiko la umeme, unatumia karibu nusu tani ya makaa ya mawe kila mwaka. Kifaa cha umeme cha kupasha maji joto kitahitaji tani mbili za makaa ya mawe kwa kipindi hichohicho, nayo friji yako itatumia nusu tani kila mwaka.

▪ Wanasayansi wanakadiria kuwa kuna akiba ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni milioni moja inayotosha kutumiwa kwa mamia ya miaka ijayo kulingana na kiwango kinachotumika sasa.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 12, 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mgodi wa Makaa ya Mawe Chini ya Ardhi

Rundo la makaa ya mawe

Njia ya kuingia kwenye mgodi

[Picha]

Mashini inayoitwa “longwall miner”

[Picha]

Gari dogo

Mabomba ya kuondoa gesi

Pipa la makaa ya mawe

Sakafu ya mgodi

[Picha]

Sehemu ya mkanda wa kusafirishia vitu wenye urefu wa kilometa tano

[Picha katika ukurasa wa 13]

Magogo na maboriti hutegemeza mashimo yaliyochimbwa zamani